Kumbukumbu la Sheria 12:1-7
Kumbukumbu la Sheria 12:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hizi ndizo amri na hukumu mtakazotunza kuzifanya katika nchi aliyokupa BWANA, Mungu wa baba zako, uimiliki, siku zote mtakazoishi juu ya nchi. Vunjeni kabisa mahali pote walipokuwa wakiitumikia miungu yao mataifa mtakayoyamiliki, juu ya milima mirefu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti wenye majani mabichi; nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo. Wala msimfanyie hivyo BWANA, Mungu wenu. Lakini mahali atakapochagua BWANA, Mungu wenu, katika kabila zenu zote, apaweke jina lake, maana, ni makao yake, elekezeni nyuso zenu hapo, nawe wende huko; pelekeni huko sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu, na sadaka zenu za hiari, na wazaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ng’ombe na ya kondoo; na huko mtakula mbele za BWANA, Mungu wenu, nanyi furahini katika yote mtakayotia mikono yenu, ninyi na wa nyumbani mwenu, aliyokubarikia BWANA, Mungu wako.
Kumbukumbu la Sheria 12:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
“Yafuatayo ni masharti na maagizo ambayo mtayatimiza katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, amewapa muimiliki, siku zote za maisha yenu nchini. Haribuni kabisa mahali pote ambapo watu wanaabudu miungu yao kwenye milima mirefu, vilima na chini ya miti yenye majani mabichi. Zivunjilieni mbali madhabahu zao na kuzibomoa kabisa nguzo zao. Ziteketezeni kwa moto sanamu zao za Ashera na kuzikatakata sanamu zao za kuchonga na kufutilia mbali jina lao na mahali hapo. “Wala msimwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, namna hiyo yao. Bali mtakwenda mahali ambapo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atachagua katika makabila yote ili kuliweka jina lake na makao yake hapo; huko ndiko mtakakokwenda. Huko mtapeleka tambiko zenu za kuteketezwa na sadaka zenu, zaka zenu za matoleo yenu, sadaka zenu za nadhiri, matoleo yenu ya hiari na wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe na kondoo wenu. Huko, mtakula mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na mtafurahi nyinyi pamoja na watu wa nyumbani mwenu kwa ajili ya mafanikio yenu aliyowabarikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.
Kumbukumbu la Sheria 12:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hizi ndizo amri na hukumu mtakazofuataa kuzifanya katika nchi aliyokupa BWANA, Mungu wa baba zako, uimiliki, siku zote mtakazoishi juu ya nchi. Vunjeni kabisa mahali pote walipokuwa wakiitumikia miungu yao mataifa mtakayoyamiliki, juu ya milima mirefu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti wenye majani mabichi; nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo. Wala msimfanyie hivyo BWANA, Mungu wenu. Lakini mahali atakapochagua BWANA, Mungu wenu, katika makabila yenu yote, apaweke jina lake, maana, ni makao yake, elekezeni nyuso zenu hapo, nawe uende huko; pelekeni huko sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu, na sadaka zenu za hiari, na wazaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ng'ombe na ya kondoo; na huko mtakula mbele za BWANA, Mungu wenu, nanyi furahini katika yote mtakayotia mikono yenu, ninyi na wa nyumbani mwenu, aliyokubarikia BWANA, Mungu wako.
Kumbukumbu la Sheria 12:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hizi ndizo amri na sheria ambazo ni lazima mwe waangalifu kuzifuata katika nchi ambayo BWANA, Mungu wa baba zenu, amewapa kumiliki, kwa muda wote mtakaoishi katika nchi. Haribuni kabisa kila mahali pao pa kuabudia kwenye milima mirefu, vilima na chini ya kila mti mkubwa ambamo mataifa haya mnayokwenda kuchukua ardhi yao huabudia miungu yao. Bomoeni madhabahu zao, vunjeni yale mawe wanayoabudu, chomeni moto nguzo zao za Ashera; katilieni mbali sanamu za miungu yao na mfute majina yao mahali hapo. Kamwe msimwabudu BWANA Mungu wenu kama wanavyoabudu wao. Bali mtatafuta mahali BWANA Mungu wenu atakapopachagua katika makabila yenu yote ili aliweke jina lake huko kuwa makao yake. Mahali hapo ndipo iwapasapo kwenda; hapo ndipo mtakapoleta sadaka zenu za kuteketezwa na dhabihu, zaka zenu na changizo zenu, kile ulichoweka nadhiri kutoa, sadaka zenu za hiari na malimbuko ya makundi yenu ya ngʼombe pamoja na mbuzi na kondoo. Hapo, katika uwepo wa BWANA Mungu wenu, ninyi pamoja na jamaa zenu, mtakula na kufurahia kila kitu ambacho mmegusa kwa mikono yenu, kwa sababu BWANA Mungu wenu amewabariki.