Ezra 3:7-13
Ezra 3:7-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Watu walitoa fedha za kuwalipa maseremala na waashi, walitoa pia chakula, vinywaji na mafuta, ili vipelekwe katika miji ya Tiro na Sidoni kupata miti ya mierezi kutoka Lebanoni. Miti hiyo ililetwa kwa njia ya bahari hadi Yopa. Haya yote yalifanyika kwa msaada wa mfalme Koreshi wa Persia. Basi, watu walianza kazi mnamo mwezi wa pili wa mwaka wa pili baada ya kufikia nyumba ya Mungu mjini Yerusalemu. Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, Yeshua mwana wa Yosadaki, ndugu zao wengine, makuhani, Walawi na watu wengine wote waliorudi Yerusalemu kutoka uhamishoni, walijiunga nao katika kazi hiyo. Walawi wote waliokuwa na umri wa miaka ishirini au zaidi, waliteuliwa ili kusimamia kazi ya kuijenga upya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Yeshua, wanawe na jamaa yake, pamoja na Kadmieli na wanawe, (wa ukoo wa Yuda) walishirikiana kusimamia ujenzi wa nyumba ya Mungu. Walisaidiwa na wazawa wa Henadadi na ndugu zao Walawi. Wajenzi walipoanza kuweka msingi wa hekalu la Mwenyezi-Mungu, makuhani wakiwa wamevalia mavazi yao rasmi, walisimama mahali pao na tarumbeta mikononi, nao Walawi wa ukoo wa Asafu wakisimama na matoazi yao; basi, walimtukuza Mwenyezi-Mungu kufuatana na maagizo ya mfalme Daudi wa Israeli. Waliimba kwa kupokezana, wakimsifu na kumtukuza Mwenyezi-Mungu: “Kwa kuwa yu mwema, fadhili zake kwa Israeli zadumu milele.” Watu wote walipaza sauti kwa nguvu zao zote, wakamsifu Mwenyezi-Mungu kwa sababu ya kuanza kujengwa msingi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Wengi wa makuhani, Walawi, na viongozi wa koo waliokuwa wazee na ambao walikuwa wameiona nyumba ya kwanza, walilia kwa sauti kubwa walipouona msingi wa nyumba hii mpya unawekwa, ingawa watu wengine wengi walipaza sauti kwa furaha. Watu hawakuweza kutofautisha kati ya sauti za furaha na za kilio kwa sababu zilikuwa nyingi na zilisikika mbali sana.
Ezra 3:7-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tena waliwapa waashi na maseremala fedha; wakawapa watu wa Sidoni, na watu wa Tiro, chakula, na vinywaji, na mafuta, ili walete mierezi kutoka Lebanoni mpaka Yafa kwa njia ya bahari, kwa kadiri walivyopewa ruhusa na Koreshi, mfalme wa Uajemi. Katika mwaka wa pili wa kufika kwao katika nyumba ya Mungu, huko Yerusalemu, mwezi wa pili, Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na Yoshua, mwana wa Yosadaki, na ndugu zao wengine, makuhani na Walawi, na watu wote, waliotoka katika uhamisho na kufika Yerusalemu, wakaanza; nao wakawaweka Walawi, hao wenye miaka ishirini na waliozidi, ili kuisimamia kazi ya nyumba ya BWANA. Ndipo wakasimama Yeshua, na wanawe na ndugu zake, Kadmieli, na wanawe, wana wa Hodavia, pamoja, ili kuwasimamia hao wafanyao kazi katika nyumba ya Mungu; wana wa Henadadi, pamoja na wana wao, na ndugu zao, Walawi. Hata wajenzi walipouweka msingi wa hekalu la BWANA, wakawaweka makuhani, wamevaa mavazi yao, wenye baragumu, na Walawi, wana wa Asafu, wenye matoazi, ili wamhimidi BWANA, kama alivyoagiza Daudi, mfalme wa Israeli. Wakaimbiana, wakimhimidi BWANA, na kumshukuru, wakasema, Kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake kwa Israeli ni za milele. Kisha watu wote wakapaza sauti zao, na kupiga kelele, walipomhimidi BWANA, kwa sababu msingi wa nyumba ya BWANA umekwisha kuwekwa. Bali makuhani wengi, na Walawi, na wakuu wa koo za mababa, waliokuwa wameiona nyumba ya kwanza, wakati msingi wa nyumba hii ulipowekwa mbele ya macho yao, walilia kwa sauti kuu; na watu wengi walipiga kelele za furaha; hata watu wasiweze kupambanua kelele za furaha, na kelele za vilio vya watu; maana watu walipiga kelele kwa sauti kuu, na kelele zao zikasikika mbali sana.
