Kutoka 1:17-22
Kutoka 1:17-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini hao wakunga walikuwa wacha Mungu, hawakufanya kama walivyoamriwa na huyo mfalme wa Misri, lakini wakawahifadhi hai wale watoto wa kiume. Basi mfalme wa Misri akawaita wale wakunga na kuwauliza, Kwa nini kufanya jambo hili la kuwahifadhi watoto wa kiume wawe hai? Wakunga wakamwambia Farao, Ni kwa sababu hao wanawake wa Kiebrania si kama wanawake wa Kimisri; kwa kuwa ni hodari hao, nao huzaa kabla mkunga hajapata kuwafikia. Basi Mungu akawatendea mema wale wakunga; na hao watu wakaongezeka sana, wakaendelea na kuzidi kuwa na nguvu nyingi. Ilikuwa kwa sababu wale wakunga walikuwa wakimcha Mungu, akawasimamishia nyumba. Kisha huyo Farao akawaagiza watu wake wote, akisema, Kila mtoto wa kiume atakayezaliwa mtamtupa mtoni, na kila mtoto wa kike mtamhifadhi hai.
Kutoka 1:17-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini kwa kuwa wakunga hao walimcha Mungu, hawakufanya kama walivyoamriwa na mfalme wa Misri, bali waliwaacha watoto wa kiume wa Waisraeli waishi. Basi, mfalme wa Misri akawaita wakunga hao, akawauliza, “Kwa nini mmefanya hivyo? Mbona mmewaacha watoto wa kiume waishi?” Wao wakamjibu Farao, “Wanawake wa Kiebrania si sawa na wanawake wa Misri. Wao ni hodari; kabla mkunga hajafika, wao huwa wamekwisha jifungua.” Basi, Mungu akawajalia mema wakunga hao, nao Waisraeli wakazidi kuongezeka na kuwa na nguvu sana. Na kwa vile wakunga hao walimcha Mungu, Mungu akawajalia kupata jamaa zao wenyewe. Kisha Farao akawaamuru watu wake wote hivi, “Kila mtoto wa kiume atakayezaliwa kwa Waebrania mtupeni mtoni Nili. Lakini kila mtoto wa kike, mwacheni aishi.”
Kutoka 1:17-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini wale wazalisha walikuwa wakimcha Mungu, wasifanye kama walivyoamriwa na huyo mfalme wa Misri, lakini wakawahifadhi hai wale wanaume. Basi mfalme wa Misri akawaita wale wazalisha na kuwauliza, Kwa nini kufanya jambo hili, na kuwahifadhi watoto waume wawe hai? Wazalisha wakamwambia Farao, Ni kwa sababu hao wanawake wa Kiebrania si kama wanawake wa Kimisri; kwa kuwa ni hodari hao, nao huzaa kabla mzalisha hajapata kuwafikilia. Basi Mungu akawatendea mema wale wazalisha; na hao watu wakaongezeka sana, wakaendelea na kuzidi kuwa na nguvu nyingi. Ilikuwa kwa sababu wale wazalisha walikuwa wakimcha Mungu, akawasimamishia nyumba. Kisha huyo Farao akawaagiza watu wake, akisema, Kila mtoto mwanamume atakayezaliwa mtamtupa mtoni, na kila mtoto mwanamke mtamhifadhi hai.
Kutoka 1:17-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Lakini hao wakunga walimcha Mungu na hawakufanya kile mfalme wa Misri alichowaambia kufanya, bali wakawaacha watoto wa kiume waishi. Ndipo mfalme wa Misri akawaita hao wakunga, akawauliza, “Kwa nini mmefanya hivi? Mbona mmeacha watoto wa kiume waishi?” Wakunga wakamjibu Farao, “Wanawake wa Kiebrania ni tofauti na wanawake wa Kimisri; wao wana nguvu, nao hujifungua watoto kabla wakunga hawajafika.” Kwa hiyo Mungu akawatendea mema wakunga hao. Waisraeli wakaongezeka na kuendelea kuwa wengi zaidi. Kwa vile hao wakunga walimcha Mungu, Mungu akawajalia kuwa na jamaa zao wenyewe. Kisha Farao akatoa agizo hili kwa watu wake wote: “Kila mtoto wa kiume atakayezaliwa kwa Waebrania lazima atupwe katika Mto Naili, bali kila mtoto wa kike aachwe aishi.”