Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 3:7-22

Kutoka 3:7-22 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nimeyaona mateso ya watu wangu walioko nchini Misri na nimekisikia kilio chao kinachosababishwa na wanyapara wao. Najua mateso yao, na hivyo, nimeshuka ili niwaokoe mikononi mwa Wamisri. Nitawatoa humo nchini na kuwapeleka katika nchi nzuri na kubwa; nchi inayotiririka maziwa na asali, nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. Naam, kilio cha Waisraeli kimenifikia; nimeona jinsi Wamisri wanavyowatesa. Sasa, nitakutuma kwa Farao ili uwatoe watu wangu, watu hao wa Israeli, kutoka nchini Misri.” Lakini Mose akamwambia Mungu, “Mimi ni nani hata nimwendee Farao na kuwatoa Waisraeli nchini Misri?” Mungu akamwambia, “Mimi nitakuwa pamoja nawe. Utawatoa watu wa Israeli na kuja kuniabudu mimi Mungu juu ya mlima huu. Hiyo itakuwa ishara kwamba ni mimi Mungu niliyekutuma wewe.” Hapo, Mose akamwambia Mungu, “Sasa, nikiwaendea Waisraeli na kuwaambia, ‘Mungu wa babu zenu amenituma kwenu,’ nao wakiniuliza, ‘Jina lake ni nani,’ nitawaambia nini?” Mungu akamjibu, “MIMI NDIMI NILIYE. Waambie hivi watu wa Israeli: Yule anayeitwa, NDIMI NILIYE, amenituma kwenu. Waambie hivi Waisraeli: Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu. Hili ndilo jina langu milele, na hivyo ndivyo nitakavyokumbukwa katika vizazi vyote. Nenda ukawakusanye wazee wa Israeli na kuwaambia: Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu: Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenitokea na kusema, ‘Nimewachunguzeni na kuyaona mambo mnayotendewa nchini Misri! Naahidi kuwa nitawatoa katika mateso yenu huko Misri na kuwapeleka katika nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi; nitawapeleka katika nchi inayotiririka maziwa na asali.’ “Wao watakusikiliza, nawe pamoja na wazee wa Waisraeli mtamwendea mfalme wa Misri na kumwambia, ‘Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Waebrania, ametutokea. Sasa, uturuhusu tuende safari ya mwendo wa siku tatu jangwani, tukamtambikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.’ Najua kuwa mfalme wa Misri hatawaacha mwende asipolazimishwa kwa mkono wenye nguvu. Kwa hiyo nitaunyosha mkono wangu na kuipiga nchi ya Misri kwa maajabu ambayo nitayafanya huko. Baadaye mfalme atawaacha mwondoke. Tena nitahakikisha Wamisri wanawapendelea Waisraeli, na mtakapoondoka Misri, hamtatoka mikono mitupu. Kila mwanamke Mwebrania atamwomba jirani yake Mmisri, au mgeni wake aliye nyumbani kwake, ampe vito vya fedha na dhahabu pamoja na nguo. Hivyo mtawavisha watoto wenu wa kiume na wa kike. Ndivyo mtakavyowapokonya Wamisri mali yao.”

Shirikisha
Soma Kutoka 3

Kutoka 3:7-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)

BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe kutoka kwa mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hadi nchi njema, kisha pana; nchi itiririkayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi. Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa. Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri. Musa akamwambia Mungu, Mimi ni nani, hata niende kwa Farao, nikawatoe wana wa Israeli watoke Misri? Akasema, Bila shaka mimi nitakuwa pamoja nawe; na dalili ya kuwa nimekutuma ndiyo hii; utakapokuwa umekwisha kuwatoa hao watu katika Misri, mtamwabudu Mungu katika mlima huu. Musa akamwambia Mungu, Tazama, nitakapofika kwa wana wa Israeli, na kuwaambia, Mungu wa baba zenu amenituma kwenu; nao wakaniuliza, Jina lake ni nani? Niwaambie nini? Mungu akamwambia Musa, MIMI NIKO AMBAYE NIKO; akasema, Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli; MIMI NIKO amenituma kwenu. Tena Mungu akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli maneno haya, BWANA, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu; hili ndilo jina langu hata milele, nalo ni kumbukumbu langu hata vizazi vyote. Nenda, ukawakusanye wazee wa Israeli pamoja, ukawaambie, BWANA, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenitokea, akaniambia, Hakika nimewajilieni, tena nimeyaona mnayotendewa huko Misri; Nami nimesema, Nitawapandisha kutoka katika mateso ya Misri na kuwaingiza katika nchi ya Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, nchi ijaayo maziwa na asali. Nao watakusikia sauti yako; nawe utakwenda, wewe na wazee wa Israeli kwa mfalme wa Misri, na kumwambia, BWANA Mungu wa Waebrania, amekutana nasi; basi sasa twakuomba, tupe ruhusa twende mwendo wa siku tatu jangwani, ili tumtolee dhabihu BWANA Mungu wetu. Nami najua ya kuwa huyo mfalme wa Misri hatawapa ruhusa mwende zenu, la, hata kwa mkono wa nguvu. Nami nitaunyosha mkono wangu, na kuipiga Misri kwa ajabu zangu zote, nitakazofanya kati yake, kisha baadaye atawapa ruhusa kwenda. Nami nitawapa watu hao kufadhiliwa mbele ya Wamisri; hata itakuwa, hapo mtakapokwenda zenu hamtakwenda kitupu; Lakini kila mwanamke ataomba kwa jirani, na kwa huyo akaaye naye nyumbani, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi; nanyi mtawavika wana wenu na binti zenu; nanyi mtawateka nyara Wamisri.

Shirikisha
Soma Kutoka 3

Kutoka 3:7-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi. Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa. Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri. Musa akamwambia Mungu, Mimi ni nani, hata niende kwa Farao, nikawatoe wana wa Israeli watoke Misri? Akasema, Bila shaka mimi nitakuwa pamoja nawe; na dalili ya kuwa nimekutuma ndiyo hii; utakapokuwa umekwisha kuwatoa hao watu katika Misri, mtamwabudu Mungu katika mlima huu. Musa akamwambia Mungu, Tazama, nitakapofika kwa wana wa Israeli, na kuwaambia, Mungu wa baba zenu amenituma kwenu; nao wakaniuliza, Jina lake n’nani? Niwaambie nini? Mungu akamwambia Musa, MIMI NIKO AMBAYE NIKO; akasema, Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli; MIMI NIKO amenituma kwenu. Tena Mungu akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli maneno haya, BWANA, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu; hili ndilo jina langu hata milele, nalo ni kumbukumbu langu hata vizazi vyote. Enenda, ukawakusanye wazee wa Israeli pamoja, ukawaambie, BWANA, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenitokea, akaniambia, Hakika nimewajilieni, tena nimeyaona mnayotendewa huko Misri; Nami nimesema, Nitawapandisha kutoka katika mateso ya Misri na kuwaingiza katika nchi ya Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, nchi ijaayo maziwa na asali. Nao watakusikia sauti yako; nawe utakwenda, wewe na wazee wa Israeli kwa mfalme wa Misri, na kumwambia, BWANA Mungu wa Waebrania, amekutana nasi; basi sasa twakuomba, tupe ruhusa twende mwendo siku tatu jangwani, ili tumtolee dhabihu BWANA Mungu wetu. Nami najua ya kuwa huyo mfalme wa Misri hatawapa ruhusa mwende zenu, la, hata kwa mkono wa nguvu. Nami nitaunyosha mkono wangu, na kuipiga Misri kwa ajabu zangu zote, nitakazofanya kati yake, kisha baadaye atawapa ruhusa kwenda. Nami nitawapa watu hao kufadhiliwa mbele ya Wamisri; hata itakuwa, hapo mtakapokwenda zenu hamtakwenda kitupu; Lakini kila mwanamke ataomba kwa jirani, na kwa huyo akaaye naye nyumbani, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi; nanyi mtawavika wana wenu na binti zenu; nanyi mtawateka nyara Wamisri.

Shirikisha
Soma Kutoka 3

Kutoka 3:7-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

BWANA akamwambia, “Hakika nimeona mateso ya watu wangu katika Misri. Nimesikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao, nami naguswa na mateso yao. Basi nimeshuka niwaokoe kutoka mkono wa Wamisri, niwatoe na kuwapandisha kutoka nchi hiyo, niwapeleke katika nchi nzuri na kubwa, nchi itiririkayo maziwa na asali, nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. Sasa kilio cha Waisraeli kimenifikia, nami nimeona jinsi Wamisri wanavyowatesa. Basi, sasa nenda. Ninakutuma kwa Farao ili kuwatoa watu wangu Waisraeli kutoka Misri.” Lakini Mose akamwambia Mungu, “Mimi ni nani hata niende kwa Farao kuwatoa Waisraeli nchini Misri?” Naye Mungu akasema, “Mimi nitakuwa pamoja nawe. Hii itakuwa ishara kwako kwamba ni Mimi nimekutuma: Hapo utakapokuwa umewatoa watu Misri, mtamwabudu Mungu katika mlima huu.” Mose akamwambia Mungu, “Ikiwa nitawaendea Waisraeli na kuwaambia, ‘Mungu wa baba zenu amenituma kwenu,’ nao wakiniuliza, ‘Jina lake ni nani?’ Nitawaambia nini?” Mungu akamwambia Mose, “MIMI NIKO AMBAYE NIKO. Hivyo ndivyo utakavyowaambia Waisraeli: ‘MIMI NIKO amenituma kwenu.’ ” Vilevile Mungu akamwambia Mose, “Waambie Waisraeli, ‘BWANA, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo amenituma kwenu.’ Hili ndilo Jina langu milele, Jina ambalo mtanikumbuka kwalo kutoka kizazi hadi kizazi. “Nenda, ukawakusanye wazee wa Israeli, uwaambie, ‘BWANA, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Abrahamu, Isaki na Yakobo, alinitokea akaniambia: Nimewatazama, nami nimeona mliyofanyiwa katika Misri. Nami nimeahidi kuwapandisha kutoka mateso yenu katika nchi ya Misri, niwapeleke nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, nchi itiririkayo maziwa na asali.’ “Wazee wa Israeli watakusikiliza. Kisha wewe na wazee mtakwenda kwa mfalme wa Misri na kumwambia, ‘BWANA, Mungu wa Waebrania ametutokea. Turuhusu twende safari ya siku tatu huko jangwani kutoa dhabihu kwa BWANA Mungu wetu.’ Lakini nafahamu kwamba mfalme wa Misri hatawaruhusu kwenda, mpaka mkono wenye nguvu umlazimishe. Kwa hiyo nitaunyoosha mkono wangu na kuwapiga Wamisri kwa maajabu yote nitakayofanya miongoni mwao. Baada ya hayo, atawaruhusu mwondoke. “Nami nitawapa hawa watu upendeleo mbele ya Wamisri, kwa hiyo mtakapoondoka nchini hamtaondoka mikono mitupu. Kila mwanamke Mwisraeli atamwomba jirani yake Mmisri na mwanamke yeyote anayeishi nyumbani kwake ampe vyombo vya fedha, dhahabu na nguo, ambavyo mtawavika wana wenu na binti zenu. Hivyo mtawateka nyara Wamisri.”

Shirikisha
Soma Kutoka 3