Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Esta 6:1-14

Esta 6:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Usiku ule mfalme hakupata usingizi; akaamuru aletewe kitabu cha kumbukumbu nacho kikasomwa mbele ya mfalme. Ikaonekana kuwa imeandikwa ya kwamba Mordekai aliwasema Bigthana na Tereshi, wasimamizi wawili wa mfalme, katika hao waliolinda mlango, waliotaka kumwua mfalme Ahasuero. Mfalme akasema, Je! Ni heshima gani au hadhi gani Mordekai aliyofanyiwa kwa ajili ya hayo? Watumishi wa mfalme waliomhudumia wakamwambia, Hakuna alilofanyiwa. Mfalme akasema, Yupo nani behewani? Ikawa Hamani alikuwa ameingia katika ua wa nje wa nyumba ya mfalme, aseme na mfalme, ili kumtundika Mordekai juu ya mti ule aliomwandalia. Basi watumishi wa mfalme wakamwambia, Tazama, Hamani yupo, amesimama behewani. Mfalme akasema, Na aingie. Basi Hamani akaingia. Mfalme akamwambia, Afanyiwe nini yule ambaye mfalme apenda kumheshimu? Hamani akasema moyoni mwake, Ni nani ambaye mfalme apenda kumheshimu kuliko mimi? Basi Hamani akamwambia mfalme, Yule ambaye mfalme apenda kumheshimu, na aletewe mavazi ya kifalme ambayo mfalme amezoea kuyavaa, na farasi ambaye mfalme humpanda mwenyewe, ambaye ametiwa taji la kifalme kichwani; na yale mavazi na yule farasi akabidhiwe mkononi mmojawapo wa wakuu wa mfalme aliye mstahiki; ili makusudi amvike yule ambaye mfalme apenda kumheshimu, na kumpandisha juu ya farasi na kumtembeza kupitia njia kuu ya mjini, na kupiga mbiu mbele yake, kusema, Hivyo ndivyo atakavyofanyiwa mtu yule ambaye mfalme apenda kumheshimu. Basi mfalme akamwambia Hamani, Hima! Twaa mavazi na farasi kama ulivyosema, ukamfanyie vivyo hivyo Mordekai, Myahudi, aketiye mlangoni pa mfalme; lisipungue neno lolote katika yote uliyoyasema. Ndipo Hamani alipoyatwaa mavazi na farasi, akamvika Mordekai yale mavazi, akampandisha juu ya farasi na kumtembeza kupitia njia kuu ya mjini, akapiga mbiu mbele yake, Hivyo ndivyo atakavyofanyiwa mtu yule ambaye mfalme apenda kumheshimu. Kisha Mordekai akarudi kwenye lango la mfalme. Bali Hamani akaenda mbio nyumbani kwake, akiomboleza na kichwa chake kimefunikwa. Basi Hamani akawasimulia Zereshi mkewe na marafiki zake wote kila neno lililompata. Kisha watu wake wenye hekima na Zereshi mkewe wakamwambia, Ikiwa huyu Mordekai, ambaye umeanza kuanguka mbele yake, ni wa uzao wa Wayahudi, wewe hutamweza, bali kuanguka utaanguka mbele yake. Walipokuwa wangali wakisema naye, matowashi wa mfalme walifika, wakahimiza kumleta Hamani katika karamu ile aliyoiandaa Esta.

