Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu la Sheria 33:1-11

Kumbukumbu la Sheria 33:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Hii ndiyo baraka Mose mtu wa Mungu aliyotamka kwa Waisraeli kabla ya kifo chake. Alisema: “BWANA alikuja kutoka Mlima Sinai, akachomoza kama jua juu yao kutoka Mlima Seiri, akaangaza kutoka Mlima Parani. Alikuja pamoja na watakatifu makumi elfu kutoka kusini, kutoka materemko ya mlima wake. Hakika ni wewe ambaye huwapenda watu, watakatifu wako wote wamo mkononi mwako. Miguuni pako wote wanasujudu na kutoka kwako wanapokea mafundisho, sheria ile Mose aliyotupa sisi, tulio milki ya kusanyiko la Yakobo. Alikuwa mfalme juu ya Yeshuruni wakati viongozi wa watu walipokusanyika, pamoja na makabila ya Israeli. “Reubeni na aishi, asife, wala watu wake wasiwe wachache.” Akasema hili kuhusu Yuda: “Ee BWANA, sikia kilio cha Yuda, mlete kwa watu wake. Kwa mikono yake mwenyewe hujitetea. Naam, uwe msaada wake dhidi ya adui zake!” Kuhusu Lawi alisema: “Thumimu yako na Urimu yako ulimpa, mtu yule uliyemfadhili. Ulimjaribu huko Masa na kushindana naye kwenye maji ya Meriba. Alinena hivi kuhusu baba yake na mama yake, ‘Mimi siwahitaji kamwe.’ Akawasahau jamaa zake, asiwatambue hata watoto wake, lakini akaliangalia neno lako na kulilinda Agano lako. Humfundisha Yakobo mausia yako na Israeli sheria yako. Hufukiza uvumba mbele zako na sadaka nzima za kuteketezwa juu ya madhabahu yako. Ee BWANA, bariki ustadi wake wote, nawe upendezwe na kazi ya mikono yake. Vipige viuno vya wale wainukao dhidi yake; wapige adui zake hata wasiinuke tena.”

Kumbukumbu la Sheria 33:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

Hii ndiyo baraka ambayo Mose, mtu wa Mungu aliwatakia Waisraeli kabla ya kufariki kwake. Alisema: Mwenyezi-Mungu alikuja kutoka mlima Sinai, alitutokea kutoka mlima Seiri; aliiangaza kutoka mlima Parani. Alitokea kati ya maelfu ya malaika, na moto uwakao katika mkono wake wa kulia. Mwenyezi-Mungu aliwapenda watu wake; na huwalinda watakatifu wake wote. Hivyo, malaika wake walifuata nyayo zake, na kupata maagizo kutoka kwake. Mose alituamuru tutii sheria; kitu cha thamani kuu cha taifa letu. Mwenyezi-Mungu akawa mfalme wa Israeli, wakati viongozi wao walipokutana, na makabila yote yalipokusanyika. Mose alisema juu ya kabila la Reubeni: “Reubeni aishi wala asife, na watu wake wasiwe wachache.” Juu ya kabila la Yuda alisema: “Ee Mwenyezi-Mungu usikilize kilio cha kabila la Yuda; umrudishe tena kwa watu wale wengine. Upigane kwa mikono yako kwa ajili yake, ulisaidie kabila la Yuda dhidi ya adui zake.” Juu ya kabila la Lawi, alisema: “Ee Mwenyezi-Mungu ulipatie Lawi kauli yako ya Urimu, kauli yako ya thumimu kwa hao waaminifu wako, ambao uliwajaribu huko Masa. Ulishindana nao kwenye maji ya Meriba. Walawi walioamua kuwaacha wazee wao, wakawasahau jamaa zao, wasiwatambue hata watoto wao maana walizingatia amri zako, na kushika agano lako. Na wawafundishe wazawa wa Yakobo maagizo yako; wawafundishe watu wa Israeli sheria yako. Walawi na wafukize ubani mbele yako, sadaka nzima za kuteketezwa madhabahuni pako. Ee Mwenyezi-Mungu, uzibariki nguvu zao, uzikubali kazi za mikono yao; uzivunjilie mbali nguvu za maadui zao, nguvu za wanaowachukia hata wasiinuke tena.”

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha