Kutoka 31:1-11
Kutoka 31:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Angalia, nimemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda; nami nimemjaza Roho ya Mungu, katika hekima, na maarifa, na ujuzi, na mambo ya kazi ya kila aina, ili abuni kazi za ustadi, kuwa fundi wa dhahabu, na wa fedha, na wa shaba, na kukata vito kwa kutiwa mahali, na kuchora miti, na kufanya kazi ya ustadi iwayo yote. Tena, tazama, nimemchagua, awe pamoja naye, huyo Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani; nami nimetia hekima katika mioyo ya wote wenye moyo wa hekima, ili wapate kutengeneza vyote nilivyokuagiza; yaani, hema ya kukutania na sanduku la ushuhuda, na kiti cha rehema kilicho juu yake, na vyombo vyote vya Hema; na meza, na vyombo vyake, na kinara cha taa safi pamoja na vyombo vyake vyote, na madhabahu ya kufukizia uvumba; na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote, na birika na kitako chake; na mavazi yenye kufumwa kwa uzuri, na mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika kwa ajili ya huduma yao ya ukuhani; na mafuta ya kutiwa, na uvumba wa manukato mazuri, kwa ajili ya mahali patakatifu; sawasawa na yote niliyokuagiza ndivyo watakavyofanya wao.
Kutoka 31:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mimi nimemteua Bezaleli, mwana wa Uri, mjukuu wa Huri, wa kabila la Yuda na kumjaza roho wangu. Nimempatia uzoefu na akili, maarifa na ufundi, ili abuni kazi za usanii na kufanya kazi za kufua dhahabu, fedha na shaba. Nimempatia ujuzi wa kuchonga mawe ya kupambia, kuchonga mbao, na ujuzi wa kila aina ya ufundi. Vilevile nimemteua Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, afanye kazi pamoja naye. Hali kadhalika nimewapa uwezo mkubwa watu wengine kwa ajili ya kazi mbalimbali, ili watengeneze vifaa vyote nilivyoagiza vifanywe: Hema la mkutano, sanduku la ushuhuda na kiti cha ushuhuda juu yake, pamoja na vifaa vyake vyote; meza na vyombo vyake, kinara safi cha taa na vyombo vyake, madhabahu ya kufukizia ubani, madhabahu ya sadaka za kuteketezwa na vyombo vyake vyote, birika la maji pamoja na tako lake, mavazi matakatifu ya kuhani Aroni na wanawe ambao watafanya huduma ya ukuhani, mafuta ya kupaka na ubani wenye harufu nzuri kwa ajili ya mahali patakatifu. Vitu hivyo vyote vitatengenezwa kulingana kabisa na jinsi nilivyokuamuru.”
Kutoka 31:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Angalia, nimemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda; nami nimemjaza roho ya Mungu, katika hekima, na maarifa, na ujuzi, na mambo ya kazi ya kila aina, ili abuni kazi za ustadi, kuwa fundi wa dhahabu, na wa fedha, na wa shaba, na kukata vito kwa kutiwa mahali, na kuchora miti, na kufanya kazi ya ustadi iwayo yote. Tena, tazama, nimemchagua, awe pamoja naye, huyo Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila ya Dani; nami nimetia hekima katika mioyo ya wote wenye moyo wa hekima, ili wapate kufanya vyote nilivyokuagiza; yaani, hema ya kukutania na sanduku la ushuhuda, na kiti cha rehema kilicho juu yake, na vyombo vyote vya Hema; na meza, na vyombo vyake, na kinara cha taa safi pamoja na vyombo vyake vyote, na madhabahu ya kufukizia uvumba; na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote, na birika na tako lake; na mavazi yenye kufumwa kwa uzuri, na mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani; na mafuta ya kutiwa, na uvumba wa manukato mazuri, kwa ajili ya mahali patakatifu; sawasawa na yote niliyokuagiza ndivyo watakavyofanya wao.
Kutoka 31:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndipo BWANA akamwambia Mose, “Tazama, nimemchagua Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda, nami nimemjaza Roho wa Mungu, pamoja na ustadi, uwezo na ujuzi katika aina zote za ufundi, ili kubuni michoro ya kupendeza katika ufundi wa dhahabu, fedha na shaba, kuchonga vito na kuvitia mahali, kufanya ufundi kwa mbao, na kujishughulisha na aina zote za ufundi. Tena nimemteua Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, ili kumsaidia. Pia mafundi wote nimewapa ustadi wa kutengeneza kila kitu nilichokuamuru wewe: Hema la Kukutania, Sanduku la Ushuhuda pamoja na kiti cha rehema juu yake, pia na vifaa vyote vya kwenye hema, meza na vifaa vyake, kinara cha taa cha dhahabu safi na vifaa vyake vyote, madhabahu ya kufukizia uvumba, madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote, sinia na kinara chake, pamoja na mavazi matakatifu yaliyofumwa ya kuhani Aroni, na mavazi kwa ajili ya wanawe wakati wanahudumu katika kazi ya ukuhani, pia mafuta ya upako na uvumba wenye harufu nzuri kwa ajili ya Mahali Patakatifu. Watavitengeneza sawasawa kama vile nilivyokuagiza wewe.”