Kutoka 16:1-35
Kutoka 16:1-35 Biblia Habari Njema (BHN)
Jumuiya yote ya Waisraeli iliondoka, ikafika jangwa la Sini kati ya Elimu na Sinai. Hii ilikuwa siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili tangu walipoondoka nchini Misri. Basi, jumuiya yote ya Waisraeli ikawalalamikia Mose na Aroni huko jangwani, “Laiti Mwenyezi-Mungu angelituua tulipokuwa nchini Misri ambako tulikaa, tukala nyama na mikate hata tukashiba. Lakini nyinyi mmetuleta huku jangwani kuiua jumuiya hii yote kwa njaa!” Ndipo Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mimi nitawanyeshea mikate kutoka mbinguni. Kila siku watu watatoka na kukusanya chakula cha siku hiyo. Kwa njia hii nitawajaribu nione kama watazifuata sheria zangu au hawatazifuata. Lakini siku ya sita, wakati watakapoandaa chakula walichokusanya, kiasi hicho kitakuwa mara mbili ya chakula cha kila siku.” Basi, Mose na Aroni wakawaambia watu wote wa Israeli, “Jioni, mtatambua kwamba Mwenyezi-Mungu ndiye aliyewatoa nchini Misri! Tena, kesho asubuhi, mtauona utukufu wa Mwenyezi-Mungu kwani ameyasikia manunguniko mliyomnungunikia. Sisi ni nani hata mtunungunikie?” Tena Mose akasema, “Jioni, Mwenyezi-Mungu atawapeni nyama mle, na asubuhi atawapeni mikate mle mshibe, maana yeye ameyasikia manunguniko mliyomnungunikia. Sisi ni nani hata mtunungunikie? Msitunungunikie sisi bali mnungunikieni Mwenyezi-Mungu.” Kisha Mose akamwambia Aroni, “Iambie jumuiya yote ya Waisraeli ikusanyike mbele ya Mwenyezi-Mungu kwani ameyasikia manunguniko yenu.” Wakati Aroni alipokuwa akizungumza na jumuiya ya Waisraeli, watu wote walitazama huko jangwani, na mara utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukaonekana mawinguni. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nimeyasikia manunguniko ya Waisraeli. Basi, waambie kwamba wakati wa jioni watakula nyama, na asubuhi watakula mkate. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.” Basi, mnamo wakati wa jioni kukaja kware wengi, wakafunika kambi ya Waisraeli. Asubuhi yake kukatokea umande, ukatanda kandokando ya kambi yao. Umande huo ulipotoweka, kukabaki huko nyikani kitu kama mkate mwembamba na mwepesi. Waisraeli walipoona kitu hicho walishangaa, wakaulizana, “Nini hiki?” Hawakujua kilikuwa kitu gani. Basi, Mose akawaambia, “Huu ni mkate ambao Mwenyezi-Mungu amewapa mle. Mwenyezi-Mungu ameamuru mfanye hivi: Kila mtu na akusanye chakula kiasi anachoweza kula; ataokota kiasi cha pishi moja kwa kila mtu hemani mwake.” Basi, Waisraeli wakafanya hivyo, na ikawa kwamba, wengine waliokota kwa wingi na wengine kidogo. Lakini wote walipokipima kipimo walichookota katika pishi, waligundua kuwa aliyeokota kingi hakuwa na cha ziada, na aliyeokota kidogo, hakupungukiwa. Kila mmoja alikuwa ameokota kiasi alichoweza kula. Mose akawaambia watu, “Mtu yeyote asibakize chakula hicho mpaka asubuhi.” Lakini watu hawakumsikiliza Mose. Baadhi yao walijibakizia chakula mpaka asubuhi. Lakini asubuhi chakula hicho kikawa kimeoza na kuwa na mabuu. Mose akawakasirikia sana watu. Basi, kila asubuhi walikusanya chakula kila mtu kiasi alichohitaji kula. Jua lilipopanda juu na kuwa kali, kile chakula kingine kiliyeyuka. Katika siku ya sita, Waisraeli walikusanya chakula hicho maradufu, pishi nne kwa kila mtu. Basi, wazee wote wa jumuiya ya Waisraeli walimwendea Mose, wakamweleza jambo hilo. Mose akawaambia, “Hii ndiyo amri ya Mwenyezi-Mungu. Kesho ni siku rasmi ya mapumziko; ni Sabato takatifu ya Mwenyezi-Mungu. Basi, nendeni mkapike au mkachemshe kile chakula mnachohitaji leo, na chakula kitakachosalia kiwekeni mpaka kesho.” Basi, wakafanya hivyo na kukiacha chakula kingine mpaka kesho yake kama Mose alivyosema. Asubuhi yake waliona kwamba hakikuharibika wala kuwa na mabuu. Basi, Mose akawaambia, “Kuleni chakula hicho kilichosalia kwa sababu leo ni Sabato ya Mwenyezi-Mungu. Leo hamtapata chakula huko nje. Kwa siku sita mtakuwa mkikusanya chakula hiki, lakini siku ya saba ambayo ni Sabato hakitakuwapo.” Mnamo siku ya saba watu kadhaa walitoka kwenda kutafuta chakula, lakini hawakukipata. Hapo Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mpaka lini mtakataa kuzitii amri na Sheria zangu? Fahamuni kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nimewapa siku ya Sabato, ndiyo maana nikawapa chakula cha siku mbili mnamo siku ya sita. Basi, pumzikeni kila mtu nyumbani mwake; mtu yeyote asitoke katika siku ya saba.” Kwa hiyo, watu walipumzika siku ya saba. Waisraeli walikiita chakula hicho “Mana.” Kilikuwa kama mbegu za mtama mweupe na ladha yake ilikuwa kama mkate mwembamba uliotiwa asali. Mose akawaambia, “Hili ndilo agizo la Mwenyezi-Mungu: Chukueni kiasi cha pishi moja ya mana na kuiweka kwa ajili ya wazawa wenu, ili waweze kuona chakula nilichowalisha jangwani wakati nilipowatoa nchini Misri.” Mose akamwambia Aroni, “Chukua gudulia utie ndani pishi moja ya mana na kuiweka mbele ya Mwenyezi-Mungu, iwe kwa ajili ya wazawa wenu.” Basi, Aroni akaiweka mana mahali patakatifu mbele ya sanduku la agano ili ihifadhiwe kama vile Mwenyezi-Mungu alivyomwagiza Mose. Waisraeli walikula mana kwa muda wa miaka arubaini, mpaka walipofika katika nchi iliyofaa kuishi, nchi iliyokuwako mpakani mwa Kanaani ambako walifanya makao yao.
Kutoka 16:1-35 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha wakasafiri kutoka Elimu, na mkutano wote wa wana wa Israeli wakafikia jangwa la Sini, lililoko kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka kwao nchi ya Misri. Na mkutano mzima wa wana wa Israeli ukawanung'unikia Musa na Haruni, huko barani; wana wa Israeli wakawaambia, Laiti tungalikufa kwa mkono wa BWANA katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula vyakula hata kushiba; kwani mmetutoa huko na kututia katika bara hii, ili kutuua kwa njaa kusanyiko hili lote. Ndipo BWANA akamwambia Musa, Tazama, mimi nitawanyeshea ninyi mvua ya mkate kutoka mbinguni; na hao watu watatoka nje na kuokota kila siku sehemu ya siku; ili nipate kuwajaribu, kwamba watakwenda katika sheria yangu, ama sivyo. Kisha itakuwa siku ya sita, ya kwamba watayaandaa hayo watakayoleta ndani, nayo yatakuwa ni mara mbili kuliko wayaokotayo kila siku. Musa na Haruni wakawaambia wana wote wa Israeli, Jioni ndipo mtakapojua ya kuwa BWANA amewaleta kutoka nchi ya Misri; na asubuhi ndipo mtakapouona utukufu wa BWANA; kwa kuwa yeye husikia manung'uniko yenu mliyomnung'unikia BWANA; na sisi tu nani, hata mkatunung'unikia? Musa akasema, Ndilo litakalokuwa, hapo BWANA atakapowapa nyama wakati wa jioni mle, na asubuhi mikate hata mkakinai; kwa kuwa BWANA asikia manung'uniko yenu mliyomnung'unikia yeye; na sisi tu nani? Manung'uniko yenu hayakuwa juu yetu sisi, ila juu ya BWANA. Musa akamwambia Haruni, Haya, sema na mkutano wote wa wana wa Israeli, Njoni karibu mbele ya BWANA; kwa kuwa yeye ameyasikia manung'uniko yenu. Ilikuwa Haruni aliponena na huo mkutano wote wa wana wa Israeli, wakaangalia upande wa bara, na tazama, utukufu wa BWANA ukaonekana katika hilo wingu. BWANA akasema na Musa, akinena, Nimeyasikia manung'uniko ya wana wa Israeli; haya sema nao ukinena, Wakati wa jioni mtakula nyama, na wakati wa asubuhi mtashiba mkate; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Ikawa wakati wa jioni, kware wakaja, wakaifunikiza kambi; na wakati wa asubuhi umande ulikuwa juu ya nchi pande zote za kituo. Na ulipokauka ule umande uliokuwa juu ya nchi, kumbe! Juu ya uso wa bara kitu kidogo kilichoviringana, kidogo kama barafu juu ya nchi. Wana wa Israeli walipokiona, wakaambiana, Nini hiki? Maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, Ndio mkate ambao BWANA amewapa ninyi, mle. Neno hili ndilo aliloagiza BWANA, Okoteni ninyi kitu hicho kila mtu kama ulaji wake ulivyo; kila mtu pishi moja kama hesabu ya watu wenu ilivyo; ndivyo mtakavyotwaa, kila mtu kwa ajili ya hao walioko hemani mwake. Wana wa Israeli wakafanya hivyo, wakaokota wengine zaidi, wengine kupungua. Nao walipoipima kwa pishi, yeye aliyekuwa ameokota kingi hakubakiwa na kitu, na yeye aliyekuwa ameokota kichache hakupungukiwa; wakaokota kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa. Musa akawaambia, Mtu awaye yote asikisaze hata asubuhi. Lakini hawakumsikiza Musa; wengine miongoni mwao wakakisaza hata asubuhi, nacho kikaingia mabuu na kutoa uvundo; Musa akawakasirikia sana. Basi wakaokota asubuhi baada ya asubuhi, kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa; na hapo jua lilipokuwa ni kali, kikayeyuka. Basi ikawa siku ya sita wakaokota kile chakula sehemu maradufu, kila mtu pishi mbili; na wazee wote wa mkutano wakaenda na kumwambia Musa. Akawaambia, Ndilo neno alilonena BWANA Kesho ni starehe takatifu, Sabato takatifu kwa BWANA; okeni mtakachooka, na kutokosa mtakachotokosa; na hicho kitakachowasalia jiwekeeni kilindwe hata asubuhi. Basi wakakiweka hata asubuhi, kama Musa alivyowaagiza; nacho hakikutoa uvundo wala kuingia mabuu. Musa akasema, Haya, kuleni hiki leo; kwa kuwa leo ni Sabato ya BWANA; leo hamtakiona nje barani. Siku sita mtaokota; lakini siku ya saba ni Sabato, siku hiyo hakitapatikana. Ikawa siku ya saba wengine wakatoka kwenda kukiokota, wasikione. BWANA akamwambia Musa, Mtakataa kuyashika maagizo yangu na sheria zangu hata lini? Angalieni, kwa kuwa BWANA amewapa ninyi hiyo Sabato, kwa sababu hii huwapa siku ya sita chakula cha siku mbili; kaeni kila mtu mahali pake, mtu awaye yote asiondoke mahali pake kwa siku ya saba. Basi hao watu wakapumzika kwa siku ya saba. Na nyumba ya Israeli wakakiita jina lake Mana; nacho kilikuwa mfano wa chembe za mtama, nyeupe; na utamu wake ulikuwa kama utamu wa maandazi membamba yaliyoandaliwa kwa asali. Musa akasema, Hili ni neno BWANA aliloliamuru, Pishi moja ya kitu hicho na kiwekwe kwa ajili ya vizazi vyenu; ili kwamba wao wapate kukiona kile chakula nilichowalisha ninyi barani, hapo nilipowaleta kutoka nchi ya Misri. Basi Musa akamwambia Haruni, Twaa kopo, ukatie pishi moja ya hiyo Mana ndani yake, uiweke mbele ya BWANA, ilindwe kwa ajili ya vizazi vyenu. Kama vile BWANA alivyomwagizia Musa ndivyo Haruni alivyoiweka hapo mbele ya Ushahidi, ili ilindwe. Na wana wa Israeli walikula Mana muda wa miaka arubaini, hata walipofikia nchi iliyo na watu, wakala ile Mana, hata walipofikia mipakani mwa nchi ya Kanaani.
Kutoka 16:1-35 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha wakasafiri kutoka Elimu, na mkutano wote wa wana wa Israeli wakafikilia bara ya Sini, iliyoko kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka kwao nchi ya Misri. Na mkutano mzima wa wana wa Israeli ukawanung’unikia Musa na Haruni, huko barani; wana wa Israeli wakawaambia, Laiti tungalikufa kwa mkono wa BWANA katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula vyakula hata kushiba; kwani mmetutoa huko na kututia katika bara hii, ili kutuua kwa njaa kusanyiko hili lote. Ndipo BWANA akamwambia Musa, Tazama, mimi nitawanyeshea ninyi mvua ya mkate kutoka mbinguni; na hao watu watatoka nje na kuokota kila siku sehemu ya siku; ili nipate kuwajaribu, kwamba watakwenda katika sheria yangu, ama sivyo. Kisha itakuwa siku ya sita, ya kwamba watayaandaa hayo watakayoleta ndani, nayo yatakuwa ni mara mbili kuliko wayaokotayo kila siku. Musa na Haruni wakawaambia wana wote wa Israeli, Jioni ndipo mtakapojua ya kuwa BWANA amewaleta kutoka nchi ya Misri; na asubuhi ndipo mtakapouona utukufu wa BWANA; kwa kuwa yeye asikia manung’uniko yenu mliyomnung’unikia BWANA; na sisi tu nani, hata mkatunung’unikia? Musa akasema, Ndilo litakalokuwa, hapo BWANA atakapowapa nyama wakati wa jioni mle, na asubuhi mikate hata mkakinai; kwa kuwa BWANA asikia manung’uniko yenu mliyomnung’unikia yeye; na sisi tu nani? Manung’uniko yenu hayakuwa juu yetu sisi, ila juu ya BWANA. Musa akamwambia Haruni, Haya, sema na mkutano wote wa wana wa Israeli, Njoni karibu mbele ya BWANA; kwa kuwa yeye ameyasikia manung’uniko yenu. Ilikuwa Haruni aliponena na huo mkutano wote wa wana wa Israeli, wakaangalia upande wa bara, na tazama, utukufu wa BWANA ukaonekana katika hilo wingu. BWANA akasema na Musa, akinena, Nimeyasikia manung’uniko ya wana wa Israeli; haya sema nao, ukinena, Wakati wa jioni mtakula nyama, na wakati wa asubuhi mtashiba mkate; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Ikawa wakati wa jioni, kware wakakaribia, wakakifunikiza kituo; na wakati wa asubuhi umande ulikuwa juu ya nchi pande zote za kituo. Na ulipoinuka ule umande uliokuwa juu ya nchi, kumbe! Juu ya uso wa bara kitu kidogo kilichoviringana, kidogo kama sakitu juu ya nchi. Wana wa Israeli walipokiona, wakaambiana, Nini hiki? Maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, Ndio mkate ambao BWANA amewapa ninyi, mle. Neno hili ndilo aliloagiza BWANA, Okoteni ninyi kitu hicho kila mtu kama ulaji wake ulivyo; kichwa pishi, kama hesabu ya watu wenu ilivyo; ndivyo mtakavyotwaa, kila mtu kwa ajili ya hao walioko hemani mwake. Wana wa Israeli wakafanya hivyo, wakaokota wengine zaidi, wengine kupungua. Nao walipoipima kwa pishi, yeye aliyekuwa ameokota kingi hakubakiwa na kitu, na yeye aliyekuwa ameokota kichache hakupungukiwa; wakaokota kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa. Musa akawaambia, Mtu awaye yote asikisaze hata asubuhi. Lakini hawakumsikiza Musa; wengine miongoni mwao wakakisaza hata asubuhi, nacho kikaingia mabuu na kutoa uvundo; Musa akawakasirikia sana. Basi wakaokota asubuhi baada ya asubuhi, kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa; na hapo jua lilipokuwa ni kali, kikayeyuka. Basi ikawa siku ya sita wakaokota kile chakula sehemu maradufu, kila mtu pishi mbili; na wazee wote wa mkutano wakaenda na kumwambia Musa. Akawaambia, Ndilo neno alilonena BWANA Kesho ni starehe takatifu, Sabato takatifu kwa BWANA; okeni mtakachooka, na kutokosa mtakachotokosa; na hicho kitakachowasalia jiwekeeni kilindwe hata asubuhi. Basi wakakiweka hata asubuhi, kama Musa alivyowaagiza; nacho hakikutoa uvundo wala kuingia mabuu. Musa akasema, Haya, kuleni hiki leo; kwa kuwa leo ni Sabato ya BWANA; leo hamtakiona nje barani. Siku sita mtaokota; lakini siku ya saba ni Sabato, siku hiyo hakitapatikana. Ikawa siku ya saba wengine wakatoka kwenda kukiokota, wasikione. BWANA akamwambia Musa, Mtakataa kuyashika maagizo yangu na sheria zangu hata lini? Angalieni, kwa kuwa BWANA amewapa ninyi hiyo Sabato, kwa sababu hii huwapa siku ya sita chakula cha siku mbili; kaeni kila mtu mahali pake, mtu awaye yote asiondoke mahali pake kwa siku ya saba. Basi hao watu wakapumzika kwa siku ya saba. Na nyumba ya Israeli wakakiita jina lake Mana; nacho kilikuwa mfano wa chembe za mtama, nyeupe; na tamu yake ilikuwa kama tamu ya maandazi membamba yaliyoandaliwa kwa asali. Musa akasema, Hili ni neno BWANA aliloliamuru, Pishi moja ya kitu hicho na kiwekwe kwa ajili ya vizazi vyenu; ili kwamba wao wapate kukiona kile chakula nilichowalisha ninyi barani, hapo nilipowaleta kutoka nchi ya Misri. Basi Musa akamwambia Haruni, Twaa kopo, ukatie pishi moja ya hiyo Mana ndani yake, uiweke mbele ya BWANA, ilindwe kwa ajili ya vizazi vyenu. Kama vile BWANA alivyomwagizia Musa ndivyo Haruni alivyoiweka hapo mbele ya Ushahidi, ili ilindwe. Na wana wa Israeli walikula Mana muda wa miaka arobaini, hata walipofikilia nchi iliyo na watu, wakala ile Mana, hata walipofikilia mipakani mwa nchi ya Kanaani.
Kutoka 16:1-35 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Jumuiya yote ya Kiisraeli ikaondoka Elimu, wakafika Jangwa la Sini, lililokuwa kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka Misri. Huko jangwani hiyo jumuiya yote wakawanungʼunikia Mose na Aroni. Waisraeli wakawaambia, “Laiti tungelikufa kwa mkono wa BWANA huko Misri! Huko tuliketi tukizunguka masufuria ya nyama na tukala vyakula tulivyovitaka, lakini ninyi mmetuleta huku jangwani ili mpate kuua mkutano huu wote kwa njaa.” Kisha BWANA akamwambia Mose, “Nitanyesha mikate kutoka mbinguni kwa ajili yenu. Watu watatoka kila siku na kukusanya kitakachowatosha kwa siku ile, kwa njia hii, nitawajaribu nione kama watafuata maelekezo yangu. Siku ya sita watatayarisha kile waletacho ndani, nacho kitakuwa mara mbili kuliko ya kile walichokusanya kila siku.” Kwa hiyo Mose na Aroni wakawaambia Waisraeli wote, “Jioni mtajua kwamba BWANA ndiye aliwatoa Misri, kisha asubuhi mtauona utukufu wa BWANA, kwa sababu amesikia manungʼuniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani hata mtunungʼunikie?” Pia Mose akasema, “Mtajua kuwa alikuwa BWANA wakati atakapowapa nyama mle ifikapo jioni na mikate yote mtakayohitaji asubuhi kwa sababu amesikia manungʼuniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani? Hamnungʼuniki dhidi yetu, bali dhidi ya BWANA.” Kisha Mose akamwambia Aroni, “Iambie jumuiya yote ya Waisraeli kwamba, ‘Mje mbele zake BWANA, kwa maana amesikia manungʼuniko yenu.’ ” Aroni alipokuwa akizungumza na jumuiya yote ya Waisraeli, wakatazama kuelekea jangwani, na huko wakaona utukufu wa BWANA ukitokeza katika wingu. BWANA akamwambia Mose, “Nimesikia manungʼuniko ya Waisraeli. Waambie, ‘Jioni mtakula nyama, na asubuhi mtashiba mikate. Ndipo mtajua ya kwamba Mimi ndimi BWANA Mungu wenu.’ ” Jioni ile kware wakaja wakaifunika kambi na asubuhi kulikuwa na tabaka la umande kuzunguka kambi. Wakati umande ulipoondoka, vipande vidogo vidogo kama theluji vilionekana juu ya uso wa jangwa. Waisraeli walipoona, wakaambiana, “Hiki ni nini?” Kwa kuwa hawakujua kilikuwa kitu gani. Mose akawaambia, “Huu ndio mkate ambao BWANA amewapa mle. Hivi ndivyo BWANA alivyoamuru: ‘Kila mmoja akusanye kiasi anachohitaji. Chukueni pishi moja kwa kila mtu mliye naye katika hema yenu.’ ” Waisraeli wakafanya kama walivyoambiwa, baadhi yao wakakusanya zaidi, wengine pungufu. Nao walipopima katika pishi, yule aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa. Kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji. Kisha Mose akawaambia, “Mtu yeyote asibakize chochote mpaka asubuhi.” Hata hivyo, wengine hawakuzingatia aliyosema Mose, wakahifadhi kiasi fulani mpaka asubuhi, lakini kile alichohifadhi kikajaa mabuu na kuanza kunuka. Kwa hiyo Mose akawakasirikia. Kila asubuhi, kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji na jua lilipokuwa kali, iliyeyuka. Siku ya sita, wakakusanya mara mbili, kiasi cha pishi mbili kwa kila mtu, nao viongozi wa jumuiya wakaja kumwarifu Mose. Mose akawaambia, “Hivi ndivyo alivyoagiza BWANA: ‘Kesho itakuwa siku ya mapumziko, Sabato takatifu kwa BWANA. Kwa hiyo okeni kile mnachotaka kuoka na mchemshe kile mnachotaka kuchemsha. Hifadhini chochote kinachobaki na mkiweke mpaka asubuhi.’ ” Kwa hiyo wakavihifadhi mpaka asubuhi, kama Mose alivyoagiza, na havikunuka wala kuwa na mabuu. Mose akawaambia, “Kuleni leo, kwa sababu leo ni Sabato kwa BWANA. Hamtapata chochote juu ya nchi leo. Kwa siku sita mtakusanya, lakini siku ya saba, yaani Sabato, hakutakuwepo chochote.” Hata hivyo, baadhi ya watu wakatoka kwenda kukusanya siku ya saba, lakini hawakupata chochote. Ndipo BWANA akamwambia Mose, “Je, mtaacha kushika maagizo na maelekezo yangu mpaka lini? Fahamuni kuwa BWANA amewapa ninyi Sabato, ndiyo sababu katika siku ya sita amewapa mikate ya siku mbili. Kila mmoja inampasa kukaa pale alipo katika siku ya saba. Hata mmoja haruhusiwi kutoka.” Kwa hiyo watu wakapumzika siku ya saba. Watu wa Israeli wakaita ile mikate mana Ilikuwa myeupe kama mbegu za mtama na ladha yake ilikuwa kama mkate mwembamba uliotengenezwa kwa asali. Mose akasema, “Hivi ndivyo alivyoagiza BWANA: ‘Chukueni pishi ya mana na kuhifadhi kwa ajili ya vizazi vijavyo ili vione mikate niliyowapa mle jangwani nilipowatoa katika nchi ya Misri.’ ” Kwa hiyo Mose akamwambia Aroni, “Chukua gudulia na uweke pishi moja ya mana ndani yake. Kisha uweke mbele za BWANA ili kihifadhiwe kwa ajili ya vizazi vijavyo.” Kama BWANA alivyomwagiza Mose, hatimaye Aroni alikuja kuihifadhi ndani ya Sanduku la Ushuhuda. Waisraeli wakala mana kwa miaka arobaini, mpaka walipofika katika nchi iliyokaliwa na watu; walikula mana hadi walipofika mpakani mwa Kanaani.