Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 18:1-27

Kutoka 18:1-27 Biblia Habari Njema (BHN)

Yethro, kuhani wa Midiani, baba mkwe wa Mose, alisikia juu ya mambo yote ambayo Mwenyezi-Mungu alimtendea Mose na Waisraeli alipowatoa katika nchi ya Misri. Kwa hiyo Yethro, akiwa na Sipora, mkewe Mose, ambaye Mose alikuwa amemrudisha kwa baba yake, alimwendea Mose, pamoja na watoto wawili wa Mose. Mtoto wa kwanza aliitwa Gershomu. Mose alimpa jina hili kwa vile alisema, “Nimekimbilia katika nchi ya kigeni.” Wa pili aliitwa Eliezeri, kwa vile Mose alisema, “Mungu wa baba yangu ndiye aliyenisaidia nisiuawe na Farao.” Yethro, mkwewe Mose, alikuja pamoja na binti yake, yaani mkewe Mose, pamoja na watoto, akamkuta Mose jangwani alikokuwa amepiga kambi kwenye mlima wa Mungu. Mose alipoambiwa kuwa baba mkwe wake pamoja na mkewe na wanawe wawili wanakuja, alitoka kwenda kumlaki baba mkwe wake, akamwinamia na kumbusu. Wakasalimiana, kisha wakaingia hemani. Mose akamweleza mkwewe mambo yote Mwenyezi-Mungu aliyomtenda Farao na Wamisri kwa ajili ya Waisraeli. Alimwambia pia juu ya shida zote zilizowapata safarini na jinsi Mwenyezi-Mungu alivyowaokoa. Yethro akafurahishwa na yote aliyotenda Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya Waisraeli, kwa kuwaokoa mikononi mwa Wamisri. Yethro akasema, “Na atukuzwe Mwenyezi-Mungu ambaye amewaokoa mikononi mwa Wamisri na kutoka utumwa wa Farao. Sasa najua kwamba Mwenyezi-Mungu ni mkuu kuliko miungu yote, kwani amewakomboa watu hawa mikononi mwa Wamisri ambao waliwatendea ujeuri.” Hapo Yethro, baba mkwe wa Mose, akamtolea Mungu sadaka za kuteketezwa na tambiko. Naye Aroni akaja pamoja na wazee wa Israeli ili kula chakula pamoja na Yethro, mbele ya Mwenyezi-Mungu. Kesho yake, Mose aliketi kuamua matatizo ya Waisraeli, nao wakasimama wakiwa wamemzunguka, tangu asubuhi mpaka jioni. Yethro, baba mkwe wa Mose, alipoyaona mambo yote ambayo Mose aliwafanyia Waisraeli, alimwuliza, “Kwa nini unawafanyia watu mambo haya? Mbona unaketi peke yako huku watu wamekuzunguka tangu asubuhi mpaka jioni?” Mose akamjibu mkwewe, “Kwa sababu watu huja kwangu kuuliza matakwa ya Mungu. Wakiwa na ugomvi wowote ule wao huja kwangu nami huamua kati ya mtu na mwenzake, na kuwafunza amri za Mungu na maamuzi yake.” Basi, Yethro akamwambia Mose, “Unavyofanya si vizuri! Utajidhuru mwenyewe na hawa watu kwa uchovu, kwani hii ni kazi ngumu usiyoweza kuifanya peke yako. Sikiliza shauri langu kwako, na Mungu awe pamoja nawe. Wewe utawawakilisha watu mbele ya Mungu na kumletea Mungu matatizo yao. Hali kadhalika utawafundisha amri na maamuzi ya Mungu na kuwaonesha jinsi inavyowapasa kuishi na kufanya. Lakini kuhusu mambo mengine, chagua miongoni mwa watu wote, watu wanaostahili, watu wanaomcha Mungu, waaminifu na wanaochukia kuhongwa. Wape hao mamlaka, wawe na jukumu la kuwasimamia watu katika makundi ya watu elfu, mia, hamsini na kumikumi. Hao ndio watakaokuwa na vikao kila siku kutatua matatizo ya watu. Matatizo magumu watakuletea wewe, lakini yale madogomadogo watayaamua wenyewe. Kwa njia hiyo utaweza kurahisisha kazi yako kwa vile watashirikiana nawe katika jukumu hilo. Ukifanya hivyo, na kama ndivyo atakavyo Mungu, utaweza kustahimili na watu hawa wote wataweza kurudi makwao kwa amani.” Mose alilisikiliza shauri hilo la mkwewe na kufanya kama alivyoshauriwa. Basi, akawateua watu wenye uwezo kati ya Waisraeli, akawafanya kuwa viongozi wa makundi ya watu elfu, watu mia, watu hamsini na watu kumikumi. Nao wakawa wanaamua matatizo ya watu kila wakati. Matatizo magumu walimletea Mose, lakini yale madogomadogo waliyatatua wao wenyewe. Baada ya kufanya hivyo, Mose na mkwewe wakaagana naye Yethro akarudi nchini kwake.

Shirikisha
Soma Kutoka 18

Kutoka 18:1-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi Yethro, kuhani wa Midiani, mkwewe Musa, alisikia habari ya mambo hayo yote Mungu aliyokuwa amemtendea Musa, na Waisraeli watu wake, jinsi BWANA alivyowaleta Israeli watoke Misri. Ndipo Yethro mkwewe Musa akamtwaa Sipora, mke wa Musa, baada ya yeye kumrudisha, pamoja na wanawe wawili; katika hao, jina la mmoja ni Gershomu, maana alisema, Mimi nimekuwa mgeni katika nchi za kigeni; na jina la wa pili ni Eliezeri, kwa kuwa alisema, Yeye Mungu wa baba yangu alikuwa msaada wangu, akaniokoa na upanga wa Farao. Basi Yethro, mkwewe Musa, pamoja na mke wa Musa na wanawe wawili wakamwendea Musa huko nyikani, hapo alipokuwa amepiga kambi, kwenye mlima wa Mungu; naye akamwambia Musa, Mimi Yethro mkweo nimekuja kwako, na mkeo, na wanawe wawili pamoja naye. Basi Musa akatoka nje ili amlaki mkwewe, akasujudia na kumbusu; nao wakaulizana habari; kisha wakaingia hemani. Musa akamwambia mkwewe mambo hayo yote BWANA aliyomtenda Farao na Wamisri kwa ajili ya Israeli, na mambo mazito yote yaliyowapata njiani, na jinsi BWANA alivyowaokoa. Yethro alifurahi kwa ajili ya wema wote BWANA aliowatendea Israeli, kwa alivyowaokoa mikononi mwa Wamisri. Kisha Yethro akasema, Na ahimidiwe BWANA aliyewaokoa na mikono ya Wamisri, na mkono wa Farao; aliyewaokoa watu hao watoke mikononi mwa Wamisri. Sasa najua ya kuwa BWANA ni mkuu kuliko miungu yote; naam, katika jambo hilo walilowatenda kwa ujeuri. Yethro mkwewe Musa akamletea Mungu sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; na Haruni akaja, na wazee wote wa Israeli, wale chakula pamoja na mkwewe Musa mbele za Mungu. Asubuhi yake Musa akaketi ili awapishie hukumu watu; na hao watu wakasimama kumzunguka Musa tangu asubuhi hata jioni. Mkwewe Musa alipoyaona yote aliyowafanyia watu, akasema, Ni jambo gani hili uwatendealo hao watu? Kwani wewe kuketi hapo peke yako, na watu wote kusimama kwako tangu asubuhi hata jioni? Musa akamwambia mkwewe, Ni kwa sababu watu hunijilia mimi wapate kumwuliza Mungu; wakiwa na neno, hunijia; nami naamua kati ya mtu na mwenziwe, nami nawajulisha amri za Mungu, na sheria zake. Mkwewe Musa akamwambia, Jambo hili ufanyalo si jema. Kwa kweli utajidhoofisha mwenyewe, na hawa watu walio pamoja nawe pia; maana jambo hili ni zito mno kwako; huwezi wewe kulitenda peke yako. Sikiza sasa neno langu, nitakupa shauri, na Mungu na awe pamoja nawe; uwe wewe kwa ajili ya watu mbele ya Mungu, nawe umletee Mungu maneno yao; nawe utawafundisha zile amri na sheria, nawe utawaonesha njia ambayo inawapasa kuiendea, na kazi ambayo inawapasa kuifanya. Zaidi ya hayo utajipatia katika watu hawa watu walio na uwezo, wenye kumcha Mungu, watu wa kweli, wenye kuchukia mapato ya udhalimu; ukawaweka juu yao, wawe wakuu wa maelfu, na wakuu wa mamia, na wakuu wa hamsini hamsini, na wakuu wa kumi kumi; nao wawaamue watu hawa sikuzote; kisha, kila neno lililo kubwa watakuletea wewe, lakini kila neno dogo wataliamua wenyewe; basi kwako wewe mwenyewe utapata nafasi zaidi, nao watauchukua huo mzigo pamoja nawe. Kwamba utafanya jambo hili, na Mungu akikuagiza hivyo, basi utaweza kusimama wewe, na watu hawa wote nao watakwenda mahali pao kwa amani. Basi Musa akasikiza neno la mkwewe, akayafanya yote aliyokuwa amemwambia. Musa akawachagua watu wenye uwezo katika Israeli yote, akawaweka wawe vichwa juu ya watu, wakuu wa maelfu, na wakuu wa mamia, na wakuu wa hamsini hamsini, na wakuu wa kumi kumi. Nao wakawaamua watu sikuzote; mashauri magumu wakamletea Musa, lakini kila neno dogo wakaliamua wenyewe. Kisha Musa akaagana na mkwewe; naye akaenda zake, mpaka nchi yake mwenyewe.

Shirikisha
Soma Kutoka 18

Kutoka 18:1-27 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Basi Yethro, kuhani wa Midiani, baba mkwe wa Mose, akawa amesikia kila kitu Mungu alichomfanyia Mose na watu wake wa Israeli, pia jinsi BWANA alivyowatoa Israeli Misri. Baada ya Mose kumrudisha mkewe Sipora, Yethro baba mkwe wake alimpokea pamoja na wanawe wawili. Jina la mmoja aliitwa Gershomu, kwa kuwa Mose alisema, “Nimekuwa mgeni katika nchi ya kigeni.” Mwingine aliitwa Eliezeri, kwa kuwa alisema, “Mungu wa baba yangu alikuwa msaada wangu, akaniokoa kutoka upanga wa Farao.” Yethro, baba mkwe wa Mose, pamoja na wana wawili wa Mose na mkewe, wakamjia Mose huko jangwani, mahali alipokuwa amepiga kambi karibu na mlima wa Mungu. Yethro alikuwa ametuma ujumbe kwake Mose, kusema, “Mimi Yethro baba mkwe wako ninakuja kwako pamoja na mke wako na wanao wawili.” Kwa hiyo Mose akatoka kumlaki baba mkwe wake, akainama na kumbusu. Wakasalimiana, kisha wakaingia hemani. Mose akamwambia baba mkwe wake kuhusu kila kitu BWANA alichomfanyia Farao na Wamisri kwa ajili ya Israeli, na pia kuhusu shida zote walizokutana nazo njiani na jinsi BWANA alivyowaokoa. Yethro akafurahishwa sana kusikia juu ya mambo yote mazuri BWANA aliyowatendea Waisraeli kuwaokoa kutoka mkono wa Wamisri. Yethro akasema, “Sifa na ziwe kwa BWANA, aliyekuokoa wewe kutoka mikononi mwa Wamisri na Farao, na aliyewaokoa watu kutoka mikononi mwa Wamisri. Sasa najua ya kuwa BWANA ni mkuu kuliko miungu mingine yote, kwa kuwa amewatendea hivi wale waliowatenda Israeli kwa ujeuri.” Kisha Yethro, baba mkwe wa Mose, akaleta sadaka ya kuteketezwa na dhabihu nyingine kwa Mungu, naye Aroni pamoja na wazee wote wa Israeli wakaja kula chakula pamoja na baba mkwe wa Mose mbele za Mungu. Siku iliyofuata, Mose akachukua nafasi yake kama hakimu wa watu, nao wakasimama kumzunguka kuanzia asubuhi hadi jioni. Baba mkwe wake alipoona yote Mose anayowafanyia watu, akasema, “Ni nini hiki unachowafanyia watu? Kwa nini wewe unakuwa mwamuzi wa watu hawa peke yako, wakati watu hawa wamesimama wakikuzunguka tangu asubuhi mpaka jioni?” Mose akamjibu, “Kwa sababu watu wananijia kutaka mapenzi ya Mungu. Kila wakiwa na shauri huletwa kwangu, nami huamua kati ya mtu na mwenzake na kuwajulisha juu ya amri na sheria za Mungu.” Baba mkwe wa Mose akamjibu, “Unachofanya sio kizuri. Wewe pamoja na watu hawa wanaokujia mtajichosha bure. Kazi ni nzito sana kwako, huwezi kuibeba mwenyewe. Sasa nisikilize mimi, nitakupa shauri, naye Mungu na awe pamoja nawe. Yapasa wewe uwe mwakilishi wa watu mbele za Mungu na ulete mashauri yao kwake. Uwafundishe amri na sheria, tena uwaonyeshe namna ya kuishi na kazi zinazowapasa wao kufanya. Lakini uchague watu wenye uwezo miongoni mwa watu wote, watu wanaomwogopa Mungu, watu waaminifu wanaochukia mali ya dhuluma, uwateuwe wawe maafisa juu ya maelfu, mamia, hamsini na makumi. Waweke wawe waamuzi wa watu kwa wakati wote, lakini waambie wakuletee kila shauri lililo gumu; yale yaliyo rahisi wayaamue wao wenyewe. Hii itafanya mzigo wako kuwa mwepesi, kwa sababu watashirikiana nawe. Kama ukifanya hivi, na ikiwa Mungu ameagiza hivyo, utaweza kushinda uchovu, nao watu hawa wote watarudi nyumbani wameridhika.” Mose akamsikiliza baba mkwe wake na kufanya kila kitu alichosema. Mose akawachagua watu wenye uwezo kutoka Israeli yote, akawafanya kuwa viongozi wa watu, maafisa juu ya maelfu, mamia, hamsini na makumi. Wakatumika kama waamuzi wa watu kwa wakati wote. Mashauri magumu wakayaleta kwa Mose, lakini yale yaliyo rahisi wakayaamua wenyewe. Kisha Mose akaagana na Yethro baba mkwe wake, naye akarudi kwa nchi yake.

