Matendo 8:14-25
Matendo 8:14-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Wale mitume waliokuwa kule Yerusalemu walipopata habari kwamba wenyeji wa Samaria nao wamelipokea neno la Mungu, waliwatuma huko Petro na Yohane. Walipofika waliwaombea hao waumini ili wampokee Roho Mtakatifu; maana wakati huo Roho Mtakatifu hakuwa amemshukia yeyote kati yao; walikuwa wamebatizwa tu kwa jina la Bwana Yesu. Basi, Petro na Yohane wakawawekea mikono hao waumini, nao wakampokea Roho Mtakatifu. Hapo Simoni alingamua kwamba kwa kuwekewa mikono ya mitume waumini walipewa Roho Mtakatifu. Hivyo aliwapa Petro na Yohane fedha akisema, “Nipeni na mimi uwezo huo ili yeyote nitakayemwekea mikono, apokee Roho Mtakatifu.” Lakini Petro akamjibu, “Potelea mbali na fedha zako kwa vile unafikiri kwamba unaweza kununua karama ya Mungu kwa fedha! Huna sehemu yoyote wala haki katika kazi hiyo kwa maana moyo wako hauko sawa mbele ya macho ya Mungu. Kwa hiyo, tubu ubaya wako huu na umwombe Bwana naye anaweza kukusamehe fikira kama hizo. Ni dhahiri kwangu kwamba umejaa wivu mkali na u mfungwa wa dhambi!” Simoni akajibu, “Tafadhali, niombeeni kwa Bwana lisije likanipata lolote kati ya hayo mliyosema.” Baada ya Petro na Yohane kutoa ushuhuda wao na kuutangaza ujumbe wa Bwana, walirudi Yerusalemu. Walipokuwa wanarudi walihubiri Habari Njema katika vijiji vingi vya Samaria.
Matendo 8:14-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana; ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu; kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu. Wakati Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema, Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu. Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali. Huna fungu wala huna sehemu katika jambo hili, kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu. Basi, tubia uovu wako huu, ukamwombe Bwana, ili ikiwezekana, usamehewe fikira hii ya moyo wako. Kwa maana nakuona uko katika uchungu kama nyongo, na tena uko katika kifungo cha uovu. Simoni akajibu, akasema, Niombeeni ninyi kwa Bwana, yasinifikie mambo haya mliyosema hata moja. Nao walipokwisha kushuhudia na kulihubiri neno la Bwana wakarudi Yerusalemu, wakaihubiri Injili katika vijiji vingi vya Wasamaria.
Matendo 8:14-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana; ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu; kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu. Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema, Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu. Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali. Huna fungu wala huna sehemu katika jambo hili, kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu. Basi, tubia uovu wako huu, ukamwombe Bwana, ili kama yamkini, usamehewe fikira hii ya moyo wako. Kwa maana nakuona u katika uchungu kama nyongo, na tena u katika kifungo cha uovu. Simoni akajibu, akasema, Niombeeni ninyi kwa Bwana, yasinifikilie mambo haya mliyosema hata moja. Nao walipokwisha kushuhudia na kulihubiri neno la Bwana wakarudi Yerusalemu, wakaihubiri Injili katika vijiji vingi vya Wasamaria.
Matendo 8:14-25 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi mitume waliokuwa Yerusalemu waliposikia kuwa Samaria wamelipokea neno la Mungu, wakawatuma Petro na Yohana waende huko. Nao walipofika wakawaombea ili wampokee Roho Mtakatifu, kwa sababu Roho Mtakatifu alikuwa bado hajawashukia hata mmoja ila wamebatizwa tu katika jina la Bwana Yesu. Ndipo Petro na Yohana wakaweka mikono yao juu ya wale waliobatizwa, nao wakapokea Roho Mtakatifu. Simoni alipoona kuwa watu wanapokea Roho Mtakatifu mitume walipoweka mikono juu yao, akataka kuwapa fedha akisema, “Nipeni na mimi uwezo huu ili kila mtu nitakayeweka mikono yangu juu yake apate kupokea Roho Mtakatifu.” Petro akamjibu, “Fedha yako na iangamie pamoja nawe, kwa sababu ulidhani unaweza kununua karama ya Mungu kwa fedha! Wewe huna sehemu wala fungu katika huduma hii kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu. Kwa hiyo tubu kwa uovu huu wako na umwombe Bwana. Yamkini aweza kukusamehe mawazo uliyo nayo moyoni mwako. Kwa maana ninaona kwamba wewe umejawa na uchungu na ni mfungwa wa dhambi.” Ndipo Simoni akajibu, “Niombeeni kwa Bwana, ili hayo mliyosema lolote yasinitukie.” Nao walipokwisha kutoa ushuhuda na kuhubiri neno la Bwana, wakarudi Yerusalemu wakihubiri Injili katika vijiji vingi vya Samaria.