Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezra 5:1-17

Ezra 5:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi manabii, Hagai nabii, na Zekaria mwana wa Ido, wakawafanyia unabii Wayahudi waliokuwako Yerusalemu na Yuda; waliwafanyia unabii kwa jina la Mungu wa Israeli. Ndipo akaondoka Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na Yoshua, mwana wa Yosadaki, wakaanza kuijenga nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu; na pamoja nao walikuwa manabii wa Mungu, wakiwasaidia. Wakati ule ule Tatenai, liwali wa ng’ambo ya Mto, na Shethar-Bozenai, na wenzi wao, wakawajia, wakawaambia, Ni nani aliyewapa amri kuijenga nyumba hii, na kuumaliza ukuta huu? Ndipo wakawauliza hivi, Majina ya watu wanaofanya ujenzi huu ni nani na nani? Lakini jicho la Mungu lilikuwa likiwaelekea wazee wa Wayahudi, hao wasiwazuie, hata habari ile imfikilie Dario, ndipo jawabu litakapopatikana kwa waraka. Hii ndiyo nakala ya waraka waliyompelekea mfalme Dario; na Tatenai, liwali wa ng’ambo ya Mto, na Shethar-Bozenai, na wenzake wa Kiajemi, waliokuwako huko ng’ambo ya Mto, walimpelekea waraka nao; na maneno haya yakaandikwa ndani yake; Kwa Dario, mfalme Salamu sana. Na ajue mfalme ya kuwa sisi tuliingia nchi ya Yuda, tukafika kunako nyumba ya Mungu mkuu, iliyojengwa kwa mawe makubwa, na miti imetiwa katika kuta zake, na kazi hii inaendelea kwa bidii, na kusitawi katika mikono yao. Ndipo tukawauliza wale wazee, tukawaambia hivi, Ni nani aliyewapa amri kuijenga nyumba hii, na kuumaliza ukuta huu? Tukawauliza pia majina yao, ili kukuarifu wewe, tupate kuandika majina ya watu waliokuwa wakubwa wao. Wakatujibu hivi, wakasema, Sisi tu watumishi wa Mungu wa mbingu na nchi, nasi tunaijenga nyumba iliyojengwa zamani sana, yapata miaka mingi, ambayo mfalme mkuu wa Israeli aliijenga na kuimaliza. Lakini hapo baba zetu walipomkasirisha Mungu wa mbingu na nchi, hata akaghadhibika, akawatia katika mkono wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, Mkaldayo, naye ndiye aliyeiharibu nyumba hii, akawachukua watu mateka mpaka Babeli. Lakini katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Babeli, Koreshi, mfalme, alitoa amri ijengwe tena nyumba ya Mungu. Na vyombo vya dhahabu na fedha, vya nyumba ya Mungu, alivyovitoa Nebukadreza katika hekalu lililokuwako Yerusalemu, na kuviingiza katika hekalu la Babeli, vyombo hivyo mfalme Koreshi alivitoa katika hekalu la Babeli, akakabidhiwa mtu, jina lake Sheshbaza, ambaye alikuwa amemfanya liwali; naye akamwambia, Chukua vyombo hivi, uende, ukavitie katika hekalu lililoko Yerusalemu, na nyumba ya Mungu na ijengwe mahali pake. Ndipo ye yule Sheshbaza alipokuja, akaupiga msingi wa nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu; na tangu wakati ule hata leo imekuwa ikijengwa, wala bado haijamalizika. Basi, sasa, mfalme akiona vema, watu na watafute katika nyumba ya hazina ya mfalme, iliyoko huko Babeli, kama ni kweli ya kuwa mfalme Koreshi alitoa amri kuijenga nyumba hiyo ya Mungu katika Yerusalemu, na mfalme akatuletee habari ya mapenzi yake katika jambo hili.

Shirikisha
Soma Ezra 5

Ezra 5:1-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ndipo nabii Hagai na nabii Zekaria mzao wa Ido, wakawatolea unabii Wayahudi waliokuwa Yuda na Yerusalemu kwa jina la Mungu wa Israeli, aliyekuwa pamoja nao. Ndipo Zerubabeli mwana wa Shealtieli na Yeshua mwana wa Yosadaki wakaanza kujenga tena nyumba ya Mungu huko Yerusalemu. Nao manabii wa Mungu walikuwa pamoja nao, wakiwasaidia. Wakati ule Tatenai mtawala wa ngʼambo ya mto Frati na Shethar-Bozenai na wenzao waliwaendea, wakawauliza, “Ni nani aliyewapa ruhusa ya kujenga tena Hekalu hili na kurudishia upya kama lilivyokuwa?” Pia waliwauliza, “Je, majina ya watu wanaofanya ujenzi huu ni nani?” Lakini jicho la Mungu wao lilikuwa likiwaangalia wazee wa Wayahudi, nao hawakuzuiliwa kujenga mpaka taarifa ikaandikwa kwa Dario na majibu yake kupokelewa. Hii ni nakala ya barua ile Tatenai, mtawala wa ngʼambo ya mto Frati na Shethar-Bozenai na wenzao maafisa wa ngʼambo ya mto Frati waliyompelekea Mfalme Dario. Taarifa waliyompelekea ilisomeka kama ifuatavyo: Kwa Mfalme Dario: Salamu kwa moyo mkunjufu. Inampasa Mfalme ajue kwamba tulikwenda katika eneo la Yuda, kwenye Hekalu la Mungu mkuu. Watu wanalijenga kwa mawe makubwa na kuweka mbao kwenye kuta. Kazi inafanyika kwa bidii na inaendelea kwa haraka chini ya uongozi wao. Tuliwauliza viongozi, “Ni nani aliyewapa ruhusa kujenga upya Hekalu hili na kurejeza hali ya jengo kama lilivyokuwa?” Pia tuliwauliza majina yao, ili tukuandikie kukujulisha majina ya viongozi wao. Hili ndilo jibu walilotupa: “Sisi ni watumishi wa Mungu wa mbingu na nchi, nasi tunalijenga upya Hekalu ambalo lilijengwa miaka mingi iliyopita, lile ambalo mfalme mkuu wa Israeli alilijenga na kulikamilisha. Lakini kwa sababu baba zetu walimkasirisha Mungu wa mbinguni, basi aliwatia mkononi mwa Nebukadneza, Mkaldayo, mfalme wa Babeli, ambaye aliliharibu Hekalu hili na kuwaondoa watu na kuwapeleka uhamishoni huko Babeli. “Pamoja na hayo, katika mwaka wa kwanza wa kutawala Koreshi mfalme wa Babeli, Mfalme Koreshi alitoa amri ya kujengwa upya nyumba hii ya Mungu. Yeye hata aliviondoa vyombo vya dhahabu na fedha vya nyumba ya Mungu, kutoka Hekalu la Babeli ambavyo Nebukadneza alikuwa amevichukua kutoka ndani ya Hekalu huko Yerusalemu na kuvileta katika Hekalu la Babeli. “Vyombo hivyo Mfalme Koreshi alimkabidhi mtu aliyeitwa Sheshbaza, ambaye Koreshi alikuwa amemteua awe mtawala, naye akamwambia, ‘Chukua vyombo hivi uende ukaviweke ndani ya Hekalu huko Yerusalemu. Nawe uijenge upya nyumba ya Mungu mahali pake.’ Hivyo huyu Sheshbaza alikuja na kuweka misingi ya nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu. Tangu siku hiyo hadi sasa imekuwa ikiendelea kujengwa lakini bado haijamalizika.” Sasa kama ikimpendeza mfalme, uchunguzi na ufanyike katika kumbukumbu za maandishi ya ufalme mjini Babeli, kuona kama kweli Mfalme Koreshi alitoa amri ya kujenga upya nyumba ya Mungu katika Yerusalemu. Kisha tunaomba mfalme na atutumie uamuzi wake kuhusu jambo hili.

Shirikisha
Soma Ezra 5

Ezra 5:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

Wakati huo, manabii wawili, Hagai na Zekaria, mwana wa Ido, waliwatolea unabii Wayahudi waliokuwa wanakaa Yuda na Yerusalemu, katika jina la Mungu wa Israeli. Nao Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na Yeshua, mwana wa Yosadaki, walipousikia ujumbe huo walianza tena kuijenga nyumba ya Mungu mjini Yerusalemu, wakisaidiwa na manabii wa Mungu. Baadaye Tatenai, mtawala wa mkoa wa magharibi ya Eufrate, Shethar-bozenai na wenzao, walikwenda Yerusalemu na kuuliza, “Nani aliyewaamuru kuijenga nyumba hii mpaka kuimaliza?” Pia waliuliza, “Ni akina nani wanaojenga nyumba hii? Tunataka majina yao.” Lakini Mungu alikuwa anawalinda viongozi wa Wayahudi, kwa hiyo maofisa hao hawakuwakataza mpaka hapo walipomwandikia mfalme Dario na kupata maoni yake. Basi, Tatenai, mtawala wa mkoa wa magharibi ya Eufrate, Shethar-bozenai na wenzao, wakamwandikia mfalme Dario. Ifuatayo ni ripoti waliyompelekea mfalme: “Kwa mfalme Dario; tunakutakia amani. Tungetaka kukufahamisha ee mfalme, kuwa tulikwenda mkoani Yuda ilipo nyumba ya Mungu Mkuu. Nyumba hii inajengwa upya kwa mawe makubwamakubwa na kuta zake zinawekwa boriti za miti. Kazi hiyo inafanywa kwa uangalifu mkubwa na inaendelea vizuri sana. Tuliwauliza viongozi hao watuambie ni nani aliyewapa amri ya kuijenga upya nyumba hii mpaka kuimaliza. Tuliwauliza pia majina yao ili tuweze kukujulisha wale wanaoongoza kazi hiyo. “Wao walitujibu hivi: ‘Sisi ni watumishi wa Mungu wa mbingu na dunia, na tunaijenga upya nyumba ambayo ilikuwa imejengwa na kumalizika hapo awali na mfalme mmoja mkuu wa Israeli. Lakini kwa kuwa babu zetu walimkasirisha Mungu wa mbingu, yeye aliwatia mikononi mwa mfalme Nebukadneza wa Babuloni, Mkaldayo, aliyeiharibu nyumba hii na kuwapeleka watu uhamishoni huko Babuloni. Lakini mnamo mwaka wa kwanza wa utawala wake mfalme Koreshi wa Babuloni alitoa amri nyumba hii ya Mungu ijengwe upya. Pia alivirudisha vyombo vya dhahabu na fedha ambavyo mfalme Nebukadneza alikuwa amevichukua kutoka katika hekalu huko Yerusalemu na kuviweka katika hekalu la Babuloni. Vyombo hivyo Koreshi aliviondoa hekaluni Babuloni na kumkabidhi Sheshbaza ambaye alikuwa amemteua awe mtawala wa Yuda; alimwamuru achukue vyombo hivyo na kuvirudisha katika hekalu la Yerusalemu, na kuijenga upya nyumba ya Mungu mahali pake. Kisha Sheshbaza alikuja na kuweka msingi wa nyumba ya Mungu mjini Yerusalemu, na tangu wakati huo ujenzi umekuwa ukiendelea mpaka sasa, lakini bado haijamalizika.’ Basi, ukipenda ewe mfalme, amuru uchunguzi ufanywe katika kumbukumbu za kifalme mjini Babuloni kama mfalme Koreshi alitoa amri nyumba hii ya Mungu ijengwe upya mjini Yerusalemu. Kisha, tunakuomba utujulishe maoni yako kuhusu jambo hili.”

Shirikisha
Soma Ezra 5

Ezra 5:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi manabii, Hagai nabii, na Zekaria mwana wa Ido, wakawafanyia unabii Wayahudi waliokuwako Yerusalemu na Yuda; waliwafanyia unabii kwa jina la Mungu wa Israeli. Ndipo akaondoka Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na Yoshua, mwana wa Yosadaki, wakaanza kuijenga nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu; na pamoja nao walikuwa manabii wa Mungu, wakiwasaidia. Wakati ule ule Tatenai, Mkuu wa mkoa wa ng'ambo ya Mto, na Shethar-Bozenai, na wenzao, wakawajia, wakawaambia, Ni nani aliyewapa amri kuijenga nyumba hii, na kuumaliza ukuta huu? Ndipo wakawauliza hivi, Majina ya watu wanaofanya ujenzi huu ni gani? Lakini jicho la Mungu lilikuwa likiwaelekea wazee wa Wayahudi, hao wasiwazuie hadi habari ile imfikie Dario, ndipo jawabu itakapopatikana kwa waraka. Hii ndiyo nakala ya waraka ambao; Tatenai, Mkuu wa mkoa wa ng'ambo ya Mto, na Shethar-Bozenai, na wenzake wa Kiajemi, waliokuwako huko ng'ambo ya Mto; walimtumia mfalme Dario. Walimtumia ripoti; na maneno haya yakaandikwa ndani yake; Kwa Dario, mfalme Salamu sana. Na ajue mfalme ya kuwa sisi tuliingia nchi ya Yuda, tukafika kunako nyumba ya Mungu mkuu, iliyojengwa kwa mawe makubwa, na miti imetiwa katika kuta zake, na kazi hii inaendelea kwa bidii, na kusitawi katika mikono yao. Ndipo tukawauliza wale wazee, tukawaambia hivi, Ni nani aliyewapa amri kuijenga nyumba hii, na kuumaliza ukuta huu? Tukawauliza pia majina yao, ili kukuhakikishia, tupate kuandika majina ya watu waliokuwa wakubwa wao. Wakatujibu hivi, wakasema, Sisi tu watumishi wa Mungu wa mbingu na nchi, nasi tunaijenga nyumba iliyojengwa zamani sana, yapata miaka mingi, ambayo mfalme mkuu wa Israeli aliijenga na kuimaliza. Lakini hapo baba zetu walipomkasirisha Mungu wa mbingu na nchi, hata akaghadhibika, akawatia katika mkono wa Nebukadneza, mfalme wa Babeli, Mkaldayo, naye ndiye aliyeiharibu nyumba hii, akawachukua watu mateka mpaka Babeli. Lakini katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Babeli, Koreshi, mfalme, alitoa amri ijengwe tena nyumba ya Mungu. Na vyombo vya dhahabu na fedha, vya nyumba ya Mungu, alivyovitoa Nebukadneza katika hekalu lililokuwako Yerusalemu, na kuviingiza katika hekalu la Babeli, vyombo hivyo mfalme Koreshi alivitoa katika hekalu la Babeli, akakabidhiwa mtu, jina lake Sheshbaza, ambaye alikuwa amemfanya mtawala; naye akamwambia, Chukua vyombo hivi, uende, ukavitie katika hekalu lililoko Yerusalemu, na nyumba ya Mungu na ijengwe mahali pake. Ndipo yule Sheshbaza alipokuja, akaupiga msingi wa nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu; na tangu wakati ule hadi leo imekuwa ikijengwa, wala bado haijamalizika. Basi, sasa, mfalme akiona vema, watu na wachunguze katika nyumba ya hazina ya mfalme, iliyoko huko Babeli, kama ni kweli ya kuwa mfalme Koreshi alitoa amri kuijenga nyumba hiyo ya Mungu katika Yerusalemu, na mfalme akatutumie habari ya mapenzi yake kuhusu jambo hili.

Shirikisha
Soma Ezra 5