Danieli 1:17-21
Danieli 1:17-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Mungu aliwajalia vijana hao wanne maarifa na ujuzi katika elimu na hekima. Zaidi ya hayo, alimjalia Danieli kipawa cha kufasiri maono na ndoto. Muda ulipotimia ambapo hao vijana wangepelekwa kwa mfalme kama alivyokuwa ameagiza, yule towashi mkuu akawapeleka vijana wote mbele ya Nebukadneza. Mfalme alipozungumza nao wote, hakuna walioonekana kuwa bora kama Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria. Basi, wakakubaliwa kumhudumia mfalme. Jambo lolote la hekima au maarifa ambalo mfalme aliwauliza alijionea mwenyewe kwamba vijana hao wanne walikuwa bora mara kumi kuliko waaguzi na wachawi wote katika utawala wake. Danieli alidumu katika huduma ya ikulu mpaka mwaka wa kwanza wa mfalme Koreshi.
Danieli 1:17-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi, kwa habari za hao vijana wanne, Mungu aliwapa maarifa na ujuzi katika elimu na hekima; Danieli naye alikuwa na ufahamu katika maono yote, na ndoto. Hata mwisho wa siku zile alizoziagiza mfalme za kuwaingiza, mkuu wa matowashi akawaingiza mbele ya mfalme Nebukadneza. Naye mfalme akazungumza nao; na miongoni mwao wote hawakuonekana waliokuwa kama Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria; kwa hiyo wakasimama mbele ya mfalme. Na katika kila jambo la hekima na ufahamu alilowauliza mfalme, akawaona kuwa walifaa mara kumi zaidi ya waganga na wachawi waliokuwa katika ufalme wake. Tena, Danieli huyo akadumu huko hata mwaka wa kwanza wa mfalme Koreshi.
Danieli 1:17-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi, kwa habari za hao vijana wanne, Mungu aliwapa maarifa na ujuzi katika elimu na hekima; Danieli naye alikuwa na ufahamu katika maono yote, na ndoto. Hata mwisho wa siku zile alizoziagiza mfalme za kuwaingiza, mkuu wa matowashi akawaingiza mbele ya mfalme Nebukadreza. Naye mfalme akazungumza nao; na miongoni mwao wote hawakuonekana waliokuwa kama Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria; kwa hiyo wakasimama mbele ya mfalme. Na katika kila jambo la hekima na ufahamu alilowauliza mfalme, akawaona kuwa walifaa mara kumi zaidi ya waganga na wachawi waliokuwa katika ufalme wake. Tena, Danieli huyo akadumu huko hata mwaka wa kwanza wa mfalme Koreshi.
Danieli 1:17-21 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Mungu akawapa hawa vijana wanne maarifa na ufahamu wa kila aina ya maandiko na elimu. Naye Danieli aliweza kufahamu maono na aina zote za ndoto. Mwisho wa muda uliowekwa na mfalme ili kuwaingiza kwake, mkuu wa maafisa akawaleta mbele ya Mfalme Nebukadneza. Mfalme akazungumza nao, akaona hakuna aliyelingana na Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria. Hivyo wakaingia katika utumishi wa mfalme. Katika kila jambo la hekima na ufahamu kuhusu kile mfalme alichowauliza, aliwapata kuwa bora mara kumi zaidi ya waganga na wasihiri wote katika ufalme wake wote. Naye Danieli akabaki huko hadi mwaka wa kwanza wa utawala wa Mfalme Koreshi.