Kutoka 40:12-16
Kutoka 40:12-16 Biblia Habari Njema (BHN)
“Utamwita Aroni na wanawe waje mlangoni mwa hema la mkutano, kisha uwatawadhe. Mvike Aroni yale mavazi matakatifu; utampaka mafuta na kumweka wakfu, ili aweze kunitumikia kama kuhani. Waite wanawe na kuwavisha zile kanzu. Kisha uwapake mafuta kama ulivyompaka baba yao, ili nao pia wanitumikie kama makuhani. Kupakwa mafuta huku kutawaingiza katika ukuhani wa kudumu katika vizazi vyao vyote.” Basi, Mose alitekeleza kikamilifu kabisa maagizo yote ya Mwenyezi-Mungu.
Kutoka 40:12-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha utamleta Haruni na wanawe hapo mlangoni pa hema ya kukutania, nawe utawaosha kwa maji. Kisha utamvika Haruni mavazi matakatifu; nawe utamtia mafuta, na kumweka awe mtakatifu, ili apate kunitumikia katika kazi ya ukuhani. Kisha utawaleta wanawe, na kuwavika kanzu zao; nawe utawatia mafuta kama ulivyomtia mafuta baba yao, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani; na huko kutiwa mafuta kwao kutakuwa ni kwa ukuhani wa milele katika vizazi vyao vyote. Musa akafanya hayo yote; kama yote BWANA aliyoagiza ndivyo alivyofanya.
Kutoka 40:12-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Mlete Aroni na wanawe kwenye ingilio la Hema la Kukutania na uwaoshe kwa maji. Kisha mvike Aroni yale mavazi matakatifu, umtie mafuta na kumweka wakfu ili apate kunitumikia katikati ya ukuhani. Walete wanawe na uwavike makoti. Kisha watie mafuta kama ulivyomtia baba yao, ili nao pia wanitumikie katika kazi ya ukuhani. Kutiwa mafuta kwao kutakuwa kwa ajili ya ukuhani utakaoendelea kwa vizazi vyote vijavyo.” Mose akafanya kila kitu sawa kama vile BWANA alivyomwagiza.
Kutoka 40:12-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha utamleta Haruni na wanawe hapo mlangoni pa hema ya kukutania, nawe utawaosha kwa maji. Kisha utamvika Haruni mavazi matakatifu; nawe utamtia mafuta, na kumweka awe mtakatifu, ili apate kunitumikia katika kazi ya ukuhani. Kisha utawaleta wanawe, na kuwavika kanzu zao; nawe utawatia mafuta kama ulivyomtia mafuta baba yao, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani; na huko kutiwa mafuta kwao kutakuwa ni kwa ukuhani wa milele katika vizazi vyao vyote. Musa akafanya hayo yote; kama BWANA aliyoagiza ndivyo alivyofanya yote.