Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Esta 8:1-17

Esta 8:1-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Siku ile ile Mfalme Ahasuero akampa Malkia Esta shamba la Hamani, adui wa Wayahudi. Naye Mordekai akaja mbele ya mfalme, kwa kuwa Esta alikuwa amesema jinsi anavyohusiana naye. Mfalme akaivua pete yake ya muhuri, ambayo alikuwa amemnyangʼanya Hamani, akampa Mordekai, naye Esta akamweka Mordekai juu ya shamba la Hamani. Esta alimsihi tena mfalme, akianguka miguuni pake na kulia. Akamwomba akomeshe mpango mwovu wa Hamani Mwagagi ambao alikuwa ameupanga dhidi ya Wayahudi. Kisha mfalme alimnyooshea Esta fimbo yake ya utawala ya dhahabu naye aliinuka na kusimama mbele yake. Esta akasema, “Kama ikimpendeza mfalme, nami kama nikipata kibali naye akiona ni jambo lililo sawa kunitendea na kama akipendezwa nami, basi iandikwe amri ya kuzitangua barua zile Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, alizotunga na kuandika kuangamiza Wayahudi katika majimbo yote ya mfalme. Kwa maana nitawezaje kuvumilia kuona maafa yakiwapata watu wangu? Nitawezaje kuvumilia kuona maangamizi ya jamaa yangu?” Mfalme Ahasuero akawajibu Malkia Esta na Mordekai Myahudi, “Kwa sababu Hamani aliwashambulia Wayahudi, nimetoa shamba la Hamani kwa Esta, naye ameangikwa kwenye mti wa kunyongea. Basi andika amri nyingine kwa jina la mfalme kwa ajili ya Wayahudi kama unavyoona vyema, kisha uifunge kwa kutia muhuri kwa pete ya mfalme kwa kuwa hakuna andiko lililoandikwa kwa jina la mfalme na kutiwa muhuri kwa pete ya mfalme linaloweza kutanguliwa.” Mara moja waandishi wa mfalme wakaitwa kwenye siku ya ishirini na tatu, mwezi wa tatu, ndio mwezi wa Siwani. Wakaandika yote Mordekai aliyoamuru kwa Wayahudi, kwa majemadari, watawala na wakuu wa majimbo 127 kuanzia Bara Hindi mpaka Kushi. Maagizo haya yaliandikwa kwa maandishi ya kila jimbo na kwa lugha ya kila mtu pia kwa Wayahudi kwa maandishi yao wenyewe na lugha yao. Mordekai aliandika nyaraka kwa jina la Mfalme Ahasuero, akazitia muhuri kwa pete ya mfalme na kuzipeleka kwa njia ya matarishi, ambao waliendesha farasi waendao kasi waliozalishwa maalum kwa ajili ya mfalme. Waraka wa mfalme uliwaruhusu Wayahudi katika kila mji kuwa na haki ya kukusanyika na kujilinda wenyewe; kuharibu, kuua na kuangamiza jeshi lolote, taifa lolote au jimbo lile litakalowashambulia wao, wake zao, watoto wao na kuteka mali za adui zao. Siku ambayo iliwekwa kwa Wayahudi kufanya hili katika majimbo yote ya Mfalme Ahasuero ilikuwa siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, yaani mwezi wa Adari. Nakala ya tangazo ilikuwa itolewe kama sheria katika kila jimbo na iweze kujulikana kwa watu wa kila taifa, ili kwamba Wayahudi wawe tayari siku hiyo kulipiza kisasi kwa adui zao. Matarishi, wakiwa wamepanda farasi wa kifalme, walitoka mbio wakichochewa na agizo la mfalme. Tangazo lilitolewa pia katika ngome ya mji wa Shushani. Mordekai akaondoka mbele ya mfalme akiwa amevaa mavazi ya kifalme ya buluu na nyeupe, taji kubwa la dhahabu na joho la zambarau la kitani safi. Na mji wa Shushani ukasherehekea kwa furaha. Kwa maana kwa Wayahudi ulikuwa wakati wa raha na furaha, shangwe na heshima. Katika kila jimbo na katika kila jiji, popote waraka wa mfalme ulipofika, kulikuwepo furaha na shangwe miongoni mwa Wayahudi, pamoja na karamu na kushangilia. Na watu wengi wa mataifa mengine wakajifanya Wayahudi kwa sababu ya kuwahofu Wayahudi.

Shirikisha
Soma Esta 8

Esta 8:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

Siku hiyohiyo, mfalme Ahasuero alimkabidhi malkia Esta mali yote ya Hamani, adui ya Wayahudi. Esta akamjulisha mfalme kwamba Mordekai ni jamaa yake. Basi, tangu wakati huo, Mordekai akaruhusiwa kumwona mfalme. Mfalme akaivua pete yake ya mhuri aliyokuwa amemnyanganya Hamani, akampa Mordekai. Esta naye akampa Mordekai mamlaka juu ya mali ya Hamani. Kisha Esta akazungumza tena na mfalme; akajitupa chini, miguuni pa mfalme, huku analia, akamsihi mfalme aukomeshe mpango mbaya ambao Hamani, wa uzao wa Agagi, alikuwa amepanga dhidi ya Wayahudi. Mfalme akamnyoshea Esta fimbo yake ya dhahabu, naye Esta akasimama na kusema, “Ukipenda, ewe mfalme, na kama unanijali na ukiona inafaa, tafadhali, toa tangazo la kufutilia mbali mipango ambayo Hamani alikuwa ameamuru itekelezwe. Mipango hiyo ni ile ya mwana wa Hamedatha, mzaliwa wa Agagi, aliyopanga ili kuwaangamiza Wayahudi wote katika mikoa yote. Maana, ninawezaje kuvumilia kuona watu wangu wanaangamizwa na jamaa zangu wanauawa?” Mfalme Ahasuero akawaambia malkia Esta na Mordekai, yule Myahudi, “Tazameni! Nimempa Esta mali yake Hamani, naye wamekwisha mnyonga kwa sababu ya njama zake dhidi ya Wayahudi. Mwaweza kuwaandikia Wayahudi lolote mpendalo. Tena mwaweza kuandika kwa jina langu na kutumia mhuri wa kifalme, kwa sababu tangazo ambalo limetolewa kwa jina la mfalme na kupigwa mhuri wa mfalme, haliwezi kubatilishwa.” Basi, mnamo siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa tatu uitwao Siwani, Mordekai aliwaita makatibu wote wa mfalme, akawaagiza waandike barua kwa Wayahudi na wakuu, watawala na maofisa wa mikoa yote 127, kuanzia India mpaka Kushi. Nyaraka hizo ziliandikwa kwa kila mkoa katika lugha yake na hati yake ya maandishi, hali kadhalika kwa Wayahudi. Mordekai alikuwa ameandika nyaraka hizo kwa jina la mfalme Ahasuero, akazipiga mhuri kwa pete ya mfalme. Na waliozipeleka walikuwa matarishi waliopanda farasi wenye nguvu waendao kasi. Kwa njia ya nyaraka hizi mfalme aliwaruhusu Wayahudi katika kila mji kukusanyika ili kuyalinda maisha yao. Walikuwa na ruhusa ya kuharibu, kuua bila huruma na kuangamiza kundi lolote la watu au mkoa, lenye kuwashambulia kwa silaha pamoja na wanawake na watoto wao, na kuziteka nyara mali zao. Jambo hili lingefanyika katika mikoa yote ya mfalme Ahasuero, mnamo siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, yaani Adari. Nakala za tangazo hili ambalo lilitolewa kama sheria katika kila mkoa zilisambazwa kwa kila mtu katika kila mkoa, ili Wayahudi wajiandae kulipiza kisasi siku hiyo ifikapo. Kwa amri ya mfalme, matarishi waliopanda farasi wenye nguvu waendao kasi, waliondoka mbio. Tangazo hili pia lilitolewa katika mji mkuu, Susa. Mordekai alipotoka ikulu kwa mfalme, akiwa amevalia mavazi ya kifalme ya rangi ya urujuani na nyeupe, joho la kitani safi la rangi ya zambarau, na taji kubwa ya dhahabu, mji wa Susa ulijaa shangwe na vigelegele. Hapo Wayahudi waliona fahari, heshima na furaha, wakajisikia wenye nafuu na ushindi. Katika kila mkoa na kila mji, popote pale tangazo hili liliposomwa, Wayahudi walifurahi na kushangilia, wakafanya sherehe na mapumziko; na watu wengine wengi wakajifanya kuwa Wayahudi, maana waliwaogopa sana Wayahudi.

Shirikisha
Soma Esta 8

Esta 8:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Siku ile mfalme Ahasuero alimpa malkia Esta nyumba yake Hamani, yule adui ya Wayahudi. Mordekai naye akaja mbele ya mfalme; kwa maana Esta alikuwa amedhihirisha alivyomhusu. Basi mfalme akaivua pete yake, aliyompokonya Hamani, akampa Mordekai. Naye Esta akamweka Mordekai kuwa juu ya mlango wake Hamani. Tena Esta akasema na mfalme mara ya pili, akaanguka miguuni pake, akamsihi kwa machozi ayaondoe madhara ya Hamani, Mwagagi, na shauri alilowafanyia Wayahudi. Ndipo mfalme alipomnyoshea Esta fimbo yake ya dhahabu. Basi Esta akaondoka, akasimama mbele ya mfalme. Akasema, Mfalme akiona vema, nami nikiwa nimepata kibali machoni pake, na neno likionekana jema mbele ya mfalme, nami nikimpendeza machoni pake, na iandikwe amri kuzitangua barua za Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, alizotunga na kuziandika ili kuwaangamiza Wayahudi walioko katika mikoa yote ya mfalme. Maana, ninawezaje kustahimili kuyaona mabaya yatakayowajia watu wangu? Au kuyatazama maangamizi ya jamaa zangu? Mfalme Ahasuero akawaambia malkia Esta na Mordekai, Myahudi, akasema, Tazama, nimekwisha kumpa Esta nyumba yake Hamani, naye mwenyewe wamekwisha kumtundika juu ya mti, kwa sababu aliwatia mikono Wayahudi. Basi nanyi pia waandikieni Wayahudi vyovyote mpendavyo, kwa jina la mfalme, mkatie mhuri kwa pete ya mfalme; kwa kuwa andiko lililoandikwa kwa jina la mfalme na kutiwa mhuri kwa pete ya mfalme, hakuna awezaye kulitangua. Basi, waandishi wa mfalme wakaitwa pale pale, siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa tatu, ndio mwezi wa Siwani; na kama vile Mordekai alivyoamuru, Wayahudi wakaandikiwa, pamoja na wakuu wa tarafa na wakuu wa mikoa kuanzia Bara Hindi mpaka Kushi, mikoa mia moja na ishirini na saba, kila mkoa kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake; na Wayahudi kwa mwandiko wao na kwa lugha yao. Akaandika kwa jina la mfalme Ahasuero, na kutia mhuri kwa pete ya mfalme, barua zikapelekwa na matarishi, wamepanda farasi, wamepanda wanyama wepesi sana waliotumika kwa huduma ya mfalme, ndio waliozalishwa katika zizi la mfalme. Katika barua hizo mfalme aliwaruhusu Wayahudi katika kila mji wakusanyike na kuyalinda maisha yao, kwa kuangamiza, kuua, na kulimaliza jeshi lote la watu au mkoa watakaowashambulia, pamoja na watoto na wanawake; na kuyachukua mali yao kuwa nyara; siku moja, katika mikoa yote ya mfalme Ahasuero, yaani, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari. Nakala ya andiko, ya kupigwa mbiu katika kila jimbo, ilitangazwa kwa mataifa yote, na kwa Wayahudi, wawe tayari siku ile ile kujilipiza kisasi juu ya adui zao. Matarishi wakaondoka, wamepanda wanyama wepesi sana waliotumika kwa huduma ya mfalme, huku wakihimizwa na kusukumizwa kwa amri ya mfalme; kukapigwa mbiu huko Susa mjini. Naye Mordekai akatoka usoni pa mfalme, amevaa mavazi ya kifalme, ya rangi ya samawati na nyeupe, mwenye taji kubwa la dhahabu, na joho la kitani safi na rangi ya zambarau. Mji wa Susa wakapaza sauti, wakashangilia. Ikawa nuru na furaha na shangwe na heshima kwa Wayahudi. Na katika kila mkoa, na kila mji, popote palipowasili amri ya mfalme na mbiu yake, Wayahudi wakapata furaha na shangwe, karamu na sikukuu. Hata wengi wa watu wa nchi wakajifanya Wayahudi, maana waliwaogopa Wayahudi.

Shirikisha
Soma Esta 8

Esta 8:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Siku ile mfalme Ahasuero alimpa malkia Esta nyumba yake Hamani, yule adui ya Wayahudi. Mordekai naye akahudhuria mbele ya mfalme; kwa maana Esta alikuwa amedhihirisha alivyomhusu. Basi mfalme akaivua pete yake, aliyompokonya Hamani, akampa Mordekai. Naye Esta akamweka Mordekai kuwa juu ya mlango wake Hamani. Tena Esta akasema na mfalme mara ya pili, akaanguka miguuni pake, akamsihi kwa machozi ayaondoe madhara ya Hamani, Mwagagi, na shauri alilowafanyia Wayahudi. Ndipo mfalme alipomnyoshea Esta fimbo yake ya dhahabu. Basi Esta akaondoka, akasimama mbele ya mfalme. Akasema, Mfalme akiona vema, nami nikiwa nimepata kibali machoni pake, na neno likionekana jema mbele ya mfalme, nami nikimpendeza machoni pake, iandikwe kuzitangua barua za Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, alizotunga na kuziandika ili kuwaangamiza Wayahudi walioko katika majimbo yote ya mfalme. Kwa maana niwezeje kuyaona mabaya yatakayowajia watu wangu? Au niwezeje kuyatazama maangamizo ya jamaa zangu? Mfalme Ahasuero akawaambia malkia Esta na Mordekai, Myahudi, kusema, Tazama, nimekwisha kumpa Esta nyumba yake Hamani, naye mwenyewe wamekwisha kumtundika juu ya mti, kwa sababu aliwatia mikono Wayahudi. Basi waandikieni Wayahudi pia vyo vyote mpendavyo, kwa jina la mfalme, mkatie muhuri kwa pete ya mfalme; kwa kuwa andiko lililoandikwa kwa jina la mfalme na kutiwa muhuri kwa pete ya mfalme hakuna awezaye kulitangua. Basi, waandishi wa mfalme wakaitwa pale pale, siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa tatu, ndio mwezi wa Siwani; na kama vile Mordekai alivyoamuru, Wayahudi wakaandikiwa, pamoja na maakida na maliwali, na wakuu wa majimbo toka Bara Hindi mpaka Kushi, majimbo mia na ishirini na saba, kila jimbo kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake; na Wayahudi kwa mwandiko wao na kwa lugha yao. Akaandika kwa jina la mfalme Ahasuero, na kutia muhuri kwa pete ya mfalme, akazipeleka barua kwa matarishi, wamepanda farasi, wamepanda wanyama wepesi sana waliotumika kwa huduma ya mfalme, ndio waliozalishwa katika zizi la mfalme. Katika barua hizo mfalme aliwaruhusu Wayahudi wakusanyike katika kila mji na kuzisimamia maisha zao, kuangamiza, na kuua, na kulifisha jeshi lote la watu na la jimbo watakaowaondokea, wao na wadogo wao na wanawake; na kuyachukua mali yao kuwa nyara; siku moja, katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero, yaani, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari. Nakili ya andiko, ya kupigwa mbiu katika kila jimbo, ilitangazwa kwa mataifa yote, na kwa Wayahudi, wawe tayari siku ile ile kujilipiza kisasi juu ya adui zao. Matarishi wakaondoka, wamepanda wanyama wepesi sana waliotumika kwa huduma ya mfalme, huku wakihimizwa na kusukumizwa kwa amri ya mfalme; kukapigwa mbiu huko Shushani ngomeni. Naye Mordekai akatoka usoni pa mfalme, amevaa mavazi ya kifalme, ya rangi ya samawi na nyeupe, mwenye taji kubwa ya dhahabu, na joho ya kitani safi na rangi ya zambarau. Mji wa Shushani wakapaza sauti, wakashangilia. Ikawa nuru na furaha na shangwe na heshima kwa Wayahudi. Na katika kila jimbo, na kila mji, po pote palipowasili amri ya mfalme na mbiu yake, Wayahudi wakapata furaha na shangwe, karamu na sikukuu. Hata wengi wa watu wa nchi wakajifanya Wayahudi, kwa kuwa hofu ya Wayahudi imewaangukia.

Shirikisha
Soma Esta 8