Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 33:7-19

Kutoka 33:7-19 Biblia Habari Njema (BHN)

Mose alikuwa na desturi ya kulichukua lile hema na kulisimika nje ya kambi. Hema hilo alilipa jina, Hema la Mkutano. Mtu yeyote aliyetaka shauri kwa Mwenyezi-Mungu alikwenda kwenye hema la mkutano nje ya kambi. Kila mara Mose alipotoka kwenda kwenye hema hilo, kila mtu alisimama penye mlango wa hema lake na kumwangalia Mose mpaka alipoingia ndani ya hilo hema. Wakati Mose alipoingia ndani ya hilo hema, mnara wa wingu ulitua kwenye mlango wa hema, na Mwenyezi-Mungu akaongea naye. Watu wote walipouona ule mnara wa wingu umesimama mlangoni mwa hema, kila mmoja wao alisimama na kuabudu mlangoni mwa hema lake. Hivyo ndivyo Mwenyezi-Mungu alivyokuwa akiongea na Mose uso kwa uso, kama mtu na rafiki yake. Kisha Mose alirudi tena kambini. Naye kijana Yoshua mwana wa Nuni ambaye alikuwa mtumishi wake hakuondoka hemani. Mose akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Tazama! Wewe waniambia, ‘Waongoze watu hawa,’ lakini hujanijulisha ni nani utakayemtuma anisaidie. Hata hivyo umesema kwamba unanijua kwa jina na pia kwamba nimepata fadhili mbele zako. Sasa basi, nakusihi, kama kweli nimepata fadhili mbele yako, nioneshe sasa njia zako, ili nipate kukujua na kupata fadhili mbele zako. Naomba ukumbuke pia kwamba taifa hili ni watu wako.” Mungu akasema, “Mimi mwenyewe nitakwenda pamoja nawe, na nitakupa faraja.” Mose akasema, “Kama wewe binafsi hutakwenda pamoja nami, basi, usituondoe mahali hapa. Maana nitajuaje kuwa nimepata fadhili mbele zako, mimi na watu wako kama usipokwenda pamoja nasi? Ukienda pamoja nasi itatufanya mimi na watu wako kuwa watu wa pekee miongoni mwa watu wote duniani.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kwa kuwa umepata fadhili mbele yangu, nami nakujua kwa jina lako, jambo hilihili ulilolisema nitalifanya.” Mose akasema, “Nakusihi unioneshe utukufu wako.” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Nitapita mbele yako na kukuonesha wema wangu wote nikilitangaza jina langu, ‘Mwenyezi-Mungu’. Mimi nitamrehemu yule ninayependa kumrehemu, na kumhurumia yule ninayependa kumhurumia.

Shirikisha
Soma Kutoka 33

Kutoka 33:7-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi desturi ya Musa, ilikuwa kuitwaa ile hema, na kuikita nje ya kambi na mbali hiyo kambi; akaiita, hema ya kukutania. Hata kila mtu aliyekuwa akitaka neno kwa BWANA, akatoka, akaenda hata hema ya kukutania, iliyokuwa nje ya kambi. Hata Musa alipotoka kuiendea ile hema, watu wote waliondoka wakasimama, kila mtu mlangoni pa hema yake, akamtazama Musa, hata alipokwisha kuingia hemani. Ikawa Musa alipoingia humo hemani, ile nguzo ya wingu ikashuka, ikasimama mlangoni pa ile hema; naye BWANA akasema na Musa. Watu wote wakaiona nguzo ya wingu ikisimama penye mlango wa hema; watu wote wakaondoka wakasujudu, kila mtu mlangoni pa hema yake. Naye BWANA akasema na Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka akarejea hata kambini; bali mtumishi wake Yoshua, mwana wa Nuni, naye ni kijana, hakutoka mle hemani. Musa akamwambia BWANA, Angalia, wewe waniambia, Wachukue watu hawa; nawe hukunijulisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Lakini umesema, Nakujua jina lako, nawe umepata neema mbele zangu. Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unioneshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako. Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha. Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa. Kwa maana itajulikanaje kuwa nimepata neema mbele zako, mimi na watu wako? Siyo kwa sababu unakwenda pamoja nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na watu wote walio juu ya uso wa nchi? BWANA akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako. Akasema, Nakusihi unioneshe utukufu wako. Akasema, Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza jina la BWANA mbele yako; nami nitamfadhili yeye nitakayemfadhili; nitamrehemu yeye nitakayemrehemu.

Shirikisha
Soma Kutoka 33

Kutoka 33:7-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi desturi ya Musa, ilikuwa kuitwaa ile hema, na kuikita nje ya marago mbali na hayo marago; akaiita, hema ya kukutania. Hata kila mtu aliyekuwa akitaka neno kwa BWANA, akatoka, akaenda hata hema ya kukutania, iliyokuwa nje ya marago. Hata Musa alipotoka kuiendea ile hema, watu wote waliondoka wakasimama, kila mtu mlangoni pa hema yake, akamtazama Musa, hata alipokwisha kuingia hemani. Ikawa Musa alipoingia humo hemani, ile nguzo ya wingu ikashuka, ikasimama mlangoni pa ile hema; naye BWANA akasema na Musa. Watu wote wakaiona nguzo ya wingu ikisimama penye mlango wa hema; watu wote wakaondoka wakasujudu, kila mtu mlangoni pa hema yake. Naye BWANA akasema na Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka akarejea hata maragoni; bali mtumishi wake Yoshua, mwana wa Nuni, naye ni kijana, hakutoka mle hemani. Musa akamwambia BWANA, Angalia, wewe waniambia, Wachukue watu hawa; nawe hukunijulisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Walakini umesema, Nakujua jina lako, nawe umepata neema mbele zangu. Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako. Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha. Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa. Kwa maana itajulikanaje kuwa nimepata neema mbele zako, mimi na watu wako? Siyo kwa sababu unakwenda pamoja nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na watu wote walio juu ya uso wa nchi? BWANA akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako. Akasema, Nakusihi unionyeshe utukufu wako. Akasema, Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza jina la BWANA mbele yako; nami nitamfadhili yeye nitakayemfadhili; nitamrehemu yeye nitakayemrehemu.

Shirikisha
Soma Kutoka 33

Kutoka 33:7-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Basi Mose alikuwa na desturi ya kuchukua hema na kuliweka wakfu nje ya kambi umbali kiasi, akaliita “Hema la Kukutania.” Kila aliyekuwa akiulizia shauri kwa BWANA, angelikwenda katika Hema la Kukutania nje ya kambi. Wakati wowote Mose alipokwenda kwenye Hema, watu wote waliinuka na kusimama kwenye maingilio ya mahema yao, wakimwangalia Mose mpaka aingie kwenye Hema. Kila mara Mose alipoingia ndani ya hema, nguzo ya wingu ingeshuka chini na kukaa kwenye ingilio, wakati Mungu akizungumza na Mose. Kila mara watu walipoona hiyo nguzo ya wingu ikiwa imesimama kwenye ingilio la hema, wote walisimama wakaabudu, kila mmoja kwenye ingilio la hema lake. BWANA angezungumza na Mose uso kwa uso, kama vile mtu azungumzavyo na rafiki yake. Kisha Mose angerudi kambini, lakini msaidizi wake kijana Yoshua mwana wa Nuni hakuondoka mle Hemani. BWANA Mose akamwambia BWANA, “Umekuwa ukiniambia, ‘Ongoza watu hawa,’ lakini hujanifahamisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Umesema, ‘Ninakujua wewe kwa jina lako, nawe umepata kibali mbele zangu.’ Ikiwa umependezwa nami, nifundishe njia zako ili nipate kukujua, nami nizidi kupata kibali mbele zako. Kumbuka kuwa taifa hili ni watu wako.” BWANA akajibu, “Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha.” Kisha Mose akamwambia, “Kama Uso wako hauendi pamoja nasi, usituondoe hapa. Mtu yeyote atajuaje kuwa mimi pamoja na watu wako tumepata kibali mbele zako, usipokwenda pamoja nasi? Ni nini kingine kitakachoweza kututofautisha mimi na watu wako miongoni mwa watu wengine wote walio katika uso wa dunia?” BWANA akamwambia Mose, “Nitakufanyia jambo lile uliloomba, kwa sababu ninapendezwa nawe, nami ninakujua kwa jina lako.” Kisha Mose akasema, “Basi nionyeshe utukufu wako.” Ndipo BWANA akasema, “Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza Jina langu, BWANA, mbele ya uso wako. Nitamrehemu yeye nimrehemuye, na pia nitamhurumia yeye nimhurumiaye.”

Shirikisha
Soma Kutoka 33

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha