Kutoka 17:1-7
Kutoka 17:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Kutoka jangwa la Sini, jumuiya yote ya Waisraeli ilisafiri hatua kwa hatua kama alivyoamuru Mwenyezi-Mungu, watu wakapiga kambi huko Refidimu. Lakini huko hakukuwa na maji ya kunywa. Kwa hiyo watu wakamnungunikia Mose wakisema, “Tupe maji ya kunywa.” Mose akawauliza, “Mbona mnaninungunikia? Mbona mnamjaribu Mwenyezi-Mungu?” Lakini wote walikuwa na kiu, wakamnungunikia Mose wakisema, “Kwa nini ulitutoa kule Misri utuue kwa kiu sisi sote na watoto wetu na mifugo yetu?” Basi, Mose akamlilia Mwenyezi-Mungu akisema, “Nitawafanyia nini watu hawa? Wako karibu kunipiga mawe!” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Pita mbele ya watu hawa ukiwachukua wazee wao kadhaa; chukua pia mkononi mwako ile fimbo uliyoipiga nayo mto Nili. Tazama mimi nitasimama mbele yako mwambani pale Horebu, nawe utaupiga huo mwamba na maji yatabubujika kutoka humo ili watu wote wapate kunywa.” Basi, Mose akafanya hivyo mbele ya wazee wa Waisraeli. Mahali hapo Mose akapaita “Masa” na “Meriba”, kwa sababu Waisraeli walimnungunikia na kumjaribu Mwenyezi-Mungu wakisema, “Je, kweli Mwenyezi-Mungu yu pamoja nasi?”
Kutoka 17:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mkutano wote wa wana wa Israeli ukasafiri, kutoka bara ya Sini kwa safari zao, kama BWANA alivyowaagiza, wakatua Refidimu; napo hapakuwa na maji, watu wanywe. Kwa hiyo hao watu wakamgombeza Musa, wakasema, Tupe maji tunywe. Musa akawaambia, Kwa nini mnanigombeza? Mbona mnamjaribu BWANA? Watu wakawa na kiu huko; nao wakamnung'unikia Musa, wakasema, Mbona umetupandisha kutoka Misri, kutuua sisi na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu? Musa akamlilia BWANA, akisema, Niwatendee nini watu hawa? Bado kidogo nao watanipiga kwa mawe. BWANA akamwambia Musa, Pita mbele ya watu, ukawachukue baadhi ya wazee wa Israeli pamoja nawe; na ile fimbo yako ambayo uliupiga mto kwayo, uitwae mkononi mwako, ukaende. Tazama, nitasimama mbele yako huko, juu ya lile jabali katika Horebu; nawe utalipiga jabali, na maji yatatoka, watu wapate kunywa. Musa akafanya hivyo mbele ya wazee wa Israeli. Akapaita mahali pale jina lake Masa, na Meriba kwa sababu ya ugomvi wa wana wa Israeli, na kwa sababu walimjaribu BWANA, wakisema, Je! BWANA yu kati yetu au sivyo?
Kutoka 17:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mkutano wote wa wana wa Israeli ukasafiri, kutoka bara ya Sini kwa safari zao, kama BWANA alivyowaagiza, wakatua Refidimu; napo hapakuwa na maji, watu wanywe. Kwa hiyo hao watu wakateta na Musa, wakasema, Tupe maji tunywe. Musa akawaambia, Kwani kuteta na mimi? Mbona mnamjaribu BWANA? Watu wakawa na kiu huko; nao wakamnung’unikia Musa, wakasema, Mbona umetupandisha kutoka Misri, kutuua sisi na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu? Musa akamlilia BWANA, akisema, Niwatendee nini watu hawa? Bado kidogo nao watanipiga kwa mawe. BWANA akamwambia Musa, Pita mbele ya watu, ukawachukue baadhi ya wazee wa Israeli pamoja nawe; na ile fimbo yako ambayo uliupiga mto kwayo, uitwae mkononi mwako, ukaende. Tazama, nitasimama mbele yako huko, juu ya lile jabali katika Horebu; nawe utalipiga jabali, na maji yatatoka, watu wapate kunywa. Musa akafanya hivyo mbele ya wazee wa Israeli. Akapaita mahali pale jina lake Masa, na Meriba; kwa sababu ya mateto ya wana wa Israeli, na kwa sababu walimjaribu BWANA, wakisema, Je! BWANA yu kati yetu au sivyo?
Kutoka 17:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Jumuiya yote ya Israeli ikaondoka kutoka Jangwa la Sini, ikisafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine kama BWANA alivyoagiza. Wakapiga kambi huko Refidimu, lakini hapakuwa na maji ya watu kunywa. Kwa hiyo wakagombana na Mose wakisema, “Tupe maji ya kunywa.” Mose akajibu, “Mbona mnagombana nami? Kwa nini mnamjaribu BWANA?” Lakini watu walikuwa na kiu huko, wakanungʼunika dhidi ya Mose, wakisema, “Kwa nini ulitutoa kule Misri, ukatuleta hapa utuue kwa kiu sisi, watoto wetu na mifugo yetu?” Kisha Mose akamlilia BWANA, akasema, “Niwafanyie nini watu hawa? Sasa wanakaribia kunipiga kwa mawe.” BWANA akamjibu Mose, “Pita mbele ya watu. Wachukue pamoja nawe baadhi ya wazee wa Israeli, ichukue mkononi mwako ile fimbo uliyopiga nayo Mto Naili, nawe uende. Huko nitasimama mbele yako karibu na mwamba wa Horebu. Uupige mwamba na maji yatatoka ndani yake kwa ajili ya watu kunywa.” Kwa hiyo Mose akafanya haya mbele ya wazee wa Israeli. Naye akapaita mahali pale Masa, na Meriba kwa sababu Waisraeli waligombana na kumjaribu BWANA wakisema, “Je, BWANA yu pamoja nasi au la?”