Shirikisha
Soma Esta 6

Esta 6:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Usiku huo, mfalme hakupata usingizi. Basi, akaamuru kitabu cha kumbukumbu za matukio ya kila siku kiletwe, nacho kikasomwa mbele yake. Ikaonekana ilivyoandikwa jinsi Mordekai alivyongamua njama ya kumwua mfalme iliyokuwa imefanywa na Bigthana na Tereshi, wawili kati ya matowashi wa mfalme waliokuwa walinzi wa vyumba vya mfalme. Mfalme akauliza, “Je, tumempa Mordekai heshima au tuzo gani kwa jambo hili?” Watumishi wake wakamjibu, “Hujafanya kitu kwa ajili yake.” Mfalme akauliza, “Kuna ofisa yeyote uani?” Ikawa wakati huo Hamani alikuwa ameingia katika ua wa nje wa ikulu; alikuwa amekuja kwa mfalme kuomba Mordekai auawe kwenye mti wa kuulia ambao alikuwa amekwisha mtayarishia. Basi, watumishi wakamjibu mfalme, “Hamani yuko uani.” Mfalme akasema, “Mkaribishe ndani.” Hamani alipoingia ndani, mfalme akamwuliza, “Je, nimfanyie nini mtu ambaye ningependa sana kumtunukia heshima?” Hamani akafikiria moyoni mwake: “Ni nani huyo ambaye mfalme angependa kumtunukia sana heshima? Bila shaka ni mimi.” Basi, Hamani akamjibu mfalme, “Mtu huyo ambaye mfalme angependa kumtunukia heshima, yafaa watumishi wa mfalme walete mavazi safi ya kitani aliyovaa mfalme na farasi wake mwenyewe, na mmoja wa washauri wako wa kuheshimika, ee mfalme, amvishe mtu huyo mavazi hayo ya kifalme, na kumwongoza mtu huyo akiwa amepanda farasi wako mpaka kwenye uwanja wa mji, huku anatangaza: ‘Hivi ndivyo anavyotendewa mtu ambaye mfalme amependa kumpa heshima.’” Hapo mfalme akamwambia Hamani, “Fanya haraka! Chukua mavazi hayo na farasi, ukamtunukie heshima hii Mordekai, Myahudi ambaye hukaa penye lango la ikulu. Usiache kumfanyia hata jambo moja kati ya hayo uliyoyataja.” Basi, Hamani akachukua mavazi hayo na kumvisha Mordekai, akamtembeza kwenye uwanja wa mji akiwa juu ya farasi wa mfalme, huku anatangaza: “Hivi ndivyo anavyotendewa mtu ambaye mfalme amependa kumpa heshima.” Kisha Mordekai akarudi kwenye lango la ikulu. Lakini Hamani akakimbilia nyumbani kwake, amejaa huzuni na amekifunika kichwa chake kwa aibu. Huko akawasimulia Zereshi, mkewe, na rafiki zake wote mambo yote yaliyompata. Zereshi na hao rafiki zake wakamwambia: “Ikiwa huyu Mordekai, ambaye umeanza kupoteza madaraka yako kwake ni wa kabila la Wayahudi, basi, hutamweza; atakushinda kabisa.” Walipokuwa bado wanaongea hayo, matowashi wa mfalme wakafika hima kumchukua Hamani kwenda kwenye karamu ya Esta.

Shirikisha
Soma Esta 6

Esta 6:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Usiku ule mfalme hakupata usingizi; akaamuru aletewe kitabu cha maandiko ya taarifa, nayo yakasomwa mbele ya mfalme. Ikaonekana kuwa imeandikwa ya kwamba Mordekai aliwachongea Bigthana na Tereshi, wasimamizi wawili wa mfalme, katika hao waliolinda mlango, waliotaka kumtia mikono mfalme Ahasuero. Mfalme akasema, Je! Ni heshima gani au jaha gani Mordekai aliyofanyiziwa kwa ajili ya hayo? Watumwa wa mfalme waliomhudumu wakamwambia, Hakuna alilofanyiziwa. Mfalme akasema, Yupo nani behewani? Ikawa Hamani alikuwa ameingia katika ua wa nje wa nyumba ya mfalme, aseme na mfalme, ili kumtundika Mordekai juu ya mti ule aliomwekea tayari. Basi watumwa wa mfalme wakamwambia, Tazama, Hamani yupo, amesimama behewani. Mfalme akasema, Na aingie. Basi Hamani akaingia. Mfalme akamwambia, Afanyiziwe nini yule ambaye mfalme apenda kumheshimu? Hamani akasema moyoni mwake, Ni nani ambaye mfalme apenda kumheshimu kuliko mimi? Basi Hamani akamwambia mfalme, Yule ambaye mfalme apenda kumheshimu, na aletewe mavazi ya kifalme ambayo mfalme amezoea kuyavaa, na farasi ambaye mfalme humpanda mwenyewe, ambaye ametiwa taji ya kifalme kichwani; na yale mavazi na yule farasi akabidhiwe mkononi mmojawapo wa maakida wa mfalme aliye mstahiki; ili makusudi amvike yule ambaye mfalme apenda kumheshimu, na kumrakibisha juu ya farasi kuipitia njia kuu ya mjini, na kupiga mbiu mbele yake, kusema, Hivyo ndivyo atakavyofanyiziwa mtu yule ambaye mfalme apenda kumheshimu. Basi mfalme akamwambia Hamani, Hima! Twaa mavazi na farasi kama ulivyosema, ukamfanyizie vivyo hivyo Mordekai, Myahudi, aketiye mlangoni pa mfalme; lisipungue neno lo lote katika yote uliyoyasema. Ndipo Hamani alipoyatwaa mavazi na farasi, akamvika Mordekai yale mavazi, akamrakibisha juu ya farasi kuipitia njia kuu ya mjini, akapiga mbiu mbele yake, Hivyo ndivyo atakavyofanyiziwa mtu yule ambaye mfalme apenda kumheshimu. Kisha Mordekai akarudi kwenye mlango wa mfalme. Bali Hamani akaenda mbio nyumbani kwake, mwenye msiba, na kichwa chake kimefunikwa. Basi Hamani akawasimulia Zereshi mkewe na rafiki zake wote kila neno lililompata. Kisha watu wake wenye hekima na Zereshi mkewe wakamwambia, Ikiwa huyu Mordekai, ambaye umeanza kuanguka mbele yake, ni wa uzao wa Wayahudi, wewe hutamweza, bali kuanguka utaanguka mbele yake. Hata walipokuwa katika kusema naye, wasimamizi-wa-nyumba wa mfalme walifika, wakahimiza kumleta Hamani katika karamu ile aliyoiandaa Esta.

Shirikisha
Soma Esta 6

Esta 6:1-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Usiku ule mfalme hakupata usingizi, hivyo akaagiza aletewe kitabu cha kumbukumbu za matukio ya utawala wake, asomewe. Kitabu hicho kilikutwa na kumbukumbu kwamba Mordekai alikuwa amefichua jinsi Bigthana na Tereshi, waliokuwa maafisa wawili wa mfalme, walinzi wa lango walivyokuwa wamepanga hila ya kumuua Mfalme Ahasuero. Mfalme akauliza, “Je, ni heshima na shukrani gani Mordekai alipokea kwa ajili ya jambo hili?” Watumishi wake wakajibu, “Hakuna lolote alilofanyiwa.” Mfalme akasema, “Ni nani yuko uani?” Wakati huo huo Hamani alikuwa ameingia ua wa nje wa jumba la mfalme kusema na mfalme kuhusu kumwangika Mordekai katika mahali pa kuangikia watu alipokuwa amepajenga kwa ajili yake. Watumishi wake wakamjibu, “Hamani amesimama uani.” Mfalme akaamuru, “Mleteni ndani.” Hamani alipoingia, mfalme alimuuliza, “Afanyiwe nini mtu ambaye mfalme apenda kumheshimu?” Basi Hamani akawaza moyoni mwake, “Ni nani mwingine ambaye mfalme angemheshimu kuliko mimi?” Kwa hiyo akamjibu mfalme, “Kwa mtu ambaye mfalme apenda kumheshimu, aletewe joho la kifalme ambalo mfalme ameshalivaa na farasi ambaye mfalme alishampanda, ambaye amevikwa taji ya kifalme kichwani mwake. Kisha joho na farasi vikabidhiwe kwa mmojawapo wa wakuu wa mfalme anayeheshimika sana. Nao wamvike mtu yule ambaye mfalme anapenda kumheshimu, na aongozwe akiwa juu ya farasi kupitia barabara za mji, wakitangaza mbele yake, ‘Hivi ndivyo anavyofanyiwa mtu ambaye mfalme apenda kumheshimu!’ ” Mfalme akamwamuru Hamani, “Nenda mara moja, chukua joho na farasi na ufanye kama vile ulivyopendekeza kwa Mordekai Myahudi, akaaye langoni mwa mfalme. Usipuuze kufanya kitu chochote ulichoshauri.” Hivyo Hamani akachukua joho na farasi. Akamvika Mordekai, na kumpandisha juu ya farasi akamtembeza katika barabara za mji akitangaza mbele yake, “Hivi ndivyo anavyofanyiwa mtu ambaye mfalme anapenda kumheshimu!” Baadaye Mordekai akarudi kwenye lango la mfalme. Lakini Hamani akakimbia nyumbani, akiwa amejaa huzuni, naye akamweleza Zereshi mkewe pamoja na rafiki zake wote kila kitu ambacho kimempata. Washauri wake pamoja na Zereshi mkewe wakamwambia, “Kwa kuwa Mordekai, ambaye mbele yake umeanza kuanguka ni wa asili ya Kiyahudi, huwezi kushindana naye; kwa hakika utaanguka!” Walipokuwa bado wakizungumza naye, matowashi wa mfalme wakaja na kumharakisha Hamani aende katika karamu aliyoiandaa Esta.

Shirikisha
Soma Esta 6

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha