Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Esta 5:1-14

Esta 5:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Siku ya tatu ya mfungo wake, Esta alivalia mavazi yake ya kimalkia, akaenda akasimama katika ua wa ndani wa nyumba ya mfalme, kuelekea ukumbi wa mfalme. Mfalme alikuwamo ndani, amekaa katika kiti chake cha enzi, kuelekea mlango wa nyumba ya mfalme. Mfalme alipomwona malkia Esta amesimama uani, alipendezwa naye, akamnyoshea fimbo ya dhahabu aliyokuwa ameshika mkononi mwake. Esta akakaribia, akagusa ncha ya fimbo. Hapo mfalme akauliza, “Unataka nini Esta? Niambie unachotaka, nawe utapata – hata kama ni nusu ya ufalme wangu.” Esta akamjibu, “Ukipenda, ewe mfalme, uje leo pamoja na Hamani, kwenye karamu ninayoandaa kwa ajili yako, mfalme.” Mfalme akatoa amri Hamani aje upesi, kama Esta alivyoomba. Basi, mfalme na Hamani wakaenda kwenye karamu aliyoandaa Esta. Walipokuwa wanakunywa divai, mfalme akamwuliza tena Esta: “Unataka nini? Niambie, nawe utapata. Ombi lako ni nini? Hata kama ni nusu ya ufalme wangu, utapewa.” Esta akamjibu, “Ombi langu ni hili: Kama u radhi, ewe mfalme, kukubali ombi langu, basi, naomba wewe na Hamani mje kesho kwenye karamu nyingine nitakayowaandalieni. Wakati huo nitakujulisha ombi langu.” Hamani alitoka huko karamuni mwenye furaha tele na moyo mkunjufu. Lakini alipomwona Mordekai penye lango la ikulu, hasimami wala hampi heshima, Hamani akawaka hasira. Hata hivyo, alijizuia, akaenda zake nyumbani. Halafu akawaalika nyumbani kwake rafiki zake, na kumwomba Zereshi mkewe ajiunge nao. Ndipo akaanza kuelezea juu ya utajiri aliokuwa nao, wana aliokuwa nao, jinsi mfalme alivyompandisha cheo, na jinsi alivyopewa madaraka zaidi kuliko maofisa wengine wote wa mfalme. Hamani akaendelea kujitapa, “Isitoshe malkia Esta hakumwalika mtu mwingine yeyote pamoja na mfalme isipokuwa mimi tu. Hata kesho pia, ametualika mimi na mfalme. Lakini yote haya hayaniridhishi iwapo nitaendelea kumwona yule Myahudi Mordekai penye lango la ikulu.” Basi, Zereshi, mkewe, na marafiki zake, wakamshauri hivi: “Kwa nini asitengenezewe mti wa kuulia, wenye urefu wa mita ishirini na mbili? Kesho asubuhi, unaweza kuzungumza na mfalme ili Mordekai auawe juu yake, kisha uende ukale karamu na mfalme kwa furaha.” Wazo hilo lilimfurahisha Hamani, naye akatengeneza mti wa kuulia.

Shirikisha
Soma Esta 5

Esta 5:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa siku ya tatu Esta alijivika mavazi yake ya kifalme, akasimama katika ua wa ndani wa nyumba ya mfalme, kuielekea nyumba ya mfalme; naye mfalme akaketi juu ya kiti chake cha enzi katika nyumba ya mfalme, kuuelekea mlango wa kasri. Ikawa, mfalme alipomwona malkia Esta amesimama uani, yeye akapata kibali machoni pake; naye mfalme akamnyoshea Esta fimbo ya dhahabu aliyokuwa nayo mkononi. Basi Esta akakaribia, akaigusa ncha ya fimbo. Mfalme akamwambia, malkia Esta, unataka nini? Nayo ni haja gani uliyo nayo? Utapewa hata nusu ya ufalme. Esta akasema, Mfalme akiona vema, na aje leo, mfalme na Hamani, kwenye karamu niliyomwandalia. Basi mfalme akasema, Mhimize Hamani, ili ifanyike kama Esta alivyoomba. Hivyo mfalme na Hamani wakafika katika karamu ile aliyoiandaa Esta. Basi mfalme akamwambia Esta pale penye karamu ya divai, Dua yako ni nini? Nawe utapewa; na haja yako ni nini? Hata nusu ya ufalme utatimiziwa. Esta akajibu, na kusema, Dua yangu ni hii, na haja yangu ni hii, Ikiwa nimepata kibali machoni pa mfalme, na mfalme akiona vema kunipa niombalo, na kunitimizia haja yangu, na aje tena mfalme na Hamani kwenye karamu nitakayowaandalia, nami kesho nitafanya kama vile mfalme alivyosema. Basi Hamani alitoka siku ile kwa furaha na ukunjufu wa moyo; lakini Hamani alipomwona Mordekai mlangoni pa mfalme, ya kwamba hasimami wala kunyenyekea mbele yake, alijaa ghadhabu juu ya Mordekai. Lakini Hamani akajizuia, akaenda zake nyumbani kwake; akatuma watu kuwaita marafiki zake na Zereshi mkewe. Naye Hamani akawasimulia habari za fahari ya mali zake, na wingi wa watoto wake, na pia mambo yote ambayo mfalme amemfanikisha kwayo, na jinsi alivyompandisha cheo juu ya wakuu na watumishi wa mfalme. Zaidi ya hayo Hamani akasema, Naye malkia Esta hakumkaribisha mtu yeyote pamoja na mfalme katika karamu aliyoiandaa, ila mimi peke yangu; hata na kesho pia nimealikwa naye pamoja na mfalme. Bali haya yote yanifaa nini, niendeleapo kumwona yule Mordekai, Myahudi, ameketi mlangoni pa mfalme? Basi Zereshi mkewe na marafiki wote wa Hamani wakamwambia, Na kitengenezwe kiunzi cha mti wa kunyongea wa urefu wa mikono hamsini, na kesho asubuhi useme na mfalme ili Mordekai atundikwe juu yake; ndipo utakapoingia kwa furaha pamoja na mfalme karamuni. Basi ushauri huu ukamridhisha Hamani, akautengeneza mti wa kunyongea.

Shirikisha
Soma Esta 5

Esta 5:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa siku ya tatu Esta alijivika mavazi yake ya kifalme, akasimama katika ua wa ndani wa nyumba ya mfalme, kuielekea nyumba ya mfalme; naye mfalme akaketi juu ya kiti chake cha enzi katika nyumba ya mfalme, kuuelekea mlango wa nyumba. Ikawa, mfalme alipomwona malkia Esta amesimama uani, yeye akapata kibali machoni pake; naye mfalme akamnyoshea Esta fimbo ya dhahabu aliyokuwa nayo mkononi. Basi Esta akakaribia, akaigusa ncha ya fimbo. Mfalme akamwambia, Malkia Esta, wataka nini? Nayo ni haja gani uliyo nayo? Utapewa hata nusu ya ufalme. Esta akasema, Mfalme akiona vema, na aje leo, mfalme na Hamani, kwenye karamu niliyomwandalia. Basi mfalme akasema, Mhimize Hamani, ili ifanyike kama Esta alivyosema. Hivyo mfalme na Hamani wakafika katika karamu ile aliyoiandaa Esta. Basi mfalme akamwambia Esta pale penye karamu ya divai, Dua yako ni nini? Nawe utapewa; na haja yako ni nini? Hata nusu ya ufalme utafanyiziwa. Esta akajibu, na kusema, Dua yangu ni hii, na haja yangu ni hii, Ikiwa nimepata kibali machoni pa mfalme, na mfalme akiona vema kunipa niombalo, na kunifanyizia haja yangu, na aje tena mfalme na Hamani kwenye karamu nitakayowaandalia, nami kesho nitafanya kama vile mfalme alivyosema. Basi Hamani alitoka siku ile kwa furaha na ukunjufu wa moyo; lakini Hamani alipomwona Mordekai mlangoni pa mfalme, ya kwamba hasimami wala kutetemeka mbele yake, alijaa ghadhabu juu ya Mordekai. Walakini Hamani akajizuia, akaenda zake nyumbani kwake; akatuma kuwaita rafiki zake na Zereshi mkewe. Naye Hamani akawasimulia habari za fahari ya mali zake, na wingi wa watoto wake, nayo mambo yote pia ambayo mfalme amemfanikisha katika hayo, na jinsi alivyompandisha juu ya maakida na watumishi wa mfalme. Zaidi ya hayo Hamani akasema, Naye malkia Esta hakumkaribisha mtu ye yote pamoja na mfalme katika karamu aliyoiandaa, ila mimi peke yangu; hata na kesho pia nimealikwa naye pamoja na mfalme. Bali haya yote yanifaa nini, pindi nimwonapo yule Mordekai, Myahudi, ameketi mlangoni pa mfalme? Basi Zereshi mkewe akamwambia, na rafiki zake wote, Na ufanyizwe mti wa mikono hamsini urefu wake, na kesho asubuhi useme na mfalme ili Mordekai atundikwe juu yake; ndipo utakapoingia kwa kicheko pamoja na mfalme karamuni. Basi neno likampendeza Hamani, akaufanyiza ule mti.

Shirikisha
Soma Esta 5

Esta 5:1-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Siku ya tatu, Esta alivaa mavazi yake ya kimalkia, naye akasimama katika ua wa ndani wa jumba la mfalme, mbele ya ukumbi wa mfalme. Naye mfalme alikuwa akiketi katika kiti chake cha kifalme katika ukumbi, akielekea langoni. Alipomwona Malkia Esta amesimama uani alipendezwa naye, akamnyooshea fimbo ya utawala ya dhahabu ile iliyokuwa mkononi mwake. Kwa hiyo Esta alikaribia na kuigusa ncha ya fimbo ya mfalme. Kisha mfalme aliuliza, “Malkia Esta, ni nini? Ombi lako ni nini? Hata kama ni nusu ya ufalme, utapewa.” Esta akajibu, “Kama itampendeza mfalme, mfalme pamoja na Hamani waje leo katika karamu ambayo nimeiandaa kwa ajili yake.” Mfalme akasema, “Mleteni Hamani mara moja, ili tupate kufanya lile Esta analoomba.” Kwa hiyo mfalme na Hamani walihudhuria karamu aliyoiandaa Esta. Walipokuwa wakinywa mvinyo mfalme akamuuliza Esta tena, “Sasa haja yako ni nini? Utapewa. Ombi lako ni nini? Hata nusu ya ufalme, utapewa.” Esta akajibu, “Haja yangu na ombi langu ni hili: Kama mfalme ameona vyema, nami nimepata kibali kwake na kama ikimpendeza mfalme kunipa ombi langu na kunitimizia haja yangu, mfalme na Hamani waje kwangu kesho katika karamu nitakayowaandalia. Kisha nitajibu swali la mfalme.” Hamani alitoka siku hiyo kwa furaha na moyo mchangamfu. Lakini alipomwona Mordekai langoni mwa mfalme na kuona kwamba hakusimama wala hakuonyesha hofu mbele yake, alijawa na ghadhabu dhidi ya Mordekai. Hata hivyo, Hamani alijizuia akaenda zake nyumbani. Akawaita pamoja rafiki zake na Zereshi, mkewe. Hamani akajisifia kwao juu ya utajiri wake mwingi, wanawe wengi na kwa njia zote ambazo mfalme amemheshimu kwazo na jinsi alivyomweka juu ya wakuu na maafisa wengine. Hamani akaongeza, “Si hayo tu. Mimi ndiye mtu pekee ambaye Malkia Esta amemwalika kumsindikiza mfalme kwenye karamu aliyomwandalia. Naye amenialika pamoja na mfalme kesho. Lakini haya yote hayanipi kuridhika iwapo ninaendelea kumwona yule Myahudi Mordekai akiketi kwenye lango la mfalme.” Zereshi mkewe na rafiki zake wote wakamwambia, “Tengeneza mahali pa kuangika watu kimo chake dhiraa hamsini, kisha kesho asubuhi mwombe mfalme Mordekai aangikwe juu yake. Ndipo uende na mfalme kwenye karamu kwa furaha.” Shauri hili lilimpendeza Hamani, naye akajenga mahali pa kuangika watu.

Shirikisha
Soma Esta 5

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha