Ezekieli 12:1-16
Ezekieli 12:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Wewe mtu! Wewe unakaa kati ya watu waasi. Wana macho lakini hawaoni; wana masikio lakini hawasikii. Wao ni watu waasi. Basi, ewe mtu, fanya kama vile unakwenda uhamishoni: Ondoka wakiwa wanakuona, ukimbilie mahali pengine. Nenda kama mkimbizi kutoka mahali ulipo mpaka mahali pengine wao wakikuona. Labda wataelewa, ingawa wao ni waasi. Hakikisha wanaona unachofanya. Funga mzigo wako uutoe nje na kuwa tayari kuondoka jioni kama wafanyavyo watu wanaokwenda uhamishoni. Wakiwa wanakuangalia toboa ukuta wa nyumba, upitie hapo na kwenda nje. Wakiwa wanakuona, jitwike mabegani mzigo wako na kuondoka wakati wa giza. Funika uso wako usiweze kuona unakwenda wapi. Ndivyo ninavyokufanya uwe ishara kwa Waisraeli.” Basi, nikafanya kama nilivyoamriwa. Siku hiyo, wakati wa mchana, nikafunga mzigo wangu kama mzigo wa mtu anayekimbia. Jioni nikautoboa ukuta na giza lilipokuwa likiingia, nikatoka, nimejitwika mzigo wangu mabegani, watu wote wakiniona. Kesho yake asubuhi, Mwenyezi-Mungu akaniuliza: “Wewe mtu! Je, hao waasi wa Israeli hawajakuuliza maana ya hicho ulichofanya? Waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Kauli hii yangu yahusu mambo yatakayompata mtawala wa Yerusalemu na watu wote wa Israeli wanaoishi humo. Waambie kuwa wewe ni ishara kwao; kama ulivyofanya ndivyo itakavyotendeka kwao: Watakwenda uhamishoni; naam, watachukuliwa mateka. Naye mtawala wao atajitwika mzigo wake mabegani wakati wa usiku, atatoka kupitia ukuta atakaotoboa apate kutoka; atafunika uso wake ili asiione nchi kwa macho yake. Lakini nitatandaza wavu wangu juu yake, naye atanaswa katika mtego wangu. Nitampeleka Babuloni, nchi ya Wakaldayo; naye akiwa huko atakufa bila kuiona hiyo nchi. Wafuasi wake wote, washauri wake na vikosi vyake vyote, nitawatawanya nje kila upande. Nitauchomoa upanga na kuwafuatilia nyuma. Nitakapowatawanya kati ya mataifa mengine na nchi za mbali, ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. Lakini nitawaacha wachache waokoke vitani, wanusurike njaa na maradhi mabaya; ili hao waweze kuwasimulia watu wa mataifa wanamoishi jinsi walivyotenda mabaya. Ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”
Ezekieli 12:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Neno la BWANA likanijia tena, kusema, Mwanadamu, wewe unakaa kati ya nyumba iliyoasi, watu ambao wana macho ya kuona, ila hawaoni, wana masikio ya kusikia, ila hawasikii; kwa maana ni nyumba iliyoasi. Basi, mwanadamu, funga tayari vyombo kwa uhamisho, ukahame wakati wa mchana mbele ya macho yao; nawe utahama toka mahali pako hapa mpaka mahali pengine mbele ya macho yao; labda watafahamu, wajapokuwa ni nyumba iliyoasi. Nawe utatoa vyombo vyako, wakati wa mchana, mbele ya macho yao, kana kwamba ni vyombo vya kuhamishwa; nawe mwenyewe utatoka, wakati wa jioni, mbele ya macho yao, kama watu watokavyo katika kuhamishwa. Toboa mahali ukutani mbele ya macho yao, ukachukue vitu kwa kuvipitisha pale. Mbele ya macho yao utajitwika begani pako, na kuvichukua nje gizani; utafunika uso wako, hata usiione nchi; kwa maana nimekuweka uwe ishara kwa nyumba ya Israeli. Nikafanya vile vile kama nilivyoamriwa; nilitoa vyombo vyangu wakati wa mchana kana kwamba ni vyombo vya kuhamishwa, na wakati wa jioni nikautoboa ukuta kwa mkono wangu; nikavitoa gizani, nikavichukua begani, mbele ya macho yao. Asubuhi neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, nyumba ya Israeli, je! Nyumba ile iliyoasi, hawakukuambia, Unafanya nini wewe? Waambie, Bwana MUNGU asema hivi; Ufunuo huu wamhusu mkuu wa Yerusalemu, na nyumba yote ya Israeli walio kati yao. Sema, Mimi ni ishara kwenu; kama mimi nilivyotenda, wao nao watatendwa vile vile; watahamishwa, watakwenda kufungwa. Naye mkuu aliye kati yao atachukua begani katika giza; naye atatoka kwenda zake; watatoboa mahali ukutani, wapate kuvichukua vyombo vyao nje; atafunika uso wake, kwa sababu hataiona nchi kwa macho yake. Tena wavu wangu nitautandika juu yake, naye atanaswa kwa mtego wangu; nami nitampeleka Babeli, mpaka nchi ya Wakaldayo; lakini hataiona, ingawa atakufa huko. Nami nitawatawanya kwa pepo zote wote wamzungukao ili wamsaidie, na vikosi vyake vyote; nami nitaufuta upanga nyuma yao. Nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA; nitakapowatawanya kati ya mataifa, na kuwatapanya katika nchi zote. Lakini nitawasaza watu wachache miongoni mwao na kuwaokoa na upanga, na njaa, na tauni ili watangaze habari ya machukizo yao yote, kati ya mataifa huko waendako; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
