Kutoka 34:27-35
Kutoka 34:27-35 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Andika maneno haya, maana kulingana na maneno haya, ninafanya agano nawe na watu wa Israeli.” Mose alikaa huko mlimani pamoja na Mwenyezi-Mungu siku arubaini, mchana na usiku; hakula chakula wala kunywa maji. Aliandika maneno yote ya agano na zile amri kumi. Mose alipokuwa anashuka mlimani Sinai akiwa na vile vibao viwili vyenye maneno ya agano mikononi mwake, hakujua kuwa uso wake ulikuwa unangaa kwa sababu alikuwa ameongea na Mwenyezi-Mungu. Aroni na watu Waisraeli wote walipomwona waliogopa kumkaribia, kwani uso wake ulikuwa unangaa. Lakini Mose alimwita Aroni na viongozi wa jumuiya ya Waisraeli waende karibu naye, kisha akazungumza nao. Baadaye Waisraeli wote wakaja karibu naye, naye akawapa amri zote ambazo Mwenyezi-Mungu alimpa kule mlimani Sinai. Mose alipomaliza kuzungumza na watu aliufunika uso wake kwa kitambaa. Lakini ikawa kwamba kila mara Mose alipokwenda kuongea na Mwenyezi-Mungu katika hema la mkutano, alikiondoa kile kitambaa mpaka alipotoka nje. Na alipotoka nje aliwaambia Waisraeli mambo yote aliyoamriwa, nao Waisraeli waliuona uso wake unangaa. Ndipo Mose alipoufunika tena uso wake kwa kitambaa mpaka alipokwenda kuongea na Mwenyezi-Mungu.
Kutoka 34:27-35 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akamwambia Musa, Andika maneno haya; kwa kuwa mimi nimefanya agano nawe, na pamoja na Israeli, kwa mujibu wa maneno haya. Naye alikuwa huko pamoja na BWANA siku arubaini na masiku yake; hakula chakula, wala hakunywa maji. Naye akaandika katika hizo mbao, hayo maneno ya maagano, hizo amri kumi. Hata ikawa, Musa aliposhuka katika mlima Sinai, na zile mbao mbili za ushuhuda zilikuwa mkononi mwa Musa, hapo aliposhuka katika mlima, Musa hakujua ya kuwa ngozi ya uso wake iling'aa kwa sababu amesema naye. Basi Haruni na wana wote wa Israeli walipomwona Musa, tazama, ngozi ya uso wake iling'aa; nao wakaogopa kumkaribia. Musa akawaita; Haruni na wakuu wote wa kusanyiko wakarudi kwake; Musa akasema nao. Baadaye wana wa Israeli wote wakakaribia; akawausia maneno yote ambayo BWANA amemwambia katika mlima Sinai. Na Musa alipokuwa amekwisha kusema nao, akatia utaji juu ya uso wake. Lakini desturi ya Musa ilikuwa alipoingia mbele za BWANA kusema naye, kuuvua huo utaji mpaka atoke; akatoka akawaambia wana wa Israeli maneno yote aliyoambiwa. Wana wa Israeli wakauona uso wa Musa ya kuwa ngozi ya uso wake Musa iling'aa; naye Musa akautia utaji juu ya uso wake tena, hata alipoingia kusema naye.
Kutoka 34:27-35 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akamwambia Musa, Andika maneno haya; kwa kuwa mimi nimefanya agano nawe, na pamoja na Israeli, kwa mujibu wa maneno haya. Naye alikuwa huko pamoja na BWANA siku arobaini na masiku yake; hakula chakula, wala hakunywa maji. Naye akaandika katika hizo mbao, hayo maneno ya maagano, hizo amri kumi. Hata ikawa, Musa aliposhuka katika mlima Sinai, na zile mbao mbili za ushuhuda zilikuwa mkononi mwa Musa, hapo aliposhuka katika mlima, Musa hakujua ya kuwa ngozi ya uso wake iling’aa kwa sababu amesema naye. Basi Haruni na wana wote wa Israeli walipomwona Musa, tazama, ngozi ya uso wake iling’aa; nao wakaogopa kumkaribia. Musa akawaita; Haruni na wakuu wote wa kusanyiko wakarudi kwake; Musa akasema nao. Baadaye wana wa Israeli wote wakakaribia; akawausia maneno yote ambayo BWANA amemwambia katika mlima Sinai. Na Musa alipokuwa amekwisha kusema nao, akatia utaji juu ya uso wake. Lakini desturi ya Musa ilikuwa alipoingia mbele za BWANA kusema naye, kuuvua huo utaji mpaka atoke; akatoka akawaambia wana wa Israeli maneno yote aliyoambiwa. Wana wa Israeli wakauona uso wa Musa ya kuwa ngozi ya uso wake Musa iling’aa; naye Musa akautia utaji juu ya uso wake tena, hata alipoingia kusema naye.
Kutoka 34:27-35 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha BWANA akamwambia Mose, “Andika maneno haya, kwa maana kulingana na maneno haya, nimefanya Agano na wewe pamoja na Israeli.” Mose alikuwa huko pamoja na BWANA kwa siku arobaini usiku na mchana bila kula chakula wala kunywa maji. Naye akaandika juu ya vibao maneno ya Agano, yaani zile Amri Kumi. Mose alipoteremka kutoka Mlima Sinai akiwa na vile vibao viwili vya Ushuhuda mikononi mwake, hakujua kuwa uso wake ulikuwa ukingʼaa, kwa sababu alikuwa amezungumza na BWANA. Aroni na Waisraeli wote walipomwona Mose, kuwa uso wake unangʼaa, waliogopa kumkaribia. Lakini Mose akawaita, kwa hiyo Aroni na viongozi wote wa jumuiya wakarudi, naye akazungumza nao. Baadaye Waisraeli wote wakamkaribia, naye akawapa amri zote BWANA alizompa katika Mlima wa Sinai. Mose alipomaliza kuzungumza nao, akaweka utaji kwenye uso wake. Lakini kila wakati Mose alipoingia mbele za BWANA kuzungumza naye, aliondoa ule utaji mpaka alipotoka nje. Naye alipotoka nje na kuwaambia Waisraeli lile ambalo ameagizwa, waliona kuwa uso wake unangʼaa. Kisha Mose angeliweka tena utaji juu ya uso wake mpaka alipokwenda kuzungumza na BWANA.