Kutoka 4:1-9
Kutoka 4:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Musa akajibu akasema, Lakini, tazama, hawataniamini, wala hawataisikia sauti yangu; maana watasema, BWANA hakukutokea. BWANA akamwambia, Ni nini hiyo uliyo nayo mkononi mwako? Akasema, Ni fimbo. Akamwambia, Itupe chini; akaitupa chini, nayo ikawa nyoka; Musa akakimbia mbele yake. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako, kamshike mkia; (akaunyosha mkono wake akamshika, naye akageuka kuwa fimbo mkononi mwake;) ili kwamba wapate kusadiki ya kwamba BWANA, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amekutokea. BWANA akamwambia tena, Sasa tia mkono wako kifuani mwako. Akautia mkono wake kifuani mwake; naye alipoutoa, kumbe! Mkono wake ulikuwa una ukoma, umekuwa mweupe kama theluji. Akasema, Tia mkono wako kifuani mwako tena. Akautia mkono wake kifuani mwake tena, na alipoutoa kifuani mwake, kumbe! Umerudia hali ya mwili wake. Basi itakuwa, wasipokusadiki, wala kuisikiliza sauti ya ishara ya kwanza, wataisikiliza sauti ya ishara ya pili. Kisha itakuwa wasipoamini hata ishara hizo mbili, wala kuisikiliza sauti yako, basi, yatwae maji ya mtoni uyamwage juu ya nchi kavu, na yale maji uyatwaayo mtoni yatakuwa damu juu ya nchi kavu.
Kutoka 4:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Mose akamwambia Mungu, “Lakini Waisraeli hawataniamini wala kunisikiliza, bali watasema kuwa wewe Mwenyezi-Mungu hukunitokea.” Hapo Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Unashika nini mkononi mwako?” Mose akamwambia, “Fimbo.” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Itupe chini.” Mose akaitupa fimbo chini, nayo ikageuka kuwa nyoka! Mose akaikimbia. Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako, umkamate mkia!” Mose akanyosha mkono wake, akamkamata; nyoka akageuka tena kuwa fimbo mkononi mwake. Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Hivyo Waisraeli watapata kuamini kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa baba zao, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo, nimekutokea.” Tena, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Ingiza mkono wako kifuani mwako.” Mose akafanya hivyo, lakini alipoutoa nje, kumbe ukawa na ukoma; mweupe kama theluji. Kisha Mungu akamwambia, “Ingiza tena mkono wako kifuani mwako!” Mose akauingiza mkono wake kifuani. Na alipoutoa nje, kumbe ukarudia hali yake ya kawaida kama ulivyo mwili wake. Mungu akamwambia Mose, “Wasipokuamini au kusadiki ishara ya kwanza, yawezekana wakaamini ishara ya pili. Lakini wasipoamini hata ishara hizi mbili, au kuamini maneno yako, utachota maji ya mto Nili na kuyamwaga juu ya nchi kavu. Maji hayo yatakuwa damu juu ya nchi kavu.”
Kutoka 4:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Musa akajibu akasema, Lakini, tazama, hawataniamini, wala hawataisikia sauti yangu; maana watasema, BWANA hakukutokea. BWANA akamwambia, Ni nini hiyo uliyo nayo mkononi mwako? Akasema, Ni fimbo. Akamwambia, Itupe chini; akaitupa chini, nayo ikawa nyoka; Musa akakimbia kutoka mbele yake. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako, kamshike mkia; (akaunyosha mkono wake akamshika, naye akageuka kuwa fimbo mkononi mwake;) ili kwamba wapate kusadiki ya kwamba BWANA, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amekutokea. BWANA akamwambia tena, Sasa tia mkono wako kifuani mwako. Akautia mkono wake kifuani mwake; naye alipoutoa, kumbe! Mkono wake ulikuwa una ukoma, umekuwa mweupe kama theluji. Akasema, Tia mkono wako kifuani mwako tena. Akautia mkono wake kifuani mwake tena, na alipoutoa kifuani mwake, kumbe! Umerudia hali ya mwili wake. Basi itakuwa, wasipokusadiki, wala kuisikiliza sauti ya ishara ya kwanza, wataisikiliza sauti ya ishara ya pili. Kisha itakuwa wasipoamini hata ishara hizo mbili, wala kuisikiliza sauti yako, basi, yatwae maji ya mtoni uyamwage juu ya nchi kavu, na yale maji uyatwaayo mtoni yatakuwa damu juu ya nchi kavu.
Kutoka 4:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mose akamjibu, “Itakuwaje kama hawataniamini au kunisikiliza, waseme, ‘BWANA hakukutokea’?” Ndipo BWANA akamwambia, “Ni nini hicho kilicho mkononi mwako?” Akajibu, “Fimbo.” BWANA akasema, “Itupe chini.” Mose akaitupa chini hiyo fimbo nayo ikawa nyoka, naye akaikimbia. Kisha BWANA akamwambia, “Nyoosha mkono wako umkamate mkiani.” Basi Mose akanyoosha mkono akamkamata yule nyoka, naye akabadilika tena kuwa fimbo mkononi mwake. BWANA akasema, “Hivi ndivyo Waisraeli watakavyoamini kuwa BWANA, Mungu wa baba zao, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo, amekutokea wewe.” Kisha BWANA akamwambia, “Weka mkono wako ndani ya joho lako.” Basi Mose akaweka mkono wake ndani ya joho lake, naye alipoutoa, ulikuwa na ukoma, mweupe kama theluji. Mungu akamwambia, “Sasa urudishe tena huo mkono ndani ya joho lako.” Basi Mose akaurudisha mkono wake ndani ya joho lake na alipoutoa, ulikuwa mzima, kama sehemu zingine za mwili wake. Ndipo BWANA akamwambia, “Kama hawatakuamini wewe, au kutojali ishara ya kwanza, wataamini ishara ya pili. Lakini kama hawataamini ishara hizi mbili au hawatawasikiliza ninyi, chukua kiasi cha maji kutoka Mto Naili uyamimine juu ya ardhi kavu. Maji mtakayotoa mtoni yatakuwa damu juu ya ardhi.”