Ezra 3:7-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tena waliwapa waashi na maseremala fedha; wakawapa watu wa Sidoni, na watu wa Tiro, chakula, na vinywaji, na mafuta, ili walete mierezi kutoka Lebanoni mpaka Yafa kwa njia ya bahari, kwa kadiri walivyopewa ruhusa na Koreshi, mfalme wa Uajemi. Hata mwaka wa pili wa kufika kwao nyumbani kwa Mungu, huko Yerusalemu, mwezi wa pili, Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na Yoshua, mwana wa Yosadaki, na ndugu zao wengine, makuhani na Walawi, na watu wote, waliotoka katika uhamisho na kufika Yerusalemu, wakaanza; nao wakawaweka Walawi, hao wenye miaka ishirini na waliozidi, ili kuisimamia kazi ya nyumba ya BWANA. Ndipo wakasimama Yeshua, na wanawe na ndugu zake, Kadmieli, na wanawe, wana wa Hodavia, pamoja, ili kuwasimamia hao wafanyao kazi katika nyumba ya Mungu; wana wa Henadadi, pamoja na wana wao, na ndugu zao, Walawi. Hata wajenzi walipouweka msingi wa hekalu la BWANA, wakawaweka makuhani, wamevaa mavazi yao, wenye baragumu, na Walawi, wana wa Asafu, wenye matoazi, ili wamhimidi BWANA, kama alivyoagiza Daudi, mfalme wa Israeli. Wakaimbiana, wakimhimidi BWANA, na kumshukuru, wakasema, Kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake kwa Israeli ni za milele. Kisha watu wote wakapaza sauti zao, na kupiga kelele, walipomhimidi BWANA, kwa sababu msingi wa nyumba ya BWANA umekwisha kuwekwa. Bali makuhani wengi, na Walawi, na wakuu wa mbari za mababa, waliokuwa wameiona nyumba ya kwanza, wakati msingi wa nyumba hii ulipowekwa mbele ya macho yao, walilia kwa sauti kuu; na watu wengi walipiga kelele za furaha; hata watu wasiweze kupambanua kelele za furaha, na kelele za vilio vya watu; maana watu walipiga kelele kwa sauti kuu, na kelele zao zikasikilikana mbali sana.
Ezra 3:7-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha watu wakawapa mafundi wa uashi na useremala fedha, wakawapa watu wa Sidoni na Tiro vyakula, vinywaji na mafuta ili waweze kuleta magogo ya mierezi kwa njia ya bahari kutoka Lebanoni hadi Yafa, kama alivyoagiza Koreshi mfalme wa Uajemi. Katika mwezi wa pili wa mwaka wa pili baada ya Waisraeli kufika kwenye nyumba ya Mungu huko Yerusalemu, Zerubabeli mwana wa Shealtieli, Yeshua mwana wa Yosadaki na ndugu zao wengine (makuhani, Walawi na wote waliorejea Yerusalemu kutoka uhamishoni) walianza kazi, wakiteua Walawi wenye umri kuanzia miaka ishirini au zaidi kusimamia ujenzi wa nyumba ya BWANA. Yeshua na wanawe, pamoja na ndugu zake, Kadmieli na wanawe (wazao wa Hodavia), wana wa Henadadi na wana wao na ndugu zao, Walawi wote walijiunga pamoja kusimamia wale waliofanya kazi katika nyumba ya Mungu. Wajenzi walipoweka msingi wa Hekalu la BWANA, makuhani wakiwa wamevalia mavazi yao wakiwa na tarumbeta na Walawi (wana wa Asafu) wakiwa na matoazi, walishika nafasi zao za kumtukuza BWANA, kama ilivyoagizwa na Daudi mfalme wa Israeli. Waliimba nyimbo za sifa na za shukrani kwa BWANA hivi: “Yeye ni mwema; upendo wake kwa Israeli wadumu milele.” Watu wote wakapaza sauti kubwa za sifa kwa BWANA, kwa sababu msingi wa nyumba ya BWANA ulikuwa umewekwa. Lakini wengi wa makuhani wazee, Walawi na viongozi wa jamaa waliokuwa wameona Hekalu la mwanzoni, walilia kwa sauti walipoona msingi wa Hekalu hili ukiwekwa, huku wengine wengi wakipiga kelele kwa furaha. Hakuna mtu ambaye angeweza kutofautisha sauti hizo za furaha na za kilio, kwa sababu watu walipiga kelele sana. Nayo hiyo sauti ikasikika mbali.