Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezra 3:1-13

Ezra 3:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Hata ulipowadia mwezi wa saba, na wana wa Israeli walipokuwa katika miji yao, watu wakakusanyika pamoja huko Yerusalemu. Ndipo akasimama Yoshua, mwana wa Yosadaki, na ndugu zake makuhani, na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na ndugu zake, nao wakaijenga madhabahu ya Mungu wa Israeli, ili kutoa sadaka za kuteketezwa juu yake, kama ilivyoandikwa katika Torati ya Musa, mtu wa Mungu. Wakaiweka madhabahu juu ya msingi wake; maana hofu imewashika kwa sababu ya watu wa nchi; wakamtolea BWANA sadaka za kuteketezwa juu yake, sadaka za kuteketezwa za asubuhi na jioni. Wakaishika sikukuu ya vibanda, kama ilivyoandikwa, wakatoa sadaka za kuteketezwa za kila siku kwa hesabu yake, kama ilivyoagizwa, kama ilivyopasa kila siku; na baadaye sadaka ya kuteketezwa ya daima, na za mwandamo wa mwezi, na za sikukuu za BWANA, zilizoamriwa na kuwekwa wakfu, na za kila mtu aliyemtolea BWANA sadaka kwa hiari yake. Tangu siku ya kwanza ya mwezi wa saba walianza kumtolea BWANA sadaka za kuteketezwa, lakini msingi wa hekalu la BWANA ulikuwa haujawekwa bado. Tena waliwapa waashi na maseremala fedha; wakawapa watu wa Sidoni, na watu wa Tiro, chakula, na vinywaji, na mafuta, ili walete mierezi kutoka Lebanoni mpaka Yafa kwa njia ya bahari, kwa kadiri walivyopewa ruhusa na Koreshi, mfalme wa Uajemi. Katika mwaka wa pili wa kufika kwao katika nyumba ya Mungu, huko Yerusalemu, mwezi wa pili, Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na Yoshua, mwana wa Yosadaki, na ndugu zao wengine, makuhani na Walawi, na watu wote, waliotoka katika uhamisho na kufika Yerusalemu, wakaanza; nao wakawaweka Walawi, hao wenye miaka ishirini na waliozidi, ili kuisimamia kazi ya nyumba ya BWANA. Ndipo wakasimama Yeshua, na wanawe na ndugu zake, Kadmieli, na wanawe, wana wa Hodavia, pamoja, ili kuwasimamia hao wafanyao kazi katika nyumba ya Mungu; wana wa Henadadi, pamoja na wana wao, na ndugu zao, Walawi. Hata wajenzi walipouweka msingi wa hekalu la BWANA, wakawaweka makuhani, wamevaa mavazi yao, wenye baragumu, na Walawi, wana wa Asafu, wenye matoazi, ili wamhimidi BWANA, kama alivyoagiza Daudi, mfalme wa Israeli. Wakaimbiana, wakimhimidi BWANA, na kumshukuru, wakasema, Kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake kwa Israeli ni za milele. Kisha watu wote wakapaza sauti zao, na kupiga kelele, walipomhimidi BWANA, kwa sababu msingi wa nyumba ya BWANA umekwisha kuwekwa. Bali makuhani wengi, na Walawi, na wakuu wa koo za mababa, waliokuwa wameiona nyumba ya kwanza, wakati msingi wa nyumba hii ulipowekwa mbele ya macho yao, walilia kwa sauti kuu; na watu wengi walipiga kelele za furaha; hata watu wasiweze kupambanua kelele za furaha, na kelele za vilio vya watu; maana watu walipiga kelele kwa sauti kuu, na kelele zao zikasikika mbali sana.

