Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 33:21-33

Ezekieli 33:21-33 Biblia Habari Njema (BHN)

Siku ya tano ya mwezi wa kumi, mwaka wa kumi na mbili wa uhamisho wetu, mtu mmoja aliyetoroka kutoka Yerusalemu alinijia, akasema: “Mji wa Yerusalemu umetekwa!” Wakati alipofika huyo mtu ilikuwa asubuhi kumbe jana yake jioni mimi nilisikia uzito wa nguvu yake Mwenyezi-Mungu. Basi, huyo mkimbizi alipowasili kwangu kesho yake asubuhi, nikaacha kuwa bubu, nikaanza kuongea tena. Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Wakazi waliobaki katika miji iliyoharibiwa nchini Israeli wanasema, ‘Abrahamu alikuwa peke yake, hata hivyo, alipata kuimiliki nchi hii. Lakini sisi ni wengi; ni dhahiri tumepewa nchi hii iwe yetu!’ Basi, waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nyinyi mnakula nyama yenye damu, mnaziabudu sanamu za miungu yenu na kuua! Je, mnadhani mtapewa nchi hii iwe yenu? Mnategemea silaha zenu, mnafanya mambo ya kuchukiza na kila mwanamume miongoni mwenu anatembea na mke wa jirani yake! Je, mnadhani mtapewa nchi hii iwe yenu? Waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kama niishivyo mimi naapa kwamba hao wanaokaa katika miji hiyo iliyo magofu, wataangamia kwa upanga; aliye uwanjani nitamtoa aliwe na wanyama wakali; na wale walio ndani ya ngome na mapangoni watakufa kwa maradhi mabaya. Nitaifanya nchi kuwa jangwa na tupu. Mashujaa wake wenye kiburi nitawaua. Milima ya Israeli itakuwa jangwa na hakuna mtu atakayepita huko. Naam, nitakapoifanya hiyo nchi kuwa jangwa na tupu kwa sababu ya mambo yote ya kuchukiza waliyotenda, ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.” Mwenyezi-Mungu aliniambia, “Wewe mtu! Wananchi wenzako wanazungumza juu yako, wameketi kutani na milangoni mwa nyumba zao na kuambiana: ‘Haya! Twende tukasikie neno alilosema Mwenyezi-Mungu!’ Basi, hukujia makundi kwa makundi na kuketi mbele yako kama watu wangu, wasikie unachosema, lakini hawafanyi unachowaambia wafanye. Wanasema kwamba wana upendo, lakini hayo ni maneno matupu; wanachotafuta kwa moyo ni faida yao tu. Kwao, wewe umekuwa tu kama mwimbaji wa kutumbuiza mwenye sauti nzuri ikiandamana na muziki safi! Wanayasikia yale unayosema, lakini hawatekelezi hata mojawapo. Lakini hayo unayosema yatakapotukia – nayo kweli yatatukia – basi, ndipo watakapotambua kuwa nabii amekuwapo miongoni mwao.”

Ezekieli 33:21-33 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Mwaka wa kumi na mbili wa uhamisho wetu, mwezi wa kumi, siku ya tano, mtu aliyekuwa ametoroka kutoka Yerusalemu akanijia na kusema, “Mji wa Yerusalemu umeanguka!” Basi jioni kabla mtu huyo hajaja, mkono wa BWANA, ulikuwa juu yangu, naye alifungua kinywa changu kabla ya mtu yule aliyenijia asubuhi hajafika. Basi kinywa changu kilifunguliwa na sikuweza tena kunyamaza. Ndipo neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, watu wanaoishi katika magofu hayo katika nchi ya Israeli wanasema hivi, ‘Abrahamu alikuwa mtu mmoja tu, hata hivyo akaimiliki nchi. Lakini sisi ni wengi, hakika tumepewa nchi kuwa milki yetu.’ Kwa hiyo waambie, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Kwa kuwa mnakula nyama pamoja na damu na kuinulia sanamu zenu macho na kumwaga damu, je, mtaimiliki nchi? Mnategemea panga zenu, mnafanya mambo ya machukizo na kila mmoja wenu humtia unajisi mke wa jirani yake. Je, mtaimiliki nchi?’ “Waambie hivi: ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Hakika kama niishivyo, wale waliobaki katika magofu wataanguka kwa upanga, wale walio nje mashambani nitawatoa wararuliwe na wanyama pori, nao wale walio katika ngome na kwenye mapango watakufa kwa tauni. Nitaifanya nchi kuwa ukiwa na utupu na kiburi cha nguvu zake zitafikia mwisho, nayo milima ya Israeli itakuwa ukiwa ili mtu yeyote asipite huko. Kisha watajua kuwa Mimi ndimi BWANA, nitakapokuwa nimeifanya nchi kuwa ukiwa na utupu kwa sababu ya mambo yote ya machukizo waliyotenda.’ “Kwa habari yako wewe, mwanadamu, watu wako wanaongea habari zako wakiwa karibu na kuta na kwenye milango ya nyumba, wakiambiana kila mmoja na mwenzake, ‘Njooni msikie ujumbe ule utokao kwa BWANA.’ Watu wangu wanakujia, kama wafanyavyo, nao wanaketi mbele yako kama watu wangu na kusikiliza maneno yako, lakini hawayatendi. Kwa maana udanganyifu u katika midomo yao, lakini mioyo yao ina tamaa ya faida isiyo halali. Naam, mbele yao umekuwa tu kama yeye aimbaye nyimbo za mapenzi kwa sauti nzuri za kuvutia na kupiga vyombo kwa ustadi, kwa kuwa wanasikia maneno yako lakini hawayatendi. “Wakati mambo haya yote yatakapotimia, kwa kuwa hakika yatatokea, ndipo watakapojua kwamba nabii amekuwepo miongoni mwao.”

Ezekieli 33:21-33 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa, katika mwaka wa kumi na mbili wa kuhamishwa kwetu, mwezi wa kumi, siku ya tano ya mwezi, mtu mmoja aliyekuwa ametoroka toka Yerusalemu akanijia, akisema, Mji umetekwa. Basi mkono wa Bwana umekuwa juu yangu wakati wa jioni, kabla hajafika yeye aliyetoroka; naye alikuwa amenifumbua kinywa changu, hata aliponijia wakati wa asubuhi; na kinywa changu kilikuwa wazi, wala sikuwa bubu tena. Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, watu wale wakaao mahali palipoharibika katika nchi ya Israeli husema ya kwamba, Abrahamu alikuwa mmoja, akairithi nchi hii; lakini sisi tu watu wengi; tumepewa nchi hii iwe urithi wetu. Basi, waambie, Bwana MUNGU asema hivi; Mnakula nyama pamoja na damu yake, na kuviinulia vinyago vyenu macho yenu, na kumwaga damu; je, mtaimiliki nchi hii? Mnategemea upanga wenu, mnatenda machukizo, kila mmoja wenu anamnajisi mke wa jirani yake; je! Mtaimiliki nchi hii? Hivi ndivyo utakavyowaambia, Bwana MUNGU asema hivi; Kama mimi niishivyo, hakika watu wale wakaao mahali palipoharibika wataanguka kwa upanga, naye mtu aliye katika uwanda, nitamtoa na kuwapa wanyama wakali, ili aliwe; na hao walio ndani ya ngome na mapango watakufa kwa tauni. Nami nitaifanya nchi kuwa ukiwa na ajabu, na kiburi cha uwezo wake kitakoma; nayo milima ya Israeli itakuwa ukiwa, asipite mtu. Ndipo watakapojua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapoifanya nchi kuwa ukiwa na ajabu, kwa sababu ya machukizo yao yote waliyoyatenda. Nawe, mwanadamu, wana wa watu wako husimulia habari zako karibu na kuta, na ndani ya milango ya nyumba zao, na kuambiana, kila mtu na ndugu yake, wakisema, Haya! Twende tukasikie ni neno gani hilo litokalo kwa BWANA. Nao huja kwako kama watu wajavyo, nao hukaa mbele yako kama watu wangu, nao husikia maneno yako, wasiyatende; maana kwa vinywa vyao hujifanya kuwa wenye upendo mwingi, lakini mioyo yao inatafuta faida yao. Na tazama, wewe umekuwa kwao kama wimbo mzuri sana, wa mtu mwenye sauti ipendezayo, awezaye kupiga kinanda vizuri; maana, wasikia maneno yako, lakini hawayatendi. Na hayo yatakapokuwapo (tazama, yanakuja), ndipo watakapojua ya kuwa nabii amekuwapo kati yao.

Ezekieli 33:21-33 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa, katika mwaka wa kumi na mbili wa kuhamishwa kwetu, mwezi wa kumi, siku ya tano ya mwezi, mtu mmoja aliyekuwa ametoroka toka Yerusalemu akanijia, akisema, Mji umepigwa. Basi mkono wa Bwana umekuwa juu yangu wakati wa jioni, kabla hajafika yeye aliyetoroka; naye alikuwa amenifumbua kinywa changu, hata aliponijia wakati wa asubuhi; na kinywa changu kilikuwa wazi, wala sikuwa bubu tena. Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, watu wale wakaao mahali palipoharibika katika nchi ya Israeli husema ya kwamba, Ibrahimu alikuwa mmoja, akairithi nchi hii; lakini sisi tu watu wengi; tumepewa nchi hii iwe urithi wetu. Basi, waambie, Bwana MUNGU asema hivi; Mnakula nyama pamoja na damu yake, na kuviinulia vinyago vyenu macho yenu, na kumwaga damu; je, mtaimiliki nchi hii? Mnategemea upanga wenu, mnatenda machukizo, mnanajisi kila mtu mke wa jirani yake; je! Mtaimiliki nchi hii? Hivi ndivyo utakavyowaambia, Bwana MUNGU asema hivi; Kama mimi niishivyo, hakika watu wale wakaao mahali palipoharibika wataanguka kwa upanga, naye mtu aliye katika uwanda, nitamtoa na kuwapa wanyama wakali, ili aliwe; na hao walio ndani ya ngome na mapango watakufa kwa tauni. Nami nitaifanya nchi kuwa ukiwa na ajabu, na kiburi cha uwezo wake kitakoma; nayo milima ya Israeli itakuwa ukiwa, asipite mtu. Ndipo watakapojua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapoifanya nchi kuwa ukiwa na ajabu, kwa sababu ya machukizo yao yote waliyoyatenda. Nawe, mwanadamu, wana wa watu wako husimulia habari zako karibu na kuta, na ndani ya milango ya nyumba zao, na kuambiana, kila mtu na ndugu yake, wakisema, Haya! Twende tukasikie ni neno gani hilo litokalo kwa BWANA. Nao huja kwako kama watu wajavyo, nao hukaa mbele yako kama watu wangu, nao husikia maneno yako, wasiyatende; maana kwa vinywa vyao hujifanya kuwa wenye upendo mwingi, lakini mioyo yao inatafuta faida yao. Na tazama, wewe umekuwa kwao kama wimbo mzuri sana, wa mtu mwenye sauti ipendezayo, awezaye kupiga kinanda vizuri; maana, wasikia maneno yako, lakini hawayatendi. Na hayo yatakapokuwapo (tazama, yanakuja), ndipo watakapojua ya kuwa nabii amekuwapo kati yao.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha