Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 9:1-27

Danieli 9:1-27 Biblia Habari Njema (BHN)

“Katika mwaka Dario mwana wa Ahasuero, Mmedi, alipoanza kutawala juu ya milki ya Wakaldayo, mimi Danieli nilikuwa nikivisoma kwa makini vitabu vitakatifu, na humo nikaelewa maana ya jambo lile Mwenyezi-Mungu alilomfahamisha nabii Yeremia kuhusu ile miaka sabini, muda ambao utahusika na kuharibiwa kwa Yerusalemu. Nilimwomba Mwenyezi-Mungu, kwa moyo, nikimtolea dua pamoja na kufunga, nikavaa vazi la gunia na kuketi kwenye majivu. Nilimwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, na kuungama, nikisema: “Ee Bwana, wewe ni Mungu mkuu na wa kuogofya. Wewe ni mwaminifu kwa agano lako na unawafadhili wakupendao na kuzitii amri zako. Tumetenda dhambi, tumekosa, tumetenda maovu na kukuasi. Tumezikiuka amri zako na kanuni zako. Hatukuwasikiliza watumishi wako manabii, ambao kwa jina lako waliongea na wafalme wetu, wakuu wetu, wazee wetu na taifa letu lote. Kwako, ee Bwana, kuna uadilifu, lakini sisi daima tumejaa aibu. Jambo hili ni kweli kwetu sote tuishio Yudea, wakazi wa mji wa Yerusalemu na Waisraeli wote ambao umewatawanya katika nchi za mbali na za karibu kwa sababu ya kukosa uaminifu kwako. Aibu, ee Bwana, ni juu yetu, wafalme wetu, wakuu wetu na wazee wetu, kwa sababu tumekukosea. Wewe, Bwana Mungu wetu, una huruma na msamaha, ingawa sisi tumekuasi. Tulikataa kukusikiliza, ee Bwana, Mungu wetu; hatukuishi kulingana na sheria zako ulizotupa kwa njia ya watumishi wako manabii. Waisraeli wote wameiasi sheria yako, wamekuacha wakakataa kukutii. Kwa sababu tumekukosea, tumemwagiwa laana na viapo vilivyoandikwa katika sheria ya Mose, mtumishi wako. Umethibitisha yale uliyosema utatutenda sisi pamoja na watawala wetu kwa kuuadhibu mji wa Yerusalemu vikali zaidi ya mji mwingine wowote duniani. Umetuadhibu kama ilivyoandikwa katika sheria ya Mose, lakini mpaka sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, hatukuomba msamaha wako kwa kuziacha dhambi zetu na kutafakari uaminifu wako. Kwa hiyo, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ulikuwa tayari kutuadhibu, na ukafanya hivyo, kwa kuwa daima unafanya yaliyo ya haki, nasi hatukukusikiliza. “Na sasa ee Bwana, Mungu wetu, uliyewatoa watu wako nchini Misri kwa nguvu yako kuu na kulifanya jina lako litukuke mpaka sasa, tunasema kwamba tumetenda dhambi; tumefanya maovu. Ee Bwana, kwa kadiri ya matendo yako ya haki usiukasirikie wala kuughadhibikia mji wako wa Yerusalemu, mlima wako mtakatifu. Watu wote wa nchi za jirani wanaudharau mji wa Yerusalemu na watu wako, kwa sababu ya dhambi zetu na maovu waliyotenda wazee wetu. Kwa hiyo, ee Mungu, isikilize sala yangu na maombi yangu mimi mtumishi wako. Kwa hisani yako, uifadhili tena maskani yako iliyoharibiwa. Tega sikio, ee Mungu wangu; angalia uone taabu tulizo nazo na jinsi unavyotaabika huo mji uitwao kwa jina lako. Tunakutolea maombi yetu si kwa sababu tumetenda haki, bali kwa sababu wewe una huruma nyingi. Ee Mwenyezi-Mungu, utusikie; utusamehe ee Mwenyezi-Mungu. Ee Mwenyezi-Mungu, kwa hisani yako utusikie na kuchukua hatua, wala usikawie, ee Mungu wangu, kwa ajili ya mji huu na watu hawa wanaoitwa kwa jina lako! “Basi, nilipokuwa nikiomba, nikiungama dhambi zangu na dhambi za watu wangu wa Israeli, pamoja na kumsihi Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya mlima wake mtakatifu, yule mtu Gabrieli, ambaye nilikuwa nimemwona katika maono hapo awali, alishuka kwa haraka mpaka mahali nilipokuwa. Ilikuwa wakati wa kutoa sadaka ya jioni. Basi, akaniambia, ‘Danieli, nimekuja kukupa hekima na uwezo wa kufahamu. Ulipoanza kuomba, Mungu alitoa jibu, nami nimekuja kukueleza jibu hilo kwa kuwa unapendwa sana. Kwa hiyo, usikilize kwa makini jibu hilo na kuelewa maono hayo. “ ‘Muda wa miaka saba mara sabini umewekwa kwa ajili ya watu wako na juu ya mji wako mtakatifu ili kumaliza makosa, kukomesha dhambi, kusamehe uovu, kuleta haki ya milele, kutia mhuri maono na unabii na kupaka mafuta mahali patakatifu kabisa. Basi, ujue na kufahamu jambo hili: Tangu wakati itakapotolewa amri ya kujengwa upya mji wa Yerusalemu hadi kuja kwake aliyepakwa mafuta, yule aliye mkuu, ni muda wa majuma saba. Kwa muda wa majuma sitini na mawili, mji wa Yerusalemu utajengwa upya, wenye barabara kuu na mahandaki, lakini wakati huo utakuwa wa taabu. Baada ya majuma hayo sitini na mawili, yule aliyepakwa mafuta atakatiliwa mbali hatabaki na kitu. Mji na mahali patakatifu kabisa vitaharibiwa na jeshi la mtawala atakayekuja kushambulia. Mwisho wake utafika kama mafuriko, kukiwa na vita na maangamizi kama yalivyopangwa na Mungu. Mtawala huyo atafanya mapatano imara na watu wengi kwa muda wa miaka saba. Baada ya nusu ya muda huo atakomesha tambiko na sadaka. Mahali pa juu hekaluni patasimamishwa chukizo haribifu, nalo litabaki hapo mpaka yule aliyelisimamisha atakapoangamizwa kama ilivyopangwa na Mungu.’”

Shirikisha
Soma Danieli 9

Danieli 9:1-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Katika mwaka wa kwanza wa Dario, mwana wa Ahasuero, wa uzao wa Wamedi, aliyetawazwa kuwa mfalme juu ya milki ya Wakaldayo; katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danieli, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la BWANA lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini. Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu. Nikamwomba BWANA, Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake; tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako; wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na watu wote wa nchi. Ee Bwana, haki ina wewe, lakini kwetu sisi kuna haya ya uso, kama hivi leo; kwa watu wa Yuda, na kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa Israeli wote, walio karibu na hao walio mbali, katika nchi zote ulikowafukuza, kwa sababu ya makosa yao waliyokukosa. Ee Bwana, kwetu sisi kuna haya ya uso, kwa wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, kwa sababu tumekutenda dhambi. Rehema na msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi; wala hatukuitii sauti ya BWANA, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake, manabii. Naam, Israeli wote wameihalifu sheria yako, kwa kugeuka upande, wasiisikilize sauti yako; basi kwa hiyo laana imemwagwa juu yetu, na uapo ule ulioandikwa katika sheria ya Musa, mtumishi wa Mungu; kwa sababu tumemtenda dhambi. Naye ameyathibitisha maneno yake, aliyoyanena juu yetu, na juu ya waamuzi wetu waliotuamua, kwa kumletea mambo maovu makuu; maana chini ya mbingu zote halikutendeka jambo kama hili, lilivyotendeka juu ya Yerusalemu. Kama ilivyoandikwa katika sheria ya Musa, mabaya haya yote yametupata lakini hata hivyo hatukumwomba BWANA, Mungu wetu, atupe fadhili zake, ili tugeuke na kuyaacha maovu yetu, na kuitambua kweli yake. Basi BWANA ameyavizia mabaya hayo, akatuletea; maana BWANA, Mungu wetu ni mwenye haki katika kazi zake zote azitendazo; na sisi hatukuitii sauti yake. Na sasa, Ee Bwana Mungu wetu, uliyewatoa watu wako hawa katika nchi ya Misri kwa mkono hodari, ukajipatia sifa, kama ilivyo leo; tumefanya dhambi, tumetenda maovu. Ee Bwana sawasawa na haki yako yote, nakusihi, hasira yako na ghadhabu yako zigeuzwe na kuuacha mji wako Yerusalemu, mlima wako mtakatifu; maana kwa sababu ya dhambi zetu, na maovu ya baba zetu, Yerusalemu na watu wako wamepata kulaumiwa na watu wote wanaotuzunguka. Basi sasa, Ee Mungu wetu, yasikilize maombi ya mtumishi wako, na dua zake, ukaangazishe uso wako juu ya patakatifu pako palipo ukiwa, kwa ajili ya Bwana. Ee Mungu wangu, tega sikio lako, ukasikie; fumbua macho yako ukautazame ukiwa wetu, na mji ule ulioitwa kwa jina lako; maana hatukutolei maombi yetu kwa sababu ya haki yetu, lakini kwa sababu ya rehema zako nyingi. Ee Bwana, usikie; Ee Bwana, usamehe; Ee Bwana, usikilize, ukatende, usikawie; kwa ajili yako wewe, Ee Mungu wangu; kwa sababu mji wako na watu wako wanaitwa kwa jina lako. Basi hapo nilipokuwa nikisema, na kuomba, na kuiungama dhambi yangu, na dhambi ya watu wangu Israeli, na kuomba dua yangu mbele za BWANA, Mungu wangu, kwa ajili ya mlima mtakatifu wa Mungu wangu; naam, nilipokuwa nikinena katika kuomba, mtu yule, Gabrieli, niliyemwona katika njozi hapo kwanza, akirushwa upesi, alinigusa panapo wakati wa dhabihu ya jioni. Akaniagiza, akaongea nami, akasema, Ee Danieli, nimetokea sasa, ili nikupe akili upate kufahamu. Mwanzo wa maombi yako ilitolewa amri, nami nimekuja kukupasha habari; maana wewe unapendwa sana; basi itafakari habari hii, na kuyafahamu maono haya. Muda wa majuma sabini umeamriwa juu ya watu wako, na juu ya mji wako mtakatifu, ili kukomesha makosa, na kuishiliza dhambi, na kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu, na kuleta haki ya milele, na kutia muhuri maono na unabii, na kumtia mafuta yeye aliye mtakatifu. Basi ujue na kufahamu, ya kuwa tangu kuwekwa amri ya kutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu hata zamani zake masihi aliye mkuu; kutakuwa na majuma saba; na katika majuma sitini na mawili utajengwa tena pamoja na njia kuu zake na handaki, naam, katika nyakati za taabu. Na baada ya yale majuma sitini na mawili, masihi atakatiliwa mbali, naye atakuwa hana kitu; na watu wa mkuu atakayekuja watauangamiza mji, na patakatifu; na mwisho wake utakuwa pamoja na gharika, na hata mwisho ule vita vitakuwapo; ukiwa umekwisha kukusudiwa. Naye atafanya agano thabiti na watu wengi kwa muda wa juma moja; na kwa nusu ya juma hiyo ataikomesha sadaka na dhabihu; na mahali pake litasimama chukizo la uharibifu; na hivyo, hata ukomo, na ghadhabu iliyokusudiwa imemwagwa juu yake mwenye kuharibu.

Shirikisha
Soma Danieli 9

Danieli 9:1-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Katika mwaka wa kwanza wa Dario, mwana wa Ahasuero, wa uzao wa Wamedi, aliyetawazwa kuwa mfalme juu ya milki ya Wakaldayo; katika mwaka wa kwanza wa kutawala kwake, mimi Danieli, kwa kuvisoma vitabu, nilifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la BWANA lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini. Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kusihi kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu. Nikamwomba BWANA, Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake; tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako; wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na watu wote wa nchi. Ee Bwana, haki ina wewe, lakini kwetu sisi kuna aibu, kama hivi leo; kwa watu wa Yuda, na kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa Israeli wote, walio karibu na hao walio mbali, katika nchi zote ulikowafukuza, kwa sababu ya makosa yao waliyokukosa. Ee Bwana, kwetu sisi kuna aibu, kwa wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, kwa sababu tumekutenda dhambi. Rehema na msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi; wala hatukuitii sauti ya BWANA, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake, manabii. Naam, Israeli wote wameivunja sheria yako, kwa kugeuka upande, wasiisikilize sauti yako; basi kwa hiyo laana imemwagwa juu yetu, na kiapo kile kilioandikwa katika Sheria ya Musa, mtumishi wa Mungu; kwa sababu tumemtenda dhambi. Naye ameyathibitisha maneno yake, aliyoyanena juu yetu, na juu ya waamuzi wetu waliotuamua, kwa kumletea mambo maovu makuu; maana chini ya mbingu zote halikutendeka jambo kama hili, lilivyotendeka juu ya Yerusalemu. Kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Musa, mabaya haya yote yametupata lakini hata hivyo hatukumwomba BWANA, Mungu wetu, atupe fadhili zake, ili tugeuke na kuyaacha maovu yetu, na kuitambua kweli yake. Basi BWANA anayachungulia mabaya hayo, akatuletea; maana BWANA, Mungu wetu ni mwenye haki katika kazi zake zote azitendazo; na sisi hatukuitii sauti yake. Na sasa, Ee Bwana Mungu wetu, uliyewatoa watu wako hawa katika nchi ya Misri kwa mkono hodari, ukajipatia sifa, kama ilivyo leo; tumefanya dhambi, tumetenda maovu. Ee Bwana sawasawa na haki yako yote, nakusihi, hasira yako na ghadhabu yako zigeuzwe na kuuacha mji wako Yerusalemu, mlima wako mtakatifu; maana kwa sababu ya dhambi zetu, na maovu ya baba zetu, Yerusalemu na watu wako wamepata kulaumiwa na watu wote wanaotuzunguka. Basi sasa, Ee Mungu wetu, yasikilize maombi ya mtumishi wako, na dua zake, ukaangazishe uso wako juu ya patakatifu pako palipo ukiwa, kwa ajili ya Bwana. Ee Mungu wangu, tega sikio lako, ukasikie; fumbua macho yako ukautazame ukiwa wetu, na mji ule ulioitwa kwa jina lako; maana hatukutolei maombi yetu kwa sababu ya haki yetu, lakini kwa sababu ya rehema zako nyingi. Ee Bwana, usikie; Ee Bwana, usamehe; Ee Bwana, usikilize, ukatende, usikawie; kwa ajili yako wewe, Ee Mungu wangu; kwa sababu mji wako na watu wako wanaitwa kwa jina lako. Basi hapo nilipokuwa nikisema, na kuomba, na kuiungama dhambi yangu, na dhambi ya watu wangu Israeli, na kuomba dua yangu mbele za BWANA, Mungu wangu, kwa ajili ya mlima mtakatifu wa Mungu wangu; naam, nilipokuwa nikinena katika kuomba, mtu yule, Gabrieli, niliyemwona katika njozi hapo kwanza, akirushwa upesi, alinigusa panapo wakati wa dhabihu ya jioni. Akaniagiza, akaongea nami, akasema, Ee Danieli, nimetokea sasa, ili nikupe akili upate kufahamu. Mwanzo wa maombi yako ilitolewa amri, nami nimekuja kukupasha habari; maana wewe unapendwa sana; basi itafakari habari hii, na kuyafahamu maono haya. Muda wa majuma sabini umeamriwa juu ya watu wako, na juu ya mji wako mtakatifu, ili kukomesha makosa, na kumaliza dhambi, na kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu, na kuleta haki ya milele, na kutia mhuri maono na unabii, na kumtia mafuta yeye aliye mtakatifu. Basi ujue na kufahamu, ya kuwa tangu kuwekwa amri ya kutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu hata zamani zake masihi aliye mkuu; kutakuwa na majuma saba; na katika majuma sitini na mawili utajengwa tena pamoja na njia kuu zake na handaki, naam, katika nyakati za taabu. Na baada ya yale majuma sitini na mawili, masihi atakatiliwa mbali, naye atakuwa hana kitu; na watu wa mkuu atakayekuja watauangamiza mji, na patakatifu; na mwisho wake utakuwa pamoja na gharika, na hata mwisho ule vita vitakuwapo; ukiwa umekwisha kukusudiwa. Naye atafanya agano thabiti na watu wengi kwa muda wa juma moja; na kwa nusu ya juma hiyo ataikomesha sadaka na dhabihu; na mahali pake litasimama chukizo la uharibifu; na hivyo, hata ukomo, na ghadhabu iliyokusudiwa imemwagwa juu yake mwenye kuharibu.

Shirikisha
Soma Danieli 9

Danieli 9:1-27 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Dario mwana wa Ahasuero (mzaliwa wa Umedi), ambaye alifanywa mtawala juu ya ufalme wa Babeli, katika mwaka wa kwanza wa utawala wake, mimi Danieli nilielewa kutokana na Maandiko, kulingana na neno la BWANA alilopewa nabii Yeremia, kwamba ukiwa wa Yerusalemu ungetimizwa kwa miaka sabini. Kwa hiyo nikamgeukia BWANA Mungu na kumsihi katika maombi na dua, katika kufunga, na kuvaa nguo ya gunia na kujipaka majivu. Nikamwomba BWANA Mungu wangu na kutubu: “Ee Bwana, Mungu mkuu na unayetisha, anayeshika agano lake la upendo kwao wanaompenda na kutii maagizo yake, tumetenda dhambi na kufanya mabaya. Tumekuwa waovu na tumeasi; tumegeuka mbali na maagizo yako na sheria zako. Hatukuwasikiliza watumishi wako manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, wakuu wetu, baba zetu, na watu wote wa nchi. “Bwana, wewe ni mwenye haki, lakini siku hii ya leo tumefunikwa na aibu: tukiwa wanaume wa Yuda, na watu wa Yerusalemu, na Israeli yote, wote walio karibu na walio mbali, katika nchi zote ulikotutawanya kwa sababu ya kukosa uaminifu kwako. Ee BWANA, sisi na wafalme wetu, wakuu wetu na baba zetu tumefunikwa na aibu kwa sababu tumefanya dhambi dhidi yako. BWANA Mungu wetu ni mwenye rehema na anayesamehe, hata ingawa tumefanya uasi dhidi yake. Hatukumtii BWANA Mungu wetu wala kuzishika sheria alizotupa kupitia kwa watumishi wake manabii. Israeli yote imekosea sheria yako na kugeuka mbali, nao wamekataa kukutii. “Kwa hiyo laana na viapo vya hukumu vilivyoandikwa katika Sheria ya Mose, mtumishi wa Mungu, vimemiminwa juu yetu, kwa sababu tumefanya dhambi dhidi yako. Umetimiza maneno uliyosema dhidi yetu na dhidi ya watawala wetu, kwa kuleta maafa makubwa juu yetu. Chini ya mbingu yote kamwe hapajatendeka kitu kama kile kilichotendeka kwa Yerusalemu. Kama vile ilivyoandikwa katika sheria ya Mose, misiba hii yote imekuja juu yetu, lakini hatujaomba fadhili kwa BWANA Mungu wetu kwa kugeuka kutoka dhambi zetu na kuwa wasikivu katika kweli yake. BWANA hakusita kuleta maafa juu yetu, kwa maana BWANA Mungu wetu ni mwenye haki katika kila afanyalo; lakini hata hivyo hatujamtii. “Sasa, Ee Bwana Mungu wetu, ambaye uliwatoa watu wako Misri kwa mkono wenye nguvu, na ambaye umejifanyia Jina linalodumu mpaka leo, tumetenda dhambi, tumefanya mabaya. Ee Bwana, wewe kwa kadiri ya matendo yako ya haki, ondoa hasira yako na ghadhabu yako juu ya Yerusalemu, mji wako, mlima wako mtakatifu. Dhambi zetu na maovu ya baba zetu yameifanya Yerusalemu na watu wako kitu cha kudharauliwa kwa wale wote wanaotuzunguka. “Basi Mungu wetu, sasa sikia maombi na dua ya mtumishi wako. Ee Bwana, kwa ajili yako angalia kwa huruma ukiwa wa mahali pako patakatifu. Ee Mungu, tega sikio na ukasikie; fumbua macho yako ukaone ukiwa wa mji ule wenye Jina lako. Hatukutolei maombi yetu kwa sababu sisi tuna haki, bali kwa sababu ya rehema zako nyingi. Ee Bwana, sikiliza! Ee Bwana, samehe! Ee Bwana, sikia na ukatende! Kwa ajili yako, Ee Mungu wangu, usikawie, kwa sababu mji wako na watu wako wanaitwa kwa Jina lako.” Basi, nilipokuwa bado nikinena na kuomba, nikiungama dhambi yangu na dhambi ya watu wangu Israeli, na nikifanya maombi yangu kwa BWANA Mungu wangu kwa ajili ya mlima wake mtakatifu, wakati nilipokuwa bado katika maombi, Gabrieli, yule mtu niliyekuwa nimemwona katika maono hapo awali, alinijia kwa kasi karibu wakati wa kutoa dhabihu ya jioni. Akanielimisha na kuniambia, “Danieli, sasa nimekuja kukupa akili na ufahamu. Mara ulipoanza kuomba, jibu lilitolewa, ambalo nimekuja kukupasha habari, kwa maana wewe unapendwa sana. Kwa hiyo, tafakari ujumbe huu na uelewe maono haya: “Majuma sabini yameamriwa kwa ajili ya watu wako na kwa ajili ya mji wako mtakatifu, ili kumaliza makosa, kukomesha dhambi, kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu, kuleta haki ya milele, kutia muhuri maono na unabii, na pia kumtia mafuta yeye aliye mtakatifu sana. “Ujue na kuelewa hili: Tangu kutolewa kwa amri ya kuutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu mpaka kuja kwa Mpakwa mafuta, aliye mtawala, kutakuwako majuma saba na majuma sitini na mawili. Barabara zitajengwa tena pamoja na mahandaki, lakini katika wakati wa taabu. Baada ya majuma sitini na mawili, Mpakwa Mafuta atakatiliwa mbali, wala hatabaki na kitu. Watu wa mtawala atakayekuja watauharibu mji pamoja na mahali patakatifu. Mwisho utakuja kama mafuriko: Vita vitaendelea mpaka mwisho, nao ukiwa umeamriwa. Mtawala huyo atathibitisha agano na watu wengi kwa juma moja. Katikati ya juma hilo atakomesha dhabihu na sadaka. Mahali pa dhabihu katika Hekalu atasimamisha chukizo la uharibifu, hadi mwisho ulioamriwa utakapomiminwa juu yake yeye aletaye uharibifu.”

Shirikisha
Soma Danieli 9

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha