Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 31:1-18

Kutoka 31:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mimi nimemteua Bezaleli, mwana wa Uri, mjukuu wa Huri, wa kabila la Yuda na kumjaza roho wangu. Nimempatia uzoefu na akili, maarifa na ufundi, ili abuni kazi za usanii na kufanya kazi za kufua dhahabu, fedha na shaba. Nimempatia ujuzi wa kuchonga mawe ya kupambia, kuchonga mbao, na ujuzi wa kila aina ya ufundi. Vilevile nimemteua Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, afanye kazi pamoja naye. Hali kadhalika nimewapa uwezo mkubwa watu wengine kwa ajili ya kazi mbalimbali, ili watengeneze vifaa vyote nilivyoagiza vifanywe: Hema la mkutano, sanduku la ushuhuda na kiti cha ushuhuda juu yake, pamoja na vifaa vyake vyote; meza na vyombo vyake, kinara safi cha taa na vyombo vyake, madhabahu ya kufukizia ubani, madhabahu ya sadaka za kuteketezwa na vyombo vyake vyote, birika la maji pamoja na tako lake, mavazi matakatifu ya kuhani Aroni na wanawe ambao watafanya huduma ya ukuhani, mafuta ya kupaka na ubani wenye harufu nzuri kwa ajili ya mahali patakatifu. Vitu hivyo vyote vitatengenezwa kulingana kabisa na jinsi nilivyokuamuru.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Waambie Waisraeli hivi: Nyinyi mtaadhimisha Sabato zangu, kwa sababu hizo ni ishara kati yenu na mimi kwa vizazi vyote kwamba mimi ndimi ninayewatakasa. Mtaiadhimisha Sabato, nayo itakuwa kwenu siku takatifu. Yeyote atakayeitia unajisi siku hiyo lazima auawe. Na mtu atakayefanya kazi yoyote siku hiyo atatengwa mbali na watu wake. Mtafanya kazi zenu kwa muda wa siku sita, lakini siku ya saba ni siku rasmi ya mapumziko, ni siku yangu takatifu. Mtu yeyote atakayefanya kazi yoyote siku hiyo lazima atauawa. Kwa hiyo Waisraeli wataiadhimisha siku ya Sabato katika vizazi vyao vyote kama ishara ya agano la milele. Jambo hili litakuwa ishara ya kudumu kati ya Waisraeli na mimi, maana mimi Mwenyezi-Mungu nilifanya mbingu na dunia kwa muda wa siku sita, lakini siku ya saba niliacha kufanya kazi, nikapumzika.” Mwenyezi-Mungu alipomaliza kuongea na Mose mlimani Sinai, alimpatia Mose vile vibao viwili vya mawe ambavyo yeye Mungu aliviandika zile amri kwa kidole chake mwenyewe.

Shirikisha
Soma Kutoka 31

Kutoka 31:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)

BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Angalia, nimemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda; nami nimemjaza Roho ya Mungu, katika hekima, na maarifa, na ujuzi, na mambo ya kazi ya kila aina, ili abuni kazi za ustadi, kuwa fundi wa dhahabu, na wa fedha, na wa shaba, na kukata vito kwa kutiwa mahali, na kuchora miti, na kufanya kazi ya ustadi iwayo yote. Tena, tazama, nimemchagua, awe pamoja naye, huyo Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani; nami nimetia hekima katika mioyo ya wote wenye moyo wa hekima, ili wapate kutengeneza vyote nilivyokuagiza; yaani, hema ya kukutania na sanduku la ushuhuda, na kiti cha rehema kilicho juu yake, na vyombo vyote vya Hema; na meza, na vyombo vyake, na kinara cha taa safi pamoja na vyombo vyake vyote, na madhabahu ya kufukizia uvumba; na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote, na birika na kitako chake; na mavazi yenye kufumwa kwa uzuri, na mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika kwa ajili ya huduma yao ya ukuhani; na mafuta ya kutiwa, na uvumba wa manukato mazuri, kwa ajili ya mahali patakatifu; sawasawa na yote niliyokuagiza ndivyo watakavyofanya wao. BWANA akasema na Musa, na kumwambia, Kisha, nena na wana wa Israeli, na kuwaambia, Hakika mtazishika Sabato zangu, kwa kuwa ni ishara kati yenu na mimi katika vizazi vyenu vyote; ili mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA niwatakasaye ninyi. Basi mtaishika hiyo Sabato; kwa kuwa ni takatifu kwenu; kila mtu atakayeitia unajisi hana budi atauawa; na kila mtu afanyaye kazi siku hiyo, ataondolewa toka kwa watu wake. Kazi itafanywa siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, takatifu kwa BWANA; kila mtu atakayefanya kazi yoyote katika siku ya Sabato, hana budi atauawa. Kwa ajili ya hayo wana wa Israeli wataishika Sabato, kuiangalia sana hiyo Sabato katika vizazi vyao vyote, ni agano la milele. Ni ishara kati ya mimi na wana wa Israeli milele; kwani kwa siku sita BWANA alifanya mbingu na nchi, akapumzika kwa siku ya saba na kustarehe. Hapo BWANA alipokuwa amekwisha zungumza na Musa katika mlima wa Sinai, akampa hizo mbao mbili za ushuhuda, mbao mbili za mawe, zilizoandikwa kwa kidole cha Mungu.

Shirikisha
Soma Kutoka 31

Kutoka 31:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Angalia, nimemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda; nami nimemjaza roho ya Mungu, katika hekima, na maarifa, na ujuzi, na mambo ya kazi ya kila aina, ili abuni kazi za ustadi, kuwa fundi wa dhahabu, na wa fedha, na wa shaba, na kukata vito kwa kutiwa mahali, na kuchora miti, na kufanya kazi ya ustadi iwayo yote. Tena, tazama, nimemchagua, awe pamoja naye, huyo Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila ya Dani; nami nimetia hekima katika mioyo ya wote wenye moyo wa hekima, ili wapate kufanya vyote nilivyokuagiza; yaani, hema ya kukutania na sanduku la ushuhuda, na kiti cha rehema kilicho juu yake, na vyombo vyote vya Hema; na meza, na vyombo vyake, na kinara cha taa safi pamoja na vyombo vyake vyote, na madhabahu ya kufukizia uvumba; na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote, na birika na tako lake; na mavazi yenye kufumwa kwa uzuri, na mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani; na mafuta ya kutiwa, na uvumba wa manukato mazuri, kwa ajili ya mahali patakatifu; sawasawa na yote niliyokuagiza ndivyo watakavyofanya wao. BWANA akasema na Musa, na kumwambia, Kisha, nena wewe na wana wa Israeli, na kuwaambia, Hakika mtazishika Sabato zangu, kwa kuwa ni ishara kati ya mimi na ninyi katika vizazi vyenu vyote; ili mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA niwatakasaye ninyi. Basi mtaishika hiyo Sabato; kwa kuwa ni takatifu kwenu; kila mtu atakayeitia unajisi hakika yake atauawa; kwa kuwa kila mtu afanyaye kazi katika siku hiyo, nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake. Kazi itafanywa siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, takatifu kwa BWANA; kila mtu atakayefanya kazi yo yote katika siku ya Sabato, hakika yake atauawa. Kwa ajili ya hayo wana wa Israeli wataishika Sabato, kuiangalia sana hiyo Sabato katika vizazi vyao vyote, ni agano la milele. Ni ishara kati ya mimi na wana wa Israeli milele; kwani kwa siku sita BWANA alifanya mbingu na nchi, akastarehe kwa siku ya saba na kupumzika. Hapo BWANA alipokuwa amekwisha zungumza na Musa katika mlima wa Sinai, akampa hizo mbao mbili za ushuhuda, mbao mbili za mawe, zilizoandikwa kwa chanda cha Mungu.

Shirikisha
Soma Kutoka 31

Kutoka 31:1-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ndipo BWANA akamwambia Mose, “Tazama, nimemchagua Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda, nami nimemjaza Roho wa Mungu, pamoja na ustadi, uwezo na ujuzi katika aina zote za ufundi, ili kubuni michoro ya kupendeza katika ufundi wa dhahabu, fedha na shaba, kuchonga vito na kuvitia mahali, kufanya ufundi kwa mbao, na kujishughulisha na aina zote za ufundi. Tena nimemteua Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, ili kumsaidia. Pia mafundi wote nimewapa ustadi wa kutengeneza kila kitu nilichokuamuru wewe: Hema la Kukutania, Sanduku la Ushuhuda pamoja na kiti cha rehema juu yake, pia na vifaa vyote vya kwenye hema, meza na vifaa vyake, kinara cha taa cha dhahabu safi na vifaa vyake vyote, madhabahu ya kufukizia uvumba, madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote, sinia na kinara chake, pamoja na mavazi matakatifu yaliyofumwa ya kuhani Aroni, na mavazi kwa ajili ya wanawe wakati wanahudumu katika kazi ya ukuhani, pia mafuta ya upako na uvumba wenye harufu nzuri kwa ajili ya Mahali Patakatifu. Watavitengeneza sawasawa kama vile nilivyokuagiza wewe.” Kisha BWANA akamwambia Mose, “Waambie Waisraeli, ‘Ninyi ni lazima mzishike Sabato zangu. Hii itakuwa ni ishara kati yangu na ninyi kwa ajili ya vizazi vijavyo, ili mpate kujua kwamba Mimi Ndimi BWANA, niwafanyaye ninyi watakatifu. “ ‘Mtaishika Sabato, kwa sababu ni takatifu kwenu. Yeyote atakayeinajisi lazima auawe, yeyote atakayefanya kazi siku hiyo lazima akafie mbali na watu wake. Kwa siku sita, mtafanya kazi, lakini siku ya saba ni Sabato ya kupumzika, takatifu kwa BWANA. Yeyote afanyaye kazi yoyote siku ya Sabato ni lazima auawe. Waisraeli wataishika Sabato, kuiadhimisha kwa vizazi vijavyo kuwa Agano la milele. Itakuwa ishara kati yangu na Waisraeli milele, kwa kuwa kwa muda wa siku sita BWANA aliumba mbingu na dunia, na siku ya saba akaacha kufanya kazi, akapumzika.’ ” BWANA alipomaliza kusema na Mose juu ya Mlima Sinai, Mungu akampa vile vibao viwili vya Ushuhuda, vibao vya mawe vilivyoandikwa kwa kidole cha Mungu.

Shirikisha
Soma Kutoka 31