Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Esta 9:1-32

Esta 9:1-32 Biblia Habari Njema (BHN)

Siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, yaani mwezi wa Adari, ilipofika, siku ambayo tangazo la mfalme lingetekelezwa, na maadui wa Wayahudi walitarajia kuwashinda Wayahudi, iligeuzwa kuwa siku ya ushindi kwa Wayahudi dhidi ya adui zao. Katika kila mji wa kila mkoa wa mfalme Ahasuero, Wayahudi walijiandaa vizuri kumshambulia mtu yeyote ambaye angejaribu kuwadhuru. Ikawa viongozi wote wa mikoa, watawala, wakuu na maofisa wa mfalme pia waliwasaidia Wayahudi, maana wote walimwogopa Mordekai. Mordekai sasa alikuwa mtu mwenye madaraka makubwa katika ikulu, na habari zake zilienea katika mikoa yote kwamba uwezo wake ulikuwa unazidi kuongezeka. Basi, Wayahudi waliwashambulia maadui zao kwa upanga, wakawachinja, wakawaangamiza na kuwatenda kama walivyopenda. Huko mjini Susa, Wayahudi waliwaua watu 500. Pia waliwaua Parshandatha, Dalfoni, Aspatha, Poratha, Adalia, Aridatha, Parmashta, Arisai, Aridai na Waizatha, wana kumi wa Hamani mwana wa Hamedatha, adui ya Wayahudi. Hata hivyo, hawakuteka nyara. Siku hiyohiyo, mfalme alijulishwa idadi ya watu waliouawa katika mji mkuu wa Susa. Ndipo mfalme akamwambia malkia Esta: “Katika mji mkuu peke yake Wayahudi wamewaua watu 500, pamoja na wana kumi wa Hamani. Unafikiri wamefanyaje huko mikoani! Unataka nini sasa? Maana utatimiziwa. Niambie, unataka nini zaidi, nawe utapewa.” Esta akasema, “Ukiona ni vema, ewe mfalme, kesho waruhusu Wayahudi waliomo Susa wafanye kama agizo la leo lilivyokuwa. Tena, uamuru wana kumi wa Hamani watundikwe kwenye miti ya kuulia.” Mfalme akaamuru hayo yatekelezwe, na tangazo likatolewa mjini Susa. Wana kumi wa Hamani wakanyongwa hadharani. Siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, Wayahudi walikusanyika tena, wakawaua watu 300 zaidi mjini Susa. Lakini hawakuteka nyara mali za watu. Wayahudi waliokuwa katika mikoa nao pia walijiandaa kuyalinda maisha yao. Wakaokolewa kutoka kwa maadui wao; waliwaua watu wapatao 75,000, lakini hawakuchukua nyara. Siku hiyo ilikuwa ya kumi na tatu ya mwezi wa Adari. Siku iliyofuata ya kumi na nne, walipumzika, wakaifanya kuwa siku ya karamu na sherehe. Lakini Wayahudi wa mji mkuu wa Susa walikusanyika pia siku ya kumi na nne lakini hawakupumzika. Waliadhimisha siku ya kumi na tano kwa furaha na shangwe. Kutokana na sababu hii, Wayahudi wakaao vijijini na katika miji midogo huadhimisha siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari kuwa sikukuu ya furaha, na kupelekeana zawadi hali wale waishio katika miji mikubwa huadhimisha siku ya kumi na tano ya mwezi wa Adari kama siku ya mapumziko, wakapelekeana pia zawadi. Mordekai aliandika matukio haya yote. Kisha aliwaandikia barua Wayahudi wote waliokuwa katika utawala wa Ahasuero. Aliwataka kila mwaka waadhimishe sikukuu, siku ya kumi na nne na siku ya kumi na tano ya mwezi wa Adari. Wayahudi waliwashinda maadui zao katika siku hizo, na katika mwezi huo huzuni yao iligeuzwa kuwa furaha, na misiba yao kuwa sikukuu. Waliagizwa wawe wakizikumbuka siku hizo kwa kufanya karamu na sherehe, kupelekeana zawadi za chakula na kuwapa maskini vitu. Basi, Wayahudi walikubaliana kufanya kama walivyoanza na kama Mordekai alivyowaandikia. Hamani mwana wa Hamedatha, wa Agagi na adui wa Wayahudi alikuwa amefanya hila dhidi ya Wayahudi kuwaangamiza, pia alikuwa amepiga Puri, yaani kura, ili kuamua siku ya kuwaponda na kuwaangamiza Wayahudi. Lakini Esta alipomwendea mfalme, naye mfalme alitoa amri kwa maandishi kwamba ile hila mbaya ambayo Hamani alikuwa amefanya dhidi ya Wayahudi, impate yeye mwenyewe; na ya kuwa yeye na wanawe wauawe kwa kutundikwa kwenye mti wa kuulia. Kwa hiyo, waliita siku hizo Purimu, kutokana na neno puri yaani kura. Kwa sababu ya barua ya Mordekai na mambo waliyoyaona wenyewe na yale yaliyowapata, Wayahudi waliifanya kuwa sheria rasmi kwao, kwa wazawa wao na kwa mtu yeyote ambaye angejiunga nao, kwamba katika wakati maalumu kila mwaka, bila kukosa, siku hizo mbili ziadhimishwe kulingana na maagizo ya Mordekai. Pia walikubaliana kwamba kila jamaa ya Kiyahudi, kizazi baada ya kizazi, katika kila mkoa na mji, sharti ikumbuke siku za Purimu na kuzisherehekea daima. Ndipo malkia Esta, binti Abihaili, akaandika barua kwa mamlaka yake yote, pamoja na Mordekai Myahudi kuthibitisha yale aliyoandika Mordekai hapo awali kuhusu Purimu. Barua hiyo waliandikiwa Wayahudi wote, na nakala zake kupelekewa mikoa yote 127 ya utawala wa Ahasuero. Barua hiyo iliwatakia Wayahudi amani na usalama, na kuwahimiza wao na wazawa wao waadhimishe sikukuu za Purimu kwa wakati wake maalumu, kama vile walivyokuwa wanazikumbuka sheria za kufunga wakati wa kuomboleza. Maagizo haya yalitolewa na Mordekai, Myahudi, pamoja na malkia Esta. Amri yake Esta ikathibitisha mambo hayo ya Purimu; ikaandikwa kitabuni.

Shirikisha
Soma Esta 9

Esta 9:1-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Hata ulipofika mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari, siku yake ya kumi na tatu, amri ya mfalme na mbiu yake ilipowadia kutekelezwa; ambayo siku ile adui za Wayahudi walitumaini kuwatawala, bali kumebadilika kinyume, hata Wayahudi waliwatawala wale waliowachukia; siku ile ile Wayahudi wakakusanyika mijini mwao katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero ili kuwatia mikono wale watu waliowatakia hasara; wala asiweze mtu kuwazuia, kwa kuwa hofu yao imewaangukia watu wote. Nao maakida wa majimbo, na majumbe, na maliwali, na wale waliofanya shughuli ya mfalme, waliwasaidia Wayahudi; kwa sababu hofu ya Mordekai imewaangukia. Maana Mordekai alikuwa mkuu nyumbani mwa mfalme, na sifa yake imevuma katika majimbo yote, kwa kuwa huyo Mordekai amezidi kukuzwa. Basi Wayahudi wakawapiga adui zao wote mapigo ya upanga, na machinjo, na maangamizo, wakawatenda kama wapendavyo wale waliowachukia. Hata huko Shushani ngomeni Wayahudi wakawaua watu mia tano, na kuwaangamiza. Wakawaua na Parshandatha, na Dalfoni, na Aspatha, na Poratha, na Adalia, na Aridatha, na Parmashta, na Arisai, na Aridai, na Waizatha, wana kumi wa Hamani bin Hamedatha, adui ya Wayahudi; walakini juu ya nyara hawakuweka mikono. Siku ile mfalme akaletewa hesabu ya hao waliouawa huko Shushani ngomeni. Mfalme akamwambia malkia Esta, Wayahudi wamewaua watu mia tano hapa Shushani ngomeni na kuwaangamiza, pamoja na wana kumi wa Hamani, je! Wamefanyaje basi katika majimbo ya mfalme yaliyosalia! Basi, una nini uombalo? Nawe utapewa; ama unayo haja gani tena? Nayo itatimizwa. Ndipo Esta aliposema, Mfalme akiona vema, Wayahudi walioko Shushani na wapewe ruhusa kufanya tena kesho sawasawa na mbiu ya leo, na hao wana kumi wa Hamani watundikwe juu ya mti ule. Mfalme akaamuru vifanyike vivyo hivyo, mbiu ikapigwa huko Shushani, wakawatundika wale wana kumi wa Hamani. Basi Wayahudi wa Shushani wakakusanyika tena siku ya kumi na nne pia ya mwezi wa Adari, wakawaua watu mia tatu huko Shushani; walakini juu ya nyara hawakuweka mikono. Nao Wayahudi wengine waliokaa katika majimbo ya mfalme walikusanyika, wakazishindania maisha zao, wakajipatia raha mbele ya adui zao, wakawaua waliowachukia, watu sabini na tano elfu; walakini juu ya nyara hawakuweka mikono. Hii ndiyo siku ya kumi na tatu ya mwezi wa Adari; na siku ya kumi na nne ya mwezi huo wakapumzika, wakaifanya kuwa siku ya karamu na furaha. Lakini Wayahudi wa Shushani walikusanyika siku ya kumi na tatu ya mwezi huo, na siku ya kumi na nne pia; na siku ya kumi na tano ya mwezi uo huo wakapumzika, wakaifanya kuwa siku ya karamu na furaha. Kwa sababu hii Wayahudi wa vijijini, wakaao katika miji isiyo na boma, huishika siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, kuwa siku ya furaha na karamu, sikukuu ya kupelekeana zawadi. Basi Mordekai aliyaandika mambo hayo; naye akapeleka barua kwa Wayahudi wote waliokaa katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero, waliokuwa karibu na waliokuwa mbali, kuwaonya wazishike siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, na siku ya kumi na tano yake, mwaka kwa mwaka, ambazo ni siku Wayahudi walipojipatia raha mbele ya adui zao, na mwezi uliogeuzwa kwao kuwa furaha badala ya huzuni, na kuwa sikukuu badala ya kilio; wazifanye siku hizo ziwe za karamu na furaha, za kupeana zawadi na za kuwapa maskini vipawa. Nao Wayahudi wakakubali kufanya kama walivyoanza, na kama Mordekai alivyowaandikia; kwa sababu Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, adui ya Wayahudi wote, alikuwa amefanya shauri juu ya Wayahudi ili kuwaangamiza, akapiga Puri, yaani kura, ili kuwakomesha na kuwaangamiza pia; bali mfalme alipoarifiwa, aliamuru kwa barua ya kwamba hilo shauri baya alilolifanya juu ya Wayahudi limrudie kichwani pake mwenyewe; na ya kwamba yeye na wanawe watundikwe juu ya mti. Hivyo wakaziita siku hizo Purimu, kwa jina la Puri. Basi, kwa ajili ya maneno yote ya barua hiyo, na kwa yale waliyoyaona wenyewe juu ya jambo hilo, na mambo yenyewe yaliyowajia, Wayahudi wakaagiza na kutadariki juu yao wenyewe, na juu ya wazao wao, na juu ya wote watakaojiunga nao, isikome, ya kwamba watazishika siku hizo mbili sawasawa na andiko lile, na kwa majira yake kila mwaka; siku hizo zikumbukwe na kushikwa kwa vizazi vyote na kila jamaa, katika kila jimbo na kila mji; wala siku hizo za Purimu zisikome katikati ya Wayahudi, wala kumbukumbu lake lisiishe kwa wazao wao. Ndipo malkia Esta, binti Abihaili, pamoja na Mordekai Myahudi, alipoandika kwa mamlaka yote kuithibitisha barua hii ya pili ya Purimu. Akapeleka barua kwa Wayahudi wote katika majimbo yote mia na ishirini na saba ya ufalme wake Ahasuero, maneno ya amani na kweli, ili kuzithibitisha siku hizo za Purimu kwa majira yake, kama Mordekai Myahudi na malkia Esta walivyoamuru, na kama walivyojiagizia juu yao wenyewe, na juu ya wazao wao, kwa habari ya kufunga na kilio. Amri yake Esta ikayathibitisha mambo hayo ya Purimu; ikaandikwa katika kitabu.

Shirikisha
Soma Esta 9

Esta 9:1-32 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Katika siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, yaani mwezi wa Adari, amri iliyoagizwa na mfalme ilikuwa itekelezwe. Siku hii adui wa Wayahudi walikuwa wametumaini kuwashinda, lakini sasa mambo yaliwageukia na Wayahudi wakawashinda wale waliokuwa wanawachukia. Wayahudi walikusanyika katika miji yao, katika majimbo ya Mfalme Ahasuero kuwashambulia wale waliokuwa wanatafuta kuwaangamiza. Hakuna yeyote aliyeweza kushindana nao, kwa sababu watu wa mataifa mengine yote waliwaogopa. Nao wakuu wote wa majimbo, majemadari, watawala na maafisa wa mfalme wakawasaidia Wayahudi, kwa sababu walimhofu Mordekai. Mordekai alikuwa mtu mashuhuri katika jumba la mfalme; sifa zake zilienea katika majimbo yote naye alipata uwezo zaidi na zaidi. Wayahudi waliwaangusha adui zao wote kwa upanga wakiwaua na kuwaangamiza, nao walifanya kile walichotaka kwa wale waliowachukia. Katika ngome ya Shushani Wayahudi waliua na kuangamiza wanaume 500. Pia waliwaua Parshendatha, Dalfoni, Aspatha, Poratha, Adalia, Ardatha, Parmashta, Arisai, Aridai na Waizatha, wana kumi wa Hamani mwana wa Hamedatha, adui wa Wayahudi. Lakini hawakuchukua nyara. Mfalme aliarifiwa siku iyo hiyo hesabu ya waliouawa katika ngome ya Shushani. Mfalme akamwambia Malkia Esta, “Wayahudi wamewaua wanaume 500 na wana kumi wa Hamani ndani ya ngome ya Shushani. Wamefanyaje katika majimbo mengine ya mfalme yaliyobaki? Je, sasa haja yako ni nini? Nayo pia utapewa. Nalo ombi lako ni nini? Nalo utafanyiwa.” Esta akajibu, “Ikimpendeza mfalme, uwape ruhusa Wayahudi walioko Shushani warudie amri ya leo kesho pia, na wana wa Hamani kumi wanyongwe mahali pa kunyongea watu.” Basi mfalme akaamuru kwamba hili litendeke. Amri ilitolewa huko Shushani, nao wakawanyonga wana kumi wa Hamani. Wayahudi huko Shushani wakakusanyika pamoja siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, nao wakawaua wanaume 300 huko Shushani, lakini hawakuchukua nyara zao. Wakati ule ule, Wayahudi wengine waliokuwa kwenye majimbo ya mfalme, wakakusanyika kujilinda nao wakapata nafuu kutokana na adui zao. Waliua adui zao wapatao 75,000 lakini hawakugusa nyara zao. Hili lilitendeka siku ya kumi na tatu ya mwezi wa Adari na siku ya kumi na nne walipumzika na kuifanya siku ya karamu na furaha. Wayahudi huko Shushani, hata hivyo, walikuwa wamekusanyika siku ya kumi na tatu na ya kumi na nne, pia siku ya kumi na tano walipumzika na kuifanya siku ya karamu na furaha. Ndiyo sababu Wayahudi wanaokaa vijijini na katika miji midogo huadhimisha siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari kama siku ya furaha na karamu, siku ambayo wao hupeana zawadi mmoja kwa mwingine. Mordekai aliandika matukio haya, naye akapeleka barua kwa Wayahudi wote walioko katika majimbo ya Mfalme Ahasuero, majimbo yaliyo mbali na karibu, akiwataka kila mwaka washerehekee siku ya kumi na nne na ya kumi na tano ya mwezi wa Adari kama wakati ambao Wayahudi walipata nafuu kutoka kwa adui zao na kama mwezi ambao huzuni yao iligeuzwa kuwa furaha na kuomboleza kwao kuwa siku ya kusherehekea. Aliwaandikia kushika siku hizo kama siku za karamu na za furaha na kupeana zawadi za vyakula wao kwa wao na zawadi kwa maskini. Hivyo Wayahudi walikubali kuendeleza sherehe walizokuwa wamezianza, wakifanya lile Mordekai alilokuwa amewaandikia. Kwa maana Hamani mwana wa Hamedatha Mwagagi, adui wa Wayahudi wote, alikuwa amepanga hila dhidi ya Wayahudi ili kuwaangamiza, na alikuwa amepiga puri (yaani kura) kwa ajili ya maangamizi na uharibifu wao. Lakini wakati shauri hilo baya lilipoarifiwa kwa mfalme, alitoa amri iliyoandikwa kwamba mipango mibaya ambayo Hamani ameipanga dhidi ya Wayahudi inapasa imrudie juu ya kichwa chake mwenyewe, na kwamba yeye na wanawe waangikwe mahali pa kunyongea watu. (Kwa hiyo siku hizi ziliitwa Purimu, kutokana na neno puri.) Kwa sababu ya kila kitu kilichoandikwa kwenye barua hii na kwa sababu ya yale waliyoyaona na yale yaliyowatokea, Wayahudi wakachukua na kuifanya desturi kwamba wao na wazao wao na wote ambao walijiunga nao wangefanya bila kuacha kushika siku hizi mbili kila mwaka, kwa njia ilivyoelekezwa na kwa wakati wake. Siku hizi zinapasa zikumbukwe na kuadhimishwa katika kila kizazi, kila jamaa na katika kila jimbo na kila jiji. Nazo siku hizi za Purimu kamwe zisikome kusherehekewa na Wayahudi, wala kumbukumbu zake zisipotee miongoni mwa wazao wake. Basi Malkia Esta binti Abihaili, pamoja na Mordekai, Myahudi, waliandika kwa mamlaka yote kuthibitisha barua hii ya pili kuhusu Purimu. Naye Mordekai akatuma barua kwa Wayahudi wote katika majimbo 127 ya ufalme wa Ahasuero, barua zenye maneno ya amani na matumaini, ili kuimarisha siku hizi za Purimu katika majira yake yaliyowekwa, kama Mordekai, Myahudi na Malkia Esta walivyowaamuru, na walivyojiimarisha wenyewe na wazao wao kuhusu nyakati za kufunga na kuomboleza. Amri ya Esta ilithibitisha taratibu hizi kuhusu Purimu, nayo ikaandikwa katika kumbukumbu.

Shirikisha
Soma Esta 9

Esta 9:1-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Hata ulipofika mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari, siku yake ya kumi na tatu, amri ya mfalme na mbiu yake ilipowadia kutekelezwa; ambayo siku ile adui za Wayahudi walitumaini kuwatawala, bali kumebadilika kinyume, hata Wayahudi waliwatawala wale waliowachukia; siku ile ile Wayahudi wakakusanyika mijini mwao katika mikoa yote ya mfalme Ahasuero ili kuwatia mikono wale watu waliowatakia hasara; wala asiweze mtu kuwazuia, kwa kuwa waogopwa na watu wote. Nao wakuu wa mikoa, na majumbe, na watawala, na wale waliofanya shughuli ya mfalme, waliwasaidia Wayahudi; maana walimwogopa Mordekai. Maana Mordekai alikuwa mkuu nyumbani mwa mfalme, na sifa yake imevuma katika mikoa yote, kwa kuwa huyo Mordekai amezidi kukuzwa. Basi Wayahudi wakawapiga adui zao wote mapigo ya upanga, na kuwachinja, na kuwaangamiza, wakawatenda kama wapendavyo wale waliowachukia. Hata huko Susa mjini Wayahudi wakawaua watu mia tano, na kuwaangamiza. Wakawaua na Parshandatha, na Dalfoni, na Aspatha, na Poratha, na Adalia, na Aridatha, na Parmashta, na Arisai, na Aridai, na Waizatha, wana kumi wa Hamani mwana wa Hamedatha, adui ya Wayahudi; lakini juu ya nyara hawakuweka mikono. Siku ile mfalme akaletewa hesabu ya hao waliouawa huko Susa mjini. Mfalme akamwambia malkia Esta, Wayahudi wamewaua watu mia tano hapa Shushani ngomeni na kuwaangamiza, pamoja na wana kumi wa Hamani, je! Wamefanyaje basi katika majimbo ya mfalme yaliyosalia! Basi, una nini uombalo? Nawe utapewa; ama unayo haja gani tena? Nayo itatimizwa. Ndipo Esta aliposema, Mfalme akiona vema, Wayahudi walioko Susa na wapewe ruhusa kufanya tena kesho sawasawa na mbiu ya leo, na hao wana kumi wa Hamani watundikwe juu ya mti ule. Mfalme akaamuru ifanyike vivyo hivyo, mbiu ikapigwa huko Susa, wakawatundika wale wana kumi wa Hamani. Basi Wayahudi wa Susa wakakusanyika tena siku ya kumi na nne pia ya mwezi wa Adari, wakawaua watu mia tatu huko Susa; lakini juu ya nyara hawakuweka mikono. Nao Wayahudi wengine waliokaa katika mikoa ya mfalme walikusanyika, wakayapigania maisha yao, wakajipatia raha mbele ya adui zao, wakawaua waliowachukia, watu elfu sabini na tano; lakini juu ya nyara hawakuweka mikono. Hii ndiyo siku ya kumi na tatu ya mwezi wa Adari; na siku ya kumi na nne ya mwezi huo wakapumzika, wakaifanya kuwa siku ya karamu na furaha. Lakini Wayahudi wa Susa walikusanyika siku ya kumi na tatu ya mwezi huo, na siku ya kumi na nne pia; na siku ya kumi na tano ya mwezi uo huo wakapumzika, wakaifanya kuwa siku ya karamu na furaha. Kwa sababu hii Wayahudi wa vijijini, wakaao katika miji isiyo na ngome, huishika siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, kuwa siku ya furaha na karamu, sikukuu ya kupelekeana zawadi. Basi Mordekai aliyaandika mambo hayo; naye akatuma barua kwa Wayahudi wote waliokaa katika mikoa yote ya mfalme Ahasuero, waliokuwa karibu na waliokuwa mbali, kuwaonya wazishike siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, na siku ya kumi na tano yake, kila mwaka, siku ambazo Wayahudi walijipatia raha mbele ya adui zao, na mwezi uliogeuzwa kwao kuwa furaha badala ya huzuni, na kuwa sikukuu badala ya kilio; wazifanye siku hizo ziwe za karamu na furaha, za kupeana zawadi na za kuwapa maskini tunu. Nao Wayahudi wakakubali kufanya kama walivyoanza, na kama Mordekai alivyowaandikia; kwa sababu Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, adui ya Wayahudi wote, alikuwa amefanya shauri juu ya Wayahudi ili kuwaangamiza, akapiga Puri, yaani kura, ili kuwakomesha na kuwaangamiza pia; bali mfalme alipoarifiwa, aliamuru kwa barua ya kwamba huo mpango mwovu alioufanya juu ya Wayahudi umrudie kichwani pake mwenyewe; na ya kwamba yeye na wanawe watundikwe juu ya mti. Hivyo wakaziita siku hizo Purimu, kwa jina la Puri. Basi, kwa ajili ya maneno yote ya barua hiyo, na kwa yale waliyoyaona wenyewe juu ya jambo hilo, na mambo yenyewe yaliyowapata, Wayahudi wakaagiza na kutadaraki juu yao wenyewe, na juu ya wazao wao, na juu ya wote watakaojiunga nao, isikome, ya kwamba watazishika siku hizo mbili kulingana na andiko lile, na kwa majira yake kila mwaka; siku hizo zikumbukwe na kushikwa kwa vizazi vyote na kila jamaa, katika kila jimbo na kila mji; wala siku hizo za Purimu zisikome katikati ya Wayahudi, wala kumbukumbu lake lisiishe kwa wazao wao. Ndipo malkia Esta, binti Abihaili, pamoja na Mordekai Myahudi, alipoandika kwa mamlaka yote kuithibitisha barua hii ya pili ya Purimu. Akapeleka barua kwa Wayahudi wote katika majimbo yote mia moja ishirini na saba ya ufalme wake Ahasuero, maneno ya amani na kweli, ili kuzithibitisha siku hizo za Purimu kwa majira yake, kama Mordekai Myahudi na malkia Esta walivyoamuru, na kama walivyojiagizia juu yao wenyewe, na juu ya wazawa wao, kwa kufunga na kulia. Amri yake Esta ikayathibitisha mambo hayo ya Purimu; ikaandikwa katika kitabu.

Shirikisha
Soma Esta 9