Ezra 10:1-19
Ezra 10:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati Ezra alipokuwa anaomba na kuungama huku analia na kujiangusha kifudifudi mbele ya nyumba ya Mungu, umati mkubwa wa watu wa Israeli, wanaume, wanawake na watoto, walikusanyika karibu naye wakilia kwa uchungu mwingi. Ndipo Shekania, mwana wa Yehieli, wa ukoo wa Elamu, akamwambia Ezra, “Tumekosa uaminifu kwa Mungu kwa kuoa wanawake wa kigeni wa nchi hii, lakini hata hivyo bado kuna tumaini kwa ajili ya Israeli. Kwa hiyo, na tufanye agano na Mungu wetu, tuachane na wanawake hawa pamoja na watoto wao, kwa kufuatana na ushauri wako na wa wengine wanaotii amri za Mungu. Yote yatendeke kwa kufuatana na sheria. Amka uchukue hatua, sisi tutakuunga mkono. Kwa hiyo jipe moyo ufanye hivyo.” Ezra alianza kwa kuwafanya makuhani, viongozi, Walawi na Waisraeli wengine wote waape kwamba watafanya kama ilivyosemwa, nao wakakubali kula kiapo. Kisha, Ezra akaondoka mbele ya nyumba ya Mungu, akaenda nyumbani kwa Yehohanani, mwana wa Eliashibu. Huko, Ezra alilala usiku kucha bila kula wala kunywa maji, kwa huzuni aliyokuwa nayo juu ya ukosefu wa imani ya watu waliotoka uhamishoni. Tangazo lilitolewa kila mahali nchini Yuda na mjini Yerusalemu kwa wote waliotoka uhamishoni kuwa wakusanyike Yerusalemu. Ikiwa mtu yeyote atashindwa kufika katika muda wa siku tatu, kulingana na amri iliyotolewa na viongozi, mali yake yote itachukuliwa, naye binafsi atapigwa marufuku kujiunga na jumuiya ya watu waliorudi kutoka uhamishoni. Katika siku hizo tatu, mnamo siku ya ishirini ya mwezi wa tisa, watu wote walioishi katika Yuda na Benyamini walifika Yerusalemu na kukusanyika katika uwanja wa nyumba ya Mungu. Watu wote walikuwa wakitetemeka kwa sababu ya jambo waliloitiwa na kwa ajili ya mvua nyingi iliyokuwa ikinyesha. Kuhani Ezra alisimama kuzungumza na watu, akawaambia: “Hamkuwa waaminifu kwa kuoa wanawake wa kigeni, na hivyo mmeiongezea Israeli hatia. Sasa, tubuni dhambi zenu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, na kufanya yale yanayompendeza. Jitengeni na wakazi wa nchi hii na kuwaacha wake zenu wa kigeni.” Watu wote walipaza sauti na kujibu kwa pamoja, “Ni sawa! Ni lazima tufanye kama unavyosema.” Lakini wakaongeza kusema, “Watu ni wengi na mvua inanyesha sana. Hatuwezi kuendelea kusimama hapa uwanjani, na hili si jambo ambalo litamalizika kwa siku moja au mbili! Tumefanya kosa kubwa sana kuhusu jambo hili. Afadhali maofisa wetu wabaki Yerusalemu kushughulikia jambo hili kwa niaba ya watu wote. Kisha, kila mmoja ambaye ameoa mwanamke wa kigeni na aje kwa zamu pamoja na viongozi na mahakimu wa mji wake, mpaka hapo ghadhabu kali ya Mungu wetu itakapoondolewa kwetu.” Hakuna aliyepinga mpango huu, ila Yonathani, mwana wa Asaheli na Yazeya, mwana wa Tikwa, nao wakaungwa mkono na Meshulamu na Mlawi Shabethai. Watu wote waliorudi kutoka uhamishoni walikubali mpango huo, kwa hiyo kuhani Ezra aliwachagua wanaume kati ya viongozi wa koo mbalimbali na kuyaorodhesha majina yao. Mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa kumi, watu hao walianza kazi yao ya uchunguzi wa jambo hilo. Siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, walikuwa wamekwisha maliza uchunguzi wao kuhusu wanaume wote waliokuwa wameoa wanawake wa kigeni. Hii ndiyo orodha ya wanaume waliokuwa wameoa wanawake wa kigeni: Makuhani kulingana na koo zao: Ukoo wa Yeshua, mwana wa Yehosadaki na ndugu zake: Maaseya, Eliezeri, Yaribu na Gedalia. Hao waliahidi kuwaacha wake zao, na wakatoa kondoo dume kuwa sadaka kwa ajili ya hatia yao.
