Amosi 1:1-5
Amosi 1:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Maneno ya Amosi, mmojawapo wa wachungaji wa mji wa Tekoa. Mungu alimfunulia Amosi mambo haya yote kuhusu Israeli miaka miwili kabla ya lile tetemeko la ardhi, wakati Uzia alipokuwa mfalme wa Yuda, na Yeroboamu mwana wa Yoashi, alipokuwa mfalme wa Israeli. Amosi alisema hivi: Mwenyezi-Mungu ananguruma kutoka mlima Siyoni, anavumisha sauti yake kutoka Yerusalemu, hata malisho ya wachungaji yanakauka, nyasi mlimani Karmeli zinanyauka. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Watu wa Damasko wametenda dhambi tena na tena; kwa hiyo, sitaacha kuwaadhibu; waliwatendea watu wa Gileadi ukatili mbaya. Basi, nitaishushia moto ikulu ya mfalme Hazaeli, nao utaziteketeza kabisa ngome za mfalme Ben-hadadi. Nitayavunjavunja malango ya mji wa Damasko, na kuwang'oa wakazi wa bonde la Aweni, pamoja na mtawala wa Beth-edeni. Watu wa Aramu watapelekwa uhamishoni Kiri. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Amosi 1:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maneno ya Amosi, aliyekuwa mmoja wa wachungaji wa Tekoa; maono aliyoyaona katika habari za Israeli, siku za Uzia, mfalme wa Yuda, na siku za Yeroboamu, mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli, miaka miwili kabla ya tetemeko la nchi. Naye alisema, BWANA atanguruma toka Sayuni, Atatoa sauti yake toka Yerusalemu; Na malisho ya wachungaji yatakauka, Na kilele cha Karmeli kitanyauka. Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Dameski, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameipura Gileadi kwa vyombo vya kupuria vya chuma; lakini nitatuma moto uingie katika nyumba ya Hazaeli, nao utayateketeza majumba ya Ben-hadadi. Nami nitalivunja komeo la Dameski, na kuwakatilia mbali wenyeji wa bondeni mwa Aveni, na yeye aishikaye fimbo ya enzi katika Beth-Adini; na watu wa Shamu watakwenda uhamishoni hadi Kiri, asema BWANA.
Amosi 1:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maneno ya Amosi, aliyekuwa mmoja wa wachungaji wa Tekoa; maono aliyoyaona katika habari za Israeli, siku za Uzia, mfalme wa Yuda, na siku za Yeroboamu, mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli, miaka miwili kabla ya tetemeko la nchi. Naye alisema, BWANA atanguruma toka Sayuni, Atatoa sauti yake toka Yerusalemu; Na malisho ya wachungaji yataomboleza, Na kilele cha Karmeli kitanyauka. Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Dameski, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameipura Gileadi kwa vyombo vya kupuria vya chuma; lakini nitapeleka moto uingie katika nyumba ya Hazaeli, nao utayateketeza majumba ya Ben-hadadi. Nami nitalivunja komeo la Dameski, na kuwakatilia mbali wenyeji wa bondeni mwa Aveni, na yeye aishikaye fimbo ya enzi katika Beth-Adini; na watu wa Shamu watakwenda hali ya kufungwa hata Kiri, asema BWANA.
Amosi 1:1-5 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Maneno ya Amosi, mmoja wa wachunga wanyama wa Tekoa: yale aliyoyaona kuhusu Israeli miaka miwili kabla ya tetemeko la ardhi, wakati Uzia alikuwa mfalme wa Yuda, na Yeroboamu mwana wa Yehoashi alikuwa mfalme wa Israeli. Alisema: “BWANA ananguruma toka Sayuni, pia ananguruma kutoka Yerusalemu; malisho ya wachunga wanyama yanakauka, kilele cha Karmeli kinanyauka.” Hili ndilo asemalo BWANA: “Kwa dhambi tatu za Dameski, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu aliipura Gileadi kwa vyombo vya chuma vyenye meno. Nitatuma moto juu ya nyumba ya Hazaeli ambao utateketeza ngome za Ben-Hadadi. Nitalivunja lango la Dameski; nitamwangamiza mfalme aliyeko katika Bonde la Aveni, na yeye ambaye anaishika fimbo ya utawala katika Beth-Edeni. Watu wote wa Aramu watakwenda uhamishoni huko Kiri,” asema BWANA.