Danieli 10:9-14
Danieli 10:9-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Nilipoisikia sauti yake, nilianguka chini kifudifudi, nikashikwa na usingizi mzito. Hapo, mkono ukanigusa, ukanisimamisha, na kuimarisha miguu na mikono yangu. Akaniambia, ‘Danieli, wewe unayependwa sana, simama wima usikilize kwa makini maneno nitakayosema, maana nimetumwa kwako.’ Alipokuwa akiniambia maneno haya, mimi nilisimama nikitetemeka. Ndipo yeye akaniambia, ‘Danieli, usiogope. Mungu alilisikia ombi lako tangu siku ile ya kwanza ulipoamua kujinyenyekesha mbele yake ili upate ufahamu. Mimi nimekuja kwa ajili ya ombi lako hilo. Mkuu wa ufalme wa Persia alinipinga kwa muda wa siku ishirini na moja. Lakini Mikaeli, mmoja wa wakuu, akaja kunisaidia, kwa hiyo nikamwacha huko pamoja na mkuu wa ufalme wa Persia, nami nimekuja kukusaidia uyafahamu mambo yatakayowapata watu wako wakati ujao, kwani maono uliyoona yanahusu wakati ujao.’
Danieli 10:9-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini niliisikia sauti ya maneno yake; nami niliposikia sauti ya maneno yake, ndipo nikashikwa na usingizi mzito, na uso wangu umeielekea nchi. Na tazama, mkono ukanigusa, ukaniweka juu ya magoti yangu, na viganja vya mikono yangu. Akaniambia, Ee Danieli, mtu upendwaye sana, yafahamu maneno nikuambiayo, ukasimame wima; maana nimetumwa kwako sasa. Na aliponiambia neno hili, nilisimama nikitetemeka. Ndipo akaniambia, Usiogope, Danieli; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako. Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi. Sasa nimekuja kukufahamisha mambo yatakayowapata watu wako katika siku za mwisho; maana maono hayo ni ya siku nyingi bado.
Danieli 10:9-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha nikamsikia akisema, nami nilipokuwa nikimsikiliza, nikalala kifudifudi, nikapatwa na usingizi mzito. Mkono ulinigusa, ukaninyanyua, na kuniweka nikipiga magoti na mikono yangu ikashika chini, huku nikiwa bado ninatetemeka. Akasema, “Danieli, wewe mtu upendwaye sana, fikiri kwa makini maneno ninayokwenda kunena nawe sasa; simama wima, kwa maana sasa nimetumwa kwako.” Naye aliponiambia haya, nikasimama nikitetemeka. Ndipo akaendelea kusema, “Danieli, usiogope. Tangu siku ya kwanza ulipotia moyo wako ili kupata ufahamu na kujinyenyekeza mbele ya Mungu wako, maneno yako yalisikiwa, nami nimekuja ili kujibu maneno yako. Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga kwa siku ishirini na moja. Ndipo Mikaeli, mmoja wa malaika wakuu, alikuja kunisaidia, kwa sababu nilikuwa nimezuiliwa huko na mfalme wa Uajemi. Sasa nimekuja kukuelezea mambo yatakayowatokea watu wako wakati ujao, kwa maana maono hayo yanahusu wakati ambao haujaja bado.”
Danieli 10:9-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Walakini naliisikia sauti ya maneno yake; nami niliposikia sauti ya maneno yake, ndipo nikashikwa na usingizi mzito, na uso wangu umeielekea nchi. Na tazama, mkono ukanigusa, ukaniweka juu ya magoti yangu, na vitanga vya mikono yangu. Akaniambia, Ee Danieli, mtu upendwaye sana, yafahamu maneno nikuambiayo, ukasimame kiwima-wima; maana kwako nimetumwa sasa. Na aliponiambia neno hili, nalisimama nikitetemeka. Ndipo akaniambia, Usiogope, Danieli; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako. Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi. Sasa nimekuja kukufahamisha mambo yatakayowapata watu wako katika siku za mwisho; maana maono hayo ni ya siku nyingi bado.