Ezekieli 7:14-27
Ezekieli 7:14-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Tarumbeta imepigwa na kuwafanya wote wawe tayari. Lakini hakuna anayekwenda vitani, kwani ghadhabu yangu iko juu ya umati wote. Nje kuna kifo kwa upanga na ndani ya mji kuna maradhi mabaya na njaa. Walioko shambani watakufa kwa upanga; walio mjini njaa na maradhi mabaya yatawaangamiza. Wakiwapo watu watakaosalimika watakimbilia milimani kama hua waliotishwa bondeni. Kila mmoja wao ataomboleza kwa dhambi zake. Kila mtu, mikono yake itakuwa dhaifu na magoti yake yatakuwa maji. Watavaa mavazi ya gunia, hofu itawashika, nao watakuwa na aibu, vichwa vyao vyote vitanyolewa. Watatupa fedha yao barabarani na dhahabu yao itakuwa kama kitu najisi. Fedha na dhahabu zao hazitaweza kuwaokoa katika siku hiyo ya ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu; wala hawataweza kushiba au kuyajaza matumbo yao fedha na dhahabu waliyojirundikia; kwani mali hiyo ndiyo chanzo cha dhambi yao. Kwa kuwa walijifanyia utukufu usio na maana kwa njia ya vikuku, wakajifanyia sanamu za miungu zinazochukiza pamoja na vitu vyao vya aibu; vyote hivyo nitavifanya kuwa najisi kwao. Utajiri wao nitautia mikononi mwa mataifa mengine, watu waovu wa dunia watauteka na kuutia najisi. Uso wangu nitaugeuzia mbali nao ili walitie najisi hekalu langu. Wanyanganyi wataingia humo ndani na kulitia najisi. Tengeneza mnyororo. Kwa kuwa nchi imejaa makosa ya jinai ya umwagaji damu na mji umejaa dhuluma kupindukia, nitayaleta mataifa mabaya sana nao watazimiliki nyumba zao. Kiburi chao nitakikomesha, na mahali pao pa ibada patatiwa unajisi. Uchungu mkali utakapowajia, watatafuta amani, lakini haitapatikana. Watapata maafa mfululizo; nazo habari mbaya zitafuatana. Watamwomba nabii maono. Makuhani hawatakuwa na sheria yoyote; na wazee watakosa shauri la kuwapatia. Mfalme ataomboleza, mkuu atakata tamaa na watu watatetemeka kwa hofu. Nitawatenda kadiri ya mienendo yao, nitawahukumu kama nilivyowahukumu wengine. Ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”
Ezekieli 7:14-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wamepiga tarumbeta, wametayarisha vitu vyote; lakini hapana aendaye vitani; maana ghadhabu yangu imewapata umati wote. Upanga uko nje, na tauni na njaa zimo ndani; yeye aliye nje mashambani atakufa kwa upanga; na yeye aliye ndani ya mji, njaa na tauni zitamla. Lakini watakaokimbia watakimbia, nao watakuwa juu ya milima kama hua wa bondeni, wote wakilia, kila mmoja katika uovu wake. Mikono yote itakuwa dhaifu, na magoti yote yatalegea kama maji. Tena watajifungia nguo za magunia, na utisho utawafunika; na aibu itakuwa juu ya nyuso zote, na upaa juu ya vichwa vyao vyote. Watatupa fedha yao katika njia kuu za mji, na dhahabu yao itakuwa kama kitu cha unajisi; fedha yao na dhahabu yao hazitaweza kuwaokoa siku ya ghadhabu ya BWANA; hawatajishibisha roho zao, wala hawatajijaza matumbo yao; kwa sababu zilikuwa kwazo la uovu wao. Na uzuri wa pambo lake, yeye aliuweka katika enzi, lakini wao walifanya sanamu za machukizo yao, na vitu vyao vichukizavyo, ndani yake; ndiyo maana nimeifanya kuwa kama kitu cha unajisi kwao. Nami nitapatia katika mikono ya wageni pawe mateka yao, na katika mikono ya waovu wa duniani pawe mawindo yao, nao watapanajisi. Tena nitaugeuza uso wangu usiwaelekee, nao watapatia unajisi mahali pangu pa siri; na wanyang'anyi wataingia humo na kupatia unajisi. Ufue mnyororo; kwa maana nchi hii imejaa hukumu za damu, nao mji umejaa udhalimu. Kwa sababu hiyo nitawaleta watu wa mataifa walio wabaya kabisa, nao watazimiliki nyumba zao; tena nitakikomesha kiburi chao wenye nguvu; na mahali pao patakatifu patatiwa unajisi. Uharibifu utakapokuja; nao watatafuta amani, lakini haitapatikana. Madhara yatakuja juu ya madhara, na habari ya shari juu ya habari ya shari; nao watakwenda kwa nabii kutaka maono; lakini hiyo sheria itampotea kuhani, na mashauri yatawapotea wazee. Mfalme ataomboleza, na mkuu atavikwa ukiwa, na mikono ya watu wa nchi itataabika; nitawatenda kulingana na njia yao; nami nitawahukumu kulingana na kustahili kwao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
Ezekieli 7:14-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wamepiga tarumbeta, wameweka vitu vyote tayari; lakini hapana aendaye vitani; maana ghadhabu yangu imewapata wote jamii. Upanga uko nje, na tauni na njaa zimo ndani; yeye aliye nje mashambani atakufa kwa upanga; na yeye aliye ndani ya mji, njaa na tauni zitamla. Lakini watakaokimbia watakimbia, nao watakuwa juu ya milima kama hua wa bondeni, wote wakilia, kila mmoja katika uovu wake. Mikono yote itakuwa dhaifu, na magoti yote yatalegea kama maji. Tena watajifungia nguo za magunia, na utisho utawafunika; na aibu itakuwa juu ya nyuso zote, na upaa juu ya vichwa vyao vyote. Watatupa fedha yao katika njia kuu za mji, na dhahabu yao itakuwa kama kitu cha unajisi; fedha yao na dhahabu yao hazitaweza kuwaokoa siku ya ghadhabu ya BWANA; hawatajishibisha roho zao, wala hawatajijaza matumbo yao; kwa sababu zilikuwa kwazo la uovu wao. Na uzuri wa pambo lake, yeye aliuweka katika enzi, lakini wao walifanya sanamu za machukizo yao, na vitu vyao vichukizavyo, ndani yake; ndiyo maana nimeifanya kuwa kama kitu cha unajisi kwao. Nami nitapatia katika mikono ya wageni pawe mateka yao, na katika mikono ya waovu wa duniani pawe mawindo yao, nao watapanajisi. Tena nitaugeuza uso wangu usiwaelekee, nao watapatia unajisi mahali pangu pa siri; na wanyang’anyi wataingia humo na kupatia unajisi. Ufue mnyororo; kwa maana nchi hii imejaa hukumu za damu, nao mji umejaa udhalimu. Kwa sababu hiyo nitawaleta watu wa mataifa walio wabaya kabisa, nao watazimiliki nyumba zao; tena nitakikomesha kiburi chao wenye nguvu; na mahali pao patakatifu patatiwa unajisi. Uharibifu unakuja; nao watatafuta amani, lakini haitapatikana. Madhara yatakuja juu ya madhara, na habari ya shari juu ya habari ya shari; nao watakwenda kwa nabii kutaka maono; lakini hiyo sheria itampotea kuhani, na mashauri yatawapotea wazee. Mfalme ataomboleza, na mkuu atavikwa ukiwa, na mikono ya watu wa nchi itataabika; nitawatenda sawasawa na njia yao; nami nitawahukumu sawasawa na kustahili kwao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
Ezekieli 7:14-27 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wajapopiga tarumbeta na kuweka kila kitu tayari, hakuna hata mmoja atakayekwenda vitani, kwa maana ghadhabu yangu iko juu ya kundi lote. “Nje ni upanga, ndani ni tauni na njaa, wale walioko shambani watakufa kwa upanga, nao wale waliomo mjini njaa na tauni vitawala. Wale wote watakaopona na kutoroka watakuwa milimani, wakiomboleza kama hua wa mabondeni, kila mmoja kwa sababu ya dhambi zake. Kila mkono utalegea na kila goti litakuwa dhaifu kama maji. Watavaa nguo ya gunia na kufunikwa na hofu. Nyuso zao zitafunikwa na aibu na nywele za vichwa vyao zitanyolewa. Watatupa fedha yao barabarani, nayo dhahabu yao itakuwa najisi. Fedha yao na dhahabu yao havitaweza kuwaokoa katika siku hiyo ya ghadhabu ya BWANA. Hawatashibisha njaa yao au kujaza matumbo yao kwa hiyo fedha wala dhahabu, kwa sababu imewaponza wajikwae dhambini. Walijivunia vito vyao vizuri na kuvitumia kufanya sanamu za machukizo na vinyago vya upotovu. Kwa hiyo nitavifanya vitu hivyo kuwa najisi kwao. Nitavitia vyote mikononi mwa wageni kuwa nyara na kuwa vitu vilivyotekwa mikononi mwa watu waovu wa dunia, nao watavinajisi. Nitageuza uso wangu mbali nao, nao waovu wa dunia watapanajisi mahali pangu pa thamani, wanyangʼanyi watapaingia na kupanajisi. “Andaa minyororo, kwa sababu nchi imejaa umwagaji wa damu na mji umejaa udhalimu. Nitaleta taifa ovu kuliko yote ili kumiliki nyumba zao, nitakomesha kiburi cha wenye nguvu na mahali pao patakatifu patatiwa unajisi. Hofu ya ghafula itakapokuja, watatafuta amani, lakini haitakuwepo. Maafa juu ya maafa yatakuja, tetesi ya mabaya juu ya tetesi ya mabaya. Watajitahidi kupata maono kutoka kwa nabii, mafundisho ya sheria toka kwa kuhani yatapotea, vivyo hivyo shauri kutoka kwa wazee. Mfalme ataomboleza, mwana wa mfalme atavikwa kukata tamaa, nayo mikono ya watu wa nchi itatetemeka. Nitawashughulikia sawasawa na matendo yao na kwa kanuni zao wenyewe nitawahukumu. Ndipo watajua kwamba Mimi ndimi BWANA.”