Kutoka 36:1-7
Kutoka 36:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
“Bezaleli na Oholiabu, pamoja na kila mwanamume ambaye Mwenyezi-Mungu amemjalia uwezo na akili ya kujua namna ya kufanya kazi zote katika ujenzi wa hema takatifu, atafanya kazi kulingana na yote ambayo Mwenyezi-Mungu aliamuru.” Mose alimwita Bezaleli na Oholiabu na kila mtu ambaye alikuwa amejaliwa ujuzi na Mwenyezi-Mungu, na kila mtu ambaye moyo wake ulimsukuma kufanya kazi kwa hiari. Hao wakapokea kutoka kwa Mose vitu vyote vilivyotolewa na Waisraeli kwa hiari kwa ajili ya kazi ya hema takatifu. Watu waliendelea kumletea michango yao ya hiari kila asubuhi. Watu wote wenye ujuzi waliokuwa wanafanya kazi za kila namna za kujenga hema la mkutano walitoka, kila mmoja katika kazi yake, wakamwendea Mose na kumwambia, “Watu wameleta vitu vingi zaidi ya vile vinavyohitajiwa kwa kazi aliyotuagiza Mwenyezi-Mungu tuifanye.” Basi, Mose akaagiza: “Mtu yeyote, awe mwanamume au mwanamke, asilete mchango zaidi kwa ajili ya hema takatifu.” Watu wakazuiwa kuleta vitu, maana vile walivyokuwa wameleta vilitosha kwa kazi hiyo na kubaki.
Kutoka 36:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Bezaleli na Oholiabu watatenda kazi, na kila mtu mwenye moyo wa hekima, ambaye BWANA amemtia akili na hekima ili ajue kufanya kazi hiyo yote kwa huo utumishi wa mahali patakatifu, kama hayo yote BWANA aliyoyaagiza. Basi Musa akawaita Bezaleli na Oholiabu, na kila mtu aliyekuwa na moyo wa akili, ambaye BWANA alimtia moyoni mwake hekima, kila mtu ambaye moyo wake ulimhimiza ili aende kuifanya kazi hiyo; nao wakapokea mkononi mwa Musa matoleo yote, ambayo hao wana wa Israeli walikuwa wameyaleta kwa ajili ya huo utumishi wa mahali patakatifu, ili wapatengeneze. Kisha wakamletea matoleo kila siku asubuhi kwa moyo wa kupenda. Na hao watu wote wenye ustadi, waliotumika katika kazi yote ya mahali patakatifu, wakaenda kila mtu kutoka katika kazi yake aliyokuwa akiifanya; nao wakasema na Musa, na kumwambia, Watu waleta vitu vingi sana zaidi ya hivyo vitoshavyo kwa ajili ya utumishi wa hiyo kazi, ambayo BWANA aliagiza ifanywe. Basi Musa akatoa amri, nao wakatangaza mbiu katika kambi yote, wakisema, Wasifanye kazi tena, mwanamume wala mwanamke, kwa ajili ya matoleo kwa mahali patakatifu. Basi watu wakazuiwa wasilete tena. Kwani vile vitu walivyokuwa navyo vilikuwa vyatosha kwa kuifanya kazi hiyo yote, kisha vilizidi.
Kutoka 36:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Bezaleli na Oholiabu watatenda kazi, na kila mtu mwenye moyo wa hekima, ambaye BWANA amemtia akili na hekima ili ajue kufanya kazi hiyo yote kwa huo utumishi wa mahali patakatifu, kama hayo yote BWANA aliyoyaagiza. Basi Musa akawaita Bezaleli na Oholiabu, na kila mtu aliyekuwa na moyo wa akili, ambaye BWANA alimtia moyoni mwake hekima, kila mtu ambaye moyo wake ulimhimiza ili aende kuifanya kazi hiyo; nao wakapokea mkononi mwa Musa matoleo yote, ambayo hao wana wa Israeli walikuwa wameyaleta kwa ajili ya huo utumishi wa mahali patakatifu, ili wapafanye. Kisha wakamletea matoleo kila siku asubuhi kwa moyo wa kupenda. Na hao watu wote wenye hekima, waliotumika katika kazi yote ya mahali patakatifu, wakaenda kila mtu kutoka katika kazi yake aliyokuwa akiifanya; nao wakasema na Musa, na kumwambia, Watu waleta vitu vingi sana zaidi ya hivyo vitoshavyo kwa ajili ya utumishi wa hiyo kazi, ambayo BWANA aliagiza ifanywe. Basi Musa akatoa amri, nao wakatangaza mbiu katika marago yote, wakisema, Wasifanye kazi tena, mtu mume wala mwanamke, kwa ajili ya matoleo kwa mahali patakatifu. Basi watu wakazuiwa wasilete tena. Kwani vile vitu walivyokuwa navyo vilikuwa vyatosha kwa kuifanya kazi hiyo yote, kisha vilizidi.
Kutoka 36:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kwa hiyo Bezaleli, Oholiabu na kila mtu BWANA aliyempa ustadi na uwezo wa kujua jinsi ya kufanya kazi zote za kujenga mahali patakatifu wataifanya hiyo kazi kama vile BWANA alivyoagiza.” Ndipo Mose akawaita Bezaleli na Oholiabu na kila mtu mwenye ustadi ambaye BWANA alikuwa amempa uwezo na mwenye kupenda kuja na kufanya kazi. Wakapokea kutoka kwa Mose sadaka zote ambazo Waisraeli walikuwa wameleta ili kuifanya kazi ya ujenzi wa Mahali Patakatifu. Nao watu wakaendelea kuleta sadaka za hiari kila asubuhi. Ikafika wakati mafundi wote wenye ujuzi waliokuwa wakiifanya kazi yote ya mahali patakatifu wakasimamisha kazi zao, wakaja na kumwambia Mose, “Watu wanaleta vitu vingi kuliko tunavyohitaji kwa ajili ya kazi hii ambayo BWANA ameagiza ifanyike.” Ndipo Mose akatoa agizo, nao wakapeleka neno hili katika kambi yote: “Mtu yeyote mwanaume au mwanamke asilete tena kitu chochote kwa ajili ya sadaka ya mahali patakatifu.” Hivyo watu wakazuiliwa kuleta zaidi, kwa sababu walivyokuwa navyo tayari vilitosha na kuzidi kuifanya kazi yote.