Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waefeso 1:1-14

Waefeso 1:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, nawaandikia nyinyi watu wa Mungu huko Efeso, mlio waaminifu katika kuungana na Kristo Yesu. Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Maana, katika kuungana na Kristo ametubariki kwa kutujalia zawadi zote za kiroho mbinguni. Kabla ya kuumbwa ulimwengu, Mungu alituteua tuwe wake katika kuungana na Kristo ili tuwe watakatifu na bila hitilafu mbele yake. Kwa sababu ya upendo wake, Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani kutuleta kwake kama watoto wake kwa njia ya Yesu Kristo. Ndivyo alivyopenda na kunuia. Basi, tumsifu Mungu kwa sababu ya neema yake tukufu ambayo ametujalia katika Mwanae mpenzi! Maana kwa damu yake Kristo sisi tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa. Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake aliyotukirimia bila kipimo! Kwa hekima na ujuzi wake wote Mungu alitekeleza kile alichonuia, akatujulisha mpango wake uliofichika, ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza kwa njia ya Kristo. Mpango huo ambao angeutimiza wakati utimiapo ni kukusanya pamoja viumbe vyote, kila kitu mbinguni na duniani, chini ya Kristo. Katika kuungana na Kristo, sisi tumerithishwa wokovu kama tulivyopangiwa kadiri ya azimio lake Mungu atekelezaye kila kitu kulingana na uamuzi na matakwa yake. Basi, sisi tuliotangulia kumtumainia Kristo tunapaswa kuusifu utukufu wa Mungu! Nanyi pia watu wa mataifa mengine, mliusikia ujumbe wa kweli yaani Habari Njema iliyowaletea wokovu, mkamwamini Kristo; naye Mungu, ili kuonesha kuwa nyinyi ni wake, akawapiga mhuri kwa kuwapeni yule Roho Mtakatifu aliyetuahidia. Huyu Roho ni dhamana ya kupata yote yale Mungu aliyowaahidia watu wake, na jambo hili latuhakikishia kwamba Mungu atawakomboa kabisa wote walio wake. Tuusifu utukufu wake!

Shirikisha
Soma Waefeso 1

Waefeso 1:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa watakatifu walioko [Efeso] wanaomwamini Kristo Yesu. Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo; kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, kulingana na radhi ya mapenzi yake. Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa. Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake. Naye alituzidishia hiyo katika hekima yote na ujuzi; akiisha kutujulisha siri ya mapenzi yake, kulingana na radhi yake aliyoikusudia katika yeye huyo. Yaani, kuleta madaraka ya wakati mkamilifu atavijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani pia. Naam, katika yeye huyo; na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake. Nasi katika huyo tupate kuwa sifa ya utukufu wake, sisi tuliotangulia kumwekea Kristo tumaini letu. Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, Habari Njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa mhuri na Roho yule wa ahadi aliye Mtakatifu. Ndiye aliye arabuni ya urithi wetu, ili kuleta ukombozi wa milki yake, kuwa sifa ya utukufu wake.

Shirikisha
Soma Waefeso 1

Waefeso 1:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa watakatifu walioko [Efeso] wanaomwamini Kristo Yesu. Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo; kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake. Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa. Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake. Naye alituzidishia hiyo katika hekima yote na ujuzi; akiisha kutujulisha siri ya mapenzi yake, sawasawa na uradhi wake, alioukusudia katika yeye huyo. Yaani, kuleta madaraka ya wakati mkamilifu atavijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani pia. Naam, katika yeye huyo; na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake. Nasi katika huyo tupate kuwa sifa ya utukufu wake, sisi tuliotangulia kumwekea Kristo tumaini letu. Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, habari njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi aliye Mtakatifu. Ndiye aliye arabuni ya urithi wetu, ili kuleta ukombozi wa milki yake, kuwa sifa ya utukufu wake.

Shirikisha
Soma Waefeso 1

Waefeso 1:1-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu: Kwa watakatifu walioko Efeso, walio waaminifu katika Kristo Yesu: Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi. Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki sisi kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo. Kwa maana alituchagua katika yeye kabla ya kuumbwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake. Kwa upendo alitangulia kutuchagua tuwe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo kwa furaha yake na mapenzi yake mwenyewe. Kwa hiyo tunamsifu Mungu kwa huruma zake kuu alizotumiminia sisi katika Mwanawe Mpendwa. Ndani yake tunao ukombozi kwa njia ya damu yake, yaani, msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake aliyotumiminia kwa wingi, kwa hekima yote na maarifa yote. Naye alitujulisha siri ya mapenzi yake sawasawa na uradhi wa mapenzi yake, ambayo alikusudia katika Kristo, ili yapate kutimizwa wakati mkamilifu utakapowadia, yaani, kuvitia vitu vyote vya mbinguni na vya duniani pamoja, chini ya kiongozi mmoja, ndiye Kristo. Katika Kristo sisi nasi tumepata urithi, tukisha kuchaguliwa sawasawa na kusudi la Mungu, yeye ambaye hufanya mambo yote kulingana na kusudi la mapenzi yake, ili kwamba, sisi tuliokuwa wa kwanza kuweka tumaini katika Kristo, tupate kuishi kwa sifa ya utukufu wake. Ninyi pia mliingia ndani ya Kristo mliposikia Neno la kweli, Injili ya wokovu wenu. Mkiisha kuamini, ndani yake mlitiwa muhuri, yaani, Roho Mtakatifu mliyeahidiwa, yeye ambaye ni amana yetu akituhakikishia urithi wetu hadi ukombozi wa wale walio milki ya Mungu kwa sifa ya utukufu wake.

Shirikisha
Soma Waefeso 1

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha