Kutoka 19:1-8
Kutoka 19:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku ya kwanza ya mwezi wa tatu tangu walipotoka nchini Misri, watu wa Israeli walifika katika jangwa la Sinai. Walipoondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, huko walipiga kambi mbele ya mlima Sinai. Basi, Mose akapanda juu mlimani kwa Mungu. Hapo Mwenyezi-Mungu akamwita Mose kutoka huko juu mlimani, akamwambia, “Hivi ndivyo utakavyowaambia wazawa wa Yakobo, hao Waisraeli, ‘Nyinyi wenyewe mmeona nilivyowatenda Wamisri na jinsi nilivyowachukua kama tai anavyochukua watoto wake kwa mabawa, nikawaleta kwangu. Sasa basi, kama mkiitii sauti yangu na kulishika agano langu, mtakuwa watu wangu wateule kati ya mataifa yote, maana dunia yote ni yangu. Mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani na taifa takatifu.’ Hayo ndiyo maneno utakayowaambia Waisraeli.” Basi, Mose akarudi, akawakusanya pamoja wazee wa Waisraeli na kuwaambia maneno hayo aliyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Watu wote wakaitikia kwa pamoja wakisema, “Mambo yote aliyoyasema Mwenyezi-Mungu, tutayafanya.” Mose akamjulisha Mwenyezi-Mungu jibu hilo la watu.
Kutoka 19:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mwezi wa tatu baada ya Waisraeli kutoka katika nchi ya Misri, siku iyo hiyo wakafika katika jangwa la Sinai. Nao walipokuwa wameondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, wakatua katika lile jangwa; Israeli wakapiga kambi huko wakiukabili mlima. Musa akapanda kwa Mungu, na BWANA akamwita kutoka mlimani ule, akisema, Utawaambia nyumba ya Yakobo, na kuwaarifu wana wa Israeli, maneno haya; Mmeona jinsi nilivyowatendea Wamisri, na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mbawa za tai, nikawaleta ninyi kwangu mimi. Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu, nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli. Musa akaenda akawaita wazee wa watu, akawafunulia maneno hayo yote, BWANA aliyokuwa amemwagiza. Watu wote wakaitika pamoja wakisema, Hayo yote aliyoyasema BWANA tutayatenda. Naye Musa akamwambia BWANA maneno ya hao watu.
Kutoka 19:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mwezi wa tatu baada ya kutoka Waisraeli katika nchi ya Misri, siku iyo hiyo wakafika jangwa la Sinai. Nao walipokuwa wameondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, wakatua katika lile jangwa; Israeli wakapiga kambi huko wakiukabili mlima. Musa akapanda kwa Mungu, na BWANA akamwita toka mlima ule, akisema, Utawaambia nyumba ya Yakobo, na kuwaarifu wana wa Israeli, maneno haya; Mmeona jinsi nilivyowatendea Wamisri, na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mbawa za tai, nikawaleta ninyi kwangu mimi. Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu, nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli. Musa akaenda akawaita wazee wa watu, akawafunulia maneno hayo yote, BWANA aliyokuwa amemwagiza. Watu wote wakaitika pamoja wakisema, Hayo yote aliyoyasema BWANA tutayatenda. Naye Musa akamwambia BWANA maneno ya hao watu.
Kutoka 19:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mnamo mwezi wa tatu baada ya Waisraeli kuondoka Misri, siku kama iyo hiyo, wakafika katika Jangwa la Sinai. Baada ya kuondoka Refidimu, waliingia katika Jangwa la Sinai na Israeli wakapiga kambi pale jangwani mbele ya mlima. Kisha Mose akakwea kwenda kwa Mungu, naye BWANA akamwita kutoka kwenye ule mlima akasema, “Hivi ndivyo utakavyosema na nyumba ya Yakobo na utakachowaambia watu wa Israeli: ‘Ninyi wenyewe mmeona nililofanya huko Misri, jinsi nilivyowabeba kwenye mbawa za tai na kuwaleta kwangu. Sasa kama mkinitii kikamilifu na kutunza Agano langu, basi ninyi mtakuwa mali yangu ya thamani kubwa miongoni mwa mataifa yote. Ijapokuwa dunia yote ni mali yangu, ninyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani na taifa takatifu.’ Haya ndiyo maneno utakayosema kwa wana wa Israeli.” Kwa hiyo Mose akarudi, akawaita wazee wa watu na kuwaambia maneno yote ambayo BWANA alikuwa amemwamuru ayaseme. Watu wote wakajibu kwa pamoja, “Tutafanya kila kitu BWANA alichokisema.” Naye Mose akarudisha majibu yao kwa BWANA.