Kutoka 26:30-37
Kutoka 26:30-37 Biblia Habari Njema (BHN)
Hivyo utalitengeneza hema hilo kulingana na mfano niliokuonesha mlimani. “Utatengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na kitani safi iliyosokotwa. Pazia hilo utalitarizi kwa ustadi kwa viumbe wenye mabawa. Utalitundika pazia kwenye nguzo nne za mjohoro zilizopakwa dhahabu, zenye kulabu za dhahabu na vikalio vinne vya fedha. Utalitundika pazia hilo kwenye vifungo, kisha ulilete lile sanduku la ushuhuda humo ndani kukiwa na vibao viwili vya mawe, nyuma ya pazia hilo. Pazia hilo litatenga mahali patakatifu na mahali patakatifu sana. Ndani ya mahali patakatifu utakiweka kile kiti cha rehema juu ya sanduku la maamuzi. Ile meza ya mjohoro utaiweka upande wa nje wa pazia hilo, na kile kinara cha taa utakiweka upande wa kusini wa hema, mkabala wa meza. Meza hiyo itakuwa upande wa kaskazini. “Kwa ajili ya mlango wa hema utatengeneza pazia zito kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, na kutariziwa vizuri. Vilevile utatengeneza nguzo tano za mjohoro na kuzipaka dhahabu. Nguzo hizo zitakuwa na kulabu za dhahabu, na kila moja itakuwa na tako la shaba.
Kutoka 26:30-37 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nawe utaisimamisha hiyo maskani sawasawa na mfano wake uliooneshwa mlimani. Nawe fanya pazia la nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na nguo za kitani nzuri zenye kusokotwa, litafumwa na kutiwa makerubi, kazi ya fundi stadi; kisha litungike katika nguzo nne za mti wa mshita zilizofunikwa dhahabu, vifungo vyake vitakuwa vya dhahabu, katika vitako vya fedha vinne. Nawe tungika lile pazia chini ya vile vifungo, nawe lete lile sanduku la ushuhuda na kulitia humo nyuma ya pazia; na lile pazia litawagawanyia kati ya patakatifu, na mahali patakatifu sana. Nawe utaweka kiti cha rehema juu ya lile sanduku la ushuhuda ndani ya mahali pale patakatifu sana. Na ile meza utaiweka nje ya pazia, na kinara cha taa kuikabili ile meza upande wa maskani wa kuelekea kusini; na ile meza utaiweka upande wa kaskazini. Kisha utafanya kisitiri kwa mlango wa Hema, cha nyuzi za rangi ya buluu, zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa, kazi ya mshonaji wa taraza. Nawe fanya nguzo tano za mti wa mshita kwa kile kisitiri, na kuzifunika dhahabu; kulabu zake zitakuwa za dhahabu; nawe utasubu vitako vya shaba vitano kwa ajili yake.
Kutoka 26:30-37 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nawe utaisimamisha hiyo maskani sawasawa na mfano wake ulioonyeshwa mlimani. Nawe fanya pazia la nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na nguo za kitani nzuri zenye kusokotwa, litafumwa na kutiwa makerubi, kazi ya fundi stadi; kisha litungike katika nguzo nne za mti wa mshita zilizofunikwa dhahabu, vifungo vyake vitakuwa vya dhahabu, katika matako ya fedha manne. Nawe tungika lile pazia chini ya vile vifungo, nawe lete lile sanduku la ushuhuda na kulitia humo nyuma ya pazia; na lile pazia litawagawanyia kati ya patakatifu, na mahali patakatifu sana. Nawe utaweka kiti cha rehema juu ya lile sanduku la ushuhuda ndani ya mahali pale patakatifu sana. Na ile meza utaiweka nje ya pazia, na kinara cha taa kuikabili ile meza upande wa maskani wa kuelekea kusini; na ile meza utaiweka upande wa kaskazini. Kisha utafanya kisitiri kwa mlango wa Hema, cha nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa, kazi ya mshona taraza. Nawe fanya nguzo tano za mti wa mshita kwa kile kisitiri, na kuzifunika dhahabu; kulabu zake zitakuwa za dhahabu; nawe utasubu matako ya shaba matano kwa ajili yake.
Kutoka 26:30-37 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
“Simamisha maskani ya Mungu sawasawa na mfano uliooneshwa kule mlimani. “Tengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa vizuri, naye fundi stadi atirizi makerubi kwenye hilo pazia. Litundike kwa kulabu za dhahabu kwenye nguzo nne za mti wa mshita ambazo zimefunikwa kwa dhahabu, zikiwa zimesimamishwa kwenye vitako vinne vya fedha. Ning’iniza pazia hilo kwenye vifungo, kisha weka Sanduku la Ushuhuda nyuma ya pazia. Pazia litatenganisha Mahali Patakatifu kutoka Patakatifu pa Patakatifu. Weka kifuniko cha kiti cha rehema juu ya Sanduku la Ushuhuda ndani ya Patakatifu pa Patakatifu. Weka meza nje ya pazia upande wa kaskazini wa maskani ya Mungu, kisha weka kinara cha taa upande wa kusini wa maskani. “Kwa ajili ya ingilio la hema, tengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa vizuri, kazi ya mtarizi. Tengeneza kulabu za dhahabu kwa ajili ya hilo pazia, na nguzo tano za mshita zilizofunikwa kwa dhahabu. Kisha subu vitako vitano vya shaba kwa ajili yake.