Matendo 7:23-29
Matendo 7:23-29 Biblia Habari Njema (BHN)
“Alipokuwa na umri wa miaka arubaini aliamua kwenda kuwaona ndugu zake Waisraeli. Huko alimwona mmoja wao akitendewa vibaya, akaenda kumwokoa, na kwa kulipiza kisasi, akamuua yule Mmisri. ( Alidhani kwamba Waisraeli wenzake wangeelewa kwamba Mungu angemtumia yeye kuwakomboa, lakini hawakuelewa hivyo). Kesho yake, aliwaona Waisraeli wawili wakipigana, akajaribu kuwapatanisha akisema: ‘Nyinyi ni ndugu; kwa nini basi, kutendeana vibaya nyinyi kwa nyinyi?’ Yule aliyekuwa anampiga mwenzake alimsukuma Mose kando akisema: ‘Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri jana?’ Baada ya kusikia hayo, Mose alikimbia, akaenda kukaa katika nchi ya Midiani na huko akapata watoto wawili.
Matendo 7:23-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Umri wake ulipokuwa kama miaka arubaini akaazimu moyoni mwake kwenda kuwatazama ndugu zake Waisraeli. Akamwona mmoja akidhulumiwa, akamtetea, akamlipizia kisasi yule aliyekuwa akionewa, akampiga huyo Mmisri. Alidhani kwamba ndugu zake watafahamu ya kuwa Mungu anawapa wokovu kwa mkono wake, lakini hawakufahamu. Kesho yake akawatokea walipokuwa wakishindana, akataka kuwapatanisha, akisema, Enyi bwana zangu, ninyi ni ndugu. Mbona mnadhulumiana? Lakini yeye aliyemdhulumu mwenziwe akamsukumia mbali, akisema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri jana? Musa akakimbia kwa neno hilo, akakaa kama mgeni katika nchi ya Midiani, akazaa wana wawili huko.
Matendo 7:23-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Umri wake ulipopata kama miaka arobaini akaazimu moyoni mwake kwenda kuwatazama ndugu zake Waisraeli. Akamwona mmoja akidhulumiwa, akamtetea, akamlipia kisasi yule aliyekuwa akionewa, akampiga huyo Mmisri. Alidhani kwamba ndugu zake watafahamu ya kuwa Mungu anawapa wokovu kwa mkono wake, lakini hawakufahamu. Siku ya pili yake akawatokea walipokuwa wakishindana, akataka kuwapatanisha, akisema, Enyi bwana zangu, ninyi ni ndugu. Mbona mnadhulumiana? Lakini yeye aliyemdhulumu mwenziwe akamsukumia mbali, akisema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri jana? Musa akakimbia kwa neno hilo, akakaa hali ya ugeni katika nchi ya Midiani, akazaa wana wawili huko.
Matendo 7:23-29 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Mose alipokuwa na umri wa miaka arobaini aliamua kuwatembelea ndugu zake Waisraeli. Aliona mmoja wao akidhulumiwa na Mmisri, akamtetea yule aliyeonewa, akampiga yule Mmisri akamuua kulipiza kisasi. Mose alidhani kuwa ndugu zake wangetambua kwamba Mungu anamtumia ili kuwaokoa, lakini wao hawakuelewa. Siku iliyofuata Mose aliwakuta Waisraeli wawili wakigombana, akajaribu kuwapatanisha kwa kuwaambia, ‘Enyi watu, ninyi ni ndugu, mbona mnataka kudhulumiana?’ “Lakini yule mtu aliyekuwa akimdhulumu mwenzake akamsukuma Mose kando, akamuuliza, ‘Ni nani aliyekufanya mtawala na mwamuzi juu yetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri jana?’ Mose aliposikia maneno haya, alikimbilia huko Midiani alikokaa kama mgeni, naye akapata watoto wawili wa kiume.