Ezekieli 22:23-30
Ezekieli 22:23-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, uiambie nchi, Wewe u nchi isiyosafika, wala kunyeshewa mvua siku ya ghadhabu. Fitina ya manabii wake imo ndani yake, kama simba angurumaye akirarua mawindo; wamekula roho za watu; hutwaa kwa nguvu hazina na vitu vya thamani; wameongeza hesabu ya wajane wake ndani yake. Makuhani wake wameihalifu sheria yangu, wametia unajisi vitu vyangu vitakatifu; hawakuweka tofauti ya vitu vitakatifu na vitu vya kutumiwa sikuzote; wala hawakuwafundisha watu kupambanua vitu vichafu na vitu vilivyo safi, nao wamefumba macho yao, wasiziangalie sabato zangu, nami nimetiwa unajisi kati yao. Wakuu wake kati yake wamekuwa kama mbwa-mwitu wakirarua mawindo; ili kumwaga damu, na kuharibu roho za watu, wapate faida kwa njia isiyo halali. Na manabii wake wamewapakia chokaa isiyokorogwa vema, wakiona ubatili, na kuwatabiria maneno ya uongo, wakisema, Bwana MUNGU asema hivi; iwapo BWANA hakusema neno. Watu wa nchi wametumia udhalimu, wamenyang’anya kwa nguvu; naam, wamewatenda jeuri maskini na wahitaji, nao wamewaonea wageni bila haki. Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu.
Ezekieli 22:23-30 Biblia Habari Njema (BHN)
Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Waambie Waisraeli kwamba nchi yao ni kama nchi ambayo haijanyeshewa mvua, imenyauka kwa sababu ya ghadhabu yangu ikawa kama ardhi bila maji. Wakuu wenu ni kama simba anayenguruma araruapo mawindo yake. Wanaua watu, wanawanyanganya watu mali na johari, na kuongeza idadi ya wajane. Makuhani wao wanavunja sheria zangu, na kukufuru vyombo vyangu vitakatifu. Hawapambanui kati ya vitu vitakatifu na vitu visivyo vitakatifu, wala hawawafundishi watu tofauti kati ya mambo yaliyo najisi na yaliyo safi. Wameacha kuzishika sabato zangu, na kunifanya nidharauliwe kati yao. Viongozi wake waliomo mjini ni kama mbwamwitu wararuao mawindo yao; wanaua ili kujitajirisha visivyo halali. Manabii wake wanaficha maovu hayo kama mtu anapotia chokaa kwenye ukuta mbovu. Wanaona maono ya uongo na kutabiri udanganyifu mtupu, wakisema, ‘Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi,’ wakati mimi mwenyewe sijawaambia chochote. Kila mahali nchini ni dhuluma na unyanganyi. Wanawadhulumu maskini na wanyonge, na kuwaonea wageni bila kujali. Nilitafuta miongoni mwao mtu mmoja atengeneze ukuta na kusimama juu ya mahali palipobomoka mbele yangu, ili ailinde nchi na kunizuia nisiiharibu, lakini sikumpata hata mmoja.
Ezekieli 22:23-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, uiambie nchi, Wewe u nchi isiyotakasika, wala kunyeshewa mvua siku ya ghadhabu. Fitina ya manabii wake imo ndani yake, kama simba angurumaye akirarua mawindo; wamekula roho za watu; hutwaa kwa nguvu hazina na vitu vya thamani; wameongeza idadi ya wajane wake ndani yake. Makuhani wake wameivunja sheria yangu, wametia unajisi vitu vyangu vitakatifu; hawakuweka tofauti ya vitu vitakatifu na vitu vya kutumiwa sikuzote; wala hawakuwafundisha watu kupambanua vitu vichafu na vitu vilivyo safi, nao wamefumba macho yao, wasiziangalie sabato zangu, nami nimetiwa unajisi kati yao. Wakuu wake kati yake wamekuwa kama mbwamwitu wakirarua mawindo; ili kumwaga damu, na kuharibu roho za watu, wapate faida kwa njia isiyo halali. Na manabii wake wamewapakia chokaa isiyokorogwa vema, wakiwa na maono ya udanganyifu, na kuwatabiria maneno ya uongo, wakisema, Bwana MUNGU asema hivi; iwapo BWANA hakusema neno. Watu wa nchi wametumia udhalimu, wamenyang'anya kwa nguvu; naam, wamewatenda jeuri maskini na wahitaji, nao wamewaonea wageni bila haki. Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu.
Ezekieli 22:23-30 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Neno la BWANA likanijia tena kusema: “Mwanadamu, iambie nchi, ‘Wewe ni nchi ambayo haijapata mvua wala manyunyu katika siku ya ghadhabu.’ Kuna hila mbaya ya wakuu ndani yake kama simba angurumaye akirarua mawindo yake, wanakula watu, wanachukua hazina na vitu vya thamani na kuongeza idadi ya wajane ndani yake. Makuhani wake wameihalifu sheria yangu na kunajisi vitu vyangu vitakatifu, hawatofautishi kati ya vitu vitakatifu na vitu vya kawaida. Wanafundisha kuwa hakuna tofauti kati ya vitu vilivyo najisi na visivyo najisi, nao wanafumba macho yao katika kutunza Sabato zangu, hivyo katikati yao nimetiwa unajisi. Maafisa wake walioko ndani yake ni kama mbwa mwitu wararuao mawindo yao, wanamwaga damu na kuua watu ili kupata faida ya udhalimu. Manabii wake wanapaka chokaa matendo haya kwa maono ya uongo na utabiri wa udanganyifu. Wanasema, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo,’ wakati BWANA hajasema. Watu wa nchi wanatoza kwa nguvu na kufanya unyangʼanyi, wanawatenda jeuri maskini na wahitaji na kuwaonea wageni, wakiwanyima haki. “Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, ambaye angejenga ukuta na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka kwa ajili ya watu wa nchi ili nisije nikaiangamiza, lakini sikumwona mtu yeyote.