Waefeso 3:8-13
Waefeso 3:8-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Mimi ni mdogo kuliko watu wote wa Mungu; lakini amenijalia neema yake, ili niwahubirie watu wa mataifa utajiri wake Kristo usiopimika; tena niwaangazie watu wote waone jinsi mpango wa Mungu uliofichika unavyotekelezwa. Mungu aliye Muumba wa vitu vyote alificha hiyo siri yake tangu milele, kusudi sasa, kwa njia ya kanisa, wakuu na wenye enzi wa mbinguni wapate kuitambua hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi. Mungu alifanya jambo hilo kufuatana na azimio lake la milele ambalo amelifanya kwa njia ya Kristo Yesu Bwana wetu. Basi, kwa kuungana na Kristo na kwa imani kwake, sisi tunathubutu kumwendea Mungu kwa matumaini. Kwa hiyo, nawaombeni msife moyo kwa sababu ya mateso ninayopata kwa ajili yenu, maana hayo ni kwa ajili ya utukufu wenu.
Waefeso 3:8-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mimi, niliye mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nilipewa neema hii ya kuwahubiria Mataifa utajiri wake Kristo usiopimika; na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika Mungu aliyeviumba vitu vyote; ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho; kwa kadiri ya kusudi la milele alilolikusudia katika Kristo Yesu Bwana wetu. Katika yeye tunao ujasiri na uwezo wa kukaribia katika tumaini kwa njia ya kumwamini. Basi naomba msikate tamaa kwa sababu ya dhiki zangu kwa ajili yenu, zilizo utukufu wenu.
Waefeso 3:8-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mimi, niliye mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nalipewa neema hii ya kuwahubiri Mataifa utajiri wake Kristo usiopimika; na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika Mungu aliyeviumba vitu vyote; ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho; kwa kadiri ya kusudi la milele alilolikusudia katika Kristo Yesu Bwana wetu. Katika yeye tunao ujasiri na uwezo wa kukaribia katika tumaini kwa njia ya kumwamini. Basi naomba msikate tamaa kwa sababu ya dhiki zangu kwa ajili yenu, zilizo utukufu kwenu.
Waefeso 3:8-13 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Ingawa mimi ni mdogo kuliko aliye mdogo kabisa miongoni mwa watakatifu wote, nilipewa neema hii: ili niwahubirie watu wa Mataifa kuhusu utajiri usiopimika ulio ndani ya Al-Masihi, na kuweka wazi kwa kila mtu siri hii iliyokuwa imefichwa tangu zamani katika Mungu, aliyeumba vitu vyote. Ili sasa kupitia kwa jumuiya ya waumini, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ipate kujulikana kwa watawala na wenye mamlaka katika ulimwengu wa roho, sawasawa na kusudi lake la milele alilolitimiza katika Al-Masihi Isa Bwana wetu. Ndani yake na kupitia kwa imani katika yeye twaweza kumkaribia Mungu kwa uhuru na kwa ujasiri. Kwa hiyo, nawaomba msikate tamaa kwa sababu ya mateso yangu kwa ajili yenu, hayo ni utukufu wenu.