Wakolosai 4:2-18
Wakolosai 4:2-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Dumuni katika sala, na mnaposali muwe waangalifu, mkimshukuru Mungu. Vilevile, mtuombee sisi pia ili Mungu atupe fursa ya kuuhubiri ujumbe wake kuhusu siri ya Kristo. Kwa ajili hiyo mimi niko sasa kifungoni. Basi, ombeni ili niweze kusema kama inavyonipasa na kwa namna itakayodhihirisha siri hiyo. Muwe na hekima katika uhusiano wenu na watu wasioamini, mkitumia vizuri wakati mlio nao. Mazungumzo yenu yanapaswa kuwa daima mema na yaliyokolezwa kwa chumvi na ya kuvutia, na mnapaswa kujua jinsi ya kumjibu vizuri kila mmoja. Ndugu yetu mpenzi Tukiko, mfanyakazi mwaminifu na mtumishi mwenzetu katika kazi ya Bwana, atawapeni habari zangu zote. Ndiyo maana ninamtuma, ili aichangamshe mioyo yenu kwa kuwaambieni habari zetu. Anakuja pamoja na Onesimo, ndugu yetu mpenzi na mwaminifu, ambaye ni mwananchi mwenzenu. Watawapeni habari za mambo yote yanayofanyika hapa. Aristarko, ambaye yuko kifungoni pamoja nami, anawasalimuni; hali kadhalika Marko, binamu yake Barnaba, (mmekwisha pata maagizo juu yake; akifika kwenu mkaribisheni). Naye Yoshua aitwaye Yusto, anawasalimuni. Miongoni mwa Wayahudi waliokwisha pokea imani, hawa tu peke yao, ndio wanaofanya kazi pamoja nami kwa ajili ya ufalme wa Mungu; nao wamekuwa msaada mkubwa kwangu. Epafra, mwananchi mwenzenu na mtumishi wa Kristo Yesu, anawasalimuni. Daima anawaombeeni nyinyi kwa bidii ili mpate kusimama imara, mkomae na kuwa thabiti kabisa katika mambo yote anayotaka Mungu. Naweza kushuhudia kwamba anafanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu na kwa ajili ya watu wa Laodikea na Hierapoli. Luka, daktari wetu mpenzi, na Dema, wanawasalimuni. Salamu zetu kwa ndugu wa Laodikea. Msalimuni dada Nimfa pamoja na jumuiya yote ya waumini inayokutana nyumbani kwake. Mkisha soma barua hii, hakikisheni kwamba inasomwa na Wakristo wa Laodikea; na nyinyi fanyeni mpango mpate kuisoma barua waliyoipata wao. Mwambieni Arkipo aitekeleze vizuri ile huduma aliyokabidhiwa na Bwana. Naandika haya kwa mkono wangu mwenyewe: Salamu kutoka kwangu, mimi Paulo. Kumbukeni kwamba niko kifungoni. Neema ya Mungu iwe nanyi.
Wakolosai 4:2-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani; mkituombea na sisi pia, kwamba Mungu atufungulie mlango kwa lile neno lake, tuinene siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake nimefungwa, ili niidhihirishe, kama inipasavyo kunena. Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati. Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu. Tikiko, ndugu mpendwa, mtumishi mwaminifu, mjoli wangu katika Bwana, atawaarifu mambo yangu yote; ambaye nimemtuma kwenu kwa sababu iyo hiyo, ili mjue mambo yetu, naye akawafariji mioyo yenu; pamoja na Onesimo, ndugu mwaminifu, mpendwa, aliye mtu wa kwenu. Hao watawaarifu mambo yote ya hapa petu. Aristarko, aliyefungwa pamoja nami, awasalimu; na Marko, mjomba wake Barnaba, ambaye mmepokea maagizo kwa habari yake; akifika kwenu mkaribisheni. Na Yesu aitwaye Yusto; hao ni watu wa tohara. Tena hao peke yao ni watendaji wa kazi pamoja nami kwa ajili ya ufalme wa Mungu; nao walikuwa faraja kwangu. Epafra, aliye mtu wa kwenu, mtumwa wa Yesu Kristo, awasalimu, akifanya bidii siku zote kwa ajili yenu katika maombi yake, ili kwamba msimame wakamilifu na kuthibitika sana katika mapenzi yote ya Mungu. Maana namshuhudia kwamba ana juhudi nyingi kwa ajili yenu, na kwa ajili ya hao walioko Laodikia, na kwa ajili ya hao walioko Hierapoli. Luka, yule tabibu mpendwa, na Dema, wanawasalimu. Wasalimuni ndugu walioko Laodikia, na Nimfa, na kanisa lililo katika nyumba yake. Waraka huu ukiisha kusomwa kwenu fanyeni kwamba usomwe katika kanisa la Walaodikia pia; na ule wa Laodikia usomwe na ninyi. Mwambieni Arkipo, Iangalie sana huduma ile uliyopewa katika Bwana, ili uitimize. Salamu yangu mimi Paulo, kwa mkono wangu mwenyewe. Kumbukeni kufungwa kwangu. Neema na iwe pamoja nanyi.
Wakolosai 4:2-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba mkiwa na shukrani; mkituombea na sisi pia, kwamba Mungu atufungulie mlango kwa lile neno lake, tuinene siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake nimefungwa, ili niidhihirishe, kama inipasavyo kunena. Nendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati. Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolezwa chumvi, ili mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu. Tikiko, ndugu mpendwa, mtumishi mwaminifu, mwenzi wangu katika Bwana, atawaarifu mambo yangu yote; ambaye nimemtuma kwenu kwa sababu iyo hiyo, ili mjue mambo yetu, naye akawafariji mioyo yenu; pamoja na Onesimo, ndugu mwaminifu, mpendwa, aliye mtu wa kwenu. Hao watawaarifu mambo yote ya hapa petu. Aristarko, aliyefungwa pamoja nami, awasalimu; pamoja na Marko, binamu yake Barnaba, ambaye mmepokea maagizo juu yake; akifika kwenu mkaribisheni. Na Yesu aitwaye Yusto awasalimu. Hao tu ndio watu wa tohara miongoni mwa wale watendao kazi pamoja nami kwa ajili ya ufalme wa Mungu; nao wamekuwa msaada kwangu. Epafra, aliye mtu wa kwenu, mtumwa wa Yesu Kristo, awasalimu, akifanya bidii siku zote kwa ajili yenu katika maombi yake, ili msimame mkiwa wakamilifu na kuthibitika kabisa katika mapenzi yote ya Mungu. Maana namshuhudia kwamba ana juhudi nyingi kwa ajili yenu, na kwa ajili ya hao walioko Laodikia, na kwa ajili ya hao walioko Hierapoli. Luka, yule tabibu mpendwa, na Dema, wanawasalimu. Wasalimuni ndugu walioko Laodikia, na Nimfa, na kanisa lililo katika nyumba yake. Waraka huu ukiisha kusomwa kwenu hakikisheni kwamba unasomwa katika kanisa la Walaodikia pia; na ule wa Laodikia usomwe na ninyi. Mwambieni Arkipo, Iangalie sana huduma ile uliyopewa katika Bwana, ili uitimize. Naandika salamu yangu mimi Paulo, kwa mkono wangu mwenyewe. Kumbukeni kufungwa kwangu. Neema na iwe pamoja nanyi.
Wakolosai 4:2-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Dumuni sana katika maombi, mkikesha katika hayo pamoja na kushukuru. Pia tuombeeni na sisi ili Mungu atufungulie mlango wa kunena, ili tupate kuitangaza siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake pia mimi nimefungwa. Ombeni ili nipate kuitangaza Injili kwa udhahiri kama ipasavyo kunena. Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati. Maneno yenu yawe yamejaa neema siku zote, yanayofaa, ili mjue jinsi iwapasavyo na inavyofaa kumjibu kila mtu. Tikiko atawaambia habari zangu zote. Yeye ni ndugu mpendwa, mtendakazi mwaminifu na mtumishi mwenzangu katika Bwana. Nimemtuma kwenu kwa madhumuni haya ili mpate kufahamu hali yetu, na pia awatie moyo. Anakuja pamoja na Onesimo, ndugu yetu mpendwa na mwaminifu, ambaye ni mmoja wenu. Watawaambia mambo yote yanayotendeka hapa kwetu. Aristarko aliye mfungwa pamoja nami anawasalimu, vivyo hivyo Marko, binamu yake Barnaba. (Mmeshapata maagizo yanayomhusu; akija kwenu, mpokeeni.) Yesu, yeye aitwaye Yusto, pia anawasalimu. Hawa peke yao ndio Wayahudi miongoni mwa watendakazi wenzangu kwa ajili ya Ufalme wa Mungu, nao wamekuwa faraja kwangu. Epafra, ambaye ni mmoja wenu na mtumishi wa Kristo Yesu, anawasalimu. Yeye siku zote anawaombea kwa bidii kwamba msimame imara katika mapenzi yote ya Mungu, mkiwa wakamilifu na thabiti. Ninashuhudia kumhusu kwamba anafanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu, na kwa ajili ya ndugu wa Laodikia na wale wa Hierapoli. Rafiki yetu mpenzi Luka yule tabibu, pamoja na Dema, wanawasalimu. Wasalimuni ndugu wote wa Laodikia, na pia Nimfa, pamoja na kanisa linalokutana katika nyumba yake. Baada ya barua hii kusomwa kwenu, hakikisheni kwamba inasomwa pia katika kanisa la Walaodikia. Nanyi pia msome barua inayotoka Laodikia. Mwambieni Arkipo hivi: “Hakikisha kuwa unakamilisha ile huduma uliyopokea katika Bwana.” Mimi, Paulo, naandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe. Kumbukeni minyororo yangu. Neema iwe nanyi. Amen.