Kumbukumbu la Sheria 6:10-12
Kumbukumbu la Sheria 6:10-12 Biblia Habari Njema (BHN)
“Kama vile Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyowaapia babu zenu, Abrahamu, Isaka na Yakobo, yeye atawapeni nchi yenye miji mikubwa na mizuri iliyostawi ambayo nyinyi hamkuijenga. Nyumba zitakuwa zimejaa vitu vizuri ambavyo nyinyi hamkuviweka, kutakuwa na visima ambavyo hamkuvichimba na mashamba ya mizabibu na mizeituni ambayo hamkuyapanda. Mwenyezi-Mungu atakapowapeleka kwenye nchi hiyo ambako mtakuwa na chakula chote mnachohitaji, hakikisheni kwamba hamtamsahau Mwenyezi-Mungu aliyewatoa Misri ambako mlikuwa watumwa.
Kumbukumbu la Sheria 6:10-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha BWANA Mungu wako atakapokuleta katika nchi aliyowaapia babu zako, Abrahamu na Isaka na Yakobo, ya kuwa atakupa; miji mikubwa mizuri usiyoijenga wewe, na nyumba zimejaa vitu vyema vyote usizojaza wewe, na visima vilivyochimbwa usivyochimba wewe, mashamba ya mizabibu na mizeituni usiyoipanda wewe, nawe utakula na kushiba; ndipo ujitunze, usije ukamsahau BWANA aliyekutoa nchi ya Misri, nyumba ya utumwa.
Kumbukumbu la Sheria 6:10-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tena itakuwa atakapokwisha BWANA, Mungu wako, kukuleta katika nchi aliyowaapia babu zako, Ibrahimu na Isaka na Yakobo, ya kuwa atakupa; miji mikubwa mizuri usiyoijenga wewe, na nyumba zimejaa vitu vyema vyote usizojaza wewe, na visima vimefukuliwa usivyofukua wewe, mashamba ya mizabibu na mizeituni usiyoipanda wewe, nawe utakula na kushiba; ndipo ujitunze, usije ukamsahau BWANA aliyekutoa nchi ya Misri, nyumba ya utumwa.
Kumbukumbu la Sheria 6:10-12 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakapokuleta katika nchi aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, Isaka na Yakobo, kukupa wewe, nchi kubwa, yenye miji inayopendeza ambayo hukuijenga, nyumba zilizojaa vitu vizuri vya aina nyingi ambavyo hukuvijaza, visima ambavyo hukuchimba, na mashamba ya mizabibu na mizeituni ambayo hukupanda wewe, basi, utakapokula na kushiba, jihadhari usije ukamwacha Mwenyezi Mungu, aliyekutoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa.