Kutoka 11:1-10
Kutoka 11:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Bado kuna pigo moja nitakalomletea Farao na nchi ya Misri. Baadaye atawaacheni mwondoke hapa. Tena atakapowaacheni mwondoke, yeye mwenyewe atawafukuza mwondoke kabisa. Waambie Waisraeli sasa wasikie vizuri kwamba kila mmoja wao, mwanamume kwa mwanamke, ni lazima amwombe jirani yake vito vya fedha na dhahabu.” Mwenyezi-Mungu akawafanya Waisraeli wapendeke mbele ya Wamisri. Tena, Mose mwenyewe akawa mtu mashuhuri sana nchini Misri, na mbele ya maofisa wa Farao na watu wote. Mose akamwambia Farao, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Panapo usiku wa manane leo, nitapitia katikati ya nchi ya Misri. Nitakapopita, kila mzaliwa wa kwanza nchini Misri atakufa: Kuanzia mzaliwa wa kwanza wako wewe Farao ambaye ni mrithi wako, hadi mzaliwa wa kwanza wa mjakazi anayesaga nafaka kwa jiwe. Hata wazaliwa wa kwanza wa mifugo nao wote watakufa. Kutakuwa na kilio kikubwa kote nchini Misri, kilio ambacho hakijapata kutokea, wala hakitatokea tena. Lakini miongoni mwa Waisraeli hakuna mtu, mnyama au mbwa wao atakayepatwa na madhara yoyote, ili upate kutambua kwamba mimi Mwenyezi-Mungu hutofautisha kati ya Waisraeli na Wamisri.’” Mose akamalizia kwa kumwambia Farao, “Watumishi wako hawa watanijia na kuinama mbele yangu kwa heshima, wakinisihi niondoke nchini Misri, mimi pamoja na watu wote wanaonifuata. Baada ya hayo, nitaondoka.” Kisha Mose, huku akiwa ameghadhabika, akaondoka kwa Farao. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Farao hatakusikiliza, ili maajabu yangu yapate kuongezeka nchini Misri.” Basi, Mose na Aroni walifanya maajabu hayo yote mbele ya Farao. Lakini Mwenyezi-Mungu alimfanya Farao kuwa mkaidi, akakataa kuwaruhusu Waisraeli waondoke nchini mwake.
Kutoka 11:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akamwambia Musa, Liko pigo moja bado, nitakaloleta juu ya Farao na juu ya Misri; baadaye atawapa ninyi ruhusa mtoke huku; naye hapo atakapowapa ruhusa, atawafukuza mtoke huku kabisa kabisa. Basi nena wewe masikioni mwa watu hawa, na kila mwanamume na atake kwa jirani yake, na kila mwanamke atake kwa jirani yake, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu. BWANA akawapa watu hao kibali machoni pa Wamisri. Zaidi ya hayo, huyo Musa alikuwa ni mkuu sana katika nchi ya Misri, machoni pa watumishi wa Farao, na machoni pa watu wake. Musa akasema, BWANA asema hivi, Kama usiku wa manane mimi nitatoka nipite kati ya Misri; na wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri watakufa, tangu yule mzaliwa wa kwanza wa Farao aketiye katika kiti chake cha enzi, hata mzaliwa wa kwanza wa huyo kijakazi aliye pale nyuma ya jiwe la kusagia; na wazaliwa wa kwanza wote wa wanyama. Ndipo kutakuwa na kilio kikuu katika nchi yote ya Misri, ambacho mfano wake haujakuwa bado majira yoyote, wala hautakuwako mfano wake tena kabisa. Lakini katika wana wa Israeli hapana hata mbwa atakayetoa ulimi juu yao, juu ya mtu wala juu ya mnyama; ili kwamba mpate kujua jinsi BWANA anavyowatenga Wamisri na Waisraeli. Tena hao watumishi wako wote wataniteremkia kwangu mimi, nao watanisujudia, wakisema, Toka wewe, na hawa watu wote wakufuatao; na baada ya hayo nitatoka. Basi akatoka kwa Farao na hasira kuu. BWANA akamwambia Musa, Farao hatawasikiza ninyi; kusudi ajabu zangu ziongezeke katika nchi ya Misri. Musa na Haruni walifanya ajabu hizo zote mbele ya Farao; BWANA akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, asiwape wana wa Israeli ruhusa watoke nchi yake.
Kutoka 11:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akamwambia Musa, Liko pigo moja bado, nitakaloleta juu ya Farao na juu ya Misri; baadaye atawapa ninyi ruhusa mtoke huku; naye hapo atakapowapa ruhusa, atawafukuza mtoke huku kabisa kabisa. Basi nena wewe masikioni mwa watu hawa, na kila mtu mume na atake kwa jirani yake, na kila mwanamke atake kwa jirani yake, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu. BWANA akawapa watu hao kibali machoni pa Wamisri. Zaidi ya hayo, huyo Musa alikuwa ni mkuu sana katika nchi ya Misri, machoni pa watumishi wa Farao, na machoni pa watu wake. Musa akasema, BWANA asema hivi, Kama usiku wa manane mimi nitatoka nipite kati ya Misri; na wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri watakufa, tangu yule mzaliwa wa kwanza wa Farao aketiye katika kiti chake cha enzi, hata mzaliwa wa kwanza wa huyo kijakazi aliye pale nyuma ya jiwe la kusagia; na wazaliwa wa kwanza wote wa wanyama. Ndipo kutakuwa na kilio kikuu katika nchi yote ya Misri, ambacho mfano wake haujakuwa bado majira yo yote, wala hautakuwako mfano wake tena kabisa. Lakini katika wana wa Israeli hapana hata mbwa atakayetoa ulimi juu yao, juu ya mtu wala juu ya mnyama; ili kwamba mpate kujua jinsi BWANA anavyowatenga Wamisri na Waisraeli. Tena hao watumishi wako wote watanitelemkia kwangu mimi, nao watanisujudia, wakisema, Toka wewe, na hawa watu wote wakufuatao; na baada ya hayo nitatoka. Basi akatoka kwa Farao na hasira kuu. BWANA akamwambia Musa, Farao hatawasikiza ninyi; kusudi ajabu zangu ziongezeke katika nchi ya Misri. Musa na Haruni walifanya ajabu hizo zote mbele ya Farao; BWANA akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, asiwape wana wa Israeli ruhusa watoke nchi yake.
Kutoka 11:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi BWANA alikuwa amemwambia Mose, “Nitaleta pigo moja zaidi kwa Farao na katika nchi ya Misri. Baada ya hilo, atawaacha mwondoke hapa na atakapofanya hivyo, atawafukuza mtoke kabisa. Waambie watu wote waume kwa wake wawaombe majirani zao vitu vya fedha na vya dhahabu.” (BWANA akawafanya Wamisri wawe na moyo wa ukarimu kwa Waisraeli, naye Mose mwenyewe akaheshimiwa sana na maafisa wa Farao na watu wote katika nchi ya Misri.) Kwa hiyo Mose akasema, “Hili ndilo BWANA asemalo: ‘Panapo usiku wa manane Mimi nitapita katika nchi yote ya Misri. Kila mwanaume kifungua mimba katika Misri atakufa, kuanzia mzaliwa wa kwanza wa kiume wa Farao, aketiye penye kiti cha ufalme, hadi mzaliwa wa kwanza wa kiume wa mtumwa wa kike, anayesaga nafaka kwa jiwe, pamoja na kila mzaliwa wa kwanza wa mifugo. Patakuwepo kilio kikubwa katika nchi yote ya Misri, kilio kibaya ambacho hakijakuwepo wala kamwe hakitakuwepo tena. Lakini miongoni mwa Waisraeli hakuna hata mbwa atakayembwekea mwanadamu wala mnyama yeyote.’ Ndipo mtakapojua kuwa BWANA huweka tofauti kati ya Misri na Israeli. Maafisa hawa wako wote watanijia, wakisujudu mbele yangu, wakisema, ‘Ondoka, wewe pamoja na watu wako wote wanaokufuata!’ Baada ya haya nitaondoka.” Kisha Mose, huku akiwa amewaka hasira, akamwacha Farao. BWANA alikuwa amemwambia Mose, “Farao atakataa kukusikiliza, ili maajabu yangu yapate kuongezeka katika nchi ya Misri.” Mose na Aroni wakafanya maajabu haya yote mbele ya Farao, lakini BWANA akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, wala hakuwaachia Waisraeli waondoke katika nchi yake.