Shirikisha
Soma Kutoka 18

Kutoka 18:1-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi Yethro, kuhani wa Midiani, mkwewe Musa, alisikia habari ya mambo hayo yote Mungu aliyokuwa amemtendea Musa, na Waisraeli watu wake, jinsi BWANA alivyowaleta Israeli watoke Misri. Ndipo Yethro mkwewe Musa akamtwaa Sipora, mke wa Musa, baada ya yeye kumrudisha, pamoja na wanawe wawili; katika hao, jina la mmoja ni Gershomu, maana alisema, Mimi nimekuwa mgeni katika nchi ya ugenini; na jina la wa pili ni Eliezeri, kwa kuwa alisema, Yeye Mungu wa baba yangu alikuwa msaada wangu, akaniokoa na upanga wa Farao. Basi Yethro, mkwewe Musa, pamoja na mke wa Musa na wanawe wawili wakamwendea Musa huko nyikani, hapo alipokuwa amepanga, kwenye mlima wa Mungu; naye akamwambia Musa, Mimi Yethro mkweo nimekuja kwako, na mkeo, na wanawe wawili pamoja naye. Basi Musa akatoka nje ili amlaki mkwewe, akasujudia na kumbusu; nao wakaulizana habari; kisha wakaingia hemani. Musa akamwambia mkwewe mambo hayo yote BWANA aliyomtenda Farao na Wamisri kwa ajili ya Israeli, na mambo mazito yote yaliyowapata njiani, na jinsi BWANA alivyowaokoa. Yethro alifurahi kwa ajili ya wema wote BWANA aliowatendea Israeli, kwa alivyo waokoa mikononi mwa Wamisri. Kisha Yethro akasema, Na ahimidiwe BWANA aliyewaokoa na mikono ya Wamisri, na mkono wa Farao; aliyewaokoa watu hao watoke mikononi mwa Wamisri. Sasa najua ya kuwa BWANA ni mkuu kuliko miungu yote; naam, katika jambo hilo walilowatenda kwa unyeti. Yethro mkwewe Musa akamletea Mungu sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; na Haruni akaja, na wazee wote wa Israeli, wale chakula pamoja na mkwewe Musa mbele za Mungu. Asubuhi yake Musa akaketi ili awapishie hukumu watu; na hao watu wakasimama kumzunguka Musa tangu asubuhi hata jioni. Mkwewe Musa alipoyaona yote aliyowafanyia watu, akasema, Ni jambo gani hili uwatendealo hao watu? Kwani wewe kuketi hapo peke yako, na watu wote kusimama kwako tangu asubuhi hata jioni? Musa akamwambia mkwewe, Ni kwa sababu watu hunijilia mimi wapate kumwuliza Mungu; wakiwa na neno, hunijilia; nami naamua kati ya mtu na mwenziwe, nami nawajuvisha amri za Mungu, na sheria zake. Mkwewe Musa akamwambia, Jambo hili ufanyalo si jema. Huna budi utadhoofika wewe, na hawa watu walio pamoja nawe pia; maana jambo hili ni zito mno kwako; huwezi wewe kulitenda peke yako. Sikiza sasa neno langu, nitakupa shauri, na Mungu na awe pamoja nawe; uwe wewe kwa ajili ya watu mbele ya Mungu, nawe umletee Mungu maneno yao; nawe utawafundisha zile amri na sheria, nawe utawaonyesha njia ambayo inawapasa kuiendea, na kazi ambayo inawapasa kuifanya. Zaidi ya hayo utajipatia katika watu hawa watu walio na uwezo, wenye kumcha Mungu, watu wa kweli, wenye kuchukia mapato ya udhalimu; ukawaweka juu yao, wawe wakuu wa maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini, na wakuu wa kumi; nao wawaamue watu hawa sikuzote; kisha, kila neno lililo kubwa watakuletea wewe, lakini kila neno dogo wataliamua wenyewe; basi kwako wewe mwenyewe utapata nafasi zaidi, nao watauchukua huo mzigo pamoja nawe. Kwamba utafanya jambo hili, na Mungu akikuagiza hivyo, basi utaweza kusimama wewe, na watu hawa wote nao watakwenda mahali pao kwa amani. Basi Musa akasikiza neno la mkwewe, akayafanya yote aliyokuwa amemwambia. Musa akawachagua watu wenye uwezo katika Israeli yote, akawaweka wawe vichwa juu ya watu, wakuu wa maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini, na wakuu wa kumi. Nao wakawaamua watu sikuzote; mashauri magumu wakamletea Musa, lakini kila neno dogo wakaliamua wenyewe. Kisha Musa akaagana na mkwewe; naye akaenda zake, mpaka nchi yake mwenyewe.

Shirikisha
Soma Kutoka 18

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha