Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu la Sheria 11:8-32

Kumbukumbu la Sheria 11:8-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kwa hiyo yaangalieni maagizo yote niwaagizayo leo, mpate kuwa na nguvu, na kuingia mkaimiliki nchi mwivukiayo kuimiliki; nanyi mpate kuzifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi BWANA aliyowaapia baba zenu, ya kuwa atawapa wao na kizazi chao, nchi imiminikayo maziwa na asali Kwa kuwa nchi mwingiayo kuimiliki, si mfano wa nchi ya Misri mlikotoka, uliyokuwa ukipanda mbegu zako humo na kuinyunyizia maji kwa mguu wako, kama shamba la mboga; lakini nchi muivukayo kuimiliki ni nchi ya vilima na mabonde, nayo hunyunyizwa maji ya mvua ya mbinguni; nayo ni nchi itunzwayo na BWANA, Mungu wako; macho ya BWANA Mungu wako, ya juu yake, tangu mwanzo wa mwaka hadi mwisho wa mwaka. Tena itakuwa, mtakapoyazingatia kwa bidii maagizo yangu niwaagizayo leo, kwa kumpenda BWANA, Mungu wenu, na kumtumikia kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote, ndipo nitakapowapa mvua ya nchi yenu kwa wakati wake, mvua ya masika, na mvua ya vuli, upate kuvuna nafaka yako, na divai yako, na mafuta yako. Nami nitakupa nyasi katika mavue yako kulisha wanyama wako wa mifugo, nawe utakula na kushiba. Jitunzeni nafsi zenu, mioyo yenu isije ikadanganywa, mkageuka na kutumikia miungu mingine na kuiabudu; hasira za BWANA zikawaka juu yenu, naye akafunga mbingu kusiwe na mvua, wala nchi isitoe matunda yake; mkaangamia kwa upesi mtoke katika nchi nzuri awapayo BWANA. Kwa hiyo yawekeni maneno yangu mioyoni mwenu na rohoni mwenu; yafungeni yawe dalili juu ya mikono yenu, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yenu. Nayo wafunzeni watoto wenu kwa kuyazungumza uishipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako; ili siku zenu zifanywe nyingi, na za vijana vyenu nao, juu ya nchi BWANA aliyowaapia baba zenu kuwa atawapa, kama zilivyo siku za mbingu juu ya nchi. Kwa kuwa kama mtayazingatia kwa bidii maagizo haya yote niwaagizayo, kuyafanya; kumpenda BWANA, Mungu wenu, na kutembea katika njia zake zote, na kushikamana naye; ndipo BWANA atakapowafukuza mataifa haya yote mbele yenu, nanyi mtamiliki mataifa makubwa yenye nguvu kuliko ninyi. Kila mahali mtakapokanyaga kwa nyayo za miguu yenu patakuwa penu; tokea hilo jangwa, na Lebanoni, na tokea mto wa Frati, mpaka bahari ya magharibi, itakuwa ndiyo mipaka yenu. Hapatakuwa na mtu atakayeweza kusimama mbele yenu; BWANA, Mungu wenu, ataweka utisho wenu na kuhofiwa kwenu juu ya nchi yote mtakayoikanyaga, kama alivyowaambia. Angalieni, nawawekea mbele yenu hivi leo baraka na laana; baraka ni hapo mtakapoyafuata maagizo ya BWANA, Mungu wenu, niwaagizayo leo; na laana ni hapo msipotii maagizo ya BWANA, Mungu wenu, mkapotoka katika njia niwaagizayo leo, kwa kuandama miungu mingine msiyoijua. Tena itakuwa, atakapokuleta BWANA, Mungu wako, na kukutia katika nchi uendeayo kuimiliki, ndipo uiweke baraka juu ya mlima wa Gerizimu, na laana uiweke juu ya mlima wa Ebali. Je! Haiwi ng'ambo ya Yordani? Nyuma ya njia ya machweo ya jua, katika nchi ya Wakanaani waishio katika Araba kuelekea Gilgali, kando ya hiyo mialoni ya More? Kwani ninyi mtavuka Yordani mwingie kuimiliki nchi awapayo BWANA, Mungu wenu, nanyi muimiliki na kuketi humo. Nanyi angalieni mzifanye amri na hukumu zote niwawekeazo leo mbele yenu.

Kumbukumbu la Sheria 11:8-32 Biblia Habari Njema (BHN)

“Tiini amri zote ninazowaamuru siku hii ya leo, ili muweze kuingia na kuimiliki nchi mnayoiendea, mpate kuishi kwa muda mrefu katika nchi hiyo inayotiririka maziwa na asali; nchi ambayo Mwenyezi-Mungu aliahidi kuwapa babu zenu na wazawa wao. Kwa kuwa nchi mnayokwenda kuimiliki si kama nchi ya Misri mlikotoka, ambako mlipanda nafaka, mkamwagilia maji kwa miguu kama mashamba ya mboga. Lakini nchi mnayokwenda kuimiliki, ni nchi ya milima na mabonde, nchi ambayo hupata maji ya mvua kutoka mbinguni, nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, huitunza; Mwenyezi-Mungu huiangalia daima tangu mwanzo wa mwaka hadi mwisho wa mwaka. “Basi, mkizitii amri zangu ninazowapeni leo, mkampenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mkamtumikia kwa moyo wenu wote na kwa roho yenu yote, yeye ataipatia mvua nchi yenu wakati wake, mvua za masika na mvua za vuli, nanyi mtavuna nafaka yenu, divai yenu na mafuta yenu. Ataotesha majani mashambani kwa ajili ya ng'ombe wenu, nanyi mtakula na kushiba. Jihadharini, mioyo yenu isije ikadanganywa, mkageuka na kuitumikia miungu mingine na kuiabudu, nayo hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi yenu, akazifunga mbingu hata pasiwepo mvua na nchi ikaacha kutoa mazao yake, halafu mkaangamia upesi kutoka katika nchi nzuri ambayo Mwenyezi-Mungu anawapa. “Yawekeni maneno yangu haya mioyoni mwenu na rohoni mwenu. Yafungeni mikononi mwenu kama alama na kuyavaa katika paji la uso. Wafundisheni watoto wenu maneno haya mkiyazungumzia mketipo katika nyumba zenu, mnapotembea, mnapolala na mnapoamka. Ziandikeni katika vizingiti vya nyumba zenu, na katika malango yenu, ili nyinyi na watoto wenu mpate kuishi maisha marefu katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliapa kuwapa babu zenu, siku zote mbingu zitakapodumu juu ya dunia. “Mkijihadhari kutenda amri zote ambazo nimewapa: Kumpenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kuzifuata njia zake zote na kuambatana naye, basi Mwenyezi-Mungu atayafukuza mataifa yote hayo mbele yenu, nanyi mtamiliki nchi iliyo mali ya mataifa makubwa na yenye nguvu kuliko nyinyi. Kila mahali mtakapokanyaga kwa nyayo za miguu yenu patakuwa penu; nchi yenu itaenea kutoka jangwani, upande wa kusini, hadi milima ya Lebanoni upande wa kaskazini, na kutoka mto Eufrate upande wa mashariki, hadi bahari ya Mediteranea upande wa magharibi. Hakuna mtu yeyote atakayeweza kuwakabili. Popote mtakapokwenda katika nchi hiyo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawatia watu hofu wawaogope, kama alivyowaahidi. “Angalieni, leo hii nawawekea mbele yenu baraka na laana: Baraka, kama mtatii amri za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ambazo nawapeni hivi leo; na laana, kama hamtazitii amri za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kuiacha njia ninayowaamuru, mkaabudu miungu mingine ambayo hata hamjawahi kuijua. Mwenyezi-Mungu atakapowafikisha kwenye nchi mnayokwenda kuimiliki, mtatangaza baraka kutoka mlima Gerizimu, na laana kutoka mlima Ebali. (Milima hii iko ngambo ya mto Yordani, magharibi ya barabara kuelekea machweo ya jua, katika nchi ya Wakanaani waishio Araba mkabala wa Gilgali). Itawabidi kuvuka mto Yordani mwingie kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawapeni. Basi, mtakapoimiliki na kukaa humo, muwe waangalifu kutimiza masharti yote na maagizo ninayowapa leo.

Kumbukumbu la Sheria 11:8-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kwa hiyo yaangalieni maagizo yote niwaagizayo leo, mpate kuwa na nguvu, na kuingia mkaimiliki nchi mwivukiayo kuimiliki; nanyi mpate kuzifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi BWANA aliyowaapia baba zenu, ya kuwa atawapa wao na kizazi chao, nchi imiminikayo maziwa na asali Kwa kuwa nchi mwingiayo kuimiliki, si mfano wa nchi ya Misri mlikotoka, uliyokuwa ukipanda mbegu zako humo na kuinywesheleza kwa mguu wako, kama shamba la mboga; lakini nchi mwivukiayo kuimiliki ni nchi ya vilima na mabonde, nayo hunyweshwa maji ya mvua ya mbinguni; nayo ni nchi itunzwayo na BWANA, Mungu wako; macho ya BWANA Mungu wako, ya juu yake, tangu mwanzo wa mwaka hata mwisho wa mwaka. Tena itakuwa, mtakaposikiza kwa bidii maagizo yangu niwaagizayo leo, kwa kumpenda BWANA, Mungu wenu, na kumtumikia kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote, ndipo nitakapowapa mvua ya nchi yenu kwa wakati wake, mvua ya masika, na mvua ya vuli, upate kuvuna nafaka yako, na divai yako, na mafuta yako. Nami nitakupa nyasi katika mavue yako kulisha wanyama wako wa mifugo, nawe utakula na kushiba. Jitunzeni nafsi zenu, mioyo yenu isije ikadanganywa, mkageuka na kutumikia miungu mingine na kuiabudu; hasira za BWANA zikawaka juu yenu, naye akafunga mbingu kusiwe na mvua, wala nchi isitoe matunda yake; mkaangamia kwa upesi mtoke katika nchi nzuri awapayo BWANA. Kwa hiyo yawekeni maneno yangu mioyoni mwenu na rohoni mwenu; yafungeni yawe dalili juu ya mikono yenu, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yenu. Nayo wafunzeni vijana vyenu kwa kuyazungumza uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako; ili siku zenu zifanywe nyingi, na za vijana vyenu nao, juu ya nchi BWANA aliyowaapia baba zenu kuwa atawapa, kama zilivyo siku za mbingu juu ya nchi. Kwa kuwa kwamba mtayashika kwa bidii maagizo haya yote niwaagizayo, kuyafanya; kumpenda BWANA, Mungu wenu, na kutembea katika njia zake zote, na kushikamana naye; ndipo BWANA atakapowafukuza mataifa haya yote mbele yenu, nanyi mtamiliki mataifa makubwa yenye nguvu kuwapita ninyi. Kila mahali mtakapokanyaga kwa nyayo za miguu yenu patakuwa penu; tokea hilo jangwa, na Lebanoni, na tokea mto wa Frati, mpaka bahari ya magharibi, itakuwa ndiyo mipaka yenu. Hapatakuwa na mtu atakayeweza kusimama mbele yenu; BWANA, Mungu wenu, ataweka utisho wenu na kuhofiwa kwenu juu ya nchi yote mtakayoikanyaga, kama alivyowaambia. Angalieni, nawawekea mbele yenu hivi leo baraka na laana; baraka ni hapo mtakapoyasikiza maagizo ya BWANA, Mungu wenu, niwaagizayo leo; na laana ni hapo msiposikiza maagizo ya BWANA, Mungu wenu, mkikengeuka katika njia niwaagizayo leo, kwa kuandama miungu mingine msiyoijua. Tena itakuwa, atakapokuleta BWANA, Mungu wako, na kukutia katika nchi uendeayo kuimiliki, ndipo uiweke baraka juu ya mlima wa Gerizimu, na laana uiweke juu ya mlima wa Ebali. Je! Haiwi ng’ambo ya Yordani? Nyuma ya njia ya machweo ya jua, katika nchi ya Wakanaani waketio katika Araba kuelekea Gilgali, kando ya hiyo mialoni ya More? Kwani ninyi mtavuka Yordani mwingie kuimiliki nchi awapayo BWANA, Mungu wenu, nanyi muimiliki na kuketi humo. Nanyi angalieni mzifanye amri na hukumu zote niwawekeazo leo mbele yenu.

Kumbukumbu la Sheria 11:8-32 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kwa hiyo fuateni maagizo yote ninayowapa leo, ili mpate kuwa na nguvu za kuingia na kuiteka nchi ile ambayo mnavuka Yordani kuimiliki, ili mpate kuishi siku nyingi katika nchi ile ambayo BWANA aliapa kuwapa baba zenu na wazao wao, nchi itiririkayo maziwa na asali. Nchi mnayoiingia kuimiliki haifanani na nchi ya Misri mlikotoka ambako mlipanda mbegu yenu na kuinywesha, kama bustani ya mboga. Lakini nchi mnayovuka Yordani kuimiliki ni nchi ya milima na mabonde inywayo mvua kutoka mbinguni. Ni nchi ambayo BWANA Mungu wenu anaitunza; macho ya BWANA Mungu wenu yanaitazama daima kutoka mwanzo wa mwaka hadi mwisho wa mwaka. Hivyo kama mkiyatii maagizo yangu ninayowapa leo kwa uaminifu, yaani kwa kumpenda BWANA Mungu wenu, na kumtumikia kwa moyo wako wote na kwa roho yenu yote, ndipo atawanyweshea mvua katika nchi yenu kwa majira yake, mvua ya masika na ya vuli, ili mpate kuvuna nafaka zenu, divai mpya na mafuta. Nitawapa majani kwa ajili ya ngʼombe wenu, nanyi mtakula na kushiba. Jihadharini, la sivyo mtashawishika kugeuka na kuabudu miungu mingine na kuisujudia. Ndipo hasira ya BWANA itawaka dhidi yenu, naye atafunga mbingu ili mvua isinyeshe nayo ardhi haitatoa mazao, nanyi mtaangamia mara katika nchi nzuri ambayo BWANA anawapa. Yawekeni haya maneno yangu katika mioyo yenu na akili zenu, yafungeni kama alama juu ya mikono yenu na kwenye paji za nyuso zenu. Wafundisheni watoto wenu, yazungumzeni wakati mketipo nyumbani na wakati mtembeapo njiani, wakati mlalapo na wakati mwamkapo. Yaandikeni juu ya miimo ya nyumba zenu na juu ya malango yenu, ili kwamba siku zenu na siku za watoto wenu zipate kuwa nyingi katika nchi ile BWANA aliyoapa kuwapa baba zenu, kama zilivyo nyingi siku za mbingu juu ya nchi. Kama mkishika kwa makini maagizo haya yote ninayowapa kuyafuata, ya kumpenda BWANA Mungu wenu, kuenenda katika njia zake zote na kushikamana naye kwa uthabiti, ndipo BWANA atawafukuza mataifa haya yote mbele yako, nawe utawafukuza mataifa yaliyo makubwa na yenye nguvu kukuliko wewe. Kila mahali mtakapoweka mguu wenu patakuwa penu: Nchi yenu itaenea kutoka jangwa la Lebanoni, na kutoka mto wa Frati hadi bahari ya magharibi Hapatakuwa na mtu atakayeweza kusimama dhidi yenu. BWANA Mungu wenu, kama alivyoahidi, ataweka juu ya nchi yote utisho na hofu kwa ajili yenu popote mwendako. Tazama, leo ninaweka mbele yenu baraka na laana: baraka kama mtatii maagizo ya BWANA Mungu wenu, ambayo ninawapa leo; laana kama hamtatii maagizo ya BWANA Mungu wenu na kuacha njia ambayo ninawaamuru leo kwa kufuata miungu mingine, ambayo hamkuijua. Wakati BWANA Mungu wenu atakapokuwa amewaleta katika nchi mnayoiingia kuimiliki, mtatangaza baraka kutoka Mlima Gerizimu, na kutangaza laana kutoka Mlima Ebali. Kama mnavyofahamu, milima hii ipo ngʼambo ya Yordani, magharibi ya barabara, kuelekea machweo ya jua, karibu na miti mikubwa ya More, katika nchi ya wale Wakanaani wanaoishi Araba, jirani na Gilgali. Karibu mvuke ngʼambo ya Yordani kuingia na kuimiliki nchi ambayo BWANA Mungu wenu anawapa. Wakati mtakapokuwa mmeichukua na mnaishi humo, hakikisheni kwamba mnatii amri na sheria zote ninazoziweka mbele yenu leo.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha