Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezra 4:1-24

Ezra 4:1-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi adui za Yuda na Benyamini, waliposikia ya kuwa wana wa uhamisho wanamjengea BWANA, Mungu wa Israeli, hekalu, wakamkaribia Zerubabeli, na wakuu wa mbari za mababa, wakawaambia, Na tujenge sisi nasi pamoja nanyi; kwa maana tunamtafuta Mungu wenu kama ninyi, nasi twamtolea dhabihu tangu zamani za Esar-hadoni, mfalme wa Ashuru, aliyetupandisha mpaka hapa. Lakini Zerubabeli, na Yoshua, na wakuu wengine wa mbari za mababa katika Israeli, wakawaambia, Ninyi haiwahusu kushirikiana nasi katika kumjengea Mungu wetu nyumba; bali sisi wenyewe peke yetu tutamjengea BWANA, Mungu wa Israeli, nyumba, kama mfalme Koreshi, mfalme wa Uajemi, alivyotuamuru. Ndipo watu wa nchi wakaidhoofisha mikono ya watu wa Yuda, wakawasumbua, walipokuwa wakijenga. Wakawaajiri washauri juu yao, ili kuwapinga kusudi lao, siku zote za Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata wakati wa kutawala kwake Dario, mfalme wa Uajemi. Tena, wakati wa kutawala kwake Ahasuero, mwanzo wa kutawala kwake, watu wakaandika mashitaka juu ya wenyeji wa Yuda na Yerusalemu. Na tena, katika siku za Artashasta, Mithredathi, na Tabeeli na mabaki ya wenziwe, wakimwandikia Artashasta, mfalme wa Uajemi, salamu za heri; na mwandiko wa waraka huo, ukaandikwa kwa herufi za Kiaramu, na kunenwa kwa lugha ya Kiaramu. Nao Rehumu, Bwana shauri, na Shimshai, mwandishi, wakaandika waraka juu ya Yerusalemu kwa Artashasta, mfalme, kama hivi; Rehumu, Bwana shauri, na Shimshai, mwandishi, na mabaki ya wenzao, makadhi wa Kiajemi na madiwani wa Kiajemi; na Waarkewi, Wababeli, Washushani, yaani, Waelami; na mabaki ya mataifa, ambao Asur-bani-pali mkuu, mwenye heshima, aliwavusha, na kuwakalisha katika mji wa Samaria, na mahali penginepo, ng’ambo ya Mto; wakadhalika. Hii ndiyo nakili ya waraka waliyompelekea mfalme Artashasta; Watumishi wako, watu walio ng’ambo ya Mto; wakadhalika. Ijulikane kwa mfalme ya kuwa Wayahudi, waliokwea kutoka kwako, wamefika kwetu Yerusalemu; nao wanaujenga ule mji mwasi, mbaya; wamemaliza kuta zake, na kuitengeneza misingi yake. Basi, ijulikane kwa mfalme, ya kuwa mji huu ukijengwa, na kuta zake zikimalizika, hawatatoa kodi, wala ada, wala ushuru, na mwisho wake wafalme watapata hasara. Na sisi, kwa kuwa tunakula chumvi ya nyumba ya mfalme, wala si wajibu wetu kumwona mfalme akivunjiwa heshima, basi tumetuma watu na kumwarifu mfalme. Ili habari zitafutwe katika kitabu cha tarehe za baba zako; ndivyo utakavyopata kujua kwa kitabu cha tarehe ya kuwa mji huo ni mji mwasi, wenye kuwadhuru wafalme, na maliwali, na ya kuwa wenyeji wake wamefanya fitina katika mji huo zamani; ndiyo sababu mji huo ukaangamizwa. Twamwarifu mfalme ya kuwa mji huo ukijengwa, na kuta zake zikimalizika, hutakuwa na sehemu ya nchi ng’ambo ya Mto. Ndipo mfalme akapeleka majibu; Kwa Rehumu, Bwana shauri, na Shimshai, mwandishi, na wenzao wengine waliokaa katika Samaria, na penginepo ng’ambo ya Mto, Salamu; wakadhalika. Ule waraka mlionipelekea umesomwa mbele yangu, nami nikaelewa na maana yake. Nikatoa amri, na watu wametafuta habari; ikaonekana ya kuwa mji huu zamani umefanya fitina juu ya wafalme, na ya kuwa uasi na fitina zimefanyika ndani yake. Tena walikuwako wafalme wakuu juu ya Yerusalemu, waliotawala nchi yote iliyo ng’ambo ya Mto; wakapewa kodi, na ada, na ushuru. Sasa toeni amri kuwakomesha watu hawa kazi yao, mji huu usijengwe, hata mimi nitakapotoa amri. Tena jihadharini, msilegee katika jambo hili; kwa nini madhara yazidi, na wafalme wapate hasara? Hata nakala ya waraka huo wa mfalme Artashasta uliposomwa mbele ya Rehumu, Bwana shauri, na Shimshai, mwandishi, na wenzao, wakaenda Yerusalemu upesi, kwa Wayahudi, wakawakomesha kwa nguvu na kwa kuwashurutisha. Hivyo kazi ya nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu ikakoma; nayo ikakoma hata mwaka wa pili wa kutawala kwake Dario, mfalme wa Uajemi.

Shirikisha
Soma Ezra 4

Ezra 4:1-24 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha maadui wa watu wa Yuda na Benyamini waliposikia kwamba watu waliorudi kutoka uhamishoni wanalijenga upya hekalu la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, walimwendea Zerubabeli na viongozi wa koo, na kumwambia, “Tafadhali tushirikiane katika ujenzi wa hekalu. Sisi kama nyinyi tunamwabudu Mungu wenu, na tumekuwa tukimtolea tambiko tangu zamani za Esar-hadoni, mfalme wa Ashuru aliyetuleta hapa.” Lakini Zerubabeli, Yeshua na viongozi wengine wa koo za Israeli wakawaambia, “Sisi hatuhitaji msaada wowote kutoka kwenu ili kuijenga nyumba ya Mungu wetu. Sisi wenyewe tutamjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kama mfalme Koreshi wa Persia alivyotuamuru.” Hapo, watu waliokuwa wanaishi mahali hapo wakaanza kuwavunja moyo na kuwatisha Wayahudi ili wasiendelee kama walivyokusudia. Tena waliwahonga maofisa wa serikali ya Persia wawapinge Wayahudi. Waliendelea kufanya hivyo muda wote wa utawala wa Koreshi, mpaka wakati wa utawala wa Dario. Mwanzoni mwa utawala wa mfalme Ahasuero, maadui wa watu waliokaa Yuda na Yerusalemu waliandika mashtaka dhidi yao. Tena wakati wa utawala wa Artashasta, mfalme wa Persia, Bishlamu, Mithredathi, Tabeeli na rafiki zao, walimwandikia barua mfalme Artashasta. Barua hiyo iliandikwa kwa herufi za Kiaramu na kutafsiriwa. Pia mtawala Rehumu na Shimshai, katibu wa mkoa, walimwandikia Artashasta barua ifuatayo dhidi ya Yerusalemu: “Kutoka kwa mtawala Rehumu na Shimshai, katibu wa mkoa pamoja na wenzetu, na mahakimu, maofisa wote ambao hapo awali walitoka Ereki, Babuloni na Susa katika nchi ya Elamu, pamoja na watu wa mataifa mengine ambao Asur-banipali, mtu mkuu na mwenye nguvu aliwahamisha na kuwaweka katika mji wa Samaria na mahali pengine katika mkoa wa magharibi ya Eufrate.” Barua yenyewe ilikuwa hivi: “Kwa mfalme Artashasta: Sisi watumishi wako katika mkoa wa magharibi ya Eufrate, tunakutumia salamu. Tungependa ufahamu, ewe mfalme, kwamba Wayahudi waliokuja hapa kutoka maeneo mengine ya ufalme wako wamekwenda Yerusalemu na wanaujenga upya mji huo mwasi na mwovu. Wanamalizia kujenga kuta zake na kutengeneza msingi. Tungependa ufahamu, ewe mfalme, kuwa mji huu ukijengwa upya na kuta zake zikimalizika, watu hawatalipa kodi, ushuru wala ada, na hazina yako itapungua. Sasa, kwa kuwa ni wajibu wetu, ee mfalme, hatungependa kuona ukivunjiwa heshima, ndiyo maana tumeona ni vizuri tukuarifu ili ufanye uchunguzi katika kumbukumbu za babu zako. Humo utagundua kwamba tangu zamani, mji huu ulikuwa mwasi na umewasumbua sana wafalme na watawala wa mikoa, na kuwa tangu zamani watu wake ni wachochezi sana; ndio sababu mji huo uliangamizwa. Kwa hiyo tunakujulisha kwamba ikiwa mji huu utajengwa upya na kuta zake zikimalizika, hutaweza kuutawala mkoa wa magharibi ya Eufrate.” Kisha mfalme akapeleka jibu lifuatalo: “Kwa mtawala Rehumu, kwa Shishai, katibu wa mkoa, pamoja na wenzenu wote wanaoishi Samaria na mahali penginepo katika mkoa wa magharibi ya Eufrate. “Barua mliyonitumia imetafsiriwa na kusomwa mbele yangu. Nimetoa amri uchunguzi ufanywe na imegunduliwa kuwa ni kweli kwamba tangu zamani mji huu wa Yerusalemu umekuwa ukiwapinga wafalme na kwamba watu wake wamekuwa waasi na wachochezi wakubwa. Wafalme wenye nguvu wamepata kuutawala mji huo pamoja na mkoa wa magharibi ya Eufrate wakitoza kodi, ushuru na ada. Kwa hiyo, toeni amri watu hao waache kuujenga upya mji huo hadi hapo nitakapotoa maagizo mengine. Tena, angalieni sana msichelewe kufanya hivyo, nisije nikapata hasara.” Mara tu waliposomewa barua hii kutoka kwa Artashasta, Rehumu, katibu Shimshai na wenzao waliharakisha kwenda Yerusalemu na kuwalazimisha kwa nguvu Wayahudi waache kuujenga mji. Kazi ya kuijenga upya nyumba ya Mungu mjini Yerusalemu ilisimama, na hali hiyo iliendelea mpaka mwaka wa pili wa utawala wa Dario, mfalme wa Persia.

Shirikisha
Soma Ezra 4

Ezra 4:1-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi adui za Yuda na Benyamini, waliposikia ya kuwa wana wa uhamisho wanamjengea BWANA, Mungu wa Israeli, hekalu, wakamkaribia Zerubabeli, na wakuu wa koo za mababa, wakawaambia, Na tujenge sisi nasi pamoja nanyi; kwa maana tunamtafuta Mungu wenu kama ninyi, nasi tumemtolea dhabihu tangu zamani za Esar-hadoni, mfalme wa Ashuru, aliyetupandisha mpaka hapa. Lakini Zerubabeli, na Yoshua, na wakuu wengine wa koo za mababa katika Israeli, wakawaambia, Ninyi haiwahusu kushirikiana nasi katika kumjengea Mungu wetu nyumba; bali sisi wenyewe peke yetu tutamjengea BWANA, Mungu wa Israeli, nyumba, kama mfalme Koreshi, mfalme wa Uajemi, alivyotuamuru. Ndipo wakazi wa nchi wakawavunja moyo watu wa Yuda, wakawafanya wawe na hofu ya kujenga. Wakawahonga maofisa, ili kuwakatisha tamaa katika mpango wao, siku zote za Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata wakati wa kutawala kwake Dario, mfalme wa Uajemi. Tena, wakati wa kutawala kwake Ahasuero, mwanzo wa kutawala kwake, watu wakaandika mashitaka juu ya wenyeji wa Yuda na Yerusalemu. Na tena, katika siku za Artashasta, Mithredathi, na Tabeeli na wenzao wengine, wakimwandikia Artashasta, mfalme wa Uajemi, salamu za heri; na mwandiko wa waraka huo, ukaandikwa kwa herufi za Kiaramu, na kusomwa kwa lugha ya Kiaramu. Nao Rehumu, mtawala, na Shimshai, mwandishi, wakaandika waraka juu ya Yerusalemu kwa Artashasta, mfalme, kama hivi; Rehumu, mtawala, na Shimshai, mwandishi, na wenzao wengine, makadhi wa Kiajemi na madiwani wa Kiajemi; na Waarkewi, Wababeli, Washushani, yaani, Waelami; na watu wengine wa mataifa, ambao Asur-bani-pali mkuu, mwenye heshima, aliwavusha, na kuwakalisha katika mji wa Samaria, na mahali penginepo, ng'ambo ya Mto; na kadhalika. Hii ndiyo nakala ya waraka waliyompelekea mfalme Artashasta; Watumishi wako, watu walio ng'ambo ya Mto; wakadhalika. Ijulikane kwa mfalme ya kuwa Wayahudi, waliokwea kutoka kwako, wamefika kwetu Yerusalemu; nao wanaujenga ule mji mwasi, mbaya; wamemaliza kuta zake, na kuitengeneza misingi yake. Basi, ijulikane kwa mfalme, ya kuwa mji huu ukijengwa, na kuta zake zikimalizika, hawatatoa kodi, wala ada, wala ushuru, na mwisho wake wafalme watapata hasara. Na sisi, kwa kuwa tunakula chumvi ya nyumba ya mfalme, wala si wajibu wetu kumwona mfalme akivunjiwa heshima, basi tumetuma watu na kumwarifu mfalme. Ili habari zichunguzwe katika kitabu cha kumbukumbu za baba zako; ndivyo utakavyopata kujua kwa kitabu cha kumbukumbu ya kuwa mji huo ni mji mwasi, wenye kuwadhuru wafalme, na wakuu wa mikoa, na ya kuwa wenyeji wake wamefanya fitina katika mji huo zamani; ndiyo sababu mji huo ukaangamizwa. Tunamwarifu mfalme ya kuwa mji huo ukijengwa, na kuta zake zikimalizika, basi utakuwa huna milki katika sehemu ya nchi iliyo ng'ambo ya mto. Ndipo mfalme akatuma majibu; Kwa Rehumu, mtawala, na Shimshai, mwandishi, na wenzao wengine waliokaa katika Samaria, na penginepo ng'ambo ya Mto, Salamu; na kadhalika. Ule barua mliotutumia umesomwa wazi mbele yangu, nami nikaielewa. Nikatoa amri, na watu wametafuta habari; ikaonekana ya kuwa mji huu zamani umewaasi wafalme, na ya kuwa uasi na fitina zimefanyika ndani yake. Tena walikuwako wafalme wakuu juu ya Yerusalemu, waliotawala nchi yote iliyo ng'ambo ya Mto; wakapewa kodi, na ada, na ushuru. Sasa toeni amri kuwakomesha watu hawa kazi yao, mji huu usijengwe, hadi nitakapotoa amri. Tena jihadharini, msilegee katika jambo hili; kwa nini madhara yazidi, na wafalme wapate hasara? Kisha nakala ya barua hiyo ya mfalme Artashasta iliposomwa mbele ya Rehumu, mtawala na Shimshai, mwandishi, na wenzao, wakaenda Yerusalemu upesi, kwa Wayahudi, wakawakomesha kwa nguvu na kwa kuwashurutisha. Hivyo kazi ya nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu ikakoma; nayo ikakoma hadi mwaka wa pili wa kutawala kwake Dario, mfalme wa Uajemi.

Shirikisha
Soma Ezra 4

Ezra 4:1-24 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Adui za Yuda na Benyamini waliposikia kwamba watu waliorudi kutoka uhamishoni wanajenga Hekalu kwa ajili ya BWANA, Mungu wa Israeli, wakamjia Zerubabeli na viongozi wa jamaa, nao wakasema, “Turuhusuni tuwasaidie kujenga, kwa sababu sisi tunamtafuta Mungu wenu kama ninyi na tumekuwa tukimtolea dhabihu tangu wakati wa Esar-Hadoni mfalme wa Ashuru, aliyetuleta hapa.” Lakini Zerubabeli, Yeshua na viongozi wengine wa jamaa ya Israeli wakawajibu, “Ninyi hamna sehemu nasi katika kujenga Hekalu la Mungu wetu. Sisi peke yetu tutajenga Hekalu kwa ajili ya BWANA, Mungu wa Israeli, kama Mfalme Koreshi, mfalme wa Uajemi alivyotuagiza.” Ndipo watu waliowazunguka wakajipanga kuwakatisha tamaa watu wa Yuda na kuwafanya waogope walipokuwa wakiendelea na ujenzi. Wakaajiri washauri kuwapinga katika kazi yao, nao wakaipinga mipango yao wakati wote wa utawala wa Koreshi mfalme wa Uajemi hadi wakati wa utawala wa Dario mfalme wa Uajemi. Mnamo mwanzo wa utawala wa Ahasuero, hao adui waliandika mashtaka dhidi ya watu wa Yuda na Yerusalemu. Pia katika siku za utawala wa Artashasta mfalme wa Uajemi, Bishlamu, Mithredathi, Tabeeli pamoja na wenzao waliandika barua kwa Artashasta. Barua hiyo iliandikwa kwa mwandiko wa Kiaramu na katika lugha ya Kiaramu. Rehumu afisa msimamizi na mwandishi Shimshai waliandika barua kwa Mfalme Artashasta dhidi ya watu wa Yerusalemu kama ifuatavyo: Rehumu afisa msimamizi na mwandishi Shimshai, pamoja na wenzao, yaani mahakimu na maafisa walio juu ya watu kuanzia Tripoli, Uajemi, Ereki na Babeli, Waelami wa Shushani, na watu wengine ambao mheshimiwa Asur-Banipali aliwahamisha na kuwakalisha katika mji wa Samaria na mahali pengine Ngʼambo ya Mto Frati. (Hii ndiyo nakala ya barua waliyompelekea.) Kwa Mfalme Artashasta, Kutoka kwa watumishi wako, watu wa Ngʼambo ya Mto Frati: Yapasa Mfalme ajue kuwa Wayahudi waliopanda kuja kwetu kutoka kwenu, wamekwenda Yerusalemu nao wanaujenga upya ule mji wa uasi na uovu. Wanajenga kuta upya na kukarabati misingi yake. Zaidi ya hayo, mfalme yampasa ajue kwamba kama mji huu ukijengwa na kuta zake zikafanywa upya, hakutakuwa na ulipaji wa kodi wala ada au ushuru, hivyo hazina za mfalme zitaathirika. Sisi sasa kwa kuwa tunawajibika kwa jumba la kifalme na kwamba siyo sawasawa kwetu kuona mfalme akidharauliwa, basi tunatuma ujumbe huu kumtaarifu mfalme, ili kwamba ufanyike uchunguzi kwenye kumbukumbu ya maandishi ya waliokutangulia. Katika kumbukumbu hizi utagundua kwamba mji huu ni wa maasi, unaowataabisha wafalme na majimbo, ni mahali pa maasi tangu zamani. Ndiyo maana mji huu uliharibiwa. Tunamjulisha mfalme kwamba kama mji huu ukijengwa na kuta zake zikifanywa upya, hutabakiwa na chochote Ngʼambo ya Mto Frati. Mfalme alirudisha jibu hili: Kwa Rehumu, afisa msimamizi, mwandishi Shimshai na wenzenu wote wanaoishi katika Samaria na penginepo Ngʼambo ya Mto Frati: Salamu. Barua mliyotutumia imesomwa na kutafsiriwa mbele yangu. Nilitoa amri na uchunguzi ukafanyika na imegundulika kwamba mji huu una historia ndefu ya maasi dhidi ya wafalme na pamekuwa mahali pa maasi na uchochezi. Yerusalemu umepata kuwa na wafalme wenye nguvu wakitawala nchi yote iliyo Ngʼambo ya Mto Frati, wakitoza kodi, ada na ushuru huko. Kwa hiyo toeni amri kwa watu hawa wasimamishe ujenzi, ili kwamba mji huu usiendelee kujengwa hadi nitakapoagiza. Mwe waangalifu msipuuze jambo hili. Kwa nini kuruhusu tishio hili kuendelea na kusababisha hasara kwa ufalme? Mara waliposomewa nakala ya barua ya Mfalme Artashasta, Rehumu na Shimshai aliyekuwa mwandishi na wenzao, walikwenda mara moja kwa Wayahudi huko Yerusalemu na kuwalazimisha kwa nguvu kusimamisha ujenzi. Hivyo kazi ya ujenzi wa nyumba ya Mungu huko Yerusalemu ikasimamishwa kabisa hadi mwaka wa pili wa utawala wa Dario mfalme wa Uajemi.

Shirikisha
Soma Ezra 4