Danieli 1:1-5
Danieli 1:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Mnamo mwaka wa tatu wa utawala wa mfalme Yehoyakimu wa Yuda, mfalme Nebukadneza wa Babuloni alikwenda Yerusalemu, akauzingira mji. Bwana akamwacha Yehoyakimu atiwe mikononi mwa mfalme Nebukadneza pamoja na baadhi ya vyombo vya nyumba ya Mungu. Basi mfalme Nebukadneza akachukua mateka na vyombo akavipeleka nchini Shinari, akaviweka katika hazina ya miungu yake. Mfalme Nebukadneza akamwamuru Ashpenazi, towashi wake mkuu, amchagulie baadhi ya vijana wa Israeli wa jamaa ya kifalme na ya watu mashuhuri. Mfalme alitaka vijana wasio na kasoro, wazuri kwa umbo, wenye uzoefu wa kila hekima, wenye akili na maarifa na wanaofaa kutoa huduma katika ikulu. Alitaka pia vijana hao wafundishwe kusoma na kuandika lugha ya Wakaldayo. Mfalme aliagiza vijana hao wapewe chakula bora ambacho yeye mwenyewe alikula na divai ambayo alikunywa. Vijana hao walitakiwa wapewe mafunzo kwa miaka mitatu, kisha wapelekwe kwa mfalme.
Danieli 1:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Katika mwaka wa tatu wa kumiliki kwake Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, Nebukadneza, mfalme wa Babeli, alikwenda Yerusalemu akauhusuru. Bwana akamtia Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, katika mkono wake, pamoja na baadhi ya vyombo vya nyumba ya Mungu; naye akavichukua mpaka nchi ya Shinari, mpaka nyumba ya mungu wake; akaviingiza vile vyombo katika nyumba ya hazina ya mungu wake. Mfalme akamwambia Ashpenazi, mkuu wa matowashi wake, awalete baadhi ya wana wa Israeli, wa uzao wa kifalme, na wa uzao wa watu mashuhuri; vijana wasio na kasoro, wazuri wa uso, wajuzi wa hekima, werevu kwa sababu ya maarifa yao, wenye kufahamu elimu, watakaoweza kusimama katika jumba la mfalme; tena alimwambia awafundishe kusoma na kuandika, lugha ya Wakaldayo. Huyo mfalme akawaagizia wapewe chakula kama cha mfalme, na divai aliyokunywa, akaagiza walishwe hivyo muda wa miaka mitatu; ili kwamba hatimaye wasimame mbele ya mfalme.
Danieli 1:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Katika mwaka wa tatu wa kumiliki kwake Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, Nebukadreza, mfalme wa Babeli, alikwenda Yerusalemu akauhusuru. Bwana akamtia Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, katika mkono wake, pamoja na baadhi ya vyombo vya nyumba ya Mungu; naye akavichukua mpaka nchi ya Shinari, mpaka nyumba ya mungu wake; akaviingiza vile vyombo katika nyumba ya hazina ya mungu wake. Mfalme akamwambia Ashpenazi, mkuu wa matowashi wake, awalete baadhi ya wana wa Israeli, wa uzao wa kifalme, na wa uzao wa kiungwana; vijana wasio na mawaa, wazuri wa uso, wajuzi wa hekima, werevu kwa sababu ya maarifa yao, wenye kufahamu elimu, watakaoweza kusimama katika jumba la mfalme; tena alimwambia awafundishe elimu ya Wakaldayo, na lugha yao. Huyo mfalme akawaagizia posho ya chakula cha mfalme, na ya divai aliyokunywa, akaagiza walishwe hivyo muda wa miaka mitatu; ili kwamba hatimaye wasimame mbele ya mfalme.
Danieli 1:1-5 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, Nebukadneza mfalme wa Babeli alikuja akazingira Yerusalemu kwa jeshi. Bwana akamtia Yehoyakimu mfalme wa Yuda mkononi mwa Nebukadneza, pamoja na baadhi ya vyombo kutoka Hekalu la Mungu. Hivi akavichukua hadi kwenye hekalu la mungu wake huko Shinari, naye akaviweka nyumbani ya hazina ya mungu wake. Kisha mfalme akamwagiza Ashpenazi, mkuu wa maafisa wa mfalme, kumletea baadhi ya Waisraeli kutoka jamaa ya mfalme na kutoka jamaa kuu, vijana wanaume wasio na dosari mwilini, wenye sura nzuri, wanaoonyesha kipaji katika kila aina ya elimu, wenye ufahamu mzuri, wepesi kuelewa, na waliofuzu kuhudumu katika jumba la kifalme. Alikuwa awafundishe lugha na maandiko ya Wakaldayo. Mfalme akawaagizia kiasi cha chakula na divai ya kila siku kutoka meza ya mfalme. Walikuwa wafundishwe kwa miaka mitatu, na hatimaye waingie kwenye utumishi wa mfalme.