Ezra 10:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi hapo Ezra alipokuwa akiomba na kuungama, akilia, na kujiangusha kifudifudi mbele ya nyumba ya Mungu, kusanyiko kubwa sana la wanaume, wanawake na watoto, kutoka katika Israeli likamkusanyikia; maana watu hao walikuwa wakilia sana. Hata Shekania, mwana wa Yehieli, mmoja wa wazawa wa Elamu, akajibu, akamwambia Ezra, Sisi tumemkosea Mungu wetu, nasi tumeoa wanawake wageni wa watu wa nchi hizi; lakini bado kuna tumaini kwa Israeli katika jambo hili. Haya basi! Na tufanye agano na Mungu wetu, kuachana na wake zetu, na wale waliozaliwa nao, tukilifuata shauri la bwana wangu, na shauri la hao wanaoitetemekea amri ya Mungu wetu; mambo haya na yatendeke kwa kuifuata torati. Inuka; maana shughuli hii yakuhusu wewe; na sisi tu pamoja nawe; uwe na moyo mkuu, ukaitende. Ndipo Ezra akaondoka, akawaapisha wakuu wa makuhani, na Walawi, na Waisraeli wote, ya kwamba watafanya hivyo. Basi wakaapa. Kisha Ezra akaondoka hapo mbele ya nyumba ya Mungu, akaingia katika chumba cha Yehohanani, mwana wa Eliashibu; hata, alipofika huko, hakula mkate, wala hakunywa maji; kwa maana alilia kwa sababu ya kosa lile la watu wa uhamisho. Wakapiga mbiu katika Yuda yote na Yerusalemu, ya kwamba wana wote wa uhamisho wakusanyike pamoja huko Yerusalemu; na ya kwamba mtu yeyote asiyekuja katika muda wa siku tatu, kwa shauri lile la wakuu na wazee, basi aondolewe mali zake zote, akatengwe yeye mwenyewe na mkutano wa uhamisho. Ndipo wanaume wote wa Yuda na Benyamini wakakusanyika katika muda wa siku tatu; ulikuwa mwezi wa tisa, siku ya ishirini ya mwezi; na watu wote wakaketi katika uwanja, mbele ya nyumba ya Mungu, wakitetemeka kwa sababu ya neno hilo, na kwa sababu ya mvua kubwa. Kisha Ezra, kuhani, akasimama, akawaambia, Mmekosa, mmeoa wanawake wageni, kuiongeza hatia ya Israeli. Sasa basi, ungameni mbele za BWANA, Mungu wa baba zenu, mkatende alipendalo; mkajitenge na watu wa nchi, tena na wanawake wageni. Ndipo mkutano wote wakajibu, wakasema, kwa sauti kuu, Kama ulivyosema katika habari yetu, ndivyo vitupasavyo kutenda. Lakini watu hawa ni wengi, tena ni wakati wa mvua nyingi, nasi hatuwezi kusimama nje, tena kazi hii si kazi ya siku moja, wala ya siku mbili; maana tumekosa sana katika jambo hili. Basi wakuu wetu na wawekwe kwa ajili ya mkutano wote, na watu wote walio katika miji yetu, waliooa wanawake wageni, na waje nyakati zilizoamriwa, tena pamoja nao na waje wazee wa kila mji, na waamuzi wa miji hiyo, hata ghadhabu kali ya Mungu wetu itakapoondolewa mbali, jambo hili likamalizike. Yonathani, mwana wa Asaheli, na Yazeya, mwana wa Tikwa, hawa peke yao ndio waliosimama kulipinga neno hilo; na Meshulamu, na Shabethai Mlawi, wakawasaidia. Basi wana wa uhamisho wakafanya hivyo. Na Ezra, kuhani, akatengwa, pamoja na baadhi ya wakuu wa koo za mababa, kwa hesabu ya koo ya baba zao; na hao wote kwa majina yao. Wakaketi siku ya kwanza ya mwezi wa kumi, ili kulichunguza jambo hilo. Wakamaliza mambo ya wanaume wote, waliokuwa wameoa wanawake wageni, siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza. Basi, miongoni mwa makuhani walionekana wengine waliokuwa wameoa wanawake wageni; wa wazawa wa wa Yoshua, mwana wa Yosadaki, na nduguze; Maaseya, na Eliezeri, na Yaribu, na Gedalia. Nao wakatoa ahadi ya kwamba wataachana na wake zao; na kwa kuwa walikuwa na hatia, wakatoa kondoo dume kwa hatia yao.
Ezra 10:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi hapo Ezra alipokuwa akiomba na kuungama, akilia, na kujiangusha kifudifudi mbele ya nyumba ya Mungu, wakamkusanyikia katika Israeli wote kusanyiko kubwa sana la wanaume, na wanawake, na watoto; maana watu hao walikuwa wakilia sana. Hata Shekania, mwana wa Yehieli, mmoja wa wana wa Elamu, akajibu, akamwambia Ezra, Sisi tumemkosa Mungu wetu, nasi tumeoa wanawake wageni wa watu wa nchi hizi; lakini kungaliko tumaini kwa Israeli katika jambo hili. Haya basi! Na tufanye agano na Mungu wetu, kuachana na wake zetu, na wale waliozaliwa nao, tukilifuata shauri la bwana wangu, na shauri la hao wanaoitetemekea amri ya Mungu wetu; mambo haya na yatendeke kwa kuifuata torati. Inuka; maana shughuli hii yakuhusu wewe; na sisi tu pamoja nawe; uwe na moyo mkuu, ukaitende. Ndipo Ezra akaondoka, akawaapisha wakuu wa makuhani, na Walawi, na Israeli wote, ya kwamba watafanya kama hayo. Basi wakaapa. Kisha Ezra akaondoka hapo mbele ya nyumba ya Mungu, akaingia katika chumba cha Yehohanani, mwana wa Eliashibu; hata, alipofika huko, hakula mkate, wala hakunywa maji; kwa maana alilia kwa sababu ya kosa lile la watu wa uhamisho. Wakapiga mbiu katika Yuda yote na Yerusalemu, ya kwamba wana wote wa uhamisho wakusanyike pamoja huko Yerusalemu; na ya kwamba mtu awaye yote asiyekuja katika muda wa siku tatu, kwa shauri lile la wakuu na wazee, basi aondolewe mali zake zote, akatengwe yeye mwenyewe na mkutano wa uhamisho. Ndipo wanaume wote wa Yuda na Benyamini wakakusanyika katika muda wa siku tatu; ulikuwa mwezi wa kenda, siku ya ishirini ya mwezi; na watu wote wakaketi katika uwanja mbele ya nyumba ya Mungu, wakitetemeka kwa sababu ya neno hilo, na kwa sababu ya mvua kubwa. Kisha Ezra, kuhani, akasimama, akawaambia, Mmekosa, mmeoa wanawake wageni, kuiongeza hatia ya Israeli. Sasa basi, ungameni mbele za BWANA, Mungu wa baba zenu, mkatende alipendalo; mkajitenge na watu wa nchi, tena na wanawake wageni. Ndipo mkutano wote wakajibu, wakasema, kwa sauti kuu, Kama ulivyosema katika habari yetu, ndivyo vitupasavyo kutenda. Lakini watu hawa ni wengi, tena ni wakati wa mvua nyingi, nasi hatuwezi kusimama nje, tena kazi hii si kazi ya siku moja, wala ya siku mbili; maana tumekosa sana katika jambo hili. Basi maakida wetu na wawekwe kwa ajili ya mkutano wote, na watu wote walio katika miji yetu, waliooa wanawake wageni, na waje nyakati zilizoamriwa, tena pamoja nao na waje wazee wa kila mji, na makadhi wa miji hiyo, hata ghadhabu kali ya Mungu wetu itakapotuondokea mbali, jambo hili likamalizike. Yonathani, mwana wa Asaheli, na Yazeya, mwana wa Tikwa, hawa peke yao ndio waliosimama kulipinga neno hilo; na Meshulamu, na Shabethai Mlawi, wakawasaidia. Basi wana wa uhamisho wakafanya hivyo. Na Ezra, kuhani, akatengwa, pamoja na baadhi ya wakuu wa mbari za mababa, kwa hesabu ya mbari ya baba zao; na hao wote kwa majina yao. Wakaketi siku ya kwanza ya mwezi wa kumi, ili kulichunguza jambo hilo. Wakamaliza mambo ya wanaume wote, waliokuwa wameoa wanawake wageni, siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza. Basi, miongoni mwa makuhani walionekana wengine waliokuwa wameoa wanawake wageni; wa wana wa Yoshua, mwana wa Yosadaki, na nduguze; Maaseya, na Eliezeri, na Yaribu, na Gedalia. Nao wakatoa ahadi ya kwamba wataachana na wake zao; na kwa kuwa walikuwa na hatia, wakatoa kondoo mume kwa hatia yao.
Ezra 10:1-19 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Ezra alipokuwa anaomba na kuungama, huku akilia na kujitupa chini mbele ya nyumba ya Mungu, umati mkubwa wa Waisraeli wakiwemo wanaume, wanawake na watoto walikusanyika kumzunguka. Nao pia wakalia sana. Kisha Shekania mwana wa Yehieli, mmoja wa wazao wa Elamu, akamwambia Ezra, “Tumekosa uaminifu kwa Mungu wetu kwa kuoa wanawake wa kigeni kutoka mataifa yanayotuzunguka. Lakini pamoja na hili, bado liko tumaini kwa ajili ya Israeli. Sasa na tufanye agano mbele za Mungu wetu kuwafukuza hawa wanawake wote pamoja na watoto wao, kulingana na maonyo ya bwana wangu pamoja na wale ambao wanaogopa amri za Mungu wetu. Hili na lifanyike sawasawa na hii Torati. Inuka, suala hili lipo mikononi mwako. Sisi tutaungana nawe, uwe na ujasiri ukatende hili.” Basi Ezra akainuka na kuwaapisha makuhani viongozi, Walawi na Waisraeli wote kufanya lile lililokuwa limependekezwa. Nao wakaapa. Ndipo Ezra akaondoka hapo mbele ya nyumba ya Mungu akaenda kwenye chumba cha Yehohanani mwana wa Eliashibu. Alipokuwa hapo, hakula chakula wala hakunywa maji, kwa sababu aliendelea kuomboleza kwa kuwa watu wa uhamishoni walikosa uaminifu kwa Mungu. Ndipo lilipotolewa tangazo Yuda yote na Yerusalemu kwa watu wote waliokuwa uhamishoni kukusanyika Yerusalemu. Yeyote ambaye hangejitokeza kwa muda wa siku tatu angepoteza mali yake yote, kulingana na uamuzi wa maafisa na wazee. Naye mtu huyo angefukuzwa kutoka kusanyiko la watu waliokuwa uhamishoni. Katika muda wa siku tatu, watu wote wa Yuda na Benyamini wakawa wamekusanyika huko Yerusalemu. Kwenye siku ya ishirini ya mwezi wa tisa, watu wote walikuwa wameketi ndani ya uwanja mbele ya nyumba ya Mungu, wakiwa na majonzi mno kwa tukio hilo na kwa sababu ya mvua kubwa. Ndipo Kuhani Ezra aliposimama akawaambia, “Mmekosa uaminifu, mmeoa wanawake wa kigeni, mkaongezea hatia ya Israeli. Sasa tubuni kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu, mkafanye mapenzi yake. Jitengeni na mataifa wanaowazunguka na wake zenu wa kigeni.” Kusanyiko lote wakajibu kwa sauti kubwa: “Uko sawa kabisa! Ni lazima tufanye kama unavyosema. Lakini hapa pana watu wengi na ni wakati wa mvua, hivyo hatuwezi kusimama nje. Hata hivyo, shauri hili haliwezi kumalizika kwa siku moja au mbili, kwa sababu tumetenda dhambi kubwa katika jambo hili. Maafisa wetu na watende kwa niaba ya kusanyiko lote. Kisha kila mmoja katika miji yetu ambaye ameoa mwanamke wa kigeni aje kwa wakati uliopangwa, akiwa pamoja na wazee na waamuzi wa kila mji, hadi hasira kali ya Mungu wetu katika shauri hili itakapoondolewa kwetu.” Yonathani mwana wa Asaheli na Yazeya mwana wa Tikwa peke yao, wakiungwa mkono na Meshulamu na Shabethai Mlawi, ndio waliopinga jambo hili. Basi watu wa uhamishoni wakafanya kama ilivyokuwa imependekezwa. Kuhani Ezra akachagua wanaume waliokuwa viongozi wa jamaa, mmoja kutoka kila mgawanyo wa jamaa, nao wote wakachaguliwa kwa majina. Katika siku ya kwanza ya mwezi wa kumi waliketi kuchunguza mashauri hayo. Katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza wakawa wamemaliza kushughulikia wanaume wote waliokuwa wameoa wanawake wa kigeni. Miongoni mwa wazao wa makuhani, wafuatao walikuwa wameoa wanawake wa kigeni: Kutoka wazao wa Yeshua mwana wa Yosadaki na ndugu zake: Maaseya, Eliezeri, Yaribu na Gedalia. (Wote walitoa nadhiri kwa kuandika kwa mikono yao kuwafukuza wake zao, kwa hatia yao, kila mmoja akatoa kondoo dume kutoka kundini mwake kuwa sadaka ya hatia.)