Danieli 7:19-24
Danieli 7:19-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha nalitaka kujua maana ya yule mnyama wa nne, aliyekuwa mbali na wenziwe wote, mwenye kutisha sana, ambaye meno yake yalikuwa ya chuma, na makucha yake ya shaba; aliyekula, na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake; na habari za zile pembe kumi zilizokuwa kichwani mwake, na ile pembe nyingine iliyozuka, ambayo mbele yake zilianguka pembe tatu; yaani, pembe ile yenye macho, na kanwa lililonena makuu, ambayo kuonekana kwake kulikuwa hodari kuliko wenzake. Nikatazama, na pembe iyo hiyo ilifanya vita na watakatifu, ikawashinda; hata akaja huyo mzee wa siku, nao watakatifu wake Aliye juu wakapewa hukumu; na majira yakawadia watakatifu waumiliki ufalme. Akanena hivi, Huyo mnyama wa nne atakuwa ni ufalme wa nne juu ya dunia, utakaokuwa mbali na falme zile zote, nao utakula dunia yote, na kuikanyaga, na kuivunja vipande vipande. Na habari za zile pembe kumi, katika ufalme huo wataondoka wafalme kumi; na mwingine ataondoka baada ya hao; naye atakuwa mbali na hao wa kwanza; naye atawashusha wafalme watatu.
Danieli 7:19-24 Biblia Habari Njema (BHN)
“Kisha nikataka nielezwe juu ya yule mnyama wa nne, ambaye alikuwa tofauti kabisa na wale wengine, wa ajabu na wa kutisha sana, ambaye meno yake yalikuwa ya chuma na makucha yake ya shaba. Aliyatumia meno hayo kula na kuvunjavunja, na mabaki aliyakanyagakanyaga kwa nyayo zake. Aidha nilitaka nielezwe juu ya zile pembe kumi alizokuwa nazo kichwani mwake, na ule upembe mmoja ambao kabla haujaota, zilingoka pembe tatu; upembe uliokuwa na macho na kinywa ambacho kilitamka maneno ya kujigamba, na ambao ulionekana kuwa mkubwa kuliko pembe nyingine. “Nikiwa bado naangalia, pembe hiyo ilipigana vita na watakatifu, nayo ikawashinda. Lakini yule ‘Mzee wa kale na kale’ akainuka, akawapa haki watakatifu wa Mungu na wakati ulipotimia, hao watakatifu wakapewa ufalme. “Nikaelezwa hivi: ‘Yule mnyama wa nne ni ufalme wa nne utakaokuwako duniani. Ufalme huo utakuwa tofauti na falme nyingine, nao utaiangamiza dunia nzima. Utaibwaga chini na kuipasua vipandevipande. Zile pembe kumi ni wafalme kumi watakaotokana na ufalme huo. Halafu watafuatwa na mfalme mwingine ambaye atakuwa tofauti na wale waliomtangulia, na atawaangusha wafalme watatu.
Danieli 7:19-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha nilitaka kujua maana ya yule mnyama wa nne, aliyekuwa mbali na wenziwe wote, mwenye kutisha sana, ambaye meno yake yalikuwa ya chuma, na makucha yake ya shaba; aliyekula, na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake; na habari za zile pembe kumi zilizokuwa kichwani mwake, na ile pembe nyingine iliyozuka, ambayo mbele yake zilianguka pembe tatu; yaani, pembe ile yenye macho, na kinywa kilichonena makuu, ambayo kuonekana kwake kulikuwa hodari kuliko wenzake. Nikatazama, na pembe iyo hiyo ilifanya vita na watakatifu, ikawashinda; hata akaja huyo mzee wa siku, nao watakatifu wake Aliye Juu wakapewa hukumu; na majira yakawadia watakatifu waumiliki ufalme. Akanena hivi, Huyo mnyama wa nne atakuwa ni ufalme wa nne juu ya dunia, utakaokuwa mbali na falme zile zote, nao utaangamiza dunia yote, na kuikanyaga, na kuivunja vipande vipande. Na habari za zile pembe kumi, katika ufalme huo wataondoka wafalme kumi; na mwingine ataondoka baada ya hao; naye atakuwa mbali na hao wa kwanza; naye atawashusha wafalme watatu.
Danieli 7:19-24 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Kisha nilitaka kufahamu maana ya kweli ya mnyama yule wa nne, ambaye alikuwa tofauti na wale wengine wote, tena wa kutisha sana, na meno yake ya chuma na makucha ya shaba: mnyama ambaye alipondaponda na kuangamiza wahanga wake, na kukanyaga chochote kilichosalia. Pia mimi nilitaka kujua kuhusu zile pembe kumi juu ya kichwa chake, na pia kuhusu ile pembe nyingine iliyojitokeza, ambayo mbele yake zile tatu za mwanzoni zilianguka, ile pembe ambayo ilionekana kuvutia macho zaidi kuliko zile nyingine, na ambayo ilikuwa na macho na kinywa kilichonena kwa majivuno. Nilipoendelea kutazama, pembe hii ilikuwa inapigana vita dhidi ya watakatifu na kuwashinda, mpaka huyo Mzee wa Siku alipokuja na kutamka hukumu kwa kuwapa ushindi watakatifu wa Yeye Aliye Juu Sana, na wakati ukawadia walipoumiliki ufalme. “Alinipa maelezo haya: ‘Mnyama wa nne ni ufalme wa nne ambao utatokea duniani. Utakuwa tofauti na falme nyingine zote, nao utaharibu dunia nzima, ukiikanyaga chini na kuipondaponda. Zile pembe kumi ni wafalme kumi watakaotokana na ufalme huu. Baada yao mfalme mwingine atainuka, ambaye atakuwa tofauti na wale waliotangulia, naye atawaangusha wafalme watatu.