Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 7:1-19

Matendo 7:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kuhani Mkuu akasema, Je! Mambo hayo ndivyo yalivyo? Naye akasema, Ndugu zangu na baba zangu, sikilizeni: Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu Ibrahimu, alipokuwa katika Mesopotamia, kabla hajakaa Harani, akamwambia, Toka katika nchi yako na katika jamaa zako, ukaende hata nchi nitakayokuonyesha. Ndipo alipotoka katika nchi ya Wakaldayo, akakaa Harani, akatoka huko baada ya kufa babaye, Mungu akamhamisha mpaka nchi hii mnayokaa ninyi sasa. Wala hakumpa urithi humu hata kiasi cha kuweka mguu; akaahidi kwamba atampa, iwe milki yake, na ya uzao wake baadaye alipokuwa hana mtoto. Mungu akanena hivi, ya kwamba wazao wake watakuwa wageni katika nchi ya watu wengine, nao watawafanya kuwa watumwa wao, na kuwatenda mabaya kwa muda wa miaka mia nne. Na lile taifa watakaowafanya watumwa nitawahukumu mimi, alisema Mungu; na baada ya hayo watatoka, nao wataniabudu mahali hapa. Akampa agano la tohara; basi Ibrahimu akamzaa Isaka, akamtahiri siku ya nane. Isaka akamzaa Yakobo. Yakobo akawazaa wale kumi na wawili, wazee wetu. Wale wazee wetu wakimwonea wivu Yusufu, wakamwuza aende Misri. Mungu akawa pamoja naye, akamtoa katika dhiki zake zote, akampa fadhili na hekima mbele ya Farao, mfalme wa Misri; naye akamfanya awe mtawala juu ya Misri na nyumba yake yote. Basi kukawa njaa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, na dhiki nyingi, wala baba zetu hawakupata chakula cha kuwatosha. Hata Yakobo aliposikia ya kwamba huko Misri kuna nafaka, akawatuma baba zetu mara ya kwanza. Hata safari ya pili Yusufu akajitambulisha kwa ndugu zake, jamaa ya Yusufu ikawa dhahiri kwa Farao. Yusufu akatuma watu akamwita Yakobo babaye na jamaa zake wote pia, watu sabini na watano. Basi Yakobo akashuka mpaka Misri; akafa yeye na baba zetu; wakachukuliwa mpaka Shekemu wakazikwa katika kaburi lile, ambalo Ibrahimu alilinunua kwa kima cha fedha kwa wana wa Hamori, huko Shekemu. Basi wakati wa ile ahadi ambayo Mungu alimpa Ibrahimu ulipokuwa unakaribia, wale watu wakazidi na kuongezeka sana huko Misri, hata mfalme mwingine akainuka juu ya Misri, asiyemfahamu Yusufu. Huyo akawafanyia hila kabila yetu, na kuwatenda mabaya baba zetu, akiwaamuru wawatupe watoto wao wachanga, ili wasiishi.

Shirikisha
Soma Matendo 7

Matendo 7:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)

Basi, kuhani mkuu akamwuliza, “Je, mambo haya ni kweli?” Naye Stefano akasema, “Ndugu zangu na akina baba, nisikilizeni! Mungu alimtokea babu yetu Abrahamu alipokuwa kule Mesopotamia kabla hajaenda kukaa kule Harani. Mungu alimwambia: ‘Ondoka katika nchi yako; waache watu wa ukoo wako; nenda katika nchi nitakayokuonesha!’ Kwa hivyo, Abrahamu alihama nchi ya Kaldayo, akaenda kukaa Harani. Baada ya kifo cha baba yake, Mungu alimtoa tena Harani akaja kukaa katika nchi hii mnayokaa sasa. Mungu hakumpa hata sehemu moja ya nchi hii iwe mali yake; hata hivyo, alimwahidi kumpa nchi hii iwe yake na ya wazawa wake, ingawaje wakati huu hakuwa na mtoto. Mungu alimwambia hivi: ‘Wazawa wako watapelekwa katika nchi inayotawaliwa na watu wengine, na huko watafanywa watumwa na kutendewa vibaya kwa muda wa miaka 400. Lakini mimi nitalihukumu taifa hilo litakalowafanya watumwa. Kisha nitawatoa katika nchi hiyo ili waje kuniabudu mahali hapa.’ Halafu Mungu akafanya naye agano ambalo tohara ni ishara yake. Hivyo, Abrahamu alimtahiri mtoto wake Isaka siku ya nane baada ya kuzaliwa. Na Isaka, vivyo hivyo, alimtahiri Yakobo. Naye Yakobo aliwatendea wale mababu kumi na wawili vivyo hivyo. “Wale mababu walimwonea wivu Yosefu, wakamwuza utumwani Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye, akamwokoa katika taabu zake zote. Mungu alimjalia fadhili na hekima mbele ya Farao, mfalme wa Misri, hata Farao akamweka awe mkuu wa ile nchi na nyumba ya kifalme. Kisha, kulizuka njaa kubwa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, ikasababisha dhiki kubwa. Babu zetu hawakuweza kupata chakula chochote. Basi, Yakobo aliposikia habari kwamba huko Misri kulikuwa na nafaka, aliwatuma watoto wake, yaani babu zetu, waende huko Misri mara ya kwanza. Katika safari yao ya pili, Yosefu alijitambulisha kwa ndugu zake, na Farao akaifahamu jamaa ya Yosefu. Yosefu alituma ujumbe kwa baba yake na jamaa yote, jumla watu sabini na watano, waje Misri. Hivyo, Yakobo alikwenda Misri ambako yeye na babu zetu wengine walikufa. Miili yao ililetwa mpaka Shekemu, ikazikwa katika kaburi ambalo Abrahamu alikuwa amenunua kutoka kwa kabila la Hamori kwa kiasi fulani cha fedha. “Wakati ulipotimia Mungu aitimize ahadi aliyompa Abrahamu, idadi ya wale watu kule Misri ilikwisha ongezeka na kuwa kubwa zaidi. Mwishowe, mfalme mmoja ambaye hakumtambua Yosefu alianza kutawala huko Misri. Alilifanyia taifa letu ukatili, akawatendea vibaya babu zetu kwa kuwalazimisha waweke nje watoto wao wachanga ili wafe.

Shirikisha
Soma Matendo 7

Matendo 7:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kuhani Mkuu akasema, Je! Mambo hayo ndivyo yalivyo? Naye akasema, Ndugu zangu na baba zangu, sikilizeni: Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu Abrahamu, alipokuwa katika Mesopotamia, kabla hajakaa Harani, akamwambia, Toka katika nchi yako na katika jamaa zako, ukaende hata nchi nitakayokuonesha. Ndipo alipotoka katika nchi ya Wakaldayo, akakaa Harani, akatoka huko baada ya kufa babaye, Mungu akamhamisha mpaka nchi hii mnayokaa ninyi sasa. Wala hakumpa urithi humu hata kiasi cha kuweka mguu; akaahidi kwamba atampa, iwe milki yake, na ya uzao wake baadaye alipokuwa hana mtoto. Mungu akanena hivi, ya kwamba wazawa wake watakuwa wageni katika nchi ya watu wengine, nao watawafanya kuwa watumwa wao, na kuwatenda mabaya kwa muda wa miaka mia nne. Na lile taifa watakaowafanya watumwa nitawahukumu mimi, alisema Mungu; na baada ya hayo watatoka, nao wataniabudu mahali hapa. Akampa agano la tohara; basi Abrahamu akamzaa Isaka, akamtahiri siku ya nane. Isaka akamzaa Yakobo. Yakobo akawazaa wale kumi na wawili, wazee wetu. Wale wazee wetu wakimwonea wivu Yusufu, wakamwuza aende Misri. Mungu akawa pamoja naye, akamtoa katika dhiki zake zote, akampa fadhili na hekima mbele ya Farao, mfalme wa Misri; naye akamfanya awe mtawala juu ya Misri na nyumba yake yote. Basi kukawa na njaa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, na dhiki nyingi, wala baba zetu hawakupata chakula cha kuwatosha. Hata Yakobo aliposikia ya kwamba huko Misri kuna nafaka, akawatuma baba zetu mara ya kwanza. Hata safari ya pili Yusufu akajitambulisha kwa ndugu zake, jamaa ya Yusufu ikawa dhahiri kwa Farao. Yusufu akatuma watu akamwita Yakobo babaye na jamaa zake wote pia, watu sabini na watano. Basi Yakobo akashuka mpaka Misri; akafa yeye na baba zetu; wakachukuliwa mpaka Shekemu wakazikwa katika kaburi lile, ambalo Abrahamu alilinunua kwa kima fulani cha fedha kutoka kwa wana wa Hamori, huko Shekemu. Basi wakati wa ile ahadi ambayo Mungu alimpa Abrahamu ulipokuwa unakaribia, wale watu wakazidi na kuongezeka sana huko Misri, hata mfalme mwingine asiyemfahamu Yusufu akaanza kutawala katika Misri. Huyo akawafanyia hila kabila yetu, na kuwatenda mabaya baba zetu, akiwaamuru wawatupe watoto wao wachanga, ili wasiishi.

Shirikisha
Soma Matendo 7

Matendo 7:1-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ndipo kuhani mkuu akamuuliza Stefano, “Je, mashtaka haya ni ya kweli?” Stefano akajibu, “Ndugu zangu na baba zangu, nisikilizeni! Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu Abrahamu, alipokuwa bado yuko Mesopotamia, kabla hajaishi Harani, akamwambia, ‘Ondoka kutoka nchi yako na kutoka kwa jamii yako, uende hadi nchi nitakayokuonyesha.’ “Hivyo aliondoka katika nchi ya Wakaldayo akaenda kukaa Harani. Baada ya kifo cha baba yake, Mungu akamtoa huko akamleta katika nchi hii ambayo mnaishi sasa. Mungu hakumpa urithi wowote katika nchi hii, hakumpa hata mahali pa kuweka wayo mmoja. Bali Mungu alimwahidi kuwa yeye na uzao wake baada yake wangeirithi hii nchi, ingawa wakati huo Abrahamu hakuwa na mtoto. Mungu akasema naye hivi: ‘Wazao wako watakuwa wageni kwenye nchi ambayo si yao, nao watafanywa watumwa na kuteswa kwa miaka mia nne.’ Mungu akasema, ‘Lakini mimi nitaliadhibu taifa watakalolitumikia kama watumwa, na baadaye watatoka katika nchi hiyo na wataniabudu mahali hapa.’ Ndipo akampa Abrahamu Agano la tohara. Naye Abrahamu akamzaa Isaki na kumtahiri siku ya nane. Baadaye Isaki akamzaa Yakobo, naye Yakobo akawazaa wale wazee wetu kumi na wawili. “Kwa sababu wazee wetu walimwonea wivu Yosefu ndugu yao, walimuuza kama mtumwa huko Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye. Akamwokoa kutoka mateso yote yaliyompata, tena akampa kibali na hekima aliposimama mbele ya Farao, mfalme wa Misri, ambaye alimweka kuwa mtawala juu ya Misri na juu ya jumba lote la kifalme. “Basi kukawa na njaa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, ikasababisha dhiki kubwa, nao baba zetu wakawa hawana chakula. Lakini Yakobo aliposikia kwamba kuna nafaka huko Misri, aliwatuma baba zetu, wakaenda huko kwa mara yao ya kwanza. Walipokwenda mara ya pili, Yosefu alijitambulisha kwa ndugu zake, nao ndugu zake Yosefu wakajulishwa kwa Farao. Ndipo Yosefu akawatuma kumleta Yakobo baba yake pamoja na jamaa yake yote, jumla yao walikuwa watu sabini na watano. Hivyo Yakobo akaenda Misri ambako yeye na baba zetu walifia. Miili yao ilirudishwa Shekemu na kuzikwa katika kaburi ambalo Abrahamu alinunua kutoka kwa wana wa Hamori kwa kiasi fulani cha fedha. “Lakini wakati ulipokuwa unakaribia wa kutimizwa kwa ile ahadi ambayo Mungu alikuwa amempa Abrahamu, watu wetu walizidi kuongezeka sana huko Misri. Ndipo mfalme mwingine ambaye hakujua lolote kuhusu Yosefu akatawala Misri. Huyu mfalme akawatendea watu wetu hila na kuwatesa baba zetu kwa kuwalazimisha wawatupe watoto wao wachanga ili wafe.

Shirikisha
Soma Matendo 7