Ezekieli 12:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Neno la BWANA likanijia tena, kusema, Mwanadamu, wewe unakaa kati ya nyumba iliyoasi, watu ambao wana macho ya kuona, ila hawaoni, wana masikio ya kusikia, ila hawasikii; kwa maana ni nyumba iliyoasi. Basi, mwanadamu, funga tayari vyombo kwa uhamisho, ukahame wakati wa mchana mbele ya macho yao; nawe utahama toka mahali pako hapa mpaka mahali pengine mbele ya macho yao; labda watafahamu, wajapokuwa ni nyumba iliyoasi. Nawe utatoa vyombo vyako, wakati wa mchana, mbele ya macho yao, kana kwamba ni vyombo vya kuhamishwa; nawe mwenyewe utatoka, wakati wa jioni, mbele ya macho yao, kama watu watokavyo katika kuhamishwa. Toboa mahali ukutani mbele ya macho yao, ukachukue vitu kwa kuvipitisha pale. Mbele ya macho yao utajitwika begani pako, na kuvichukua nje gizani; utafunika uso wako, hata usiione nchi; kwa maana nimekuweka uwe ishara kwa nyumba ya Israeli. Nikafanya vile vile kama nilivyoamriwa; nalitoa vyombo vyangu wakati wa mchana kana kwamba ni vyombo vya kuhamishwa, na wakati wa jioni nikautoboa ukuta kwa mkono wangu; nikavitoa gizani, nikavichukua begani, mbele ya macho yao. Asubuhi neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, nyumba ya Israeli, je! Nyumba ile iliyoasi, hawakukuambia, Unafanya nini wewe? Waambie, Bwana MUNGU asema hivi; Ufunuo huu wamhusu mkuu wa Yerusalemu, na nyumba yote ya Israeli walio kati yao. Sema, Mimi ni ishara kwenu; kama mimi nilivyotenda, wao nao watatendwa vile vile; watahamishwa, watakwenda kufungwa. Naye mkuu aliye kati yao atachukua begani katika giza; naye atatoka kwenda zake; watatoboa mahali ukutani, wapate kuvichukua vyombo vyao nje; atafunika uso wake, kwa sababu hataiona nchi kwa macho yake. Tena wavu wangu nitautandika juu yake, naye atanaswa kwa mtego wangu; nami nitampeleka Babeli, mpaka nchi ya Wakaldayo; lakini hataiona, angawa atakufa huko. Nami nitawatawanya kwa pepo zote wote wamzungukao ili wamsaidie, na vikosi vyake vyote; nami nitaufuta upanga nyuma yao. Nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA; nitakapowatawanya kati ya mataifa, na kuwatupa-tupa katika nchi zote. Lakini nitawasaza watu wachache miongoni mwao na kuwaokoa na upanga, na njaa, na tauni ili watangaze habari ya machukizo yao yote, kati ya mataifa huko waendako; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
Ezekieli 12:1-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, unaishi miongoni mwa watu waasi. Wana macho ya kuona, lakini hawaoni na masikio ya kusikia lakini hawasikii, kwa kuwa ni watu waasi. “Kwa hiyo, mwanadamu, funga mizigo yako kwa kwenda uhamishoni tena wakati wa mchana, wakiwa wanakutazama, toka nje na uende mahali pengine kutoka hapo ulipo. Labda wataelewa, ingawa wao ni nyumba ya kuasi. Wakati wa mchana, wakiwa wanakutazama, toa nje mizigo yako iliyofungwa kwa ajili ya kwenda uhamishoni. Kisha wakati wa jioni, wakiwa wanakutazama toka nje kama wale waendao uhamishoni. Wakiwa wanakutazama, toboa ukuta utolee mizigo yako hapo. Beba mizigo hiyo begani mwako wakikuangalia uichukue nje wakati wa giza la jioni. Funika uso wako ili usione nchi, kwa maana nimekufanya ishara kwa nyumba ya Israeli.” Basi nikafanya kama nilivyoamriwa. Wakati wa mchana nilitoa vitu vyangu nje vilivyofungwa tayari kwa uhamishoni. Kisha wakati wa jioni nikatoboa ukuta kwa mikono yangu. Nikachukua mizigo yangu nje wakati wa giza la jioni, nikiwa nimeibeba mabegani mwangu huku wakinitazama. Asubuhi neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, je, nyumba ile ya kuasi ya Israeli haikukuuliza, ‘Unafanya nini?’ “Waambie, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Neno hili linamhusu mkuu aliye katika Yerusalemu na nyumba yote ya Israeli ambao wako huko.’ Waambie, ‘Mimi ndiye ishara kwenu.’ “Kama vile nilivyotenda, basi litatendeka vivyo hivyo kwao. Watakwenda uhamishoni kama mateka. “Naye mkuu aliye miongoni mwao atabeba mizigo yake begani mwake kwenye giza la jioni na kuondoka na tundu litatobolewa ukutani kwa ajili yake ili kupitia hapo. Atafunika uso wake ili kwamba asiweze kuiona nchi. Nitatandaza wavu wangu kwa ajili yake, naye atanaswa kwenye mtego wangu, nitamleta mpaka Babeli, nchi ya Wakaldayo, lakini hataiona, naye atafia huko. Wote wanaomzunguka nitawatawanya pande zote, watumishi wake na majeshi yake yote, nami nitawafuatilia kwa upanga uliofutwa. “Wao watajua kwamba Mimi ndimi BWANA, nitakapowatawanya miongoni mwa mataifa na kuwafukuza huku na huko katika nchi zote. Lakini nitawaacha wachache wao waokoke na upanga, njaa na tauni, ili kwamba katika mataifa watakakokwenda waweze kutambua matendo ya machukizo waliotenda. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi BWANA.”