Shirikisha
Soma Ezra 3

Ezra 3:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Hata ulipowadia mwezi wa saba, na wana wa Israeli walipokuwa katika miji yao, watu wakakusanyika pamoja huko Yerusalemu kama mtu mmoja. Ndipo akasimama Yoshua, mwana wa Yosadaki, na ndugu zake makuhani, na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na ndugu zake, nao wakaijenga madhabahu ya Mungu wa Israeli, ili kutoa sadaka za kuteketezwa juu yake, kama ilivyoandikwa katika torati ya Musa, mtu wa Mungu. Wakaiweka madhabahu juu ya msingi wake; maana hofu imewashika kwa sababu ya watu wa nchi; wakamtolea BWANA sadaka za kuteketezwa juu yake, sadaka za kuteketezwa za asubuhi na jioni. Wakaishika Sikukuu ya Vibanda, kama ilivyoandikwa, wakatoa sadaka za kuteketezwa za kila siku kwa hesabu yake, kama ilivyoagizwa, kama ilivyopasa kila siku; na baadaye sadaka ya kuteketezwa ya daima, na za mwandamo wa mwezi, na za sikukuu za BWANA, zilizoamriwa na kuwekwa wakfu, na za kila mtu aliyemtolea BWANA sadaka kwa hiari yake. Tangu siku ya kwanza ya mwezi wa saba walianza kumtolea BWANA sadaka za kuteketezwa, lakini msingi wa hekalu la BWANA ulikuwa haujawekwa bado. Tena waliwapa waashi na maseremala fedha; wakawapa watu wa Sidoni, na watu wa Tiro, chakula, na vinywaji, na mafuta, ili walete mierezi kutoka Lebanoni mpaka Yafa kwa njia ya bahari, kwa kadiri walivyopewa ruhusa na Koreshi, mfalme wa Uajemi. Hata mwaka wa pili wa kufika kwao nyumbani kwa Mungu, huko Yerusalemu, mwezi wa pili, Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na Yoshua, mwana wa Yosadaki, na ndugu zao wengine, makuhani na Walawi, na watu wote, waliotoka katika uhamisho na kufika Yerusalemu, wakaanza; nao wakawaweka Walawi, hao wenye miaka ishirini na waliozidi, ili kuisimamia kazi ya nyumba ya BWANA. Ndipo wakasimama Yeshua, na wanawe na ndugu zake, Kadmieli, na wanawe, wana wa Hodavia, pamoja, ili kuwasimamia hao wafanyao kazi katika nyumba ya Mungu; wana wa Henadadi, pamoja na wana wao, na ndugu zao, Walawi. Hata wajenzi walipouweka msingi wa hekalu la BWANA, wakawaweka makuhani, wamevaa mavazi yao, wenye baragumu, na Walawi, wana wa Asafu, wenye matoazi, ili wamhimidi BWANA, kama alivyoagiza Daudi, mfalme wa Israeli. Wakaimbiana, wakimhimidi BWANA, na kumshukuru, wakasema, Kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake kwa Israeli ni za milele. Kisha watu wote wakapaza sauti zao, na kupiga kelele, walipomhimidi BWANA, kwa sababu msingi wa nyumba ya BWANA umekwisha kuwekwa. Bali makuhani wengi, na Walawi, na wakuu wa mbari za mababa, waliokuwa wameiona nyumba ya kwanza, wakati msingi wa nyumba hii ulipowekwa mbele ya macho yao, walilia kwa sauti kuu; na watu wengi walipiga kelele za furaha; hata watu wasiweze kupambanua kelele za furaha, na kelele za vilio vya watu; maana watu walipiga kelele kwa sauti kuu, na kelele zao zikasikilikana mbali sana.

Shirikisha
Soma Ezra 3

Ezra 3:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

Baadaye mwezi wa saba ulipofika, na watu wa Israeli wakiwa wamekwisha kaa katika miji yao, wote walikusanyika pamoja mjini Yerusalemu. Yeshua, mwana wa Yosadaki, pamoja na makuhani wenzake, na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, pamoja na jamaa zake, waliijenga upya madhabahu ya Mungu wa Israeli, ili waweze kumtolea sadaka za kuteketezwa kama ilivyoandikwa katika sheria ya Mose, mtu wa Mungu. Waliijenga madhabahu hiyo mahali palepale ilipokuwa hapo zamani, kwa kuwa waliwaogopa watu waliokuwa wanaishi katika nchi hiyo. Kisha wakawa wanamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa juu yake kila siku asubuhi na jioni. Waliiadhimisha sikukuu ya vibanda kama ilivyoandikwa katika sheria; kila siku walitoa sadaka za kuteketezwa zilizohitajika kwa ajili ya siku hiyo. Walitoa pia sadaka za kawaida ambazo ziliteketezwa nzima, sadaka zilizotolewa wakati wa sikukuu ya mwezi mpya na katika sikukuu nyingine zote alizoagiza Mwenyezi-Mungu. Pia, walitoa tambiko zote zilizotolewa kwa hiari. Ingawa msingi wa hekalu la Mwenyezi-Mungu ulikuwa bado kuwekwa, watu walianza kutoa sadaka za kuteketezwa tangu siku ya kwanza ya mwezi wa saba. Watu walitoa fedha za kuwalipa maseremala na waashi, walitoa pia chakula, vinywaji na mafuta, ili vipelekwe katika miji ya Tiro na Sidoni kupata miti ya mierezi kutoka Lebanoni. Miti hiyo ililetwa kwa njia ya bahari hadi Yopa. Haya yote yalifanyika kwa msaada wa mfalme Koreshi wa Persia. Basi, watu walianza kazi mnamo mwezi wa pili wa mwaka wa pili baada ya kufikia nyumba ya Mungu mjini Yerusalemu. Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, Yeshua mwana wa Yosadaki, ndugu zao wengine, makuhani, Walawi na watu wengine wote waliorudi Yerusalemu kutoka uhamishoni, walijiunga nao katika kazi hiyo. Walawi wote waliokuwa na umri wa miaka ishirini au zaidi, waliteuliwa ili kusimamia kazi ya kuijenga upya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Yeshua, wanawe na jamaa yake, pamoja na Kadmieli na wanawe, (wa ukoo wa Yuda) walishirikiana kusimamia ujenzi wa nyumba ya Mungu. Walisaidiwa na wazawa wa Henadadi na ndugu zao Walawi. Wajenzi walipoanza kuweka msingi wa hekalu la Mwenyezi-Mungu, makuhani wakiwa wamevalia mavazi yao rasmi, walisimama mahali pao na tarumbeta mikononi, nao Walawi wa ukoo wa Asafu wakisimama na matoazi yao; basi, walimtukuza Mwenyezi-Mungu kufuatana na maagizo ya mfalme Daudi wa Israeli. Waliimba kwa kupokezana, wakimsifu na kumtukuza Mwenyezi-Mungu: “Kwa kuwa yu mwema, fadhili zake kwa Israeli zadumu milele.” Watu wote walipaza sauti kwa nguvu zao zote, wakamsifu Mwenyezi-Mungu kwa sababu ya kuanza kujengwa msingi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Wengi wa makuhani, Walawi, na viongozi wa koo waliokuwa wazee na ambao walikuwa wameiona nyumba ya kwanza, walilia kwa sauti kubwa walipouona msingi wa nyumba hii mpya unawekwa, ingawa watu wengine wengi walipaza sauti kwa furaha. Watu hawakuweza kutofautisha kati ya sauti za furaha na za kilio kwa sababu zilikuwa nyingi na zilisikika mbali sana.

Shirikisha
Soma Ezra 3

Ezra 3:1-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Mwezi wa saba ulipowadia baada ya Waisraeli kukaa katika miji yao, watu wote walikusanyika huko Yerusalemu kama mtu mmoja. Yeshua mwana wa Yosadaki na makuhani wenzake, Zerubabeli mwana wa Shealtieli pamoja na wenzake walianza kujenga madhabahu ya Mungu wa Israeli ili kumtolea dhabihu za sadaka za kuteketezwa kwa moto juu yake, kulingana na ilivyoandikwa katika Sheria ya Mose mtu wa Mungu. Ingawa waliwaogopa watu waliowazunguka, walijenga madhabahu juu ya ule msingi wake, wakamtolea BWANA dhabihu za sadaka za kuteketezwa kwa moto juu yake za asubuhi na za jioni. Kisha kulingana na kile kilichoandikwa, wakaiadhimisha Sikukuu ya Vibanda wakitoa idadi ya sadaka za kuteketezwa kama ilivyohitajika kila siku sawasawa na ilivyoagizwa. Baada ya hayo, walitoa sadaka za kuteketezwa za kawaida, sadaka za Mwezi Mwandamo na dhabihu zote za sikukuu takatifu za BWANA zilizoamriwa, pamoja na zile sadaka za hiari zilizotolewa kwa BWANA. Ingawa bado msingi wa Hekalu la BWANA ulikuwa haujawekwa, watu walianza kutoa sadaka za kuteketezwa kwa moto kwa BWANA tangu siku ya kwanza ya mwezi wa saba. Kisha watu wakawapa mafundi wa uashi na useremala fedha, wakawapa watu wa Sidoni na Tiro vyakula, vinywaji na mafuta ili waweze kuleta magogo ya mierezi kwa njia ya bahari kutoka Lebanoni hadi Yafa, kama alivyoagiza Koreshi mfalme wa Uajemi. Katika mwezi wa pili wa mwaka wa pili baada ya Waisraeli kufika kwenye nyumba ya Mungu huko Yerusalemu, Zerubabeli mwana wa Shealtieli, Yeshua mwana wa Yosadaki na ndugu zao wengine (makuhani, Walawi na wote waliorejea Yerusalemu kutoka uhamishoni) walianza kazi, wakiteua Walawi wenye umri kuanzia miaka ishirini au zaidi kusimamia ujenzi wa nyumba ya BWANA. Yeshua na wanawe, pamoja na ndugu zake, Kadmieli na wanawe (wazao wa Hodavia), wana wa Henadadi na wana wao na ndugu zao, Walawi wote walijiunga pamoja kusimamia wale waliofanya kazi katika nyumba ya Mungu. Wajenzi walipoweka msingi wa Hekalu la BWANA, makuhani wakiwa wamevalia mavazi yao wakiwa na tarumbeta na Walawi (wana wa Asafu) wakiwa na matoazi, walishika nafasi zao za kumtukuza BWANA, kama ilivyoagizwa na Daudi mfalme wa Israeli. Waliimba nyimbo za sifa na za shukrani kwa BWANA hivi: “Yeye ni mwema; upendo wake kwa Israeli wadumu milele.” Watu wote wakapaza sauti kubwa za sifa kwa BWANA, kwa sababu msingi wa nyumba ya BWANA ulikuwa umewekwa. Lakini wengi wa makuhani wazee, Walawi na viongozi wa jamaa waliokuwa wameona Hekalu la mwanzoni, walilia kwa sauti walipoona msingi wa Hekalu hili ukiwekwa, huku wengine wengi wakipiga kelele kwa furaha. Hakuna mtu ambaye angeweza kutofautisha sauti hizo za furaha na za kilio, kwa sababu watu walipiga kelele sana. Nayo hiyo sauti ikasikika mbali.

Shirikisha
Soma Ezra 3