Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 37:15-28

Ezekieli 37:15-28 Biblia Habari Njema (BHN)

Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia; “Wewe mtu! Chukua kijiti kimoja, uandike juu yake maneno haya: ‘Kwa Yuda na Waisraeli wanaohusiana naye.’ Kisha chukua kijiti kingine, uandike juu yake maneno haya: ‘Kwa Yosefu (kijiti cha Efraimu) na Waisraeli wanaohusiana naye.’ Halafu vichukue vijiti hivyo na kuvishikamanisha ili vionekane kama kijiti kimoja. Wananchi wenzako watakapouliza, ‘Je, hutatueleza maana ya jambo hilo?’ Wewe utawajibu, Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: Nitakitwaa kijiti cha Yosefu (kilichomo mkononi mwa Efraimu) na makabila ya Israeli yanayounganika naye, nami nitakishikamanisha na kijiti cha Yuda ili vijiti hivyo viwili vifanywe kijiti kimoja mkononi mwangu. “Ukiwa mbele yao huku umeshika vijiti ulivyoandika juu yake, waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitawatoa Waisraeli kutoka mataifa walikokwenda; nitawakusanya toka pande zote na kuwarudisha katika nchi yao. Nitawafanya kuwa taifa moja katika nchi juu ya milima ya Israeli; mfalme mmoja atakuwa mfalme wao wote. Hawatakuwa tena mataifa mawili wala hawatagawanyika tena kuwa falme mbili. Hawatajitia unajisi tena kwa sanamu za miungu yao na kwa mambo yao ya kuchukiza wala kwa makosa yao. Nitawaokoa wasiwe tena waasi. Nao watakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wao. Mtumishi wangu Daudi atakuwa mfalme wao; naam, watakuwa na mchungaji mmoja tu. Watayafuata maagizo yangu na kuzingatia kanuni zangu. Watakaa katika nchi ya wazee wao ambayo nilimpa Yakobo. Wao na watoto wao na wajukuu wao wataishi humo milele. Naye Daudi, mtumishi wangu, atakuwa mtawala milele. Nitafanya nao agano la amani, nalo litakuwa agano la milele. Nitawabariki na kuwafanya wawe wengi, na maskani yangu nitaiweka kati yao milele. Nitaishi kati yao; nitakuwa Mungu wao nao watakuwa watu wangu. Nayo mataifa yatatambua kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, nimewatakasa Waisraeli na kwamba maskani yangu ipo kati yao milele.”

Ezekieli 37:15-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Neno la BWANA likanijia tena, kusema, Na wewe mwanadamu, twaa kijiti kimoja; ukaandike juu yake, Kwa Yuda, na kwa wana wa Israeli wenzake; kisha, twaa kijiti cha pili; ukaandike juu yake, Kwa Yusufu, kijiti cha Efraimu, na kwa nyumba yote ya Israeli wenzake; ukaviunge pamoja kwa ajili yako hiki na hiki viwe kijiti kimoja, viwe kimoja katika mkono wako. Na wana wa watu wangu watakapokuambia, wakisema, Je! Hutatuonesha maana ya mambo hayo utendayo? Waambie, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitakitwaa kijiti cha Yusufu, kilicho mkononi mwa Efraimu, na makabila ya Israeli wenzake, nami nitawaweka pamoja nacho, yaani, pamoja na kijiti cha Yuda, na kuvifanya kuwa kijiti kimoja; navyo vitakuwa kimoja mkononi mwangu. Navyo vijiti, ambavyo uliandika juu yake, vitakuwa mkononi mwako mbele ya macho yao. Ukawaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitawatwaa wana wa Israeli toka kati ya mataifa walikokwenda, nami nitawakusanya pande zote, na kuwaleta katika nchi yao wenyewe; nami nitawafanya kuwa taifa moja katika nchi hiyo, juu ya milima ya Israeli; na mfalme mmoja atakuwa mfalme wao wote; wala hawatakuwa tena mataifa mawili, wala hawatagawanyika kuwa falme mbili tena, hata milele. Wala hawatajitia uchafu tena kwa vinyago vyao, wala kwa vitu vyao vichukizavyo, wala kwa makosa yao mojawapo; lakini nitawaokoa, na kuwatoa katika makao yao yote, ambayo wamefanya dhambi ndani yake, nami nitawatakasa; basi watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao. Na mtumishi wangu, Daudi, atakuwa mfalme juu yao, nao wote watakuwa na mchungaji mmoja; nao watayafuata maagizo yangu, na kuzishika amri zangu, na kuzitenda. Nao watakaa katika nchi niliyompa Yakobo, mtumishi wangu, walimokaa baba zenu; nao watakaa humo, wao na watoto wao, na watoto wa watoto wao, milele; na Daudi, mtumishi wangu, atakuwa mkuu wao milele. Tena nitafanya agano la amani pamoja nao; litakuwa agano la milele pamoja nao; nami nitawaweka na kuwazidisha, na patakatifu pangu nitapaweka katikati yao milele. Tena maskani yangu itakuwa pamoja nao; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Na mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, mimi niwatakasaye Israeli, patakatifu pangu patakapokuwa katikati yao milele.

Ezekieli 37:15-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Neno la BWANA likanijia tena, kusema, Na wewe mwanadamu, twaa kijiti kimoja; ukaandike juu yake, Kwa Yuda, na kwa wana wa Israeli wenzake; kisha, twaa kijiti cha pili; ukaandike juu yake, Kwa Yusufu, kijiti cha Efraimu, na kwa nyumba yote ya Israeli wenzake; ukaviunge pamoja kwa ajili yako hiki na hiki viwe kijiti kimoja, viwe kimoja katika mkono wako. Na wana wa watu wangu watakapokuambia, wakisema, Je! Hutatuonyesha maana ya mambo hayo utendayo? Waambie, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitakitwaa kijiti cha Yusufu, kilicho mkononi mwa Efraimu, na kabila za Israeli wenzake, nami nitawaweka pamoja nacho, yaani, pamoja na kijiti cha Yuda, na kuvifanya kuwa kijiti kimoja; navyo vitakuwa kimoja mkononi mwangu. Navyo vijiti, ambavyo uliandika juu yake, vitakuwa mkononi mwako mbele ya macho yao. Ukawaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitawatwaa wana wa Israeli toka kati ya mataifa walikokwenda, nami nitawakusanya pande zote, na kuwaleta katika nchi yao wenyewe; nami nitawafanya kuwa taifa moja katika nchi hiyo, juu ya milima ya Israeli; na mfalme mmoja atakuwa mfalme wao wote; wala hawatakuwa tena mataifa mawili, wala hawatagawanyikana kuwa falme mbili tena, hata milele. Wala hawatajitia uchafu tena kwa vinyago vyao, wala kwa vitu vyao vichukizavyo, wala kwa makosa yao mojawapo; lakini nitawaokoa, na kuwatoa katika makao yao yote, ambayo wamefanya dhambi ndani yake, nami nitawatakasa; basi watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao. Na mtumishi wangu, Daudi, atakuwa mfalme juu yao, nao wote watakuwa na mchungaji mmoja; nao wataenenda katika hukumu zangu, na kuzishika amri zangu, na kuzitenda. Nao watakaa katika nchi niliyompa Yakobo, mtumishi wangu, walimokaa baba zenu; nao watakaa humo, wao na watoto wao, na watoto wa watoto wao, milele; na Daudi, mtumishi wangu, atakuwa mkuu wao milele. Tena nitafanya agano la amani pamoja nao; litakuwa agano la milele pamoja nao; nami nitawaweka na kuwazidisha, na patakatifu pangu nitapaweka katikati yao milele. Tena maskani yangu itakuwa pamoja nao; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Na mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, mimi niwatakasaye Israeli, patakatifu pangu patakapokuwa katikati yao milele.

Ezekieli 37:15-28 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, chukua fimbo na uandike juu yake, ‘Hii ni kwa ajili ya Yuda na Waisraeli waliofungamana naye.’ Kisha chukua fimbo nyingine, uandike juu yake, ‘Fimbo ya Efraimu, ni kwa ajili ya Yosefu na nyumba yote ya Israeli wanaofungamana naye.’ Ziunganishe pamoja kuwa fimbo moja ili kwamba ziwe fimbo moja katika mkono wako. “Watu wako watakapokuuliza, ‘Je, hutatuambia ni nini maana ya jambo hili?’ Waambie, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Nitaichukua fimbo ya Yosefu, iliyoko mikononi mwa Efraimu na ya makabila ya Israeli yanayofungamana naye na kuiunganisha na fimbo ya Yuda, nikizifanya kuwa fimbo moja, nao watakuwa wamoja katika mkono wangu.’ Inua mbele ya macho yao zile fimbo ulizoziandika kisha waambie, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Nitawatoa Waisraeli katika mataifa walikokuwa wamekwenda. Nitawakusanya popote walipo na kuwarudisha katika nchi yao wenyewe. Nitawafanya kuwa taifa moja katika nchi, katika milima ya Israeli. Patakuwa na mfalme mmoja juu yao wote na kamwe hawatagawanyika tena kuwa mataifa mawili au kugawanyika katika falme mbili. Hawatajitia tena unajisi kwa sanamu zao na vinyago vyao visivyo na maana wala kwa makosa yao yoyote, kwa maana nitawaokoa kutoka dhambi zao zote zilizowarudisha nyuma, nami nitawatakasa. Wao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao. “ ‘Mtumishi wangu Daudi atakuwa mfalme juu yao, nao wote watakuwa na mchungaji mmoja. Watafuata sheria zangu na kuzishika amri zangu kwa uangalifu. Wataishi katika nchi niliyompa mtumishi wangu Yakobo, nchi ambamo baba zenu waliishi. Wao na watoto wao na watoto wa watoto wao wataishi humo milele, naye Daudi mtumishi wangu atakuwa mkuu wao milele. Nitafanya nao Agano la amani, litakuwa Agano la milele. Nitawafanya imara na kuongeza idadi yao, nami nitaweka mahali patakatifu pangu miongoni mwao milele. Maskani yangu yatakuwa pamoja nao, nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Ndipo mataifa watakapojua kwamba Mimi BWANA ndiye ninayeifanya Israeli kuwa takatifu, wakati mahali patakatifu pangu patakapokuwa miongoni mwao milele.’ ”

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha