Ezekieli 47:13-23
Ezekieli 47:13-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Hii ndiyo mipaka ya nchi mtakayoyagawia makabila kumi na mawili ya Israeli. Lakini kabila la Yosefu lipewe maradufu. Nyote mtagawana sawa. Niliapa kuwa nitawapa wazee wenu nchi hii, nayo itakuwa mali yenu. Upande wa kaskazini mpaka utapita kutoka Bahari ya Mediteranea, kuelekea mji wa Hethloni, hadi mahali pa kuingia Hamathi na kuendelea hadi Zedadi. Kutoka hapo utaendelea hadi Berotha na Sibraimu (ulio kati ya Damasko na Hamathi), hadi mji wa Haser-hatikoni ulio mpakani mwa Haurani. Hivyo mpaka utakwenda kutoka bahari ya Mediteranea kuelekea mashariki hadi mji wa Hasar-enoni ukipakana na maeneo ya Damasko na Hamathi kwa upande wa kaskazini. Upande wa mashariki, mpaka utakuwa mto wa Yordani unaoelekea kati ya Haurani na Damasko, Gileadi na nchi ya Israeli. Pia mpaka utapitia upande wa mashariki wa Bahari ya Chumvi hadi Tamari. Upande wa kusini, toka Tamari mpaka utaendelea hadi chemchemi ya Meriba-kadeshi. Kutoka Meriba-kadeshi mpaka utaelekea kusini-magharibi hadi Bahari ya Mediteranea ukipitia mashariki ya nchi ya Misri. Upande wa magharibi, mpaka ni Bahari ya Mediteranea na utapanda kaskazini hadi mahali pa kuingilia Hamathi. “Basi, mtagawanya nchi hii kati yenu kulingana na makabila ya Israeli. Mtaigawanya kuwa mali yenu. Wageni watakaokaa kati yenu na wamezaa watoto, pia wapewe sehemu ya nchi mnapoigawanya. Hao ni lazima watendewe kama raia halisi wa Israeli na wana haki ya kupiga kura ili kupata sehemu ya nchi pamoja na makabila ya Israeli. Kila mgeni anayekaa nanyi atapewa sehemu yake pamoja na watu wa kabila ambamo anaishi. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Ezekieli 47:13-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Bwana MUNGU asema hivi; Huu ndio mpaka ambao mtaigawanya nchi iwe urithi sawasawa na makabila kumi na mawili ya Israeli; kwa Yusufu, mafungu mawili. Nanyi mtaimiliki, mtu huyu sawasawa na huyu; ambayo niliuinua mkono wangu kuwapa baba zenu; na nchi hii itawaangukia kuwa urithi. Na huu ndio mpaka wa nchi; upande wa kaskazini, toka bahari kubwa, kwa njia ya Hethloni, mpaka maingilio ya Sedada; Hamathi, na Berotha, na Sibraimu, ulio katikati ya mpaka wa Dameski na mpaka wa Hamathi; na Haser-hatikoni, ulio karibu na mpaka wa Haurani. Nao mpaka toka baharini utakuwa Hasar-enoni, penye mpaka wa Dameski, na kaskazini kuelekea upande wa kaskazini ndio mpaka wa Hamathi. Huu ndio upande wa kaskazini. Na upande wa mashariki, kati ya Haurani na Dameski, na Gileadi na nchi ya Israeli, utakuwa Mto Yordani; mtapima toka mpaka wa upande wa kaskazini hata bahari ya mashariki. Huu ndio upande wa mashariki. Na upande wa kusini, kuelekea kusini, utakuwa ni kutoka Tamari mpaka maji ya Meriba-Kadeshi, mpaka kijito cha Misri, mpaka bahari kubwa. Huu ndio upande wa kusini, kuelekea kusini. Na upande wa magharibi, utakuwa ni bahari kubwa, kutoka mpaka wa kusini mpaka mahali penye kuelekea maingilio ya Hamathi. Huu ndio upande wa magharibi. Basi ndivyo mtakavyojigawanyia nafsi zenu nchi hii, sawasawa na makabila ya Israeli. Tena itakuwa mtaigawanya kwa kura, kuwa urithi kwenu, na kwa wageni wakaao kwenu kama ugeni, watakaozaa watoto kati yenu, nao watakuwa kwenu, kama wazaliwa miongoni mwa wana wa Israeli; watakuwa na urithi pamoja nanyi kati ya makabila ya Israeli. Tena itakuwa, mgeni akaaye katika kabila iwayo yote, atapewa urithi katika kabila asema Bwana MUNGU.
Ezekieli 47:13-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Bwana MUNGU asema hivi; Huu ndio mpaka ambao mtaigawanya nchi iwe urithi sawasawa na kabila kumi na mbili za Israeli; kwa Yusufu, mafungu mawili. Nanyi mtaimiliki, mtu huyu sawasawa na huyu; ambayo naliuinua mkono wangu kuwapa baba zenu; na nchi hii itawaangukia kuwa urithi. Na huu ndio mpaka wa nchi; upande wa kaskazini, toka bahari kubwa, kwa njia ya Hethloni, mpaka maingilio ya Sedada; Hamathi, na Berotha, na Sibraimu, ulio katikati ya mpaka wa Dameski na mpaka wa Hamathi; na Haser-hatikoni, ulio karibu na mpaka wa Haurani. Nao mpaka toka baharini utakuwa Hasar-enoni, penye mpaka wa Dameski, na kaskazini kuelekea upande wa kaskazini ndio mpaka wa Hamathi. Huu ndio upande wa kaskazini. Na upande wa mashariki, kati ya Haurani na Dameski, na Gileadi na nchi ya Israeli, utakuwa mto Yordani; mtapima toka mpaka wa upande wa kaskazini hata bahari ya mashariki. Huu ndio upande wa mashariki. Na upande wa kusini, kuelekea kusini, utakuwa ni kutoka Tamari mpaka maji ya Meriba-Kadeshi, mpaka kijito cha Misri, mpaka bahari kubwa. Huu ndio upande wa kusini, kuelekea kusini. Na upande wa magharibi, utakuwa ni bahari kubwa, kutoka mpaka wa kusini mpaka mahali penye kuelekea maingilio ya Hamathi. Huu ndio upande wa magharibi. Basi ndivyo mtakavyojigawanyia nafsi zenu nchi hii, sawasawa na kabila za Israeli. Tena itakuwa mtaigawanya kwa kura, kuwa urithi kwenu, na kwa wageni wakaao kwenu hali ya ugeni, watakaozaa watoto kati yenu, nao watakuwa kwenu, kama wazaliwa miongoni mwa wana Israeli; watakuwa na urithi pamoja nanyi kati ya kabila za Israeli. Tena itakuwa, mgeni akaaye katika kabila iwayo yote, atapewa urithi katika kabila asema Bwana MUNGU.
Ezekieli 47:13-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “Hii ndiyo mipaka ambayo kwayo mtagawanya hiyo nchi kuwa urithi miongoni mwa hayo makabila kumi na mawili ya Israeli, pamoja na mafungu mawili ya Yosefu. Mtagawa kwa usawa miongoni mwao. Kwa sababu niliapa kwa mkono ulioinuliwa kuwapa baba zenu, nchi hii itakuwa urithi wenu. “Huu ndio utakuwa mpaka wa hiyo nchi: “Upande wa kaskazini utaanzia Bahari Kuu kwa njia ya Hethloni kupitia Lebo-Hamathi hadi maingilio ya Sedadi. Berotha na Sibraimu (ambao uko kwenye mpaka kati ya Dameski na Hamathi), hadi kufikia Haser-Hatikoni, ambao uko katika mpaka wa Haurani. Hivyo mpaka utaendelea kuanzia Baharini hadi Hasar-Enoni, ukiambaa na mpaka wa kaskazini wa Dameski, pamoja na mpaka wa Hamathi upande wa kaskazini. Huu utakuwa ndio mpaka wa kaskazini. Upande wa mashariki mpaka utapita kati ya Haurani na Dameski, kuambaa Yordani na kati ya Gileadi na nchi ya Israeli, hadi bahari ya mashariki na kufika Tamari. Huu utakuwa ndio mpaka wa mashariki. Upande wa kusini utaanzia Tamari hadi kufikia maji ya Meriba-Kadeshi, kisha utaambaa na Kijito cha Misri hadi Bahari Kuu. Huu utakuwa ndio mpaka wa kusini. Upande wa magharibi, Bahari Kuu itakuwa ndio mpaka hadi kwenye sehemu mkabala na Lebo-Hamathi. Huu utakuwa ndio mpaka wa magharibi. “Mtagawanya nchi hii miongoni mwenu kufuatana na makabila ya Israeli. Mtaigawanya kuwa urithi kwa ajili yenu na kwa ajili ya wageni wanaoishi miongoni mwenu na ambao wana watoto. Wao watakuwa kwenu kama wenyeji wazawa wa Israeli, pamoja na ninyi watagawiwa urithi miongoni mwa makabila ya Israeli. Katika kabila lolote mgeni atakapoishi hapo ndipo mtakapompatia urithi wake,” asema BWANA Mwenyezi.