Amosi 5:18-24
Amosi 5:18-24 Biblia Habari Njema (BHN)
Ole wenu nyinyi mnaoingojea kwa hamu siku ya Mwenyezi-Mungu! Kwa nini mnaitaka sana siku hiyo? Siku hiyo, itakuwa siku ya giza na sio ya mwanga! Mambo yatakuwa kama mtu aliyekimbia simba, halafu akakumbana na dubu! Au kama mtu anayerudi nyumbani kwake, akatia mkono ukutani, akaumwa na nyoka. Siku ya Mwenyezi-Mungu itakuwa giza, na sio mwanga; itakuwa huzuni bila uangavu wowote. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nazichukia na kuzidharau sikukuu zenu; siifurahii mikutano yenu ya kidini. Mjaponitolea sadaka zenu za kuteketezwa na za nafaka, mimi sitakubali kuzipokea; na sadaka zenu za amani za wanyama wanono mimi sitaziangalia kabisa. Ondoeni mbele yangu kelele za nyimbo zenu! Sitaki kusikiliza muziki wa vinubi vyenu! Lakini acheni haki itiririke kama maji, uadilifu uwe kama mto usiokauka.
Amosi 5:18-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ole wenu! Ninyi mnaoitamani siku ya BWANA; kwa nini kuitamani siku ya BWANA? Ni giza, wala si nuru. Ni kama mtu aliyemkimbia simba, akakutana na dubu; au aliingia katika nyumba akauegemeza mkono wake ukutani, nyoka akamwuma. Je! Siku ya BWANA haitakuwa giza, wala si nuru? Naam, yenye giza sana, wala haina mwanga. Mimi nazichukia sikukuu zenu, nazidharau, nami sitapendezwa na makutano yenu ya dini. Naam, ijapokuwa mnanitolea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za unga, sitazikubali; wala sitaziangalia sadaka zenu za amani, na za wanyama walionona. Niondoleeni kelele za nyimbo zenu; kwa maana sitaki kuzisikia sauti za vinanda vyenu. Lakini hukumu na iteremke kama maji, na haki kama maji makuu.
Amosi 5:18-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ole wenu! Ninyi mnaoitamani siku ya BWANA; kwani kuitamani siku ya BWANA? Ni giza, wala si nuru. Ni kama mtu aliyemkimbia simba, akakutana na dubu; au aliingia katika nyumba akauegemeza mkono wake ukutani, nyoka akamwuma. Je! Siku ya BWANA haitakuwa giza, wala si nuru? Naam, yenye giza sana, wala haina mwanga. Mimi nazichukia sikukuu zenu, nazidharau, nami sitapendezwa na makutano yenu ya dini. Naam, ijapokuwa mnanitolea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za unga, sitazikubali; wala sitaziangalia sadaka zenu za amani, na za wanyama walionona. Niondoleeni kelele za nyimbo zenu; kwa maana sitaki kuzisikia sauti za vinanda vyenu. Lakini hukumu na itelemke kama maji, na haki kama maji makuu.
Amosi 5:18-24 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ole wenu ninyi mnaoitamani siku ya BWANA! Kwa nini mnaitamani siku ya BWANA? Siku hiyo itakuwa giza, si nuru. Itakuwa kama vile mtu aliyemkimbia simba kumbe akakutana na dubu, kama vile mtu aliyeingia nyumbani mwake na kuupumzisha mkono wake kwenye ukuta, kumbe akaumwa na nyoka. Je, siku ya BWANA haitakuwa giza, na si nuru: giza nene, bila mwonzi wa mwanga? “Ninachukia, ninazidharau sikukuu zenu za dini; siwezi kuvumilia makusanyiko yenu. Hata ingawa mnaniletea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka za nafaka, sitazikubali. Ingawa mnaniletea sadaka nzuri za amani, sitazitambua. Niondoleeni kelele za nyimbo zenu! Sitasikiliza sauti za vinubi vyenu. Lakini acheni haki itiririke kama mto, na uadilifu uwe kama kijito kisichokauka!