Ezekieli 13:17-23
Ezekieli 13:17-23 Biblia Habari Njema (BHN)
“Na sasa, ewe mtu, wageukie wanawake wa taifa lako ambao wanatabiri mambo ambayo wameyawaza wao wenyewe. Tamka unabii dhidi yao na kuwaambia kuwa Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: Ole wenu wanawake mnaoshona tepe za hirizi za kuvaa mikononi mwa kila mtu na kutengeneza shela zenye hirizi za kila kimo ili kuyawinda maisha ya watu. Je, mnapowinda maisha ya watu wangu mnadhani mtasalimisha maisha yenu wenyewe? Mmenikufuru mbele ya watu wangu ili kupata konzi za shayiri na chakula kidogo. Mnawaua watu wasiostahili kufa na kuwaacha hai wanaostahili kuuawa, kwa uongo wenu mnaowaambia watu wangu, nao wanawaamini. “Basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Nitashambulia hirizi zenu mnazowafunga nazo watu; nitazipasuapasua kutoka mikononi mwenu na kuwaacha huru hao mnaowawinda kama ndege. Nitazirarua shela zenu na kuwaokoa watu wangu mikononi mwenu; nao hawatakuwa tena mawindo mikononi mwenu. Ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. Kwa kuwa mmewavunja moyo watu waadilifu kwa kusema uongo, hali mimi sikuwavunja moyo, mkawaimarisha waovu wasiache mienendo yao mibaya na kuokoa maisha yao, basi, nyinyi hamtaona tena maono madanganyifu, wala hamtatabiri tena. Nitawaokoa watu wangu mikononi mwenu. Hapo mtatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”
Ezekieli 13:17-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na wewe, mwanadamu, kaza uso wako juu ya binti za watu wako, watabirio kwa akili zao wenyewe; ukatabiri juu yao, useme, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wanawake wale, washonao hirizi katika viungo vyote vya mikono, wawekao leso juu ya vichwa vya kila kimo, ili wawinde roho za watu; je! Mtaziwinda roho za watu wangu, na kuzihifadhi hai roho zenu wenyewe? Nanyi mmeninajisi kati ya watu wangu, kwa ajili ya makonzi ya shayiri na vipande vya mkate, ili kuziua roho za watu ambao haiwapasi kufa, na kuzihifadhi hai roho za watu ambao haikuwapasa kuwa hai, kwa kuwaambia uongo watu wangu wasikilizao uongo. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi nazipinga hirizi zenu, ambazo kwa hizo mnaziwinda roho za watu kama ndege, nami nitazitoa katika mikono yenu kwa nguvu; nami nitaziachilia roho zile mnazoziwinda kama ndege. Na leso zenu nazo nitazirarua, na kuwaokoa watu wangu katika mikono yenu, wala hawatakuwa katika mikono yenu tena kuwindwa; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Kwa kuwa ninyi mmemhuzunisha moyo mwenye haki kwa uongo, ambaye mimi sikumhuzunisha; na kuitia nguvu mikono ya mtu mbaya, hata asigeuke, na kuiacha njia yake mbaya, na kuhifadhika; basi, kwa sababu hiyo ninyi hamtaona tena ubatili, wala kutabiri mambo; nami nitawaokoa watu wangu katika mikono yenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
Ezekieli 13:17-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na wewe, mwanadamu, kaza uso wako juu ya binti za watu wako, watabirio kwa akili zao wenyewe; ukatabiri juu yao, useme, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wanawake wale, washonao hirizi katika viungo vyote vya mikono, wawekao leso juu ya vichwa vya kila kimo, ili wawinde roho za watu; je! Mtaziwinda roho za watu wangu, na kuzihifadhi hai roho zenu wenyewe? Nanyi mmeninajisi kati ya watu wangu, kwa ajili ya makonzi ya shayiri na vipande vya mkate, ili kuziua roho za watu ambao haiwapasi kufa, na kuzihifadhi hai roho za watu ambao haikuwapasa kuwa hai, kwa kuwaambia uongo watu wangu wasikilizao uongo. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni kinyume cha hirizi zenu, ambazo kwa hizo mnaziwinda roho za watu kama ndege, nami nitazitoa katika mikono yenu kwa nguvu; nami nitaziachilia roho zile mnazoziwinda kama ndege. Na leso zenu nazo nitazirarua, na kuwaokoa watu wangu katika mikono yenu, wala hawatakuwa katika mikono yenu tena kuwindwa; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Kwa kuwa ninyi mmemhuzunisha moyo mwenye haki kwa uongo, ambaye mimi sikumhuzunisha; na kuitia nguvu mikono ya mtu mbaya, hata asigeuke, na kuiacha njia yake mbaya, na kuhifadhika; basi, kwa sababu hiyo ninyi hamtaona tena ubatili, wala kutabiri mambo; nami nitawaokoa watu wangu katika mikono yenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
Ezekieli 13:17-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Sasa, mwanadamu, kaza uso wako dhidi ya binti za watu wako wanaotabiri mambo kutoka mawazo yao wenyewe. Tabiri dhidi yao na useme, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Ole wao wanawake washonao hirizi za uchawi juu ya viwiko vyao vyote na kutengeneza shela za urefu wa aina mbalimbali kwa ajili ya kufunika vichwa vyao kwa makusudi ya kuwanasa watu. Je, mtatega uhai wa watu wangu lakini ninyi mponye wa kwenu? Ninyi mmeninajisi miongoni mwa watu wangu kwa ajili ya konzi chache za shayiri na chembe za mkate. Kwa kuwaambia uongo watu wangu, wale ambao husikiliza uongo, mmewaua wale watu ambao wasingekufa na kuwaacha hai wale ambao wasingeishi. “ ‘Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Mimi niko kinyume na hizo hirizi zenu za uchawi ambazo kwa hizo mnawatega watu kama ndege, nami nitazirarua kutoka mikononi mwenu, nitawaweka huru watu wale mliowatega kama ndege. Nitazirarua shela zenu na kuwaokoa watu wangu kutoka mikononi mwenu, nao hawatakuwa tena mawindo ya nguvu zenu. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA. Kwa sababu mliwavunja moyo wenye haki kwa uongo wenu, wakati mimi sikuwaletea huzuni na kwa kuwa mliwatia moyo waovu ili wasiziache njia zao mbaya na hivyo kuokoa maisha yao, kwa hiyo hamtaona tena maono ya uongo wala kufanya ubashiri. Nitawaokoa watu wangu kutoka mikononi mwenu. Nanyi ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA.’ ”