Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 16:1-18

Kutoka 16:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)

Jumuiya yote ya Waisraeli iliondoka, ikafika jangwa la Sini kati ya Elimu na Sinai. Hii ilikuwa siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili tangu walipoondoka nchini Misri. Basi, jumuiya yote ya Waisraeli ikawalalamikia Mose na Aroni huko jangwani, “Laiti Mwenyezi-Mungu angelituua tulipokuwa nchini Misri ambako tulikaa, tukala nyama na mikate hata tukashiba. Lakini nyinyi mmetuleta huku jangwani kuiua jumuiya hii yote kwa njaa!” Ndipo Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mimi nitawanyeshea mikate kutoka mbinguni. Kila siku watu watatoka na kukusanya chakula cha siku hiyo. Kwa njia hii nitawajaribu nione kama watazifuata sheria zangu au hawatazifuata. Lakini siku ya sita, wakati watakapoandaa chakula walichokusanya, kiasi hicho kitakuwa mara mbili ya chakula cha kila siku.” Basi, Mose na Aroni wakawaambia watu wote wa Israeli, “Jioni, mtatambua kwamba Mwenyezi-Mungu ndiye aliyewatoa nchini Misri! Tena, kesho asubuhi, mtauona utukufu wa Mwenyezi-Mungu kwani ameyasikia manunguniko mliyomnungunikia. Sisi ni nani hata mtunungunikie?” Tena Mose akasema, “Jioni, Mwenyezi-Mungu atawapeni nyama mle, na asubuhi atawapeni mikate mle mshibe, maana yeye ameyasikia manunguniko mliyomnungunikia. Sisi ni nani hata mtunungunikie? Msitunungunikie sisi bali mnungunikieni Mwenyezi-Mungu.” Kisha Mose akamwambia Aroni, “Iambie jumuiya yote ya Waisraeli ikusanyike mbele ya Mwenyezi-Mungu kwani ameyasikia manunguniko yenu.” Wakati Aroni alipokuwa akizungumza na jumuiya ya Waisraeli, watu wote walitazama huko jangwani, na mara utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukaonekana mawinguni. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nimeyasikia manunguniko ya Waisraeli. Basi, waambie kwamba wakati wa jioni watakula nyama, na asubuhi watakula mkate. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.” Basi, mnamo wakati wa jioni kukaja kware wengi, wakafunika kambi ya Waisraeli. Asubuhi yake kukatokea umande, ukatanda kandokando ya kambi yao. Umande huo ulipotoweka, kukabaki huko nyikani kitu kama mkate mwembamba na mwepesi. Waisraeli walipoona kitu hicho walishangaa, wakaulizana, “Nini hiki?” Hawakujua kilikuwa kitu gani. Basi, Mose akawaambia, “Huu ni mkate ambao Mwenyezi-Mungu amewapa mle. Mwenyezi-Mungu ameamuru mfanye hivi: Kila mtu na akusanye chakula kiasi anachoweza kula; ataokota kiasi cha pishi moja kwa kila mtu hemani mwake.” Basi, Waisraeli wakafanya hivyo, na ikawa kwamba, wengine waliokota kwa wingi na wengine kidogo. Lakini wote walipokipima kipimo walichookota katika pishi, waligundua kuwa aliyeokota kingi hakuwa na cha ziada, na aliyeokota kidogo, hakupungukiwa. Kila mmoja alikuwa ameokota kiasi alichoweza kula.

Shirikisha
Soma Kutoka 16

Kutoka 16:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kisha wakasafiri kutoka Elimu, na mkutano wote wa wana wa Israeli wakafikia jangwa la Sini, lililoko kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka kwao nchi ya Misri. Na mkutano mzima wa wana wa Israeli ukawanung'unikia Musa na Haruni, huko barani; wana wa Israeli wakawaambia, Laiti tungalikufa kwa mkono wa BWANA katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula vyakula hata kushiba; kwani mmetutoa huko na kututia katika bara hii, ili kutuua kwa njaa kusanyiko hili lote. Ndipo BWANA akamwambia Musa, Tazama, mimi nitawanyeshea ninyi mvua ya mkate kutoka mbinguni; na hao watu watatoka nje na kuokota kila siku sehemu ya siku; ili nipate kuwajaribu, kwamba watakwenda katika sheria yangu, ama sivyo. Kisha itakuwa siku ya sita, ya kwamba watayaandaa hayo watakayoleta ndani, nayo yatakuwa ni mara mbili kuliko wayaokotayo kila siku. Musa na Haruni wakawaambia wana wote wa Israeli, Jioni ndipo mtakapojua ya kuwa BWANA amewaleta kutoka nchi ya Misri; na asubuhi ndipo mtakapouona utukufu wa BWANA; kwa kuwa yeye husikia manung'uniko yenu mliyomnung'unikia BWANA; na sisi tu nani, hata mkatunung'unikia? Musa akasema, Ndilo litakalokuwa, hapo BWANA atakapowapa nyama wakati wa jioni mle, na asubuhi mikate hata mkakinai; kwa kuwa BWANA asikia manung'uniko yenu mliyomnung'unikia yeye; na sisi tu nani? Manung'uniko yenu hayakuwa juu yetu sisi, ila juu ya BWANA. Musa akamwambia Haruni, Haya, sema na mkutano wote wa wana wa Israeli, Njoni karibu mbele ya BWANA; kwa kuwa yeye ameyasikia manung'uniko yenu. Ilikuwa Haruni aliponena na huo mkutano wote wa wana wa Israeli, wakaangalia upande wa bara, na tazama, utukufu wa BWANA ukaonekana katika hilo wingu. BWANA akasema na Musa, akinena, Nimeyasikia manung'uniko ya wana wa Israeli; haya sema nao ukinena, Wakati wa jioni mtakula nyama, na wakati wa asubuhi mtashiba mkate; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Ikawa wakati wa jioni, kware wakaja, wakaifunikiza kambi; na wakati wa asubuhi umande ulikuwa juu ya nchi pande zote za kituo. Na ulipokauka ule umande uliokuwa juu ya nchi, kumbe! Juu ya uso wa bara kitu kidogo kilichoviringana, kidogo kama barafu juu ya nchi. Wana wa Israeli walipokiona, wakaambiana, Nini hiki? Maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, Ndio mkate ambao BWANA amewapa ninyi, mle. Neno hili ndilo aliloagiza BWANA, Okoteni ninyi kitu hicho kila mtu kama ulaji wake ulivyo; kila mtu pishi moja kama hesabu ya watu wenu ilivyo; ndivyo mtakavyotwaa, kila mtu kwa ajili ya hao walioko hemani mwake. Wana wa Israeli wakafanya hivyo, wakaokota wengine zaidi, wengine kupungua. Nao walipoipima kwa pishi, yeye aliyekuwa ameokota kingi hakubakiwa na kitu, na yeye aliyekuwa ameokota kichache hakupungukiwa; wakaokota kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa.

Shirikisha
Soma Kutoka 16

Kutoka 16:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kisha wakasafiri kutoka Elimu, na mkutano wote wa wana wa Israeli wakafikilia bara ya Sini, iliyoko kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka kwao nchi ya Misri. Na mkutano mzima wa wana wa Israeli ukawanung’unikia Musa na Haruni, huko barani; wana wa Israeli wakawaambia, Laiti tungalikufa kwa mkono wa BWANA katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula vyakula hata kushiba; kwani mmetutoa huko na kututia katika bara hii, ili kutuua kwa njaa kusanyiko hili lote. Ndipo BWANA akamwambia Musa, Tazama, mimi nitawanyeshea ninyi mvua ya mkate kutoka mbinguni; na hao watu watatoka nje na kuokota kila siku sehemu ya siku; ili nipate kuwajaribu, kwamba watakwenda katika sheria yangu, ama sivyo. Kisha itakuwa siku ya sita, ya kwamba watayaandaa hayo watakayoleta ndani, nayo yatakuwa ni mara mbili kuliko wayaokotayo kila siku. Musa na Haruni wakawaambia wana wote wa Israeli, Jioni ndipo mtakapojua ya kuwa BWANA amewaleta kutoka nchi ya Misri; na asubuhi ndipo mtakapouona utukufu wa BWANA; kwa kuwa yeye asikia manung’uniko yenu mliyomnung’unikia BWANA; na sisi tu nani, hata mkatunung’unikia? Musa akasema, Ndilo litakalokuwa, hapo BWANA atakapowapa nyama wakati wa jioni mle, na asubuhi mikate hata mkakinai; kwa kuwa BWANA asikia manung’uniko yenu mliyomnung’unikia yeye; na sisi tu nani? Manung’uniko yenu hayakuwa juu yetu sisi, ila juu ya BWANA. Musa akamwambia Haruni, Haya, sema na mkutano wote wa wana wa Israeli, Njoni karibu mbele ya BWANA; kwa kuwa yeye ameyasikia manung’uniko yenu. Ilikuwa Haruni aliponena na huo mkutano wote wa wana wa Israeli, wakaangalia upande wa bara, na tazama, utukufu wa BWANA ukaonekana katika hilo wingu. BWANA akasema na Musa, akinena, Nimeyasikia manung’uniko ya wana wa Israeli; haya sema nao, ukinena, Wakati wa jioni mtakula nyama, na wakati wa asubuhi mtashiba mkate; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Ikawa wakati wa jioni, kware wakakaribia, wakakifunikiza kituo; na wakati wa asubuhi umande ulikuwa juu ya nchi pande zote za kituo. Na ulipoinuka ule umande uliokuwa juu ya nchi, kumbe! Juu ya uso wa bara kitu kidogo kilichoviringana, kidogo kama sakitu juu ya nchi. Wana wa Israeli walipokiona, wakaambiana, Nini hiki? Maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, Ndio mkate ambao BWANA amewapa ninyi, mle. Neno hili ndilo aliloagiza BWANA, Okoteni ninyi kitu hicho kila mtu kama ulaji wake ulivyo; kichwa pishi, kama hesabu ya watu wenu ilivyo; ndivyo mtakavyotwaa, kila mtu kwa ajili ya hao walioko hemani mwake. Wana wa Israeli wakafanya hivyo, wakaokota wengine zaidi, wengine kupungua. Nao walipoipima kwa pishi, yeye aliyekuwa ameokota kingi hakubakiwa na kitu, na yeye aliyekuwa ameokota kichache hakupungukiwa; wakaokota kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa.

Shirikisha
Soma Kutoka 16

Kutoka 16:1-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Jumuiya yote ya Kiisraeli ikaondoka Elimu, wakafika Jangwa la Sini, lililokuwa kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka Misri. Huko jangwani hiyo jumuiya yote wakawanungʼunikia Mose na Aroni. Waisraeli wakawaambia, “Laiti tungelikufa kwa mkono wa BWANA huko Misri! Huko tuliketi tukizunguka masufuria ya nyama na tukala vyakula tulivyovitaka, lakini ninyi mmetuleta huku jangwani ili mpate kuua mkutano huu wote kwa njaa.” Kisha BWANA akamwambia Mose, “Nitanyesha mikate kutoka mbinguni kwa ajili yenu. Watu watatoka kila siku na kukusanya kitakachowatosha kwa siku ile, kwa njia hii, nitawajaribu nione kama watafuata maelekezo yangu. Siku ya sita watatayarisha kile waletacho ndani, nacho kitakuwa mara mbili kuliko ya kile walichokusanya kila siku.” Kwa hiyo Mose na Aroni wakawaambia Waisraeli wote, “Jioni mtajua kwamba BWANA ndiye aliwatoa Misri, kisha asubuhi mtauona utukufu wa BWANA, kwa sababu amesikia manungʼuniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani hata mtunungʼunikie?” Pia Mose akasema, “Mtajua kuwa alikuwa BWANA wakati atakapowapa nyama mle ifikapo jioni na mikate yote mtakayohitaji asubuhi kwa sababu amesikia manungʼuniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani? Hamnungʼuniki dhidi yetu, bali dhidi ya BWANA.” Kisha Mose akamwambia Aroni, “Iambie jumuiya yote ya Waisraeli kwamba, ‘Mje mbele zake BWANA, kwa maana amesikia manungʼuniko yenu.’ ” Aroni alipokuwa akizungumza na jumuiya yote ya Waisraeli, wakatazama kuelekea jangwani, na huko wakaona utukufu wa BWANA ukitokeza katika wingu. BWANA akamwambia Mose, “Nimesikia manungʼuniko ya Waisraeli. Waambie, ‘Jioni mtakula nyama, na asubuhi mtashiba mikate. Ndipo mtajua ya kwamba Mimi ndimi BWANA Mungu wenu.’ ” Jioni ile kware wakaja wakaifunika kambi na asubuhi kulikuwa na tabaka la umande kuzunguka kambi. Wakati umande ulipoondoka, vipande vidogo vidogo kama theluji vilionekana juu ya uso wa jangwa. Waisraeli walipoona, wakaambiana, “Hiki ni nini?” Kwa kuwa hawakujua kilikuwa kitu gani. Mose akawaambia, “Huu ndio mkate ambao BWANA amewapa mle. Hivi ndivyo BWANA alivyoamuru: ‘Kila mmoja akusanye kiasi anachohitaji. Chukueni pishi moja kwa kila mtu mliye naye katika hema yenu.’ ” Waisraeli wakafanya kama walivyoambiwa, baadhi yao wakakusanya zaidi, wengine pungufu. Nao walipopima katika pishi, yule aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa. Kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji.

Shirikisha
Soma Kutoka 16