Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 9:13-26

Kutoka 9:13-26 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kesho, amka alfajiri na mapema umwendee Farao, umwambie kwamba mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Waebrania, nasema hivi, ‘Waache watu wangu waondoke ili wakanitumikie. Maana safari hii, wewe mwenyewe, maofisa wako na watu wako mtakumbana na mapigo yangu makali. Nawe utatambua kwamba hakuna yeyote duniani aliye kama mimi. Ningalikwisha kukuangamiza tayari wewe na watu wako kwa maradhi mabaya, nanyi mngalikuwa mmekwisha angamia. Lakini nimewaacheni muishi ili kudhihirisha uwezo wangu. Kwa hiyo dunia yote itatambua kuwa mimi ni nani. Lakini bado unaonesha kiburi dhidi ya watu wangu, wala huwaachi waondoke. Kwa hiyo kesho, wakati kama huu, nitaleta mvua kubwa ya mawe ambayo haijawahi kutokea nchini Misri, tangu mwanzo wake hadi leo. Kwa hiyo agiza mifugo yako na chochote kilicho huko mashambani viwekwe mahali salama; kwa maana mvua ya mawe itamnyeshea kila mtu na mnyama aliye shambani na ambaye hayuko nyumbani; wote watakufa.’” Baadhi ya maofisa wa Farao waliyatia maanani maneno hayo ya Mwenyezi-Mungu, wakawapeleka watumwa na wanyama wao nyumbani mahali pa usalama. Lakini yule ambaye hakulijali neno la Mwenyezi-Mungu aliwaacha watumwa wake na wanyama wake mashambani. Kisha, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu mbinguni, ili mvua ya mawe inyeshe kila mahali nchini Misri. Imnyeshee mtu, mnyama na kila mmea shambani.” Basi, Mose alinyosha fimbo yake kuelekea mbinguni. Naye Mwenyezi-Mungu akaleta mvua ya mawe na ngurumo; umeme ukaipiga nchi. Mwenyezi-Mungu alinyesha mvua ya mawe nchini Misri, mvua kubwa ya mawe iliyoandamana na mfululizo wa umeme, ambayo hakuna mwananchi yeyote wa Misri aliyepata kamwe kushuhudia kabla. Mvua hiyo ya mawe ilivunjavunja kila kitu katika mashamba na kila mahali nchini Misri: Wanyama na watu. Mawe ya mvua yakavunjavunja mimea yote na miti mashambani. Jambo hilo lilifanyika kote nchini Misri isipokuwa tu sehemu ya Gosheni walimokaa Waisraeli; humo haikuwako mvua ya mawe.

Shirikisha
Soma Kutoka 9

Kutoka 9:13-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)

BWANA akamwambia Musa, Ondoka asubuhi na mapema, ukasimame mbele ya Farao, umwambie, BWANA, Mungu wa Waebrania, asema, Wape watu wangu ruhusa waende ili wanitumikie. Kwani wakati huu nitaleta mapigo yangu yote juu ya moyo wako, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako; ili upate kujua ya kuwa hapana mmoja mfano wa mimi ulimwenguni kote. Kwa kuwa wakati huu ningekwisha kuunyosha mkono wangu, na kukupiga wewe na watu wako, kwa tauni, nawe ungekatiliwa mbali na kuondolewa katika nchi; lakini, nilikusimamisha wewe kwa sababu ii hii, ili nikuoneshe uweza wangu, tena kwamba jina langu litangazwe katika dunia yote. Nawe, je! Hata sasa wajitukuza juu ya watu wangu, usiwape ruhusa waende zao? Tazama, kesho wakati kama huu, nitanyesha mvua ya mawe nzito sana, ambayo mfano wake haujakuwa huko Misri tangu siku ile ilipoanza kuwa hata hivi sasa. Basi sasa tuma watu wahimize kuingiza ndani mifugo yako na hayo yote uliyo nayo mashambani; kwani kila mtu na kila mnyama apatikanaye mashambani, wasioletwa nyumbani, hiyo mvua ya mawe itanyesha juu yao, nao watakufa. Yeye aliyelicha neno la BWANA miongoni mwa watumishi wa Farao aliwakimbiza watumishi wake na wanyama wake waingie nyumbani; na yeye asiyelitia moyoni neno la BWANA akawaacha watumishi wake na wanyama wake mashambani. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako kuelekea mbinguni, ili iwe mvua ya mawe katika nchi yote ya Misri, juu ya wanadamu na juu ya wanyama, na juu ya mboga zote za mashamba, katika nchi yote ya Misri. Musa akaunyosha mkono wake kuelekea mbinguni; na BWANA akaleta ngurumo na mvua ya mawe, na moto ukashuka juu ya nchi; BWANA akanyesha mvua ya mawe juu ya nchi yote ya Misri. Basi palikuwa na mvua ya mawe, na moto uliochanganyikana na ile mvua ya mawe, nzito sana, ambayo mfano wake haukuwapo katika nchi yote ya Misri tangu ilipoanza kuwa taifa. Na ile mvua ya mawe ikapiga kila kilichokuwako mashambani, binadamu na mnyama, katika nchi yote ya Misri; hiyo mvua ya mawe ikapiga kila mmea wa mashambani, na kuuvunja kila mti wa mashamba. Katika nchi ya Gosheni peke yake, walikokaa wana wa Israeli, haikuwako mvua ya mawe.

Shirikisha
Soma Kutoka 9

Kutoka 9:13-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

BWANA akamwambia Musa, Ondoka asubuhi na mapema, ukasimame mbele ya Farao, umwambie, BWANA, Mungu wa Waebrania, asema, Wape watu wangu ruhusa waende ili wanitumikie. Kwani wakati huu nitaleta mapigo yangu yote juu ya moyo wako, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako; ili upate kujua ya kuwa hapana mmoja mfano wa mimi ulimwenguni mwote. Kwa kuwa wakati huu ningekwisha kuunyosha mkono wangu, na kukupiga wewe na watu wako, kwa tauni, nawe ungekatiliwa mbali na kuondolewa katika nchi; lakini, nilikusimamisha wewe kwa sababu hii hii, ili nikuonyeshe uweza wangu, tena kwamba jina langu litangazwe katika dunia yote. Nawe, je! Hata sasa wajitukuza juu ya watu wangu, usiwape ruhusa waende zao? Tazama, kesho wakati kama huu, nitanyesha mvua ya mawe nzito sana, ambayo mfano wake haujakuwa huko Misri tangu siku ile ilipoanza kuwa hata hivi sasa. Basi sasa tuma wahimize waingie ndani wanyama wako na hayo yote uliyo nayo mashambani; kwani kila mtu na kila mnyama apatikanaye mashambani, wasioletwa nyumbani, hiyo mvua ya mawe itanyesha juu yao, nao watakufa. Yeye aliyelicha neno la BWANA miongoni mwa watumishi wa Farao aliwakimbiza watumishi wake na wanyama wake waingie nyumbani; na yeye asiyelitia moyoni neno la BWANA akawaacha watumishi wake na wanyama wake mashambani. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako kuelekea mbinguni, ili iwe mvua ya mawe katika nchi yote ya Misri, juu ya wanadamu na juu ya wanyama, na juu ya mboga zote za mashamba, katika nchi yote ya Misri. Musa akaunyosha mkono wake kuelekea mbinguni; na BWANA akaleta ngurumo na mvua ya mawe, na moto ukashuka juu ya nchi; BWANA akanyesha mvua ya mawe juu ya nchi yote ya Misri. Basi palikuwa na mvua ya mawe, na moto uliochanganyikana na ile mvua ya mawe, nzito sana, ambayo mfano wake haukuwapo katika nchi yote ya Misri tangu ilipoanza kuwa taifa. Na ile mvua ya mawe ikapiga kila kilichokuwako mashambani, binadamu na mnyama, katika nchi yote ya Misri; hiyo mvua ya mawe ikapiga kila mmea wa mashambani, na kuuvunja kila mti wa mashamba. Katika nchi ya Gosheni peke yake, walikokaa wana wa Israeli, haikuwako mvua ya mawe.

Shirikisha
Soma Kutoka 9

Kutoka 9:13-26 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kisha BWANA akamwambia Mose, “Amka mapema asubuhi, usimame mbele ya Farao, umwambie, ‘Hili ndilo asemalo BWANA, Mungu wa Waebrania: Waachie watu wangu waende, ili kwamba waweze kuniabudu, au wakati huu nitaleta mapigo yangu yenye nguvu dhidi yako, maafisa wako na watu wako, ili upate kujua kuwa hakuna mwingine kama Mimi katika dunia yote. Kwa kuwa mpaka sasa ningelikuwa nimenyoosha mkono wangu na kukupiga wewe na watu wako kwa pigo ambalo lingekufutilia mbali juu ya nchi. Lakini nimekuinua wewe kwa kusudi hili hasa, ili nipate kukuonyesha uwezo wangu, na ili Jina langu lipate kutangazwa duniani yote. Bado unaendelea kujiinua juu ya watu wangu, wala hutaki kuwaachia waende. Kwa hiyo, kesho wakati kama huu nitaleta mvua mbaya sana ya mawe ambayo haijapata kunyesha katika nchi ya Misri, tangu siku ilipoumbwa mpaka leo. Sasa toa amri urudishe wanyama wote watoke malishoni na chochote ambacho kipo mashambani waje mpaka mahali pa usalama, kwa sababu mvua ya mawe itanyesha juu ya kila mtu na kila mnyama ambaye hajaletwa ndani ambao bado wako nje mashambani, nao watakufa.’ ” Wale maafisa wa Farao ambao waliliogopa neno la BWANA wakafanya haraka kuwaleta watumwa wao na mifugo yao ndani. Lakini wale waliopuuza neno la BWANA wakawaacha watumwa wao na mifugo yao shambani. Ndipo BWANA akamwambia Mose, “Nyoosha mkono wako kuelekea angani ili kwamba mvua ya mawe inyeshe juu ya Misri yote, juu ya watu, wanyama na juu ya kila kitu kiotacho katika mashamba ya Misri.” Mose alipoinyoosha fimbo yake kuelekea angani, BWANA akatuma ngurumo na mvua ya mawe, umeme wa radi ulimulika hadi nchi. Kwa hiyo BWANA akaifanya mvua ya mawe kunyesha juu ya nchi ya Misri, mvua ya mawe ikanyesha na radi ikamulika pote. Ikawa dhoruba ya kutisha ambayo haijakuwako katika nchi ya Misri, tangu nchi hiyo iwe taifa. Mvua ya mawe ikaharibu kila kitu katika nchi ya Misri kilichokuwa katika mashamba, watu na wanyama, ikaharibu kila kitu kinachoota mashambani na kuvunja kila mti. Mahali pekee ambapo mvua ya mawe haikunyesha ni nchi ya Gosheni, ambako Waisraeli waliishi.

Shirikisha
Soma Kutoka 9

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha